HOTUBA
YA MHESHIMIWA PROF. PALAMAGAMBA JOHN AIDAN MWALUKO KABUDI (MB), WAZIRI WA MAMBO
YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA
MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021
1.0 UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu
likubali kupokea na kujadili taarifa
ya utekelezaji wa mpango
na bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Aidha, naomba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha mpango na bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
2.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu rahim,
mwingi wa rehema kwa kuniruzuku uhai na kunijalia afya njema ya kuniwezesha
kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
3.
Mheshimiwa Spika, kwa
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inahitimisha ngwe yake ya kwanza ya miaka mitano
mwaka huu, niruhusu kwa namna ya kipekee kabisa kumpongeza, Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake
mahiri ambao umeliletea Taifa hili maendeleo makubwa katika kipindi hiki cha
uongozi wake. Aidha, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; na Mheshimiwa Kassim
Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kuiongoza vyema nchi yetu na kutekeleza kwa mafanikio makubwa Ilani ya Uchaguzi
ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015 - 2020.
4.
Mheshimiwa Spika,
napenda kumpongeza Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb), Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa umahiri na uongozi wake madhubuti katika uendeshaji
wa shughuli za Bunge. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu
(Mb), Naibu Spika; Wenyeviti wa Bunge; na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za
Bunge kwa kazi nzuri wanazozifanya kumsaidia Mheshimiwa Spika katika kusimamia
na kuendesha shughuli za Bunge. Naomba Mwenyezi Mungu azidi kuwajaalia afya
njema, busara na hekima katika kuongoza mhimili huu muhimu katika Taifa letu.
5. Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya pekee napenda kuipongeza na kuishukuru
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini
ya uongozi wa Mheshimiwa Salim Mwinyi Rehani (Mb), kwa kazi nzuri na ya
kizalendo inayoifanya ya kuishauri Serikali hususan Wizara yangu. Aidha,
napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Mussa Azan Zungu (Mb), Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira ambaye alikuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa
kipindi kirefu.
6.
Mheshimiwa Spika, kwa
masikitiko makubwa naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwa
familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa vifo vya Waheshimiwa Rashid Ajali Akbar,
aliyekuwa Mbunge wa Newala; Askofu Dkt. Getrude Rwakatare (Mb); Richard Mganga
Ndassa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumve; na Balozi Dkt. Augustine Phillip
Mahiga (Mb), aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria na kabla ya hapo Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Mwenyezi Mungu azilaze roho za
marehemu mahali pema peponi Amina.
7.
Mheshimiwa Spika,
Hotuba yangu ni kama inavyoonekana katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti ya Wizara
kilichowasilishwa kwako. Hivyo basi, nitasoma muhtasari wake na ninaomba Hotuba
hiyo iingizwe yote kwenye kumbukumbu za Bunge lako Tukufu.
2.0 MAFANIKIO YA WIZARA KWA KIPINDI CHA SERIKALI YA AWAMU YA TANO
8. Mheshimiwa Spika, kwa
kuwa hii ni hotuba yangu ya mwisho nikiwa Waziri mwenye dhamana ya kusimamia
masuala ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kipindi cha
kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano, ninayo heshima kuelezea kwa ufupi baadhi
ya mafanikio makubwa ambayo Wizara inajivunia kuyaratibu kwa ufanisi mkubwa na
kufanikisha utekelezaji wake kwa kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya
Tano, kama ifuatavyo:
a) Ufunguzi
wa Balozi mpya nane za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nchi za Qatar;
Uturuki; Sudan; Cuba; Israel; Algeria; Jamhuri ya Korea; na Namibia.
Kufunguliwa kwa Balozi hizo, kunaifanya Tanzania kuwa na jumla ya Balozi 43 na
Konseli Kuu tatu katika miji ya Mombasa, Dubai na Jeddah. Kadhalika, Balozi za
Ethiopia na Poland zilifunguliwa hapa nchini katika kipindi hicho na kuifanya
Tanzania kuwa mwenyeji wa Balozi 62 na Mashirika ya Kimataifa 30;
b) Tumefanya jitihada kubwa katika kuifanya lugha
ya Kiswahili kutumika katika Jumuiya ya Kimataifa na nchi mbalimbali. Juhudi
hizo za Tanzania zimefanya Kiswahili kitumike katika eneo la Maziwa Makuu,
Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Jumuiya ya Afrika
Mashariki na vyombo mbalimbali vya habari vya Kimataifa.
c) Kufanikisha
kufanyika kwa viwango vya juu Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Dar es Salaam mwezi
Agosti 2019 ambapo Tanzania ilikabidhiwa rasmi Uenyekiti wa Jumuiya hiyo
utakaodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi Agosti 2020.
Katika
uenyekiti wetu wa SADC, tumepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuwa mwenyeji wa
maadhimisho ya Maonesho ya Awamu ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) ambayo yalifanyika mwezi Agosti 2019. Maonesho hayo
yalishirikisha wajasiriamali wapatao 5,352 kutoka ndani na nje ya nchi, Taasisi
za umma, viwanda mbalimbali, Taasisi za huduma za fedha na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO).
d) Wizara imefanikiwa kuhamasisha watalii kuja nchini
kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii. Kwa mfano, kuanzia mwaka 2015 hadi 2018, watalii 5,234,448 wametembelea vivutio
mbalimbali vya utalii nchini. Watalii hao walitoka nchi mbalimbali zilizopo
Bara la Afrika; Ulaya; Amerika ya Kaskazini; Asia; Mashariki ya Kati;
Australasia na nchi za Karibeani;
e) Kufanikisha uenyekiti wa Tanzania katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki ambapo mwezi Machi 2016 nchi yetu iliteuliwa kwa mara
ya pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo. Katika kipindi cha uenyekiti
wake, Tanzania ilifanikisha utekelezaji wa masuala mbalimbali ikiwemo:
i. Kuweka mifumo bora ya matumizi ya rasilimali za
Jumuiya;
ii. Kuimarisha miundombinu yenye sura ya Kikanda;
iii. Kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara kwa Nchi
Wanachama;
iv. Kuratibu
utumiaji wa Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Ofisi zote za Umma
nchini; na
v.
Matumizi
ya Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Taasisi zote za Serikali.
f) Kuratibu
Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic
(Africa - Nordic Foreign Ministers’ Meeting) uliofanyika kwa mafanikio makubwa
mwezi Novemba 2019 jijini Dar es Salaam.
Ni mara ya kwanza kwa Tanzania
kuwa mwenyeji wa Mkutano huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001. Tofauti
na mikutano iliyopita ambayo ilijikita katika masuala ya misaada, mkutano huu ulijielekeza
zaidi katika ushirikiano na kuimarisha biashara, uwekezaji, uchumi wa viwanda,
mazingira na kukuza utalii pamoja na masuala ya amani na usalama;
g) Kufanikisha
ujumuishwaji wa miradi ya Tanzania katika miradi ya kipaumbele ya miundombinu
iliyoidhinishwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
h) Katika
kipindi cha mwaka 2015 – 2019,
Tanzania ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa Itifaki ya Umoja
wa Forodha na Itifaki ya Soko la Pamoja za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama
vile:-
i. Kuondoa vikwazo vya biashara
visivyo vya kiforodha 15 kati ya vikwazo 24 vilivyoripotiwa dhidi ya
Tanzania;
ii. Kutoa
vyeti 32,536 vya uasili wa bidhaa kwa
wafanyabiashara wa Tanzania wanaofanya biashara katika nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki;
iii. Kutoa
vibali vya kuingia nchini 1,117,056 kwa raia
wa Nchi Wanachama wa Jumuiya na wananchi wetu 851,470 walipata vibali vya
kuingia katika nchi nyingine za Jumuiya;
iv.
Kufanikisha
Watanzania 1,555 kupata vibali vya kufanya kazi katika nchi nyingine wanachama
wa Jumuiya na Tanzania ilitoa vibali 2,309 vya kufanya kazi nchini kwa raia
wengine wa Nchi Wanachama wa Jumuiya;
v.
Kutoa vibali vipatavyo 879 kwa
wanafunzi wa nchi nyingine wanachama wa Jumuiya kuingia na kusoma nchini na
wanafunzi watanzania 3,129 walipata vibali vya kusoma katika nchi wanachama wa
Jumuiya; na
vi. Kutoa
vibali vya ukaazi 3,128 kwa raia wengine wa Nchi Wanachama wa Jumuiya na
Watanzania 1,002 walipata vibali vya ukaazi katika Nchi Wanachama wa Jumuiya.
i) Kuratibu
upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya
Maendeleo Afrika (AfDB) wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 200 kwa ajili
ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato jijini Dodoma na upatikanaji
wa mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 180
kutoka Benki hiyo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya pete katika jiji la Dodoma;
na
j) Kushawishi nchi marafiki kutufutia madeni, kuyapunguza au
kuweka masharti nafuu ya kuyalipa. Kutokana na ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Iran mwezi Oktoba 2017, Serikali ya
nchi hiyo iliridhia na kutangaza kusamehe riba ya deni lililokopwa mwaka 1984
ambayo ilifikia kiasi cha Dola za Marekani Milioni 150. Vilevile, mwezi Septemba 2017,
Serikali ya Brazil ilitoa msamaha wenye
thamani ya Dola za Marekani Milioni 203.6 ambayo ni asilimia 86 ya deni
lote tunalodaiwa na nchi hiyo.
9.
Mheshimiwa
Spika, hayo ni baadhi tu ya
mafanikio niliyoyataja hapa. Taarifa nzima kuhusu mafanikio ya Wizara katika
kipindi cha Awamu ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano
inapatikana kwenye Aya ya 14, Kipengele cha kwanza hadi ishirini katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
3.0 MISINGI YA TANZANIA KATIKA MAHUSIANO YA KIMATAIFA
10.
Mheshimiwa Spika, historia ya Tanzania imesheheni misingi na misimamo imara
inayoifanya iendelee kuwa miongoni mwa nchi zilizo na ushawishi mkubwa kikanda
na kimataifa tangu Uhuru. Misingi ya nchi yetu kuheshimika kimataifa iliwekwa
na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa mstari
wa mbele katika kulaani ubabe, uonevu na ukandamizaji popote pale ulipotokea
duniani na alipigania uhuru wa Afrika na kusisitiza mshikamano kati ya nchi
zinazoendelea. Kupitia misingi hii ambayo viongozi wetu wameendelea kuienzi,
Tanzania imeendelea kuheshimika sana kikanda na kimataifa.
11.
Mheshimiwa
Spika, katika kusimamia misingi
hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kulinda uhuru wa nchi, haki yetu ya
kujiamulia mambo yetu wenyewe bila kuingiliwa, mipaka ya nchi yetu; kuimarisha
ujirani mwema; na kutekeleza Sera ya Kutofungamana na Upande Wowote kama dira
na msimamo wetu kwenye mahusiano na nchi nyingine za Jumuiya ya Kimataifa.
4.0 TATHMINI YA HALI YA DUNIA KWA MWAKA 2019/2020
12. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka
2019/2020 hali ya uchumi na siasa duniani ilionesha kuendelea kuimarika na
kutoa matumaini ya kuimarika zaidi kwa kipindi cha miaka michache ijayo, licha
ya kuwepo changamoto za kiulinzi na kiusalama kwa baadhi ya maeneo. Hata hivyo,
mlipuko wa maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na
virusi vya Corona (COVID-19) unaashiria tishio kubwa la kuporomoka kwa uchumi
wa dunia.
13.
Mheshimiwa Spika, taarifa zaidi kuhusu tathmini ya hali ya uchumi, siasa,
ulinzi na usalama ya dunia inapatikana kwenye Aya ya 18 hadi 69 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
14. Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kulipa umuhimu mkubwa suala la
amani na usalama duniani ambalo ni miongoni mwa tunu za Taifa letu tangu kupata
uhuru. Ili kuenzi tunu hizi na kutambua umuhimu wa kulinda na kudumisha amani
na usalama duniani, nchi yetu imeendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa
katika ulinzi wa amani duniani. Katika kutekeleza hilo, hadi kufikia mwezi
Januari 2020, nchi yetu imepeleka walinda amani kwenye misheni za kulinda amani
za Umoja wa Mataifa zilizopo katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Darfur - Sudan, Sudan Kusini na Jimbo la
Abyei.
15. Mheshimiwa Spika, tutaendelea kushirikiana na mataifa mengine
kushughulikia masuala ya amani na usalama katika Bara letu la Afrika. Nitumie
fursa hii kuisihi Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuunga mkono jitahada za
kudumisha amani duniani. Maelezo ya kina kuhusu nafasi ya Tanzania Kimataifa na
Kikanda yanapatikana kwenye Aya ya 70
hadi 81 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
6.0 KUJENGA NA KULINDA TASWIRA YA NCHI KIMATAIFA
16.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuheshimu, wajibu wake
Kikatiba na Mikataba ya Kimataifa ya kulinda na kudumisha haki zote za binadamu
ikiwemo za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, zote zikiwa na umuhimu
ulio sawa kwa ustawi na maendeleo ya Watanzania.
17.
Mheshimiwa
Spika, Tanzania ikiwa Nchi
Mwanachama wa Umoja wa Mataifa imeendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli
za Umoja wa Mataifa, Taasisi na Mashirika yake na pia katika mikutano, mijadala
na shughuli mbalimbali za Umoja huo. Miongoni mwa mijadala hiyo ilifanyika
kwenye Kikao cha 74 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba, 2019
jijini New York, Marekani ambapo nilimwakilisha Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kikao hicho
nilitoa hotuba iliyoelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kwenye sekta
za afya; elimu; maji; usafiri wa anga; nishati na ujenzi.
18.
Mheshimiwa Spika,
katika jitihada za Serikali kuufahamisha ulimwengu namna inavyotetea na
kusimamia haki za binadamu hapa nchini, mwezi Februari 2020 jijini Geneva,
Uswisi niliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Kikao cha 43 cha Baraza la Umoja wa
Mataifa la Haki za Binadamu. Kwenye Kikao hicho nilieleza kuhusu mafanikio ya
Serikali katika kulinda na kusimamia haki za elimu, afya, upatikanaji wa maji
safi na salama, umeme na maendeleo ya kiuchumi. Aidha, nilielezea mafanikio
yaliyopatikana katika kuongeza uwajibikaji kwa watumishi na viongozi wa umma;
kupambana na vitendo vya rushwa; vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya;
kuongezeka kwa kiwango cha ukusanyaji kodi; na kupanua wigo wa vyanzo vya
mapato ili kuwahudumia wananchi wetu ipasavyo.
19.
Mheshimiwa Spika, maelezo
ya kina kuhusu kujenga na kulinda taswira ya nchi kimataifa yanapatikana kwenye
Aya ya 82 hadi 90 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
7.0 WATANZANIA KWENYE NAFASI ZA KIMATAIFA
20.
Mheshimiwa Spika,
baadhi ya Watanzania wamechaguliwa na kuteuliwa kushika nafasi mbalimbali za
uongozi kikanda na kimataifa kama inavyoonekana kwenye Aya ya 91 hadi 98 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
21. Mheshimiwa Spika, baada
ya maelezo hayo, sasa naomba nitoe taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara
kwa kipindi cha mwaka 2019/2020 na mpango wa bajeti kwa mwaka 2020/2021.
8.0 MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA MWAKA 2019/2020
22. Mheshimiwa Spika, katika
kuiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa mwaka 2019/2020, Bunge lako
Tukufu liliidhinisha kiasi cha Shilingi
bilioni mia moja sitini na sita, milioni mia tisa ishirini na sita, laki nane
na ishirini elfu (166,926,820,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni mia moja sitini na mbili,
milioni mia tisa ishirini na sita, laki nane na ishirini elfu (162,926,820,000) ni kwa ajili ya
Matumizi ya Kawaida na Shilingi bilioni
nne (4,000,000,000) ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Katika fedha
zilizotengwa kwa Matumizi ya Kawaida, Shilingi bilioni mia moja hamsini na
mbili, milioni mia saba kumi na saba, laki saba na ishirini na tatu elfu (152,717,723,000) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na
Shilingi bilioni kumi, milioni mia mbili na tisa na tisini na
saba elfu (10,209,097,000)
ni kwa ajili ya Mishahara.
23.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2020 Wizara
ilikuwa imepokea kiasi cha Shilingi
bilioni mia moja thelathini na tatu, milioni mia tatu, laki tisa, mia sita
sabini na moja (133,300,900,671). Kiasi hicho cha fedha ni
sawa na asilimia 79.8 ya fedha zote za bajeti
zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2019/2020. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni mia moja ishirini na nne,
milioni mia moja themanini na sita, laki mbili thelathini na sita, mia sita
sabini na tano (124,186,236,675) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni nane, milioni mia sita
ishirini na sita, laki saba na hamsini na nane elfu (8,626,758,000) ni kwa
ajili ya mishahara. Aidha, katika kipindi hicho Wizara imepokea fedha za bajeti
ya miradi ya maendeleo kiasi cha Shilingi
milioni mia nne themanini na saba, laki tisa na elfu tano, mia tisa tisini na
sita (487,905,996) kwa ajili ya miradi ya ukarabati wa nyumba
ya makazi ya Balozi wa Tanzania Ottawa na ujenzi wa vyumba vya madarasa katika
Chuo cha Diplomasia.
24.
Mheshimiwa Spika, katika fedha
zilizotolewa, Wizara imetumia
kiasi cha Shilingi bilioni tisini na tisa, milioni mia tatu
ishirini na nne, laki mbili, ishirini na mbili elfu, mia saba themanini na sita
(99,324,222,786). Kiasi hicho cha fedha ni sawa na asilimia 75 ya fedha zilizopokelewa.
Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni
tisini na moja, milioni mia tatu tisini, elfu sabini na tisa, mia sita arobaini
na saba (91,390,079,647) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni saba, milioni mia tano
tisini na sita, laki mbili thelathini na
saba, mia moja arobaini na mbili (7,596,237,142) ni kwa ajili ya mishahara. Aidha, Wizara
imetumia kiasi cha Shilingi milioni mia
tatu thelathini na saba, laki tisa na elfu tano, mia tisa tisini na sita (337,905,996) kwa ajili ya mradi wa
maendeleo wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Chuo cha Diplomasia.
25.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2019/2020, Wizara ilipanga kukusanya Shilingi bilioni mbili, milioni mia
tano hamsini, laki nane sabini na tisa na sabini na mbili (2,550,879,072). Kati ya kiasi hicho Shilingi milioni sitini na saba, laki tisa na
themanini elfu (67,980,000) ni maduhuli ya Makao Makuu ya
Wizara na Shilingi bilioni mbili, milioni mia nne themanini na mbili, laki
nane, elfu tisini na tisa na sabini na mbili (2,482,899,072) ni maduhuli kutoka
Balozi za Tanzania nje ya nchi. Vyanzo vya mapato hayo ni pamoja na uhakiki wa
nyaraka, pango la majengo ya Serikali nje ya nchi na mauzo ya nyaraka za
zabuni.
26.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2019 hadi tarehe 30 Aprili, 2020 Wizara
imekusanya jumla ya Shilingi bilioni
tano, milioni mia mbili hamsini na tatu, elfu tisini na moja na mia sita
hamsini (5,253,091,650) sawa na asilimia 206 ya lengo
lililopangwa kwa mwaka 2019/2020. Ongezeko la maduhuli limetokana na baadhi ya
balozi kuendelea kukusanya maduhuli ya viza kupitia utaratibu wa kawaida kabla
ya kuanza kwa utaratibu wa kielekroniki (e-visa).
Aidha, kuanzia mwezi Novemba 2019, Wizara inaendelea
kukusanya maduhuli ya visa kwa njia ya kielektroniki baada ya Balozi zetu
kufungiwa mtandao huo.
27.
Mheshimiwa
Spika, baada
ya kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2019/2020,
naomba sasa nitumie fursa hii kueleza kwa kifupi mapitio ya utekelezaji wa
majukumu ya Wizara katika kipindi hicho.
Kubuni na Kusimamia Utekelezaji wa Sera ya Nchi ya Mambo ya Nje
28.
Mheshimiwa Spika, kama
nilivyoeleza kwenye sehemu ya mafanikio ya Wizara kwa kipindi cha kwanza cha
Serikali ya Awamu ya Tano kuwa Tanzania ni mwenyekiti na mwenyeji wa mikutano
ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kipindi cha mwaka mmoja
kuanzia mwezi Agosti 2019 hadi Agosti 2020. Tangu mwezi Agosti, 2019 tulipopewa
uenyekiti tumeratibu, kuandaa na kuongoza mikutano sita ya kisekta kama
inavyoonekana kwenye Aya ya 200 hadi 207 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
29.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Wizara
imeratibu kwa mafanikio makubwa na kufanikisha kufanyika kwa Mkutano wa Baraza
la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika tarehe 18
Machi 2020. Mkutano huo ulifanyika kwa mara ya kwanza kwa njia ya mtandao ikiwa
ni tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu
unaosababishwa na virusi vya Corona.
30. Mheshimiwa Spika,
kutokana na mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 duniani, ni dhahiri
kwamba ili kukabiliana nao kunahitajika ufanisi na ushirikiano wa hali ya juu
katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa. Kufuatia hali hiyo, kwa mara nyingine tena naomba
nichukue fursa hii kumpongeza Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa SADC pamoja na Dkt. Stergomena
Lawrence Tax, Katibu Mtendaji wa SADC kwa maelekezo na ushauri wanaoendelea
kuutoa kwa Nchi Wanachama ili kuhakikisha kwamba ukanda wetu hauathiriki sana
na janga hili la COVID-19.
31.
Mheshimiwa Spika, katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu zifuatazo ni hatua
mbalimbali ambazo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikisha katika SADC.
Hatua hizo ni kufanyika kwa Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Afya wa SADC
kuhusu COVID -19 tarehe 9 Machi 2020 chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Ummy
Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Mkutano
huu ulifanyika kwa njia ya mtandao ikiwa ni hatua mojawapo ya kudhibiti
maambukizi ya ugonjwa huo. Mkutano huo pamoja na mambo mengine, ulipendekeza
kuundwa kwa Kamati ya Wataalam kwa ajili
ya kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Itifaki ya Afya ya SADC kufuatia
mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona
(COVID-19).
32.
Mheshimiwa Spika, mapendekezo hayo ya Mawaziri wa Afya, yaliridhiwa na
Baraza la Mawaziri wa SADC katika mkutano uliofanyika tarehe 18 Machi, 2020.
Aidha, tarehe 31 Machi 2020, Kamati ya Wataalam ilifanya kikao kwa njia ya
mtandao na kwa kushirikiana na Sekretarieti ya SADC ilipendekeza kuandaliwa kwa
mkutano huu wa Dharura wa Baraza la Mawaziri. Aidha, Kamati hiyo pia iliridhia
mapendekezo 11 katika maeneo yafuatayo:
i.
Ufuatiliaji
na utekelezaji wa Itifaki ya Afya kuhusu magonjwa ya mlipuko;
ii.
Kujiandaa
na kukabiliana na COVID-19;
iii.
Kubaini
wagonjwa, kufuatilia waliokutana na mgonjwa na huduma za tiba;
iv.
Uzuiaji
na udhibiti wa maambukizi;
v.
Uchunguzi
na upimaji wa kimaabara;
vi.
Uelimishaji
wa madhara na ushirikishwaji wa jamii;
vii.
Hatua
stahiki za Afya ya Jamii;
viii.
Uratibu
wa Kikanda wa kukabiliana na COVID-19;
ix.
Uwezeshaji
na usafirishaji wa bidhaa muhimu miongoni mwa nchi za SADC wakati wa mlipuko wa
ugonjwa wa COVID-19;
x.
Masuala
ya uwezeshaji wa biashara katika ukanda kwa kipindi cha ugonjwa wa COVID-19; na
xi.
Usimamizi
wa majanga hatarishi katika ukanda wa SADC.
33. Mheshimiwa Spika, tarehe 6 Aprili 2020 niliongoza Mkutano wa Dharura wa Baraza la
Mawaziri uliofanyika kwa njia ya mtandao. Mkutano huo ulipokea taarifa ya Kamati ya Wataalam ya
kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Itifaki ya Afya ya SADC kufuatia mlipuko
wa ugonjwa wa COVID-19. Aidha, Mkutano uliidhinisha mwongozo wa urazinishaji
(harmonisation) na uwezeshaji wa usafirishaji wa bidhaa muhimu na huduma katika
nchi za SADC katika kipindi hiki cha janga la COVID -19.
34.
Mheshimiwa
Spika, katika
hatua nyingine Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa SADC ameendelea kuzisisitiza Taasisi za
Fedha za Kimataifa na Washirika wengine wa Maendeleo kuzifutia madeni nchi za
SADC, ili ziweze kutumia fedha hizo katika kukabiliana na janga hili la
COVID-19.
35.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, mwezi Machi 2020 Wizara iliratibu na kushiriki
katika Mkutano wa Dharura wa Pamoja wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Masuala
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya
uliofanyika kwa njia ya mtandao. Mkutano
huo ulitoa Azimio la mikakati ya pamoja ya kukabiliana na mlipuko
wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona na mipango ya kutatua changamoto zinazojitokeza kutokana
na hatua zinazochukuliwa na Nchi Wanachama katika kukabiliana na ugonjwa huo.
36.
Mheshimiwa Spika, baadhi
ya maazimio ya Mkutano huo ni: -
i. Kutekeleza agizo
la kukaa karantini kwa lazima kwa siku 14 kwa wasafiri wote wanaoingia katika
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
ii. Kuendesha
mikutano kwa njia ya mtandao hadi hapo hali ya maambukizi itakapodhibitiwa;
iii. Kuhakikisha
malori yanayobeba bidhaa yanakuwa na wafanyakazi wawili hadi watatu tu; na
iv. Kuwapima
wafanyakazi wa malori na endapo mmoja wao atapatikana na dalili za ugonjwa wa
COVID-19 watatengwa kwa muda wa siku 14 kulingana na miongozo ya kitaifa na
nchi husika na lori hilo litapuliziwa dawa kabla ya kuendelea na safari na
wafanyakazi wengine.
37.
Mheshimiwa Spika, kama
nilivyoeleza kwenye sehemu ya mafanikio ya Wizara, mwezi Novemba 2019, kwa mara
ya kwanza nchi yetu ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa
Nchi za Afrika na Nordic uliofanyika jijini Dar es Salaam. Mkutano huo
uliofanyika kwa mafanikio makubwa ulifunguliwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tofauti na mikutano
iliyopita ambayo ilijikita katika masuala ya misaada, mkutano huu ulijielekeza
zaidi katika ushirikiano na kuimarisha biashara, uwekezaji, uchumi wa viwanda,
mazingira na kukuza utalii pamoja na masuala ya amani na usalama.
38.
Mheshimiwa Spika, mwezi
Desemba 2019, nilimwakilisha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Nchi na
Serikali wa Nchi Wanachama wa Kundi la Afrika, Karibeani na Pasifiki (ACP)
ambayo sasa inafahamika kama Organisation of Africa, Caribbean and Pacific
States (OACPS) uliofanyika jijini Nairobi, Kenya. Katika Mkutano huo,
Tanzania ilifanikiwa kuzishawishi Nchi Wanachama pamoja na mambo mengine
kukubali kujumuisha zao la korosho kwenye orodha ya mazao ya kimkakati ndani ya
ACP ambayo yatanufaika na Programu ya Mnyororo wa Thamani wa ACP.
39.
Mheshimiwa Spika, taarifa
ya kina kuhusu kusimamia Utekelezaji
wa Sera ya Nchi ya Mambo ya Nje ni kama
inavyoonekana kwenye Aya ya 107 hadi 235
katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
Kufuatilia na Kusimamia Utekelezaji wa Mikataba iliyosainiwa
40.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha mwaka 2019/2020, Wizara iliratibu na kushiriki katika
majadiliano na kusimamia uwekwaji wa saini wa Mikataba na Hati za Makubaliano
na nchi mbalimbali. Mikataba na Hati hizo za Makubaliano zilizosainiwa
zinalenga kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na nchi marafiki
pamoja na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa. Mikataba na Hati za Makubaliano
zilizosainiwa ni kama inavyoonekana kwenye Aya
ya 236 hadi 237 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
Masuala ya Diplomasia, Itifaki, Uwakilishi na Huduma za Kikonseli
41.
Mheshimiwa Spika,
katika kuimarisha mahusiano ya Tanzania na nchi nyingine, Wizara imeendelea
kuandaa na kuratibu ziara mbalimbali za Viongozi Wakuu wa Kitaifa nje ya nchi.
Aidha, Wizara imeratibu na kufanikisha ziara za Viongozi wa Mataifa mbalimbali
na Mashirika ya Kimataifa waliokuja Tanzania kwa ziara rasmi, kushiriki katika
mikutano, makongamano na kutekeleza majukumu mbalimbali ya kitaifa. Taarifa zaidi
kuhusu masuala ya diplomasia, itifaki, uwakilishi na huduma za kikonseli inapatikana
kwenye Aya ya 242 hadi 245 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
Ushirikishwaji wa Watanzania wanaoishi ughaibuni
42. Mheshimiwa Spika,
Wizara imeendelea kuwashirikisha Watanzania wanaoishi ughaibuni (Diaspora) katika kuchangia maendeleo
ya nchi yao kama inavyoonekana kwenye Aya ya 246 hadi 251 katika kitabu
cha Hotuba ya Bajeti.
Utawala na Maendeleo ya Watumishi
43. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia masuala ya utawala na
maendeleo ya watumishi kwa lengo la kuimarisha utendaji wa kazi. Wizara ina
jumla ya watumishi 439 wa kada mbalimbali. Katika kuimarisha utendaji kazi wa
Wizara, masuala mbalimbali yanayohusu utawala na maendeleo ya watumishi
yameendelea kusimamiwa kama ifuatavyo: -
(a) Uteuzi wa Viongozi
44.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020 Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
alimteua Balozi Kanali Wilbert Augustin Ibuge kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Vilevile, Mheshimiwa Rais
aliwateua Mabalozi 17 ambapo 14 kati yao wanaiwakilisha Tanzania katika nchi
mbalimbali duniani na watatu wanafanya shughuli zao hapa nchini. Naomba kutumia
fursa hii kuwapongeza kwa uteuzi huo na kuwataka waendelee kuchapa kazi kwa
bidii, uzalendo na weledi mkubwa.
(b) Upandishaji Vyeo Watumishi Maafisa Mambo ya Nje
45.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020, watumishi 19
walipandishwa vyeo kwa mserereko. Kati ya watumishi hao, watano walipandishwa
kuwa Maafisa Mambo ya Nje Wakuu Daraja la I na
watumishi 14 walipandishwa kuwa Maafisa Mambo ya Nje Wakuu Daraja la II.
(c) Umiliki wa majengo
46.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kujenga na kukarabati majengo yake
ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Miaka kumi na tano (2017/2018-2031/2032) wa
ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Balozini. Kwa sasa Tanzania inamiliki majengo 106 pamoja na viwanja
12. Taarifa kamili kuhusu utawala na maendeleo ya watumishi inapatikana kwenye Aya
ya 255 hadi 260 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
Kuratibu na Kusimamia Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Wizara na Taasisi zilizo Chini ya Wizara
a) Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Wizara
47. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara
ilipangiwa bajeti ya maendeleo ya Shilingi
Bilioni Nne (4,000,000,000) kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali
ya maendeleo iliyopo ndani na nje ya nchi.
48. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2020,
Wizara imepokea kiasi cha Shilingi
milioni mia nne themanini na saba, laki tisa na elfu tano, mia tisa tisini na
sita (487,905,996) sawa na asilimia 12.2 ya fedha zilizoidhinishwa. Tayari ukarabati wa makazi
ya Balozi wa Tanzania Ottawa nchini Canada umeanza ambao utagharimu Shilingi milioni mia moja hamsini
(150,000,000). Vilevile, Shilingi milioni mia tatu thelathini na saba, laki tisa na elfu tano,
mia tisa tisini na sita (337,905,996) zinatumika katika ujenzi wa vyumba vya
madarasa unaoendelea kwenye Chuo cha Diplomasia.
b) Utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara
49.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi hiki, Wizara
imeendelea kuzisimamia taasisi zilizo chini yake ambazo ni Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC);
Chuo cha Diplomasia (CFR); na Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani
Afrika (APRM) kama ifuatavyo:
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC)
50. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2020, Kituo
kimekusanya mapato ya Shilingi bilioni
kumi na moja, milioni mia nane kumi na tano, laki tano, elfu kumi na sita, mia
tisa kumi na sita (11,815,516,916). Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni nne, milioni mia tisa themanini na sita, laki nane,
elfu themanini na tatu, na sabini na mbili (4,986,883,072) zimetokana na huduma za kumbi za mikutano
za AICC na JNICC; Shilingi bilioni tatu, milioni mia tano, kumi na nne,
laki tano, elfu sitini na sita, mia mbili thelathini na nane (3,514,566,238) zimetokana na upangishaji wa ofisi na
nyumba za kuishi; Shilingi bilioni tatu,
milioni mia tatu kumi na nne, elfu sitini na saba na mia sita na tatu (3,314,067,603) zimetokana na huduma za hospitali.
Vilevile katika kipindi cha 2019/2020, Kituo kilitoa Shilingi milioni mia mbili (200,000,000) kama gawio la awali kwa
Serikali. Maelezo zaidi yanapatikana kwenye Aya ya
264 hadi 268 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
Chuo cha Diplomasia (CFR)
51. Mheshimiwa Spika, Chuo cha Diplomasia kimeendelea kutoa
mafunzo na kufanya tafiti katika masuala ya diplomasia; uhusiano wa kimataifa;
stratejia na usuluhishi wa migogoro; na ujenzi wa amani. Lengo ni kukifanya
Chuo kuwa Taasisi iliyobobea katika elimu ya juu na ushauri katika nyanja hizo.
Hadi tarehe 30 Aprili 2020, Chuo kilipokea Shilingi
bilioni mbili, milioni mia sita arobaini na moja, laki sita arobaini na mbili
elfu, mia nne themanini na sita (2,641,642,486). Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni moja, milioni mia sita thelathini
na saba, na sabini na mbili elfu, mia nne na tisini (1,637,072,490) ni kwa
ajili ya mishahara, Shilingi milioni mia
sita sitini na sita, laki sita na sitini na nne elfu (666,664,000) kwa ajili ya Matumizi
Mengineyo na Shilingi milioni mia tatu
thelathini na saba, laki tisa na elfu tano na mia tisa tisini na sita (337,905,996)
ni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa. Aidha, Chuo kilikusanya
jumla ya Shilingi bilioni moja, milioni
mia tano na kumi, laki tano na elfu kumi na nne, mia sita hamsini (1,510,514,650)
sawa na asilimia 97 ya lengo la
mwaka la Shilingi bilioni moja, milioni
mia tano, arobaini na tano, na elfu moja na mia tano thelathini (1,545,001,530).
Taarifa zaidi zinapatikana kwenye Aya ya 269 hadi 275 katika kitabu cha
Hotuba ya Bajeti ya Wizara.
Mpango wa Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM)
52. Mheshimiwa
Spika,
katika kipindi cha 2019/2020, APRM Tanzania
imekamilisha rasimu ya Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa APRM inayohusu
maeneo ya Siasa na Demokrasia, Usimamizi wa Uchumi, Uendeshaji wa Kampuni za
Biashara na utoaji wa huduma za jamii ambayo itawasilishwa katika Mkutano wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika. Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge
kwa ajili ya shughuli za APRM - Tanzania kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ni Shilingi milioni mia tisa arobaini na nane,
kumi na mbili elfu, mia nane na sitini na sita (948,012,866). Fedha
zilizopokelewa ni Shilingi milioni mia
sita thelathini na nane, laki mbili na arobaini elfu (638,240,000) sawa na asilimia 67. Taarifa zaidi zipo kwenye
Aya ya 276 hadi 278 katika kitabu
cha Hotuba ya Bajeti.
9.0
SHUKRANI
53.
Mheshimiwa Spika, kwa
kuwa hii ni Hotuba yangu ya mwisho ya Bajeti katika Bunge la 11, kwa mara
nyingine tena, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru kwa dhati kabisa
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa imani yake kwangu kwa kuniteua kuwa Mbunge tarehe 16 Januari 2017
na tarehe 23 Machi 2017 kuniteua kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, nafasi ambayo
nilihudumu hadi tarehe 3 Machi 2019 nilipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kutokana na imani yake kwangu nimeweza
kushirikiana na viongozi na watumishi wa Wizara zote mbili nilizohudumu
kutekeleza yale yote ambayo viongozi wangu wakuu wameniagiza. Nichukue fursa
hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kunipa fursa adhimu ya kuitumikia nchi yangu
katika nafasi hii kubwa kabisa. Nashukuru kuwa nimeweza kutoa mchango wangu
katika maendeleo ya nchi yetu na katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi
ya Mwaka 2015 – 2020.
54.
Mheshimiwa Spika, aidha
napenda kumshukuru, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini na kunipa majukumu
mbalimbali ya sekta zingine kitaifa na kimataifa. Baadhi ya majukumu hayo ni
pamoja na: kusimamia mabadiliko ya sheria na muundo wa Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali ambayo yameleta ufanisi mkubwa katika utendaji wa ofisi hiyo;
kusimamia na kuratibu mabadiliko ya sheria za madini na rasilimali za nchi ili
kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinanufaisha Taifa; na kusimamia na kuongoza
majadiliano ya mikataba mbalimbali ambayo haikuwa na tija kwa Taifa.
55.
Mheshimiwa Spika, nitakuwa
mchoyo wa fadhila iwapo sitatoa shukrani zangu za kipekee kwa Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa miongozo yao ambayo ilikuwa ni nguzo muhimu kwenye utekelezaji
wa majukumu yangu. Nalishukuru pia Bunge lako Tukufu kwa ushirikiano mkubwa
niliopatiwa katika kulitumikia Taifa na kuchangia katika kufanikisha maendeleo
makubwa yaliyopatikana katika Serikali ya Awamu ya Tano.
56.
Mheshimiwa Spika,
naomba nitumie fursa hii kwa namna ya pekee kuwashukuru Mabalozi na Wawakilishi
wa Taasisi za Umoja wa Mataifa pamoja na Mashirika mengine ya Kimataifa hapa
nchini kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kupitia nchi na mashirika yao
kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu
ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
57. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano
imeendelea kupata mafanikio makubwa kutokana na mchango wa wadau na Washirika
wa Maendeleo kutoka nchi na asasi mbalimbali za kimataifa, kikanda na kitaifa.
Tunawashukuru sana. Orodha ya nchi na mashirika ya kimataifa na kikanda ni kama
ilivyoorodheshwa kwenye Aya ya 284 hadi 287 katika kitabu cha Hotuba
ya Bajeti.
58.
Mheshimiwa Spika, kwa
moyo mkunjufu, napenda kuwashukuru watendaji na watumishi wa Wizara na Taasisi
zake kwa kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu ipasavyo. Kwa namna ya pekee,
napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro (Mb), Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Balozi Kanali Wilbert Augustin
Ibuge, Katibu Mkuu; Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu; Mabalozi
wa Tanzania Nje ya Nchi; Wakuu wa Idara na Vitengo; Wakuu wa Taasisi zilizo
chini ya Wizara; na watumishi wengine wote kwa weledi, umahiri na ufanisi wao
katika kunisaidia kutekeleza majukumu yangu ya kulinda na kutetea maslahi ya
Taifa letu.
59.
Mheshimiwa Spika, kwa
nafasi ya kipekee kabisa, napenda kumshukuru mke wangu mpenzi Dkt. Amina M. M. Kabudi na
familia yangu kwa ujumla kwa
uvumilivu wao na kuwa karibu na mimi wakati wote wa kutekeleza majukumu yangu
niliyopewa na Mheshimiwa Rais ambayo wakati mwingine yalinilazimu kuwa
mbali nao kwa muda mrefu.
60.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2020/2021, pamoja na masuala mengine, Wizara imeweka kipaumbele
katika kutekeleza majukumu yafuatayo:
i.Kutekeleza
Diplomasia ya Uchumi kwa kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nje,
kuvutia watalii, kutafuta misaada na mikopo yenye masharti nafuu, kutafuta
fursa za mafunzo, kushiriki katika Jumuiya za Kikanda kwa lengo la kuongeza
ajira na masoko ya bidhaa za Tanzania nje;
ii. Kukamilisha
Sera ya Mambo ya Nje 2020, Sera hiyo itazingatia mabadiliko ya kisiasa,
kiuchumi na kijamii;
iii. Kuboresha
Kanzidata ya Diaspora itakayotoa taarifa itakayosaidia kuandaa mwongozo wa
namna ya kuwashirikisha Diaspora wa Tanzania kuchangia katika maendeleo ya nchi
yao;
iv.
Kuendelea
kutumia Balozi zetu kutafuta mitaji ya uwekezaji, masoko na kuhamasisha
Diaspora kuchangia kwenye maendeleo ya nchi kwa kutangaza vyema miradi ya kipaumbele
na vivutio vinavyotolewa na Serikali katika maeneo yao ya uwakilishi;
v.
Kuendelea
na utafutaji wa masoko mapya ya bidhaa za Tanzania nje kwa kuendelea
kuhamasisha Taasisi za Serikali zinazohusika na biashara kushirikiana na sekta
binafsi kushiriki katika maonesho mbalimbali ya Kimataifa ambayo yanatoa fursa
kwa nchi mbalimbali kutangaza bidhaa zake pamoja na kujifunza teknolojia na
mbinu za kisasa zitakazoboresha bidhaa zetu;
vi.
Kuendelea
kutekeleza Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki
zake;
vii.
Kuendelea
kuratibu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini kwa Afrika wa mwaka 2015 - 2020 na Mkakati wa Kuendeleza Viwanda wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika wa mwaka 2015 – 2030;
viii.
Kushiriki
katika juhudi za kuleta amani, usalama na kukuza demokrasia kwenye Jumuiya za
Kikanda ambazo nchi yetu ni mwanachama;
ix. Kuendelea
kutoa elimu kwa umma juu ya fursa zitokanazo na Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki na Jumuiya nyingine za Kikanda;
x.
Kuendelea
kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Wizara na
Taasisi zilizopo chini ya Wizara; na
xi.
Kuendelea
kusimamia rasilimali watu; rasilimali fedha na rasilimali vitu vya Wizara.
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC)
61.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, AICC inatarajia
kukusanya mapato ya Shilingi bilioni
kumi na sita, milioni mia saba na moja, laki tano, na hamsini na tisa elfu (16,701,559,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni kumi na sita, milioni moja, laki tano na hamsini na
tisa elfu (16,001,559,000) ni kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani ambapo
kituo cha Arusha kinatarajia kukusanya Shilingi bilioni kumi na mbili, laki saba na themanini
na tano na elfu tisa (12,785,009,000) na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
kinatarajia kukusanya Shilingi bilioni
tatu, milioni mia mbili na kumi na sita, laki tano na hamsini elfu (3,216,550,000).
Aidha, mapato ya Shilingi milioni mia
saba (700,000,000) yatatokana na mkopo kwa ajili ya mradi
wa upanuzi wa Hospitali ya AICC.
Chuo
cha Diplomasia (CFR)
62.
Mheshimiwa Spika, malengo ya Chuo kwa mwaka
wa fedha 2020/2021 yapo kwenye Aya ya 294 ya kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
Mpango
wa Kujitathmini Kiutawala Bora Afrika (APRM)
63.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021,
APRM inatarajia kutekeleza vipaumbele vitakavyolenga kuimarisha tathmini za
utawala bora kama vinavyoonekana kwenye Aya ya 291 ya kitabu cha Hotuba
ya Bajeti.
64. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2020/2021, Wizara inatarajia kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni mbili, milioni mia tano
hamsini, laki nane na sabini na tisa elfu (2,550,879,000) ikiwa ni maduhuli
ya Serikali yatakayopatikana kutokana na vyanzo vilivyopo Makao Makuu ya Wizara
na katika Balozi za Tanzania nje. Vyanzo hivyo vya mapato vinajumuisha pango la
nyumba za Serikali zilizopo nje ya nchi; kuthibitisha nyaraka; na mauzo ya
nyaraka za zabuni.
65.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
wa fedha wa 2020/2021, Wizara imepangiwa bajeti ya Shilingi bilioni mia moja tisini na tisa, milioni mia saba hamsini,
laki sita na themanini na nne elfu (199,750,684,000).
Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni mia
moja sabini na tisa, milioni mia saba hamsini, laki sita na themanini na nne elfu
(179,750,684,000) ni kwa
ajili ya Matumizi ya Kawaida zinazojumuisha Shilingi bilioni mia moja sitini na saba, milioni mia saba kumi na
saba, laki saba na ishirini na tatu elfu (167,717,723,000) kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni kumi na mbili, milioni thelathini
na mbili, laki tisa na sitini na moja elfu (12,032,961,000) kwa ajili ya
Mishahara; na Shilingi bilioni ishirini
(20,000,000,000) kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
66.
Mheshimiwa Spika, kati
ya fedha za bajeti ya Matumizi Mengineyo ya Wizara, Shilingi milioni mia nane (800,000,000) ni kwa ajili ya Mpango wa
Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM), Shilingi bilioni moja (1,000,000,000)
ni kwa ajili ya Chuo cha Diplomasia, Shilingi
bilioni moja, milioni mia mbili sabini na mbili (1,272,000,000) ni kwa
ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na Shilingi milioni mia moja sitini na nane, na laki mbili (168,200,000) ni
kwa ajili ya Bodi ya Ushauri wa Masuala ya Rushwa ya Umoja wa Afrika. Aidha,
kati ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya Mishahara, Shilingi bilioni mbili, milioni mia nne ishirini na saba na sitini na
nne elfu (2,427,064,000) ni kwa ajili ya Chuo cha Diplomasia.
67.
Mheshimiwa
Spika, katika fedha za bajeti ya
maendeleo, kiasi cha Shilingi bilioni
ishirini (20,000,000,000) kilichopangwa kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Shilingi bilioni moja na milioni mia nane
(1,800,000,000) ni kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya Balozi na
ofisi katika Ubalozi wa Tanzania Moroni, Comoro; Shilingi bilioni tatu, milioni mia sita tisini na nne, laki nne thelathini na tisa, mia sita hamsini na tano
(3,694,439,655) ni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makazi ya Balozi wa
Tanzania Muscat, Oman; Shilingi bilioni
moja na milioni mia tano (1,500,000,000) ni kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa
viwanja vya Serikali vilivyopo Kigali, Maputo, Bujumbura, Riyadh na Lilongwe; Shilingi bilioni tatu, milioni mia tisa arobaini
na nane, laki moja ishirini na mia tatu
arobaini na tano (3,948,120,345) ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi ya
Ubalozi na Kitega Uchumi katika Ubalozi wa Tanzania Nairobi, Kenya; Shilingi bilioni mbili, milioni mia mbili
na themanini (2,280,000,000) ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi na
kitega uchumi katika Ubalozi wa Tanzania Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo; Shilingi bilioni tatu,
milioni mia nane sitini na nne, laki nne na arobaini elfu (3,864,440,000) ni
kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya ofisi yaliyopo Ubalozi wa Tanzania
Washington D.C, Marekani; Shilingi
milioni mia mbili sabini na tano (275,000,000) ni kwa ajili ya ukarabati wa
majengo ya makazi ya Balozi na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania Harare,
Zimbabwe; Shilingi milioni mia mbili na
sitini (260,000,000) ni kwa ajili ya ukarabati wa makazi ya Balozi wa
Tanzania Kigali, Rwanda; na Shilingi
bilioni mbili, milioni mia tatu na sabini na nane, (2,378,000,000) ni kwa ajili ya ujenzi wa
madarasa ya Chuo cha Diplomasia.
68.
Mheshimiwa Spika, ili
kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2020/2021,
naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi bilioni mia moja tisini na tisa, milioni mia saba hamsini,
laki sita themanini na nne elfu (199,750,684,000). Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni mia moja sabini na tisa,
milioni mia saba hamsini, laki sita themanini na nne elfu (179,750,684,000) ni kwa ajili ya
Matumizi ya Kawaida na Shilingi bilioni
ishirini (20,000,000,000) ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.
69.
Mheshimiwa Spika, naomba
kuchukua nafasi hii adhimu kukushukuru tena wewe binafsi na Waheshimiwa Wabunge
kwa kunisikiliza.
70.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.