Wednesday, May 13, 2020

HOTUBA YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021


                                                     





HOTUBA YA MHESHIMIWA PROF. PALAMAGAMBA JOHN AIDAN MWALUKO KABUDI (MB), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

 

1.0         UTANGULIZI

1.    Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2019/2020. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha mpango na bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

2.    Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu rahim, mwingi wa rehema kwa kuniruzuku uhai na kunijalia afya njema ya kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

3.    Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inahitimisha ngwe yake ya kwanza ya miaka mitano mwaka huu, niruhusu kwa namna ya kipekee kabisa kumpongeza, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri ambao umeliletea Taifa hili maendeleo makubwa katika kipindi hiki cha uongozi wake. Aidha, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiongoza vyema nchi yetu na kutekeleza kwa mafanikio makubwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015 - 2020.


4.    Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa umahiri na uongozi wake madhubuti katika uendeshaji wa shughuli za Bunge. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb), Naibu Spika; Wenyeviti wa Bunge; na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi nzuri wanazozifanya kumsaidia Mheshimiwa Spika katika kusimamia na kuendesha shughuli za Bunge. Naomba Mwenyezi Mungu azidi kuwajaalia afya njema, busara na hekima katika kuongoza mhimili huu muhimu katika Taifa letu.
5.    Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda kuipongeza na kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya uongozi wa Mheshimiwa Salim Mwinyi Rehani (Mb), kwa kazi nzuri na ya kizalendo inayoifanya ya kuishauri Serikali hususan Wizara yangu. Aidha, napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Mussa Azan Zungu (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa kipindi kirefu. 
6.    Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa vifo vya Waheshimiwa Rashid Ajali Akbar, aliyekuwa Mbunge wa Newala; Askofu Dkt. Getrude Rwakatare (Mb); Richard Mganga Ndassa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumve; na Balozi Dkt. Augustine Phillip Mahiga (Mb), aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria na kabla ya hapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi Amina. 

7.    Mheshimiwa Spika, Hotuba yangu ni kama inavyoonekana katika Kitabu cha Hotuba ya Bajeti ya Wizara kilichowasilishwa kwako. Hivyo basi, nitasoma muhtasari wake na ninaomba Hotuba hiyo iingizwe yote kwenye kumbukumbu za Bunge lako Tukufu.

2.0           MAFANIKIO YA WIZARA KWA KIPINDI CHA SERIKALI YA AWAMU YA TANO


8.   Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii ni hotuba yangu ya mwisho nikiwa Waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano, ninayo heshima kuelezea kwa ufupi baadhi ya mafanikio makubwa ambayo Wizara inajivunia kuyaratibu kwa ufanisi mkubwa na kufanikisha utekelezaji wake kwa kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano, kama ifuatavyo:

a)   Ufunguzi wa Balozi mpya nane za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nchi za Qatar; Uturuki; Sudan; Cuba; Israel; Algeria; Jamhuri ya Korea; na Namibia. Kufunguliwa kwa Balozi hizo, kunaifanya Tanzania kuwa na jumla ya Balozi 43 na Konseli Kuu tatu katika miji ya Mombasa, Dubai na Jeddah. Kadhalika, Balozi za Ethiopia na Poland zilifunguliwa hapa nchini katika kipindi hicho na kuifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa Balozi 62 na Mashirika ya Kimataifa 30;

b)    Tumefanya jitihada kubwa katika kuifanya lugha ya Kiswahili kutumika katika Jumuiya ya Kimataifa na nchi mbalimbali. Juhudi hizo za Tanzania zimefanya Kiswahili kitumike katika eneo la Maziwa Makuu, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki na vyombo mbalimbali vya habari vya Kimataifa.
c)    Kufanikisha kufanyika kwa viwango vya juu Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Dar es Salaam mwezi Agosti 2019 ambapo Tanzania ilikabidhiwa rasmi Uenyekiti wa Jumuiya hiyo utakaodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi Agosti 2020.
Katika uenyekiti wetu wa SADC, tumepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Maonesho ya Awamu ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo yalifanyika mwezi Agosti 2019. Maonesho hayo yalishirikisha wajasiriamali wapatao 5,352 kutoka ndani na nje ya nchi, Taasisi za umma, viwanda mbalimbali, Taasisi za huduma za fedha na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO).
d)    Wizara imefanikiwa kuhamasisha watalii kuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii. Kwa mfano, kuanzia mwaka 2015 hadi 2018, watalii 5,234,448 wametembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini. Watalii hao walitoka nchi mbalimbali zilizopo Bara la Afrika; Ulaya; Amerika ya Kaskazini; Asia; Mashariki ya Kati; Australasia na nchi za Karibeani;
e)     Kufanikisha uenyekiti wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo mwezi Machi 2016 nchi yetu iliteuliwa kwa mara ya pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo. Katika kipindi cha uenyekiti wake, Tanzania ilifanikisha utekelezaji wa masuala mbalimbali ikiwemo:
                                   i.  Kuweka mifumo bora ya matumizi ya rasilimali za          Jumuiya;
                                  ii. Kuimarisha miundombinu yenye sura ya Kikanda;
                                iii. Kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara kwa Nchi Wanachama;
                         iv.       Kuratibu utumiaji wa Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Ofisi zote za Umma nchini; na
                              v.          Matumizi ya Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Taasisi zote za Serikali.
 f)      Kuratibu Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic (Africa - Nordic Foreign Ministers’ Meeting) uliofanyika kwa mafanikio makubwa mwezi Novemba 2019 jijini Dar es Salaam. Ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001. Tofauti na mikutano iliyopita ambayo ilijikita katika masuala ya misaada, mkutano huu ulijielekeza zaidi katika ushirikiano na kuimarisha biashara, uwekezaji, uchumi wa viwanda, mazingira na kukuza utalii pamoja na masuala ya amani na usalama;
g)     Kufanikisha ujumuishwaji wa miradi ya Tanzania katika miradi ya kipaumbele ya miundombinu iliyoidhinishwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
h)       Katika kipindi cha mwaka 2015 – 2019, Tanzania ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Forodha na Itifaki ya Soko la Pamoja za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama vile:-
                               i.   Kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kiforodha 15 kati ya vikwazo 24 vilivyoripotiwa dhidi ya Tanzania; 
                                    ii.      Kutoa vyeti 32,536 vya uasili wa bidhaa kwa wafanyabiashara wa Tanzania wanaofanya biashara katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
                  iii.         Kutoa vibali vya kuingia nchini 1,117,056 kwa raia wa Nchi Wanachama wa Jumuiya na wananchi wetu 851,470 walipata vibali vya kuingia katika nchi nyingine za Jumuiya;
                      iv.           Kufanikisha Watanzania 1,555 kupata vibali vya kufanya kazi katika nchi nyingine wanachama wa Jumuiya na Tanzania ilitoa vibali 2,309 vya kufanya kazi nchini kwa raia wengine wa Nchi Wanachama wa Jumuiya;
                 v.           Kutoa vibali vipatavyo 879 kwa wanafunzi wa nchi nyingine wanachama wa Jumuiya kuingia na kusoma nchini na wanafunzi watanzania 3,129 walipata vibali vya kusoma katika nchi wanachama wa Jumuiya; na
                     vi.    Kutoa vibali vya ukaazi 3,128 kwa raia wengine wa Nchi Wanachama wa Jumuiya na Watanzania 1,002 walipata vibali vya ukaazi katika Nchi Wanachama wa Jumuiya.
i)       Kuratibu upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato jijini Dodoma na upatikanaji wa mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 180 kutoka Benki hiyo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya pete katika jiji la Dodoma; na

j)          Kushawishi nchi marafiki kutufutia madeni, kuyapunguza au kuweka masharti nafuu ya kuyalipa. Kutokana na ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Iran mwezi Oktoba 2017, Serikali ya nchi hiyo iliridhia na kutangaza kusamehe riba ya deni lililokopwa mwaka 1984 ambayo ilifikia kiasi cha Dola za Marekani Milioni 150. Vilevile, mwezi Septemba 2017, Serikali ya Brazil ilitoa msamaha wenye  thamani ya Dola za Marekani Milioni 203.6 ambayo ni asilimia 86 ya deni lote tunalodaiwa na nchi hiyo. 

9.            Mheshimiwa Spika, hayo ni baadhi tu ya mafanikio niliyoyataja hapa. Taarifa nzima kuhusu mafanikio ya Wizara katika kipindi cha Awamu ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano inapatikana kwenye Aya ya 14, Kipengele cha kwanza hadi ishirini katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

3.0         MISINGI YA TANZANIA KATIKA MAHUSIANO YA KIMATAIFA


10.    Mheshimiwa Spika, historia ya Tanzania imesheheni misingi na misimamo imara inayoifanya iendelee kuwa miongoni mwa nchi zilizo na ushawishi mkubwa kikanda na kimataifa tangu Uhuru. Misingi ya nchi yetu kuheshimika kimataifa iliwekwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kulaani ubabe, uonevu na ukandamizaji popote pale ulipotokea duniani na alipigania uhuru wa Afrika na kusisitiza mshikamano kati ya nchi zinazoendelea. Kupitia misingi hii ambayo viongozi wetu wameendelea kuienzi, Tanzania imeendelea kuheshimika sana kikanda na kimataifa.
11.   Mheshimiwa Spika, katika kusimamia misingi hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kulinda uhuru wa nchi, haki yetu ya kujiamulia mambo yetu wenyewe bila kuingiliwa, mipaka ya nchi yetu; kuimarisha ujirani mwema; na kutekeleza Sera ya Kutofungamana na Upande Wowote kama dira na msimamo wetu kwenye mahusiano na nchi nyingine za Jumuiya ya Kimataifa. 

4.0       TATHMINI YA HALI YA DUNIA KWA MWAKA 2019/2020


12.  Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020 hali ya uchumi na siasa duniani ilionesha kuendelea kuimarika na kutoa matumaini ya kuimarika zaidi kwa kipindi cha miaka michache ijayo, licha ya kuwepo changamoto za kiulinzi na kiusalama kwa baadhi ya maeneo. Hata hivyo, mlipuko wa maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19) unaashiria tishio kubwa la kuporomoka kwa uchumi wa dunia.

13.   Mheshimiwa Spika, taarifa zaidi kuhusu tathmini ya hali ya uchumi, siasa, ulinzi na usalama ya dunia inapatikana kwenye Aya ya 18 hadi 69 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.


 5.0         NAFASI YA TANZANIA KIMATAIFA NA KIKANDA

14.    Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kulipa umuhimu mkubwa suala la amani na usalama duniani ambalo ni miongoni mwa tunu za Taifa letu tangu kupata uhuru. Ili kuenzi tunu hizi na kutambua umuhimu wa kulinda na kudumisha amani na usalama duniani, nchi yetu imeendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika ulinzi wa amani duniani. Katika kutekeleza hilo, hadi kufikia mwezi Januari 2020, nchi yetu imepeleka walinda amani kwenye misheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa zilizopo katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Darfur - Sudan, Sudan Kusini na Jimbo la Abyei.
15.    Mheshimiwa Spika, tutaendelea kushirikiana na mataifa mengine kushughulikia masuala ya amani na usalama katika Bara letu la Afrika. Nitumie fursa hii kuisihi Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuunga mkono jitahada za kudumisha amani duniani. Maelezo ya kina kuhusu nafasi ya Tanzania Kimataifa na Kikanda yanapatikana kwenye Aya ya 70 hadi 81 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

6.0  KUJENGA NA KULINDA TASWIRA YA NCHI KIMATAIFA


16.   Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuheshimu, wajibu wake Kikatiba na Mikataba ya Kimataifa ya kulinda na kudumisha haki zote za binadamu ikiwemo za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, zote zikiwa na umuhimu ulio sawa kwa ustawi na maendeleo ya Watanzania.
17.   Mheshimiwa Spika, Tanzania ikiwa Nchi Mwanachama wa Umoja wa Mataifa imeendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za Umoja wa Mataifa, Taasisi na Mashirika yake na pia katika mikutano, mijadala na shughuli mbalimbali za Umoja huo. Miongoni mwa mijadala hiyo ilifanyika kwenye Kikao cha 74 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba, 2019 jijini New York, Marekani ambapo nilimwakilisha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kikao hicho nilitoa hotuba iliyoelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kwenye sekta za afya; elimu; maji; usafiri wa anga; nishati na ujenzi.

18.    Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali kuufahamisha ulimwengu namna inavyotetea na kusimamia haki za binadamu hapa nchini, mwezi Februari 2020 jijini Geneva, Uswisi niliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Kikao cha 43 cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu. Kwenye Kikao hicho nilieleza kuhusu mafanikio ya Serikali katika kulinda na kusimamia haki za elimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama, umeme na maendeleo ya kiuchumi. Aidha, nilielezea mafanikio yaliyopatikana katika kuongeza uwajibikaji kwa watumishi na viongozi wa umma; kupambana na vitendo vya rushwa; vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya; kuongezeka kwa kiwango cha ukusanyaji kodi; na kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ili kuwahudumia wananchi wetu ipasavyo.
19.   Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu kujenga na kulinda taswira ya nchi kimataifa yanapatikana kwenye Aya ya 82 hadi 90 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

7.0      WATANZANIA KWENYE NAFASI ZA KIMATAIFA


20.   Mheshimiwa Spika, baadhi ya Watanzania wamechaguliwa na kuteuliwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi kikanda na kimataifa kama inavyoonekana kwenye Aya ya 91 hadi 98 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

21.    Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba nitoe taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa kipindi cha mwaka 2019/2020 na mpango wa bajeti kwa mwaka 2020/2021.

8.0     MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA MWAKA 2019/2020


22.    Mheshimiwa Spika, katika kuiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa mwaka 2019/2020, Bunge lako Tukufu liliidhinisha kiasi cha Shilingi bilioni mia moja sitini na sita, milioni mia tisa ishirini na sita, laki nane na ishirini elfu (166,926,820,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni mia moja sitini na mbili, milioni mia tisa ishirini na sita, laki nane na ishirini elfu (162,926,820,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi bilioni nne (4,000,000,000) ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Katika fedha zilizotengwa kwa Matumizi ya Kawaida, Shilingi bilioni mia moja hamsini na mbili, milioni mia saba kumi na saba, laki saba na ishirini na tatu elfu (152,717,723,000) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na  Shilingi bilioni kumi, milioni mia mbili na tisa na tisini na saba elfu (10,209,097,000) ni kwa ajili ya Mishahara.

23.   Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2020 Wizara ilikuwa imepokea kiasi cha Shilingi bilioni mia moja thelathini na tatu, milioni mia tatu, laki tisa, mia sita sabini na moja (133,300,900,671). Kiasi hicho cha fedha ni sawa na asilimia 79.8 ya fedha zote za bajeti zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2019/2020. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni mia moja ishirini na nne, milioni mia moja themanini na sita, laki mbili thelathini na sita, mia sita sabini na tano (124,186,236,675) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni nane, milioni mia sita ishirini na sita, laki saba na hamsini na nane elfu (8,626,758,000) ni kwa ajili ya mishahara. Aidha, katika kipindi hicho Wizara imepokea fedha za bajeti ya miradi ya maendeleo kiasi cha Shilingi milioni mia nne themanini na saba, laki tisa na elfu tano, mia tisa tisini na sita (487,905,996) kwa ajili ya miradi ya ukarabati wa nyumba ya makazi ya Balozi wa Tanzania Ottawa na ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Chuo cha Diplomasia.

24.   Mheshimiwa Spika, katika fedha zilizotolewa, Wizara imetumia kiasi cha Shilingi  bilioni tisini na tisa, milioni mia tatu ishirini na nne, laki mbili, ishirini na mbili elfu, mia saba themanini na sita (99,324,222,786). Kiasi hicho cha fedha ni sawa na asilimia 75 ya fedha zilizopokelewa. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni tisini na moja, milioni mia tatu tisini, elfu sabini na tisa, mia sita arobaini na saba (91,390,079,647) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni saba, milioni mia tano tisini na sita, laki  mbili thelathini na saba, mia moja arobaini na mbili (7,596,237,142) ni kwa ajili ya mishahara. Aidha, Wizara imetumia kiasi cha Shilingi milioni mia tatu thelathini na saba, laki tisa na elfu tano, mia tisa tisini na sita (337,905,996) kwa ajili ya mradi wa maendeleo wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Chuo cha Diplomasia.


25.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara ilipanga kukusanya Shilingi bilioni mbili, milioni mia tano hamsini, laki nane sabini na tisa na sabini na mbili (2,550,879,072). Kati ya kiasi hicho Shilingi milioni sitini na saba, laki tisa na themanini elfu (67,980,000) ni  maduhuli ya Makao Makuu ya Wizara na Shilingi bilioni mbili, milioni mia nne themanini na mbili, laki nane, elfu tisini na tisa na sabini na mbili (2,482,899,072) ni maduhuli kutoka Balozi za Tanzania nje ya nchi. Vyanzo vya mapato hayo ni pamoja na uhakiki wa nyaraka, pango la majengo ya Serikali nje ya nchi na mauzo ya nyaraka za zabuni.

26.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2019 hadi tarehe 30 Aprili, 2020 Wizara imekusanya jumla ya Shilingi bilioni tano, milioni mia mbili hamsini na tatu, elfu tisini na moja na mia sita hamsini (5,253,091,650) sawa na asilimia 206 ya lengo lililopangwa kwa mwaka 2019/2020. Ongezeko la maduhuli limetokana na baadhi ya balozi kuendelea kukusanya maduhuli ya viza kupitia utaratibu wa kawaida kabla ya kuanza kwa utaratibu wa kielekroniki (e-visa). Aidha, kuanzia mwezi Novemba 2019, Wizara inaendelea kukusanya maduhuli ya visa kwa njia ya kielektroniki baada ya Balozi zetu kufungiwa mtandao huo.

27.    Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2019/2020, naomba sasa nitumie fursa hii kueleza kwa kifupi mapitio ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika kipindi hicho.

Kubuni na Kusimamia Utekelezaji wa Sera ya Nchi ya Mambo ya Nje


28.    Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye sehemu ya mafanikio ya Wizara kwa kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano kuwa Tanzania ni mwenyekiti na mwenyeji wa mikutano ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti 2019 hadi Agosti 2020. Tangu mwezi Agosti, 2019 tulipopewa uenyekiti tumeratibu, kuandaa na kuongoza mikutano sita ya kisekta kama inavyoonekana kwenye Aya ya 200 hadi 207 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
 29.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Wizara imeratibu kwa mafanikio makubwa na kufanikisha kufanyika kwa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika tarehe 18 Machi 2020. Mkutano huo ulifanyika kwa mara ya kwanza kwa njia ya mtandao ikiwa ni tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona.

30.   Mheshimiwa Spika, kutokana na mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 duniani, ni dhahiri kwamba ili kukabiliana nao kunahitajika ufanisi na ushirikiano wa hali ya juu katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa. Kufuatia hali hiyo, kwa mara nyingine tena naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa SADC pamoja na Dkt. Stergomena Lawrence Tax, Katibu Mtendaji wa SADC kwa maelekezo na ushauri wanaoendelea kuutoa kwa Nchi Wanachama ili kuhakikisha kwamba ukanda wetu hauathiriki sana na janga hili la COVID-19.
31.   Mheshimiwa Spika, katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu zifuatazo ni hatua mbalimbali ambazo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikisha katika SADC. Hatua hizo ni kufanyika kwa Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Afya wa SADC kuhusu COVID -19 tarehe 9 Machi 2020 chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Mkutano huu ulifanyika kwa njia ya mtandao ikiwa ni hatua mojawapo ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo. Mkutano huo pamoja na mambo mengine, ulipendekeza kuundwa kwa Kamati ya  Wataalam kwa ajili ya kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Itifaki ya Afya ya SADC kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19).

32.   Mheshimiwa Spika, mapendekezo hayo ya Mawaziri wa Afya, yaliridhiwa na Baraza la Mawaziri wa SADC katika mkutano uliofanyika tarehe 18 Machi, 2020. Aidha, tarehe 31 Machi 2020, Kamati ya Wataalam ilifanya kikao kwa njia ya mtandao na kwa kushirikiana na Sekretarieti ya SADC ilipendekeza kuandaliwa kwa mkutano huu wa Dharura wa Baraza la Mawaziri. Aidha, Kamati hiyo pia iliridhia mapendekezo 11 katika maeneo yafuatayo:
             i.      Ufuatiliaji na utekelezaji wa Itifaki ya Afya kuhusu magonjwa ya mlipuko;
                 ii.        Kujiandaa na kukabiliana na COVID-19;
             iii.        Kubaini wagonjwa, kufuatilia waliokutana na mgonjwa na huduma za tiba;
                 iv.        Uzuiaji na udhibiti wa maambukizi;
                  v.        Uchunguzi na upimaji wa kimaabara;
                  vi.        Uelimishaji wa madhara na ushirikishwaji wa jamii;
                 vii.        Hatua stahiki za Afya ya Jamii;
               viii.        Uratibu wa Kikanda wa kukabiliana na COVID-19;
                  ix.        Uwezeshaji na usafirishaji wa bidhaa muhimu miongoni mwa nchi za SADC wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19;
                   x.        Masuala ya uwezeshaji wa biashara katika ukanda kwa kipindi cha ugonjwa wa COVID-19; na
                  xi.        Usimamizi wa majanga hatarishi katika ukanda wa SADC.

33.   Mheshimiwa Spika, tarehe 6 Aprili 2020 niliongoza Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri uliofanyika kwa njia ya mtandao. Mkutano huo ulipokea taarifa ya Kamati ya Wataalam ya kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Itifaki ya Afya ya SADC kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19. Aidha, Mkutano uliidhinisha mwongozo wa urazinishaji (harmonisation) na uwezeshaji wa usafirishaji wa bidhaa muhimu na huduma katika nchi za SADC katika kipindi hiki cha janga la COVID -19.

34.   Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa SADC ameendelea kuzisisitiza Taasisi za Fedha za Kimataifa na Washirika wengine wa Maendeleo kuzifutia madeni nchi za SADC, ili ziweze kutumia fedha hizo katika kukabiliana na janga hili la COVID-19.


35.   Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mwezi Machi 2020 Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Dharura wa Pamoja wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya uliofanyika kwa njia ya mtandao. Mkutano huo ulitoa Azimio la mikakati ya pamoja ya kukabiliana na mlipuko wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona na mipango ya kutatua changamoto zinazojitokeza kutokana na hatua zinazochukuliwa na Nchi Wanachama katika kukabiliana na ugonjwa huo.

36.   Mheshimiwa Spika, baadhi ya maazimio ya Mkutano huo ni: -
       i.   Kutekeleza agizo la kukaa karantini kwa lazima kwa siku 14 kwa wasafiri wote wanaoingia katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;

       ii.     Kuendesha mikutano kwa njia ya mtandao hadi hapo hali ya maambukizi itakapodhibitiwa;

     iii.     Kuhakikisha malori yanayobeba bidhaa yanakuwa na wafanyakazi wawili hadi watatu tu; na

     iv.     Kuwapima wafanyakazi wa malori na endapo mmoja wao atapatikana na dalili za ugonjwa wa COVID-19 watatengwa kwa muda wa siku 14 kulingana na miongozo ya kitaifa na nchi husika na lori hilo litapuliziwa dawa kabla ya kuendelea na safari na wafanyakazi wengine.

37.    Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye sehemu ya mafanikio ya Wizara, mwezi Novemba 2019, kwa mara ya kwanza nchi yetu ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic uliofanyika jijini Dar es Salaam. Mkutano huo uliofanyika kwa mafanikio makubwa ulifunguliwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tofauti na mikutano iliyopita ambayo ilijikita katika masuala ya misaada, mkutano huu ulijielekeza zaidi katika ushirikiano na kuimarisha biashara, uwekezaji, uchumi wa viwanda, mazingira na kukuza utalii pamoja na masuala ya amani na usalama.

38.    Mheshimiwa Spika, mwezi Desemba 2019, nilimwakilisha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Kundi la Afrika, Karibeani na Pasifiki (ACP) ambayo sasa inafahamika kama Organisation of Africa, Caribbean and Pacific States (OACPS) uliofanyika jijini Nairobi, Kenya. Katika Mkutano huo, Tanzania ilifanikiwa kuzishawishi Nchi Wanachama pamoja na mambo mengine kukubali kujumuisha zao la korosho kwenye orodha ya mazao ya kimkakati ndani ya ACP ambayo yatanufaika na Programu ya Mnyororo wa Thamani wa ACP.

39.   Mheshimiwa Spika, taarifa ya kina kuhusu kusimamia Utekelezaji wa Sera ya Nchi ya Mambo ya Nje ni kama inavyoonekana kwenye Aya ya 107 hadi 235 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

Kufuatilia na Kusimamia Utekelezaji wa Mikataba iliyosainiwa


40.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020, Wizara iliratibu na kushiriki katika majadiliano na kusimamia uwekwaji wa saini wa Mikataba na Hati za Makubaliano na nchi mbalimbali. Mikataba na Hati hizo za Makubaliano zilizosainiwa zinalenga kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na nchi marafiki pamoja na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa. Mikataba na Hati za Makubaliano zilizosainiwa ni kama inavyoonekana kwenye Aya ya 236 hadi 237 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

 

Masuala ya Diplomasia, Itifaki, Uwakilishi na Huduma za Kikonseli


41.    Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mahusiano ya Tanzania na nchi nyingine, Wizara imeendelea kuandaa na kuratibu ziara mbalimbali za Viongozi Wakuu wa Kitaifa nje ya nchi. Aidha, Wizara imeratibu na kufanikisha ziara za Viongozi wa Mataifa mbalimbali na Mashirika ya Kimataifa waliokuja Tanzania kwa ziara rasmi, kushiriki katika mikutano, makongamano na kutekeleza majukumu mbalimbali ya kitaifa. Taarifa zaidi kuhusu masuala ya diplomasia, itifaki, uwakilishi na huduma za kikonseli inapatikana kwenye Aya ya 242 hadi 245 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

Ushirikishwaji wa Watanzania wanaoishi ughaibuni


42.    Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwashirikisha Watanzania wanaoishi ughaibuni (Diaspora) katika kuchangia maendeleo ya nchi yao kama inavyoonekana kwenye Aya ya 246 hadi 251 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

Utawala na Maendeleo ya Watumishi


43.    Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia masuala ya utawala na maendeleo ya watumishi kwa lengo la kuimarisha utendaji wa kazi. Wizara ina jumla ya watumishi 439 wa kada mbalimbali. Katika kuimarisha utendaji kazi wa Wizara, masuala mbalimbali yanayohusu utawala na maendeleo ya watumishi yameendelea kusimamiwa kama ifuatavyo: -

(a)         Uteuzi wa Viongozi


44.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua Balozi Kanali Wilbert Augustin Ibuge kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Vilevile, Mheshimiwa Rais aliwateua Mabalozi 17 ambapo 14 kati yao wanaiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani na watatu wanafanya shughuli zao hapa nchini. Naomba kutumia fursa hii kuwapongeza kwa uteuzi huo na kuwataka waendelee kuchapa kazi kwa bidii, uzalendo na weledi mkubwa.

(b)         Upandishaji Vyeo Watumishi Maafisa Mambo ya Nje


45.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020, watumishi 19 walipandishwa vyeo kwa mserereko. Kati ya watumishi hao, watano walipandishwa kuwa Maafisa Mambo ya Nje Wakuu Daraja la I na watumishi 14 walipandishwa kuwa Maafisa Mambo ya Nje Wakuu Daraja la II.  

(c)          Umiliki wa majengo


46.    Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kujenga na kukarabati majengo yake ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Miaka kumi na tano (2017/2018-2031/2032) wa ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Balozini. Kwa sasa Tanzania inamiliki majengo 106 pamoja na viwanja 12. Taarifa kamili kuhusu utawala na maendeleo ya watumishi inapatikana kwenye Aya ya 255 hadi 260 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

Kuratibu na Kusimamia Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Wizara na Taasisi zilizo Chini ya Wizara


a)           Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Wizara


47.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara ilipangiwa bajeti ya maendeleo ya Shilingi Bilioni Nne (4,000,000,000) kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo ndani na nje ya nchi.
48.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2020, Wizara imepokea kiasi cha Shilingi milioni mia nne themanini na saba, laki tisa na elfu tano, mia tisa tisini na sita (487,905,996) sawa na asilimia 12.2 ya fedha zilizoidhinishwa. Tayari ukarabati wa makazi ya Balozi wa Tanzania Ottawa nchini Canada umeanza ambao utagharimu Shilingi milioni mia moja hamsini (150,000,000). Vilevile, Shilingi milioni mia tatu thelathini na saba, laki tisa na elfu tano, mia tisa tisini na sita (337,905,996) zinatumika katika ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea kwenye Chuo cha Diplomasia.

b)            Utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara


49.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki, Wizara imeendelea kuzisimamia taasisi zilizo chini yake ambazo ni Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC); Chuo cha Diplomasia (CFR); na Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika (APRM) kama ifuatavyo:

Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC)


50.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2020, Kituo kimekusanya mapato ya Shilingi bilioni kumi na moja, milioni mia nane kumi na tano, laki tano, elfu kumi na sita, mia tisa kumi na sita (11,815,516,916). Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni nne, milioni mia tisa themanini na sita, laki nane, elfu themanini na tatu, na sabini na mbili (4,986,883,072) zimetokana na huduma za kumbi za mikutano za AICC na JNICC; Shilingi  bilioni tatu, milioni mia tano, kumi na nne, laki tano, elfu sitini na sita, mia mbili thelathini na nane (3,514,566,238) zimetokana na upangishaji wa ofisi na nyumba za kuishi; Shilingi bilioni tatu, milioni mia tatu kumi na nne, elfu sitini na saba na mia sita na tatu (3,314,067,603) zimetokana na huduma za hospitali. Vilevile katika kipindi cha 2019/2020, Kituo kilitoa Shilingi milioni mia mbili (200,000,000) kama gawio la awali kwa Serikali. Maelezo zaidi yanapatikana kwenye Aya ya 264 hadi 268 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

 Chuo cha Diplomasia (CFR)

51.     Mheshimiwa Spika, Chuo cha Diplomasia kimeendelea kutoa mafunzo na kufanya tafiti katika masuala ya diplomasia; uhusiano wa kimataifa; stratejia na usuluhishi wa migogoro; na ujenzi wa amani. Lengo ni kukifanya Chuo kuwa Taasisi iliyobobea katika elimu ya juu na ushauri katika nyanja hizo. Hadi tarehe 30 Aprili 2020, Chuo kilipokea Shilingi bilioni mbili, milioni mia sita arobaini na moja, laki sita arobaini na mbili elfu, mia nne themanini na sita (2,641,642,486). Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni moja, milioni mia sita thelathini na saba, na sabini na mbili elfu, mia nne na tisini (1,637,072,490) ni kwa ajili ya mishahara, Shilingi milioni mia sita sitini na sita, laki sita na sitini na nne elfu  (666,664,000) kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi milioni mia tatu thelathini na saba, laki tisa na elfu tano na mia tisa tisini na sita (337,905,996) ni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa. Aidha, Chuo kilikusanya jumla ya Shilingi bilioni moja, milioni mia tano na kumi, laki tano na elfu kumi na nne, mia sita hamsini (1,510,514,650) sawa na asilimia 97 ya lengo la mwaka la Shilingi bilioni moja, milioni mia tano, arobaini na tano, na elfu moja na mia tano thelathini (1,545,001,530). Taarifa zaidi zinapatikana kwenye Aya ya 269 hadi 275 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti ya Wizara.

Mpango wa Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM)


52.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2019/2020, APRM Tanzania imekamilisha rasimu ya Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa APRM inayohusu maeneo ya Siasa na Demokrasia, Usimamizi wa Uchumi, Uendeshaji wa Kampuni za Biashara na utoaji wa huduma za jamii ambayo itawasilishwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika. Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya shughuli za APRM - Tanzania kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ni Shilingi milioni mia tisa arobaini na nane, kumi na mbili elfu, mia nane na sitini na sita (948,012,866). Fedha zilizopokelewa ni Shilingi milioni mia sita thelathini na nane, laki mbili na arobaini elfu (638,240,000) sawa na asilimia 67. Taarifa zaidi zipo kwenye Aya ya 276 hadi 278 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

 

9.0     SHUKRANI

53.    Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii ni Hotuba yangu ya mwisho ya Bajeti katika Bunge la 11, kwa mara nyingine tena, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru kwa dhati kabisa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kwangu kwa kuniteua kuwa Mbunge tarehe 16 Januari 2017 na tarehe 23 Machi 2017 kuniteua kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, nafasi ambayo nilihudumu hadi tarehe 3 Machi 2019 nilipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kutokana na imani yake kwangu nimeweza kushirikiana na viongozi na watumishi wa Wizara zote mbili nilizohudumu kutekeleza yale yote ambayo viongozi wangu wakuu wameniagiza. Nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kunipa fursa adhimu ya kuitumikia nchi yangu katika nafasi hii kubwa kabisa. Nashukuru kuwa nimeweza kutoa mchango wangu katika maendeleo ya nchi yetu na katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020.

54.   Mheshimiwa Spika, aidha napenda kumshukuru, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini na kunipa majukumu mbalimbali ya sekta zingine kitaifa na kimataifa. Baadhi ya majukumu hayo ni pamoja na: kusimamia mabadiliko ya sheria na muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo yameleta ufanisi mkubwa katika utendaji wa ofisi hiyo; kusimamia na kuratibu mabadiliko ya sheria za madini na rasilimali za nchi ili kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinanufaisha Taifa; na kusimamia na kuongoza majadiliano ya mikataba mbalimbali ambayo haikuwa na tija kwa Taifa.
55.   Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila iwapo sitatoa shukrani zangu za kipekee kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miongozo yao ambayo ilikuwa ni nguzo muhimu kwenye utekelezaji wa majukumu yangu. Nalishukuru pia Bunge lako Tukufu kwa ushirikiano mkubwa niliopatiwa katika kulitumikia Taifa na kuchangia katika kufanikisha maendeleo makubwa yaliyopatikana katika Serikali ya Awamu ya Tano.

56.    Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kwa namna ya pekee kuwashukuru Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa pamoja na Mashirika mengine ya Kimataifa hapa nchini kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kupitia nchi na mashirika yao kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

57.    Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kupata mafanikio makubwa kutokana na mchango wa wadau na Washirika wa Maendeleo kutoka nchi na asasi mbalimbali za kimataifa, kikanda na kitaifa. Tunawashukuru sana. Orodha ya nchi na mashirika ya kimataifa na kikanda ni kama ilivyoorodheshwa kwenye Aya ya 284 hadi 287 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

58.    Mheshimiwa Spika, kwa moyo mkunjufu, napenda kuwashukuru watendaji na watumishi wa Wizara na Taasisi zake kwa kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu ipasavyo. Kwa namna ya pekee, napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Balozi Kanali Wilbert Augustin Ibuge, Katibu Mkuu; Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu; Mabalozi wa Tanzania Nje ya Nchi; Wakuu wa Idara na Vitengo; Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara; na watumishi wengine wote kwa weledi, umahiri na ufanisi wao katika kunisaidia kutekeleza majukumu yangu ya kulinda na kutetea maslahi ya Taifa letu.

59.    Mheshimiwa Spika, kwa nafasi ya kipekee kabisa, napenda kumshukuru mke wangu mpenzi Dkt. Amina M. M. Kabudi na familia yangu kwa ujumla kwa uvumilivu wao na kuwa karibu na mimi wakati wote wa kutekeleza majukumu yangu niliyopewa na Mheshimiwa Rais ambayo wakati mwingine yalinilazimu kuwa mbali nao kwa muda mrefu.


60.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, pamoja na masuala mengine, Wizara imeweka kipaumbele katika kutekeleza majukumu yafuatayo:
          i.Kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nje, kuvutia watalii, kutafuta misaada na mikopo yenye masharti nafuu, kutafuta fursa za mafunzo, kushiriki katika Jumuiya za Kikanda kwa lengo la kuongeza ajira na masoko ya bidhaa za Tanzania nje;
          ii.  Kukamilisha Sera ya Mambo ya Nje 2020, Sera hiyo itazingatia mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii;
           iii.  Kuboresha Kanzidata ya Diaspora itakayotoa taarifa itakayosaidia kuandaa mwongozo wa namna ya kuwashirikisha Diaspora wa Tanzania kuchangia katika maendeleo ya nchi yao;

          iv.          Kuendelea kutumia Balozi zetu kutafuta mitaji ya uwekezaji, masoko na kuhamasisha Diaspora kuchangia kwenye maendeleo ya nchi kwa kutangaza vyema miradi ya kipaumbele na vivutio vinavyotolewa na Serikali katika maeneo yao ya uwakilishi;
           v.          Kuendelea na utafutaji wa masoko mapya ya bidhaa za Tanzania nje kwa kuendelea kuhamasisha Taasisi za Serikali zinazohusika na biashara kushirikiana na sekta binafsi kushiriki katika maonesho mbalimbali ya Kimataifa ambayo yanatoa fursa kwa nchi mbalimbali kutangaza bidhaa zake pamoja na kujifunza teknolojia na mbinu za kisasa zitakazoboresha bidhaa zetu;
          vi.          Kuendelea kutekeleza Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake;
         vii.          Kuendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini kwa Afrika wa mwaka 2015 - 2020 na Mkakati wa Kuendeleza Viwanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika wa mwaka 2015 – 2030;
       viii.         Kushiriki katika juhudi za kuleta amani, usalama na kukuza demokrasia kwenye Jumuiya za Kikanda ambazo nchi yetu ni mwanachama;
     ix. Kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya fursa zitokanazo na Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya nyingine za Kikanda;
    x.    Kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Wizara na Taasisi zilizopo chini ya Wizara; na

                xi.     Kuendelea kusimamia rasilimali watu; rasilimali fedha na rasilimali vitu vya Wizara.



Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC)

61.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, AICC inatarajia kukusanya mapato ya Shilingi bilioni kumi na sita, milioni mia saba na moja, laki tano, na hamsini na tisa elfu (16,701,559,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni kumi na sita, milioni moja, laki tano na hamsini na tisa elfu (16,001,559,000) ni kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani ambapo kituo cha Arusha kinatarajia kukusanya Shilingi  bilioni kumi na mbili, laki saba na themanini na tano na elfu tisa (12,785,009,000) na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kinatarajia kukusanya Shilingi bilioni tatu, milioni mia mbili na kumi na sita, laki tano na hamsini elfu (3,216,550,000). Aidha, mapato ya Shilingi milioni mia saba (700,000,000) yatatokana na mkopo kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa Hospitali ya AICC.

Chuo cha Diplomasia (CFR)

62.    Mheshimiwa Spika, malengo ya Chuo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 yapo kwenye Aya ya 294 ya kitabu cha Hotuba ya Bajeti.


Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Afrika (APRM)

63.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021, APRM inatarajia kutekeleza vipaumbele vitakavyolenga kuimarisha tathmini za utawala bora kama vinavyoonekana kwenye Aya ya 291 ya kitabu cha Hotuba ya Bajeti.


64.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Wizara inatarajia kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni mbili, milioni mia tano hamsini, laki nane na sabini na tisa elfu (2,550,879,000) ikiwa ni maduhuli ya Serikali yatakayopatikana kutokana na vyanzo vilivyopo Makao Makuu ya Wizara na katika Balozi za Tanzania nje. Vyanzo hivyo vya mapato vinajumuisha pango la nyumba za Serikali zilizopo nje ya nchi; kuthibitisha nyaraka; na mauzo ya nyaraka za zabuni.

65.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021, Wizara imepangiwa bajeti ya Shilingi bilioni mia moja tisini na tisa, milioni mia saba hamsini, laki sita na themanini na nne elfu (199,750,684,000). Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni mia moja sabini na tisa, milioni mia saba hamsini, laki sita na themanini na nne elfu (179,750,684,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida zinazojumuisha Shilingi bilioni mia moja sitini na saba, milioni mia saba kumi na saba, laki saba na ishirini na tatu elfu (167,717,723,000) kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni kumi na mbili, milioni thelathini na mbili, laki tisa na sitini na moja elfu (12,032,961,000) kwa ajili ya Mishahara; na Shilingi bilioni ishirini (20,000,000,000) kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

66.    Mheshimiwa Spika, kati ya fedha za bajeti ya Matumizi Mengineyo ya Wizara, Shilingi milioni mia nane (800,000,000) ni kwa ajili ya Mpango wa Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM), Shilingi bilioni moja (1,000,000,000) ni kwa ajili ya Chuo cha Diplomasia, Shilingi bilioni moja, milioni mia mbili sabini na mbili (1,272,000,000) ni kwa ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na Shilingi milioni mia moja sitini na nane, na laki mbili (168,200,000) ni kwa ajili ya Bodi ya Ushauri wa Masuala ya Rushwa ya Umoja wa Afrika. Aidha, kati ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya Mishahara, Shilingi bilioni mbili, milioni mia nne ishirini na saba na sitini na nne elfu (2,427,064,000) ni kwa ajili ya Chuo cha Diplomasia.

67.   Mheshimiwa Spika, katika fedha za bajeti ya maendeleo, kiasi cha Shilingi bilioni ishirini (20,000,000,000) kilichopangwa kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Shilingi bilioni moja na milioni mia nane (1,800,000,000) ni kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya Balozi na ofisi katika Ubalozi wa Tanzania Moroni, Comoro; Shilingi bilioni tatu, milioni mia sita tisini na nne, laki nne  thelathini na tisa, mia sita hamsini na tano (3,694,439,655) ni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makazi ya Balozi wa Tanzania Muscat, Oman; Shilingi bilioni moja na milioni mia tano (1,500,000,000) ni kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa viwanja vya Serikali vilivyopo Kigali, Maputo, Bujumbura, Riyadh na Lilongwe; Shilingi bilioni tatu, milioni mia tisa arobaini na nane,  laki moja ishirini na mia tatu arobaini na tano (3,948,120,345) ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Ubalozi na Kitega Uchumi katika Ubalozi wa Tanzania Nairobi, Kenya; Shilingi bilioni mbili, milioni mia mbili na themanini (2,280,000,000) ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi na kitega uchumi katika Ubalozi wa Tanzania Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Shilingi bilioni tatu, milioni mia nane sitini na nne, laki nne na arobaini elfu (3,864,440,000) ni kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya ofisi yaliyopo Ubalozi wa Tanzania Washington D.C, Marekani; Shilingi milioni mia mbili sabini na tano (275,000,000) ni kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya makazi ya Balozi na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania Harare, Zimbabwe; Shilingi milioni mia mbili na sitini (260,000,000) ni kwa ajili ya ukarabati wa makazi ya Balozi wa Tanzania Kigali, Rwanda; na Shilingi bilioni mbili, milioni mia tatu na sabini na nane,  (2,378,000,000) ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya Chuo cha Diplomasia. 


68.    Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2020/2021, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi bilioni mia moja tisini na tisa, milioni mia saba hamsini, laki sita themanini na nne elfu (199,750,684,000). Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni mia moja sabini na tisa, milioni mia saba hamsini, laki sita themanini na nne elfu (179,750,684,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi bilioni ishirini (20,000,000,000) ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.

69.    Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii adhimu kukushukuru tena wewe binafsi na Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza.

70.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.