Tuesday, May 19, 2020

WAZIRI KABUDI AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA UMOJA WA ULAYA NCHINI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M Kabudi akielezea jambo wakati wa mazungumzo yaliyofanyika  kwa njia ya Video na Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Mhe. Manfred Fanti.
Waziri kabudi katika mazungumzo hayo amemweleza Balozi Fanti, kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19). Vilevile amemwelezea mafanikio yaliyopatikana kutokana na hatua hizo zilizochukuliwa na Serikali katika kupambana na COVID-19, ikiwa ni sambamba na kupungua kwa wagonjwa wenye maambukizi katika vituo maalumu vilivyotengwa ili kuwahudumia wagonjwa hao.
 
Mhe.Prof. Kabudi pia amesisitiza suala la kufutiwa au kupewa msamaha wa madeni kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, kutoka na athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la COVID-19.
 Waziri Prof. Kabudi amemweleza Balozi Fanti, kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kushirikiana na kujadiliana na wadau wote 
kutoka pande zote za Dunia katika kuongeza nguvu na mbinu za kukabiliana na maambukizi ya COVID-19.

Balozi Fanti kwa upande wake ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua iliyozichukua na inayoendelea kuzichukua katika kukabiliana na kuenea kwa COVID-19. Ameeleza kuwa Umoja wa Ulaya upo tayari na daima utashirikiana na Tanzania katika masula mbalimbali ikiwemo hili la sasa la COVID-19.

Aidha, Balozi Fanti ameunga mkono suala la Serikali kwa kuto kuweka katazo la kukaa ndani (lockdown) akihusisha na mtindo wa maisha wa Watanzania.  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M Kabudi akimsikiliza Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfred Fanti wakati wa mazungumzo waliyoyafanya kwa njia ya Video. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M Kabudi  akisisitiza jambo wakati alipokuwa akifanya mazungumzo kwa njia ya video na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfred Fanti

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.