Tuesday, September 29, 2020

SERIKALI YAONGEZA KASI UTEKELEZAJI WA AHADI ZA MHESHIMIWA RAIS MAGUFULI KWA WANANCHI WA KIGOMA






Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert A. Ibuge akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna wa Polisi Thobias Andeng'enye alipowasili katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kujitambulisha kabla hajaanza ziara ya ukaguzi wa miradi ya miundombinu inayoratibiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert A. Ibuge akisalimiana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Rashidi Kassim alipowasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya kujitambulisha, kabla hajaanza ziara ya kukagua miradi ya miundombinu inayoratibiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna wa Polisi Thobias Andeng'enye akiwa katika kikao cha kupeana taarifa kuhusu mkoa huo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert A. Ibuge


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert A. Ibuge akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Kanali Michael Ngayalina kwenye Mpaka wa Tanzania na Burundi, Eneo la Manyovu ambapo kutajengwa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP). 
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert A. Ibuge akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Kanali Michael Ngayalina pamoja na ujumbe wao wakikagua Eneo litakalojengwa kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani mwa Tanzania na Burundi katika miji ya Manyovu/Mugina.

Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Kanali Michael Ngayalina akimuonesha jiwe linalotenganisha Mpaka wa Tanzania na Burundi lililopo kwenye Mji wa Manyovu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert A. Ibuge.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert A. Ibuge akimsikiliza Mshauri Mwelekezi wa ujenzi wa mradi wa Barabara kutoka Kasulu hadi Kibondo ambao unajengwa na Mkandarasi kutoka China kwa fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Mipango na Miundombinu, Mhandisi Steven Mlote (Kulia) akiwasikiliza wakandarasi kutoka China wanaojenga barabara inayounganisha Tanzania na Burundi kutoka Kasulu hadi Kibondo.

Bi. Edna Chuku akibadilishana mawzo na Mhandisi wa TANROADS wa Mkoa wa Kigoma walipokuwa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert A. Ibuge akiwa katika mazungumzo na Mkuu wa Kambi ya Wakimbizi ya Nduta iliyopo mkoani Kigoma. Sehemu ya Kambi hiyo itapitiwa na barabara inayounganisha Tanzania na Burundi.

 












Wednesday, September 23, 2020

SERIKALI YAELEZA SABABU ZA VYOMBO VYA HABARI VYA KIMATAIFA KUSAJILIWA

Serikali imefafanua hatua yake ya kuvitaka vyombo vya habari vya Kimataifa vinavyotaka kuvitumia vyombo vya habari vya Tanzania kurusha matangazo yake yana lengo la kutambua vyombo hivyo vinashirikiana vyombo gani vya hapa nchini na sio kuvizuia kutangaza na kuendesha vipindi vyake hapa nchini kama inavyoripotiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi mteule wa Uingereza hapa nchini Dkt. David Concar na kufafanua kuwa mpaka sasa vyombo vyote vya habari vya Kimataifa zimekwishatekeleza matakwa hayo ya kisheria na kupata leseni ya kutangaza na kuendesha vipindi vyao.

"Leo nimekutana na Balozi mteule wa Uingereza hapa nchini Dkt. David Concar na kumueleza lengo la kusajili vyombo vya Habari vya kimataifa lilikuwa ni kutaka kujua ni chombo gani cha kimataifa kinashirikiana na chombo gana hapa nchini lakini pia ilikuwa ni matakwa ya kisheria,"  Amesema Prof. Kabudi 

Kuhusu suala la mabadiliko ya sheria za asasi za kiraia (NGOs) na vyama vya siasa Prof. kabudi amefafanua kuwa lengo lake lilikuwa ni kuongeza uwazi na uwajibikaji katika fedha zinazoingia kwa asasi hizo pamoja na matumizi yake na kuwa linaendana na sheria na taratibu za kimataifa za kuzuia utakatishaji wa fedha na kuhakikisha makundi yenye nia ovu na misimamo mikali inayokwenda kinyume na tunu za demokrasia hayatumii njia hizo kupenyeza fedha zao.

Balozi mteule wa Uingereza  Dkt. David Concar amesema mazungumzo yao mbali na kulenga masuala ya kidiplomasia na maendeleo pia yalilenga kuangalia namna ya kuondoa malalamiko kutoka kwa baadhi ya NGOs na vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni uminywaji wa haki ya uhuru wa vyombo vya habari.  

Katika tukio jingine pia Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Prof. Palamagamba John Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Denmark hapa nchini Balozi Mette Norgaard ambapo mbali na suala la uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 28 hapa nchini,wamejadili pia masuala yanayohusu mashirikiano katika sekta za elimu, afya, biashara na uwekezaji.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi akimkabidhi Balozi mteule wa Uingereza nchini, Dkt. David Concar nakala za sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi akimuonesha Balozi mteule wa Uingereza hapa nchini, Dkt. David Concar namna magazeti yanavyo ripoti habari za uchaguzi mkuu bila upendeleo  


Balozi wa Denmark nchini Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimuelezea jambo Balozi wa Denmark nchini Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet akimueleza jambo wakati walipokutana kwa mazungumzo jijini Dar es Salaam




Monday, September 21, 2020

TANZANIA IMETAJWA KAMA NCHI YA KIELELEZO CHA AMANI NA DEMOKRASIA KATIKA BARA LA AFRIKA

Norway yaitaja Tanzania kama kielelezo cha amani na demokrasia katika chaguzi Barani Afrika kutokana na mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu unavyofanyika kwa amani,utulivu na usawa kwa wagombea wa vyama vyote huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kusikiliza sera za wagombea.

Balozi wa Norway nchini Tanzania Balozi Elisabeth Jacobsen ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi na kuongeza kuwa maandalizi ya uchaguzi mkuu yamefanyika kwa kufuata taratibu za kisheria huku tume ya Taifa ya Uchaguzi ikishughulikia baadhi ya malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya vyama vya siasa na wadau mbalimbali jambo ambalo linaifanya Tanzania kuwa kinara wa demokrasia katika mchakato mzima wa uchaguzi. 

Pamoja na masuala ya kisiasa Balozi huyo amesema katika mazungumzo yao wamegusia pia masuala ya ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi hususani katika suala la elimu,afya,nishati na uwekezaji pamoja na biashara baina ya nchi hizo mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amemuomba Balozi huyo wa Norway kuendelea kushirikiana na Tanzania na kumshukuru kwa Nchi hiyo kukubali kutoa kiasi cha dola za marekani milioni 7 kwa ajili ya mradi wa TASAF jambo litakalosaidia kupunguza umasikini kwa watanzania hususani katika kipindi hiki ambapo nchi nyingi zimeathiriwa na janga la Corona. 

Mbali na Balozi huyo wa Norway pia Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden hapa nchini Balozi Anders Sjöberg ambapo amezungumzia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi,haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari na kuvipongeza vyombo vya habari hapa nchini kwa kuandika habari za wagombea wa vyama vyote bila ya ubaguzi na ameonesha kufurahishwa kwake na mwitikio wa wananchi katika mikutano ya kampeni na kuomba maamuzi ya wananchi katika sanduku la kura yaheshimiwe.

Kuhusu suala la haki za binadamu prof. Kabudi amesema taswira inayotolewa kuhusu suala hilo haiakisi hali halisi iliyopo nchini na kwamba Tanzania inaheshimu na kulinda misingi ya haki za binadamu kiasi cha suala hilo kuingizwa katika ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi ili kikiingia madarakani kitekeleze na kulinda misingi hiyo. 

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Uswis hapa Nchini Mhe. Didier Chassot.


Balozi wa Sweden nchini Mhe. Anders Sjöberg akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati alipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi akimuonesha Balozi Sweden nchini, Mhe. Anders Sjöberg moja ya vipengele vilivyopo kwenye sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi akimuonesha Balozi Norway nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen moja ya kipengele cha sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi wakati alipokuwa akimkabidhi nakala ya nyaraka hizo



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi akikagua nakala za hati za utambulisho za Balozi mteule wa Uswisi hapa nchini Mhe. Didier Chassot 



Friday, September 18, 2020

TANZANIA YAKABIDHIWA HATI MILIKI YA ARDHI NA SERIKALI YA INDIA

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akiweka saini hati miliki ya ardhi ya jengo la Ubalozi, jijini New Delhi tarehe 17 Septemba 2020.

Naibu Afisa Mkuu wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Miji ya India, Bw. Satish Kumar Singh akimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda hati miliki ya ardhi ya jengo la Ubalozi, jijini New Delhi tarehe 17 Septemba 2020.

Picha ya jengo la Ubalozi wa Tanzania Jijini New Delhi, India.
=========================================

TANZANIA YAKABIDHIWA HATI MILIKI YA ARDHI MJINI NEW DELHI.

Ubalozi wa Tanzania nchini India umekabidhiwa rasmi na Serikali ya India Hati Miliki ya Ardhi yenye ukubwa wa eneo la mita za mraba 2120.60 ambapo ndipo lilipo jengo la Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini New Delhi.

Akipokea hati hizo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Miji ya India tarehe 17 Septemba 2020, Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Baraka H. Luvanda ameishukuru Serikali ya India kwa hatua hiyo ambayo inathibitisha uhusiano mzuri uliojengeka kati ya nchi hizi mbili.

Kwa upande wake, Naibu Afisa Mkuu wa Ardhi wa Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Miji ya India, Bw. Satish Kumar Singh amesifu uhusiano mzuri wa kihistoria uliopo kati ya India na Tanzania na kueleza kuwa, hiyo ndiyo sababu India imeona fahari kubwa kuipa Tanzania umiliki wa eneo katika sehemu mahsusi ya Jumuiya ya Kidiplomasia (Diplomatic Enclave).

Ni sera na mkakati wa Serikali ya Tanzania ya kuhakikisha kuwa, Balozi zote zilizopo katika maeneo ya kimkakati zinakuwa na majengo na nyumba za watumishi ili kuipunguzia Serikali gharama kubwa za kupanga majengo na nyumba hizo. Katika hafla hiyo Balozi Luvanda aliambatana na maofisa ubalozi, Bibi Natihaika Msuya na Dkt. Kheri Goloka.

 

Wednesday, September 16, 2020

MAADHIMISHO YA TISA YA SIKU YA MARA YAFIKIA TAMATI WILAYANI BUTIAMA

Maadhimisho ya Tisa (9) ya Siku ya Mara (Mara Day) yaliyofanyika katika uwanja wa Maria Nyerere uliopo wilayani Butiama  Mkoa wa Mara yamehitimishwa tarehe 15 Septemba, 2020. Maadhimisho haya hufanyika kila mwaka, kwa mzunguko kati ya Tanzania na Kenya kwa lengo la kuhamasisha utunzaji na Ikolojia ya Bonde la Mto Mara kwa jamii inayolizunguka bonde hilo. Madhimisho ya Mwaka huu  yameongozwa na kauli mbiu "Ikolojia ya Mara iliyotunzwa - Ustawi wetu"

Kwa kutambua umuhimu na changamoto za Ikolojia ya Bonde la Mto Mara, Baraza la Kisekta la 10 la Mawaziri wa Bonde la Ziwa Victoria, lililofanyika Kigali, Rwanda mnamo Mei 4, 2012, liliazimia na kutangaza kuwa kila tarehe 15 Septemba kuwa "Siku ya Mara", kwa kuzingatia pia katika msimu huo kuna uhamaji mkubwa wa wanyamapori kutoka Hifadhi ya Serengeti ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda Pori la Akiba la Kitaifa la Maasai-Mara katika Jamhuri ya Kenya.

Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na nchi hizi mbili Tanzania na Kenya maadhimisho ya 9 ya Mto Mara ya mwaka huu , yalipaswa kufanyika nchini Kenya, lakini kutokana na  changamoto ya Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) pande zote mbili zimekubaliana kufanya maadhimisho ya siku hiyo nchini mwao. 

Madhimisho ya mwaka huu yalienda sambamba na shughuli mbalimbali kama vile, semina ya masuala ya udongo na kilimo kwa wakazi wa mkoa wa Mara waliohudhuria katika uwanja wa Maria Nyerere, Butiama, maonesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiliamali, maonesho ya mashamba darasa na kazi za sanaa na ubunifu. 

Akizungumza katika sherehe za maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima ambaye pia alikuwa  mgeni mashuhuri katika sehehe hizo amesema serikali inatambua umuhimu wa Bonde la Mto Mara katika Ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa jamii ya pande zote mbili (Tanzania na Kenya) zinazolizunguka Bonde hilo. Sambamba na hilo Mhe. Malima amewahimiza wananchi kuendelea kutunza Ikolojia ya Bonde la Mto Mara kwa kufuata taratibu zilizowekwa na kushauriwa na Wataamu katika kundesha shughuli zao za kila siku kwenye mzingira yanayozunguka Bonde hilo.

Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Judith Ngoda akizungumza na wananchi kwenye sherehe za madadhimisho hayo amepongeza utayari    na ushiriki wa hali ya juu wa wananchi katika kulitunza Bonde la Mto Mara na kuongeza kuwa juhudi, nguvu na umoja unaoonyeshwa na Serikali za nchi zote mbili za Tanzania na Kenya unadhihirisha ushirikiano na mshikamano uliopo katika kuhakikisha ustawi wa uchumi kwa jamii inayozunguka Bonde la Mto Mara unakuwa endelevu kupitia mazingira. 

Sherehe za Siku ya Mara zinaongozwa na malengo matatu yafuatayo: kujenga uelewa kwa wadau muhimu kuhusu umuhimu wa Bonde la Mto Mara na rasilimali zake; kutambua na kuhusisha mchango wa watendaji mbalimbali wa umma na binafsi katika usimamizi wa Rasilimali za Mto Mara, na kukuza ushirikiano wa umma na binafsi kama njia ya kuelekea katika usimamizi endelevu wa Maji ya Mto Mara na bionuwai.

   Moja Banda la Wadau walioshiriki katika maonesho ya Maadhimisho ya Tisa (9) ya Siku ya Mara yaliofanyika katika viwanja vya Maria Nyerere, wilayani Butiama Mkoa wa Mara tarehe 12 -15 Septemba, 2020. 

    Baadhi ya Wananchi wa kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Mara wakisikiliza mada kwenye moja ya Semina iliyokuwa ikitolewa kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mara yaliofanyika katika viwanja vya Maria Nyerere, Wilayani Butiama Mkoa wa Mara tarehe 12 -15 Septemba, 2020. 

Sehemu ya wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Maria Nyerere, wilayani Butiama kwenye sherehe za maadhimisho ya 9 ya Siku ya Mara wakifuatilia burudani iliyokuwa ikiendelea uwanjani hapo. 

    Sehemu ya wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Maria                                                                                            Nyerere, wilayani Butiama kwenye sherehe za maadhimisho ya    9 ya Siku ya Mara wakifuatilia hotubani iliyokuwa ikitolea   uwanjani hapo. 

    Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima na Mgeni Rasmi                 wa sherehe za maadhimisho ya 9 ya Siku ya Mara akiongea na moja kati ya wadau walioshiriki katika maonesho yaliyofanyika katika viwanja vya Maria Nyerere, wilayani Butiama Mkoa wa Mara 


    Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima na Mgeni Rasmi                                 
wa sherehe za maadhimisho ya 9 ya Siku ya Mara akisaini kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Maria Nyerere, wilayani Butiama, Mkoa wa Mara                                                                              

   Wawakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Mgeta Sabe na Bi. Judith Ngoda wakifuatulia jambo wakati wa sherehe za maadhimisho ya 9 ya Siku ya Mara 

Bi. Judith Ngoda mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  akitoa salam za Wizara kwa  Viongozi na Wananchi waliojitokeza kwenye Sherehe za Maadhimisho ya 9 ya Siku ya Mara.

Tuesday, September 15, 2020

NCHI 15 ZARUHUSIWA KULETA WAANGALIZI WA UCHAGUZI MKUU 2020

 Nchi 15 kupitia Balozi zao hapa nchini zimeruhusiwa kuleta waangalizi wa Kimataifa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Octoba, 2020 baada ya Balozi hizo kuwasilisha maombi na kufuata taratibu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya Balozi Manfred Fanti na kuongeza kuwa uchaguzi wa mwaka huu kwa mara ya kwanza umekuwa tofauti na miaka iliyopita kwa kuwa unafanyika kwa kugharamiwa na fedha za ndani badala ya wahisani jambo ambalo baadhi ya watu walianza kuhofia kutokuwepo kwa waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi.

"Huu ni uchaguzi mkuu ambao kwa mara ya kwanza kwa asilimia 100 tunaugharamia sisi wenyewe kama Serikali ya Tanzania, utaratibu wa uchaguzi chini ya sheria ya uchaguzi na chini ya utaratibu wa Kimataifa huwa tunakuwa na waangalizi wa uchaguzi na mwaka huu nchi hizo 15 kupitia balozi zao zimepata  kibali mara baada ya kufuata taratibu za kuomba kuleta waangalizi wa uchaguzi mkuu," Amesema Prof. Kabudi 

Mbali na Balozi wa Umoja wa Ulaya pia Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia hapa nchini Balozi Roberto Mengoni na baadae Balozi wa Poland Balozi Krzysztof Buzalski ambapo amewakabidhi vitabu vya sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi na miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya uchaguzi ili kuwapa fursa ya kufahamu namna uchaguzi unavyoendeshwa hapa nchini hasusani baada ya uwepo wa malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani juu ya kuenguliwa kwa wagombea wao. 

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Balozi Manfred Fanti amesema Nchi za Umoja huo zimekuwa zikifuatilia kwa karibu mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu zinavyoendelea hapa nchini ambapo mpaka sasa wanaridhishwa na kampeni zinavyofanyika kwa uhuru na amani na sasa wanajiandaa na zoezi la uangalizi wa uchaguzi huo. 

Balozi wa Italia hapa nchini Mhe. Roberto Mengoni amesema amevutiwa na namna vyombo vya habari vimekuwa vikitoa nafasi kwa wagombea wote kwa uhuru na bila ya ubaguzi na kupongeza namna Watanzania wanavyojitokeza kwa wingi kusikiliza sera za wagombea mbali na tishio la corona na kwamba ana imani kuwa Kiongozi atakayechaguliwa atakuwa ametokana na utashi wa wananchi.

Mbali na masuala ya uchaguzi mkuu, Waziri Kabudi na Mabalozi hao wamejadili pia masuala ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia,maendeleo ya kiuchumi,biashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu,afya,maji na miundombinu.

Balozi wa Umoja wa Ulaya Balozi Manfred Fanti akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.   Kabudi akimkabidhi Balozi wa Italia nchini Balozi Roberto Mengoni vitabu vya sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi na miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya uchaguzi      


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akimfafanulia jambo Balozi wa Poland hapa nchini, Balozi Krzysztof 




 

Monday, September 14, 2020

UMOJA WA ULAYA KUTOA BILIONI 70 KUSAIDIA MAPAMBANO YA COVID 19 -TANZANIA

 



Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya Mhe. Jestas Abuok Nyamanga pichani kulia akisisitiza vipaumbele vya Tanzania na zile za nchi za OACPS kwa Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Mhe. Charles Michel kushoto. Kulia mwa Balozi ni afisa Mwandamizi wa ubalozi Dkt Geofrey Kabakaki na Kushoto mwa Rais Michel ni Afisa wa EU anayeshughulikia masuala ya Tanzania kutoka makao makuu ya Umoja huo Bibi Christina Barrios.


Mhe. Balozi Jestas Nyamanga kuliaa akiwasilisha hati za utambulisho kwa Mkuu wa Itifaki wa Ofisi ya Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya


Thursday, September 10, 2020

Nchi za Ulaya Zahimizwa Kuondoa Vizuizi vya Kusafiri

Jumuiya ya nchi za Afrika, Carribean na Pacific (OACPS) imetoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuondoa vizuizi vya kusafiri (travel bans) kwa baadhi ya nchi za OACPS hususan zile zilizoonesha kuwa salama zaidi dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Corona kama Tanzania. Wito huo ulitolewa katika kikao maalum cha mashauriano baina ya Jumuiya ya nchi za OACPS na nchi ya Ujerumani ambayo kwa sasa ni Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya.

Mashauriano hayo yaliyofanyika tarehe 9 Septemba 2020 katika Ofisi za Jumuiya ya OACPS, Brussels nchini Ubelgiji, yaliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mabalozi wa nchi za OACPS walioko Brussels, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga na ujumbe wa Ujerumani uliongozwa na Waziri wa Masuala ya Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani, Dkt. Gerd MÙLLER.

Katika kikao hicho wajumbe walisisitiza umuhimu wa Umoja wa Ulaya kuendelea kuunga mkono Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kusimamia ithibati za tafiti za chanjo za ugonjwa wa Corona na Shirika hilo kuendelea kujengewa uwezo wa kusimamia utaratibu wa kuhakikisha kuwa chanjo itakayothibitika inawafikia mataifa yote kwa usawa na kwa gharama nafuu.

Kikao hicho kilijadili pia hatua mbalimbali zinazopaswa kuongeza msukumo kwa Umoja wa Ulaya katika kuzisaidia nchi za OACPS kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na ugonjwa wa Corona hususan katika sekta ya utalii na kilimo. Mikakati iliyojadiliwa ni pamoja na ile inayolenga kupunguza, kufuta au kubadilisha masharti ya ulipaji wa madeni ya nchi za Jumuiya ya OACPS na wito wa nchi za OACPS kuutaka Umoja wa Ulaya kusogeza mbele utekelezaji wa baadhi ya kanuni na taratibu mpya za biashara zilizopangwa kuanza kutumika mwanzoni mwa mwaka ujao ili kuzipa nafasi nchi za OACPS kujipanga zaidi kabla ya kuanza kutumia kanuni hizo.

Kupitia mashauriano hayo, pande zote mbili zilitathmini mwenendo wa majadiliano ya Mkataba mpya wa ubia wa Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya nchi za Jumuiya ya OACPS na Umoja wa Ulaya yanayoendelea hivi sasa baada ya mkataba wa sasa kufikia kikomo mwezi Desemba 2020. Pande mbili zilijadili kwa kina namna ya kushirikiana katika maeneo yanayolenga kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo, uwiano ulio sawa katika biashara na maendeleo ya teknolojia katika kukuza uchumi na maendeleo ya watu.

Kikao kilihitimishwa kwa Ujerumani kuonesha utayari wa kuyapa kipaumbele masuala yote yaliyojadiliwa katika kipindi cha uongozi wake wa Baraza la Umoja wa Ulaya na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kipindi hiki ambacho inashika nafasi ya Rais wa Baraza la Mawaziri wa nchi 79 wanachama wa Jumuiya ya nchi za Afrika, Carribean na Pacific itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya na kufanya kazi kwa karibu na uongozi wa Ujerumani kwenye Baraza la Umoja huo wa Ulaya kusukuma ajenda zenye manufaa na maslahi kwa pande zote mbili. 

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Nyamanga akiongoza Mkutano maalum wa mashauriano  kati ya Jumuiya ya nchi za Afrika, Carribean na Pacific (OACPS) na ujumbe waUjerumani uliokuwa ukingozwa na Waziri wa Masuala ya Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani, Dkt. Gerd MÙLLER ambayo kwa sasa nchi hiyo ni Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya

 Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Nyamanga akiongoza Mkutano maalum wa mashauriano  kati ya Jumuiya ya nchi za Afrika, Carribean na Pacific (OACPS) na ujumbe wa Ujerumani uliokuwa ukingozwa na Waziri wa Masuala ya Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani, Dkt. Gerd MÙLLER ambayo kwa sasa nchi hiyo ni Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya.



Mhe.Balozi Nyamanga kwa nafasi yake ya Mwenyeki wa Mabalozi wa OACPS akimtambulisha Waziri wa Ushirikiano wa Ujerumani Mhe. Dkt. Muller na timu yake katika Ukumbi wa OACPS.


Mhe. Balozi Nyamanga akimsindikiza Mgeni wake Mhe. Dkt.Muller nje ya ukumbi wa mkutano baada ya mkutano wa mashauriano kukamilika.

 




 

Tuesday, September 8, 2020

MAREKANI YAWATAKA WATANZANIA KUSHIRIKI UCHAGUZI, KUMCHAGUA KIONGOZI BORA

 Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald Wright amewataka Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Octoba mwaka huu ili kumchagua kiongozi bora atakayeweza kutekeleza malengo yao kimaendeleo.

Dkt. Wright amesema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi leo jijini Dar es Salaam ambapo wamejadili masuala ya ushirikiano wa maendeleo baina ya Tanzania na Marekani pamoja na kugusia harakati za kampeni za uchaguzi mkuu unaoendelea hapa Nchini.

Katika mazungumzo hayo Prof. Kabudi akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amemhakikishia Balozi wa Marekani Dkt. Wright kuwa Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza hususani katika sekta za utalii,kilimo,na biashara na kumhakikishia kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa huru,haki na wa amani.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa katika sekta ya utalii serikali ya awamu ya tano imedhibiti kwa kiasi kikubwa uwindaji haramu ikiwa ni pamoja na kupambana na ujangili jambo ambalo limeiwezesha serikali kuanzisha hifadhi za Taifa mpya nane ikiwa ni pamoja na kuimarisha hatua za usalama kwa watalii baada ya janga la corona kumalizika nchini.

Kwa upande wake Balozi wa Marekani hapa nchini Dkt. Donald Wright amemhakikishia Waziri kabudi kuwa atahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kuja nchini kuwekeza katika sekta za kilimo, biashara, huduma za afya na viwanda pamoja na kuhamasisha watalii kutoka marekani kuja nchini.

"Natumia fursa hii kuwasihi Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Octoba mwaka huu ili kumchagua kiongozi bora atakayeweza kutekeleza malengo yao kimaendeleo," Amesema Dkt. Wright.

Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald Wright akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi akimkabidhi Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald Wright moja ya nakala ya kitabu kinachoelezea masuala ya uchaguzi mkuu nchini Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald Wright. Kulia mwa Waziri ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.

Monday, September 7, 2020

BALOZI IBUGE AKUTANA NA BALOZI WA CHINA NCHINI

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke ofisini kwake jijini Dodoma.

Katika kikao hicho Katibu Mkuu, Balozi Ibuge na Balozi Wang Ke pamoja na mambo mengine wameongelea juu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu nafasi za uwakilishi wa kudumu kwa Bara la Afrika..

katika Kikao hicho Balozi Ibuge amesisitiza msimamo wa Tanzania kuunga mkono nia ya Bara la Afrika kuwa na nafasi mbili za uwakilishi wa kudumu katika Baraza hilo. Nchi za Afrika zinataka uwakilishi huo uwe na nguvu ikiwa ni pamoja na kupata nafasi moja ya kura ya Veto kama walivyokubaliana katika mkutano wa Ezulwini  na Azimio la Sirte la mwaka 1999. 

Balozi Ibuge pia amezungumzia kuhusu utekelezzaji wa mambo maalum ambayo yamo katika Hotuba ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli  aliyoitoa wakati wa kuzindua Bunge la 12. tarehe 13 Novemba 2020 jijini Dodoma, ambapo amemuomba Balozi Wang Ke kufikisha mambo yaliyomo katika hotuba hiyo kwa wawekezaji wa China ili kuwekeza nchini.

Balozi Ibuge amesema maono ya Mhe. Rais aliyoyasema katika hotuba yake ni utekelezaji wa moja ya kauli iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa "wakati wengine wanatembea Watanzania tunatakiwa tukimbie." ili kufikia maendeleo kwa haraka. 

Kwa Upande wake Balozi Wang Ke amemuhakikishia Balozi Ibuge, kwamba China iko pamoja na Bara la Afrika na kwamba wanaunga mkono  mapendekezo ya Bara la Afrika ya kuwa nafasi mbili za kudumu katika Baraza hilo.

Balozi Wang Ke ameelezea kufurahishwa na maono ya Mhe. Rais yaliyobainishwa katika Hotuba hiyo na kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania ili kufakisha maono hayo kwa vitendo na kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo. 

Viongozi hao pia wamejadiliana na kubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kindugu baina ya Tanzania na China kwa faida ya pande zote mbili.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimkaribisha Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke alipokutana naye ofisini kwake jijini Dodoma.



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke walipokutana ofisini kwake jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo hayo walipokutana ofisini kwake jijini Dodoma.


Balozi Wang Ke akizungumza katika kikao hicho