Wednesday, September 23, 2020

SERIKALI YAELEZA SABABU ZA VYOMBO VYA HABARI VYA KIMATAIFA KUSAJILIWA

Serikali imefafanua hatua yake ya kuvitaka vyombo vya habari vya Kimataifa vinavyotaka kuvitumia vyombo vya habari vya Tanzania kurusha matangazo yake yana lengo la kutambua vyombo hivyo vinashirikiana vyombo gani vya hapa nchini na sio kuvizuia kutangaza na kuendesha vipindi vyake hapa nchini kama inavyoripotiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi mteule wa Uingereza hapa nchini Dkt. David Concar na kufafanua kuwa mpaka sasa vyombo vyote vya habari vya Kimataifa zimekwishatekeleza matakwa hayo ya kisheria na kupata leseni ya kutangaza na kuendesha vipindi vyao.

"Leo nimekutana na Balozi mteule wa Uingereza hapa nchini Dkt. David Concar na kumueleza lengo la kusajili vyombo vya Habari vya kimataifa lilikuwa ni kutaka kujua ni chombo gani cha kimataifa kinashirikiana na chombo gana hapa nchini lakini pia ilikuwa ni matakwa ya kisheria,"  Amesema Prof. Kabudi 

Kuhusu suala la mabadiliko ya sheria za asasi za kiraia (NGOs) na vyama vya siasa Prof. kabudi amefafanua kuwa lengo lake lilikuwa ni kuongeza uwazi na uwajibikaji katika fedha zinazoingia kwa asasi hizo pamoja na matumizi yake na kuwa linaendana na sheria na taratibu za kimataifa za kuzuia utakatishaji wa fedha na kuhakikisha makundi yenye nia ovu na misimamo mikali inayokwenda kinyume na tunu za demokrasia hayatumii njia hizo kupenyeza fedha zao.

Balozi mteule wa Uingereza  Dkt. David Concar amesema mazungumzo yao mbali na kulenga masuala ya kidiplomasia na maendeleo pia yalilenga kuangalia namna ya kuondoa malalamiko kutoka kwa baadhi ya NGOs na vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni uminywaji wa haki ya uhuru wa vyombo vya habari.  

Katika tukio jingine pia Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Prof. Palamagamba John Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Denmark hapa nchini Balozi Mette Norgaard ambapo mbali na suala la uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 28 hapa nchini,wamejadili pia masuala yanayohusu mashirikiano katika sekta za elimu, afya, biashara na uwekezaji.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi akimkabidhi Balozi mteule wa Uingereza nchini, Dkt. David Concar nakala za sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi akimuonesha Balozi mteule wa Uingereza hapa nchini, Dkt. David Concar namna magazeti yanavyo ripoti habari za uchaguzi mkuu bila upendeleo  


Balozi wa Denmark nchini Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimuelezea jambo Balozi wa Denmark nchini Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet akimueleza jambo wakati walipokutana kwa mazungumzo jijini Dar es Salaam




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.