Friday, September 4, 2020

Tanzania kuwania nafasi ya Ujumbe wa Mfuko wa Pamoja wa Mazao Duniani

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju amemnadi mgombea wa Tanzania anayewania nafasi ya ujumbe kwenye Kamati ya Ushauri ya Mfuko wa Pamoja wa Mazao Duniani (Common Fund for Commodities – CFC) alipotembelea Ofisi za Mfuko huo zilizoko mjini Amsterdam, Uholanzi tarehe 02 Septemba, 2020.

Balozi Kasyanju alikwenda CFC kufanya mazungumzo na pia kumpongeza rasmi Mkurugenzi Mwendeshaji wa CFC, Mhe. Balozi Sheikh Mohammed Belal kwa kushika nafasi ya kuiongoza CFC kwa kipindi cha miaka minne, kazi aliyoianza rasmi mwezi Aprili 2020 baada ya kuchaguliwa kwa kauli moja kushika wadhifa huo wakati wa Mkutano Mkuu wa 31 wa Baraza la Uongozi la CFC uliofanyika tarehe 04 Desemba 2019. Katika mazungumzo yao Balozi Kasyanju alimhakikishia Mwenyeji wake huyo ushirikiano wa Tanzania kwa Taasisi yake na kutoa shukrani za dhati kufuatia mikopo yenye riba nafuu iliyotolewa kwa ajili ya kuboresha miradi mitatu inayoendelea hivi sasa nchini Tanzania.

Balozi Kasyanju aliitumia fursa hiyo sawia kumnadi mgombea wa Tanzania, Dkt. Jacqueline David Mkindi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa “Tanzania Horticultural Association (TAHA)” iliyoko mjini Arusha. Balozi Kasyanju alimuelezea Dkt. Mkindi kuwa ni kiongozi mahiri na mchapa kazi na akadhihirisha kwamba endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo ataiwakilisha vema Tanzania kwa kuwa mshauri bora na makini kwa CFC na Nchi zote Wanachama wa CFC na hivyo kuleta mwamko mpya kwenye Taasisi hiyo muhimu.

CFC iliundwa mwaka 1989 kwa mujibu wa taratibu za Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuboresha na kuleta maendeleo kwa jamii ya wakulima na wazalishaji wa bidhaa katika Nchi Zinazoendelea. Hivyo basi, CFC imejikita katika kutoa ufadhili wa mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kutumia rasilimali zake zinazotokana na michango ya hiari ya Nchi Wanachama na Wafadhili.

Tanzania ni Mwanachama hai wa CFC na katika Taasisi hii inawakilishwa kwenye Baraza lake la Uongozi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, kama Gavana; na Balozi wa Tanzania Nchini Uholanzi ambaye ni Gavana Msaidizi. Aidha, Tanzania imewahi kushika nafasi ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa CFC na vile vile mjumbe wa Kamati ya Ushauri ya CFC zaidi ya miaka 10 iliyopita. Hivyo, ni wakati mwingine muafaka kwa Tanzania kushika nafasi kwenye CFC hasa baada ya kutambua kwamba Mkurugenzi Mwendeshaji huyu mpya ameingia na nguvu mpya za kuleta mageuzi kwenye Taasisi yake na kuifanya iwe yenye tija zaidi kwa Wanachama wake.

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akipokea Taarifa ya Mwaka 2019 ya Mfuko wa Pamoja wa Mazao Duniani (Common Fund for Commodities – CFC) kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa CFC, Mhe. Balozi Sheikh Mohammed Belal, baada ya mazungumzo yao.

Balozi Irene Kasyanju akimkabidhi Mhe. Balozi Belal vipeperushi na majarida 20 yanayotangaza Utalii wa Tanzania yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza na Kidachi kwa ajili ya kusambazwa kwa wadau.

Balozi Irene Kasyanju na Mhe. Balozi Belal wakiwa pamoja na wasaidizi wao Bi. Linda Mkony (kushoto), Mtumishi wa Ubalozi; na kulia ni Bw.Hector Besong, CFC Portfolio and Risk Manager.


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.