Monday, September 7, 2020

PROF. KABUDI AMUAGA BALOZI WA IRAN NCHINI TANZANIA

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amemuaga Balozi wa Iran nchini, Mhe. Mousa Ahmed Farhang ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi nchini.

Akiongea katika hafla ya kumuaga balozi wa Iran iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, Prof. Kabudi amempongeza Balozi Farhang kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kudumisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi yake na Tanzania.

Pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi amemuahidi Balozi Farhang kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Iran katika sekta za elimu, afya na utalii kwa maslahi mapana ya nchi zote mbili.

"Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania nakuahidi ushirikiano kutoka kwetu, nakutakia kila la kheri katika maisha yako nje ya Tanzania na ni imani yangu kuwa utakuwa balozi mzuri wa Tanzania duniani," Amesema Prof. Kabudi

Kwa upande wake Balozi Farhang ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano wa kutosha wakati wa kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.

Balozi Farhang ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo baina ya Iran na Tanzania na amepongeza hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Tanzania imeendelea kuzichukua katika kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Balozi wa Iran Mhe. Mousa Ahmed Farhang akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati alipokuwa anamuaga baada ya kumaliza muda wa uwakilishi nchini 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimuelezea jambo Balozi wa Iran aliyemaliza muda wake wa uwakilishi nchini, Mhe. Mousa Ahmed Farhang  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro, Balozi wa Iran aliyemaliza muda wake wa uwakilishi nchini, Mhe. Mousa Ahmed Farhang

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.