Friday, December 4, 2020

WIZARA YA MAMBO YA NJE YAJIPANGA KUWAJENGEA UWEZO WA KAZI WATUMISHI WAKE

Mkurugenzi wa Kitengo cha Dispora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert Ibuge wakati wa ufunguzi rasmi wa Awamu ya Kwanza ya  Mafunzo Maalum kwa Maafisa Waandamizi wa Wizara kuhusu Utaalamu katika Uchambuzi wa masuala mbalimbali (Analytical Skills). Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Maafisa hao ili kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku. Kadhalika, Mafunzo hayo ambayo yalifanyika jijini Dodoma hivi karibuni, yaliandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI na Shirika la UNDP.

Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Peter Pinda akizungumza na mmoja wa Washiriki wa Mafunzo hayo alipotembelea eneo hilo akiwa kwenye shughuli zake za ujenzi wa Taifa na kuwasalimia Washiriki 

Sehemu ya Washiriki wa Mafunzo ya Utaalam katika Uchambuzi wakifurahia jambo

Washiriki wengine wakiwa tayari kuanza kujifunza mbinu mbalimbali za kufanya uchambuzi

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akiwasilisha Mada kwa Washiriki kuhusu "Umuhimu wa Uchambuzi katika Kufanya Maamuzi".

Sehemu ya Washiriki wakimsikiliza Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Singo (hayupo pichani) 

Sehemu nyingine ya Washiriki wakifuatilia mafunzo

Mwezeshaji kutoka Taasisi ya UONGOZI, Bibi Zuhura Muro akiwasilisha Mada kwa Washiriki kuhusu "Umuhimu wa Kutumia Akili Hisia (Emotional Intelligence) katika Uongozi". 

Mmoja wa Washiriki, Bw. Suleiman Magoma akichangia jambo wakati wa mafunzo hayo

Mwezeshaji kutoka Taasisi ya UONGOZI, Prof. Joseph  akiwasilisha Mada kwa Washiriki kuhusu "Umuhimu wa Uchambuzi katika Kutafuta Suluhisho la Matatizo mbalimbali".

Mmoja wa Washiriki, Bw. Ismail akieleza jambo kwa Washiriki wenzake ikiwa ni sehemu ya Washiriki kufanyia kazi yale waliyojifunza 

Washirki wakiwa kwenye mjadala

Sehemu nyingine ya Washiriki wa Mafunzo hayo.

 

TANZANIA, INDONESIA ZAAHIDI KUENDELEA KUKUZA BIASHARA

 Tanzania na Indonesia zimeahidi kushirikiana na kuendeleza kukuza biashara kwa kuanzisha kwa manufaa ya nchi zote mbili.  

Akihutubia katika usiku wa shukrani kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania na Indonesia kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili, Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Prof. Ratlan Pardede amesema kuwa maendeleo yaliyopatika kwenye sekta ya biashara nzuri inayofanywa na wafanyabiashara kutoka nchi zote mbili.

"Sisi Indonesia na Tanzania tumekuwa tukifanya biashara yenye manufaa kwa mataifa yetu mawili, bidhaa tunazouza ni imara na zimekuwa na ubora mzuri ambapo kwa sasa biashara imeongeza mapato zaidi ya asilimia 10," Amesema Balozi Pardede  

Ameongeza kuwa mwaka 2017 aliahidi kuwaleta wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Indonesia kuja Tanzania kwa ajili ya kuwekeza, ambapo hadi sasa tayari wameanzisha kiwanda cha Sabuni na Losheni Mkuranga

Kwa upande wake Mgeni Rasmi, ambaye ni Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga amempongeza Balozi kwa hatua na mipango mizuri ya kuinua uchumi wa mataifa yote mawili na kumuahidi ushirikiano katika kuhakikisha kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuwaboreshea mazingira wawekezaji na wafanyabiashara ili kuwawezesha kufanya biashara vizuri katika mazingira salama.

Nataka nikuhakikishie kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kati ya Indonesia na Tanzania kwa kiwango cha juu." Amesema Soraga. Pia Mhe. Waziri alielekeza wakati mwingine Baraza la kuundwe Biashara la Tanzania na Indonesia (TIBC) ili mpango huo uweze kujumuisha zaidi na kuwafikia wadau wengi nchini Tanzania.

Kulingana na rekodi za Ubalozi wa Indonesia, bidhaa takribani 54 za Kiindonesia zipo kwenye soko la Tanzania kama vile mafuta ya Mawese, nguo, karatasi pamoja na sabuni. Kwa upande mwingine, Indonesia imekuwa ikiagiza bidhaa kadhaa kutoka Tanzania, ambazo ni karanga, pamba, kakao, kahawa, chai, viungo na tumbaku.

Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Prof. Ratlan Pardede akiongea na wafanyabiashara (hawapo pichani) katika hafla ya usiku wa shukrani kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania na Indonesia iliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga akihutubia hadhara ya wafanyabiashara (hawapo pichani) katika hafla ya usiku wa shukrani kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania na Indonesia iliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Soraga akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Pardede jijini Dar es Salaam   


Waziri wa Biashara na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Soraga (katikati) akiwa pamoja na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Pardede katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Bw. Caesar Waitara (kushoto) na Afisa Mkuu Mambo ya Nje, Bw. Francis Luangisa jijini Dar es Salaam   


Washiriki (wafanyabiashara) wakifuatilia mkutano  


Baadhi ya Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Waziri Bw. Soraga pamoja na Mhe. Balozi, Pardede



Ubalozi wa Tanzania, Qatar Washiriki Tamasha la Kumi la Kiasili la Majahazi

Ubalozi wa Tanzania Qatar ukishirikiana na Wanadiaspora kutoka Tanzania unashiriki kwenye Tamasha la Kumi la Kiasili la Majahazi lijulikanalo kama 10th Katara Traditional Dhow Festival.Tamasha hilo  linafanyika Doha kuanzia tarehe 1-5 Disemba 2020 ambapo Tanzania inaelezea utamaduni wa kiasili wa jahazi wa mwambao wa Afrika Mashariki na Zanzibar ambapo ndio kitovu cha utamaduni huo. 

Utamaduni huo ulipelekea kuibuka muingiliano wa utamaduni wa lugha, mavazi, chakula na dini pamoja na matumizi ya Majahazi. Ubalozi umepata fursa pia ya kutangaza bidhaa za kitanzania kama viungo(spices) asali, korosho na kahawa pamoja na kutangaza utalii wetu. 

Mgeni Rasmi, Mhe. Hamad bin Abdulaziz Al Kawari, Waziri wa Nchi na Mkurugenzi wa Maktaba ya Taifa pamoja na Meneja Mkuu wa kijiji hicho cha Katara, Dr. Khalid bin Ibrahim Al Sulaiti  wakipata maelezo kwenye banda la Tanzania walipotembelea wakati wa uzinduzi wa Tamasha hilo.

Mabalozi wa Nchi za Afrika Mashariki waliopo Qatar wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Banda la Maonesho la Tanzania

 

Thursday, December 3, 2020

HABARI KATIKA PICHA MATUKIO MBALIMBALI ALIYOFANYA PROF. KABUDI

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akipokea barua ya pongezi kutoka kwa Balozi wa Ufaransa hapa Nchini Mhe. Frederic Clavier  iliyoandikwa na  Rais wa Ufaransa Mhe. Emmanuel Macron kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kumpongeza kwa Tanzania kuingia katika uchumi wa kati


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiteta jambo na Balozi wa Ufaransa hapa Nchini Mhe. Frederic Clavier katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (International Residual Mechanism for Criminal Tribunals -IRMCT) Bw. Abubacar Tambadou akimsikiliza Prof. Palamagamba John Kabudi wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (International Residual Mechanism for Criminal Tribunals -IRMCT) Bw. Abubacar Tambadou mara baada ya mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro Balozi wa Italia hapa nchini, Mhe. Roberto Mengoni ambaye amamaliza muda wake wa utumishi hapa nchini


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha Balozi wa Namibia hapa nchini, Mhe. Theresia Samaria ambaye amamaliza muda wake wa utumishi hapa nchini

 

 










RAIS WA UFARANSA AMTUMIA BARUA YA PONGEZI RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT JOHN POMBE MAGUFULI KWA KUIWEZESHA TANZANIA KUINGIA KATIKA ORODHA YA NCHI ZA UCHUMI WA KATI

Monday, November 30, 2020

BALOZI IBUGE ATAMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI ETHIOPIA

 Na Mwandishi wetu, Addis Ababa

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa Ubalozi pamoja na kukagua mali za Serikali nchini humo.

Balozi Ibuge kabla ya kuanza kukagua mali za Serikali, alikutana na watumishi katika mkutano ambapo amewataka kufanya kazi kwa bidii, weledi na uaminifu kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa.

"Nawasihi sana kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake tufanye kazi kwa bidii na kuwa wabunifu wa kuitangaza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," Amesema Balozi Ibuge

Pamoja na Mambo mengine, Balozi Ibuge amewasihi Ubalozi huo kuhakikisha kuwa wanatekeleza vyema vipaombele vya Serikali ya awamu ya tano kama ilivyoelekezwa kwenye ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (2020 - 2025) katika Sura ya Saba, ambapo sura hiyo imeelekezwa kuwa Balozi zote kutekeleza Diplomasia ya Uchumi pamoja na Diplomasia ya Siasa.

Pia Balozi Ibuge amekagua mali mbalimbali zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania nchini Ethiopia kwa lengo la kuijionea na kujiridhisha juu ya uwepo wa mali hizo.

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Bibi Elizabeth Rwitunga amemhakikishia Balozi Ibuge kuwa watafanya kazi kwa umoja, bidii, weledi na ubunifu kwa maslahi ya Taifa.

Bibi. Rwitunga ameongeza kuwa mashirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia ni mazuri na yanaendelea kuimarika ikiwemo ushirikiano katika masuala ya usafiri wa anga ambapo Shirika la Ndege la Ethiopia linashirikiana na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika masuala mbalimbali ikiwemo mafunzo na matengenezo ya ndege ambapo tayari watanzania watatu (3) wameshapatiwa mafunzo ya ndege.

Kuhusu Sera ya Diplomasia, Kaimu Balozi, Bibi. Rwitunga ameahidi kusimamia sera ya Diplomasia ya uchumi pamoja na Diplomasia ya siasa kwa kuhakikisha kuwa ubalozi utaendelea kuwasiliana na wawekezaji mbalimbali wa kuwekeza nchini Tanzania katika sekta za Nishati, Usafirishaji, Utalii pamoja na Biashara.

Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia unaiwakilisha Tanzania pia katika nchi za Djibouti, Yemen pamoja na Umoja wa Afrika na kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayosimamia masuala ya Uchumi Barani Afrika (UNECA).

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akisaini kitabu cha wageni katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia  


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisisitiza jambo kwa watumishi (hawapo pichani) wakati wa mkutano  


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akiendesha kikao na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini  


Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Bibi. Elizabeth Rwitunga (mwenye gauni la rangi ya bluu) akimpatia maelezo Balozi Ibuge wakati alipokuwa akikagua mali zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania nchini Ethiopia   


Balozi Ibuge akipatiwa maelekezo kutoka kwa Afisa wa Ubalozi wakati wa ukaguzi wa mali zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania nchini Ethiopia  

 



PROF. KABUDI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA, FINLAND NA SWEDEN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Finland hapa Nchini Mhe. Riitta Swan.Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiriki
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Sweden hapa Nchini Mhe. Anders Sjoberg.Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Balozi wa Sweden hapa Nchini Mhe. Anders Sjoberg. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Finland hapa Nchini Mhe. Riitta Swan. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam.

Saturday, November 28, 2020

UBALOZI WA TANZANIA AFRIKA KUSINI WAPEWA CHANGAMOTO YA KUTEKELEZA DIPLOMASIA YA UCHUMI, SIASA

Na Nelson Kessy, Pretoria

Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini wapewa changamoto ya kuhakikisha kuwa unatekeleza Diplomasia ya Uchumi pamoja na Diplomasia ya Siasa iliyopo ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM (2020-2025).

Changamoto hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge wakati alipotembelea Ubalozi huo jijini Pretoria nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kujionea utendaji kazi wa Ubalozi na mali za Serikali nchini humo. 

Balozi Ibuge ameutaka Ubalozi huo kuhakikisha kuwa unatekeleza diplomasia ya uchumi pamoja na diplomasia ya siasa kwa weledi ili kuleta manufaa ya Taifa.

"Nawapongeza kwa utendaji kazi wenu na nawasihi muendelee kujituma katika kazi (proactive) katika kuwapata wawekezaji na kutengeneza kuwa ni sehemu ya mfumo wa kuleta mabadiliko ambayo Serikali imeyapanga kupitia Ilani ya CCM ya 2020-2025," Amesema Balozi Ibuge.

Balozi Ibuge pia alipongeza utendaji wa Ubalozi huo ambao pamoja na Afrika Kusini unaiwakilisha Tanzania katika Ufalme wa Lesotho, Jamhuri ya Botswana, Jamhuri ya Namibia na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Kadhalika Balozi Ibuge alipokea changamoto mbalimbali zinazoikumba Ubalozi huo na Kuahidi kuzifanyia kazi ili kuongeza tija na ufanisi wa Ubalozi.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amemueleza Balozi Ibuge mafaniko mbalimbali ya Ubalozi katika kutekeleza diplomasia ya uchumi na siasa nchini Afrika Kusini.

Moja kati ya mafanikio hayo ni pamoja na kuenezwa kwa lugha ya Kiswahili ambapo Serikali ya Tanzania na ya Afrika Kusini zinatarajia kusaini mkataba wa kutumika lugha ya Kiswahili kama katika shule za Afrika Kusini mwezi wa Machi 2021.

"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Afrika Kusini tutasaini mkataba wa kutumika kwa lugha ya Kiswahili katika shule za Afrika Kusini mwezi wa Machi 2021," Amesema Balozi Milanzi.

Pamoja na mambo mengine Balozi Milanzi ameahidi kusimamia sera ya Diplomasia ya uchumi pamoja na Diplomasia ya siasa kwa kuhakikisha kuwa ubalozi utaendelea kuwasiliana na wawekezaji mbalimbali wa kuwekeza nchini Tanzania katika sekta za Biashara, Madini na Mawasiliano.


Balozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akiwatambulisha baadhi ya wafanyakazi kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ibuge wakati alipowasili Ubalozini leo tarehe 27 Novemba 2020


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akisaini kitabu cha wageni katika Ubalozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini leo tarehe 27 Novemba 2020


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisisitiza jambo kwa watumishi (hawapo pichani) wakati wa mkutano  


Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akiendesha kikao na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini  


Balozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akimuonesha baadhi ya mali Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi wakati alipokuwa anakagua mali za Serikali Ubalozini



 

 

 

 

 


Friday, November 27, 2020

SADC-TROIKA, UN KUBORESHA MFUMO WA USALAMA NDANI YA DRC

Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) zimekubaliana kuboresha mfumo utakao weka ulinzi bora na usalama ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akithibitisha kuhusu mashirikiano ya mfumo wa kuimarisha ulinzi na usalama nchini DRC, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amemuwakilisha Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika mkutano huo amesema kuwa kamati ya utatu inayoshughulika na usalama ndani ya jumuiya ya SADC imekutana kwa dharura ili kuweza kuangalia namna ya kukabiliana na matishio ya ugaidi yanayotishia sana hali ya amani na usalama katika nchi zilizopo ukanda wa SADC ikiwemo Msumbiji, Congo DRC na Tanzania.

Mkutano huo wa Dharura wa Wakuu wa Nchi wa Utatu wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, nchi zinazochangia Vikosi vya ulinzi na amani vya Umoja wa Mataifa kwenye Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Msumbiji  umefanyika leo Tarehe 27, Novemba 2020 mjini Gaborone, Botswana ambapo pamoja na mambo mengine umeangalia masuala mbalimbali yanayohusu amani, ulinzi na Usalama ndani ya SADC.

"Tumeangalia kwa undani mapendekezo mapya ya mfumo wa ulinzi katika enao la DRC ambapo nchi tatu zinazoshiriki katika kuimarisha Ulinzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo nchi tatu zinashiriki kuimarisha ulinzi na usalama nchini DRC (Tanzania, Malawi na Afrika Kusini) kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa zitaendelea kuimarisha masuala ya amani, Ulinzi na usalama Nchini DRC kwa kutumia mfumo mpya utakao weka ulinzi bora na amani nchini DRC," Amesema Mama Samia Suluhu Hassan.

Ameongeza kuwa, kupitia mkutano huo pia limejadiliwa suala la hali halisi ya usalama ndani ya nchi wanachama ndani ya SADC na kuona jinsi ya kutumia usalama wetu kwa ajili ya kujenga uchumi wa ukanda wetu wa kusini mwa Afrika

Kwa upande wake Rais wa Botswana, Dkt. Mokgweetsi Masisi ambae pia alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo amezipongeza nchi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Visiwa vya Shelisheli kwa kufanya chaguzi ambazo zilikuwa huru, haki na amani na kuzitaka nchi nyingine kuiga mfano huo wa kuwa na demokrisia ya uhuru, amani na haki.

"Matokeo ya chaguzi hizo ni mfano mzuri kwetu sisi kama nchi wanachama wa SADC kujifunza mfano kutoka kwa wenzetu," Amesema Dkt. Masisi.

Dkt. Masisi ameongeza kuwa pamoja kufanya chaguzi huru haki na za amani, kuna mambo ambayo yamekuwa yakijitokeza katika ukanda wa SADC kama vile, Ugaidi, uhalifu wa kimtandao na vikundi vya waasi jambo ambalo limepelekea wakuu wan chi na serikali kukutana hapa (Botswana) na kujadili namna ya kukabiliana na changamoto hizo kwa kuwa changamoto hizi siyo za nchi moja moja bali na kuzitaka nchi zote kuungana na kukabiliana na vikundi hivyo vya kigaidi.

"Mtakumbuka kuwa katika mkutano wetu wa SADC uliofanyika mwezi wa nane mwaka huu tulitoa ripoti iliyoonesha kuwa na baadhi ya ugaidi kwa baadhi ya nchi zetu za SADC, pamoja na ripoti kuonyesha kuwa kuna hali ambayo siyo shwari kwa baadhi ya nchi wananchama, kuna haja ya kuungana pamoja na kuhakikisha kuwa vikundi hivi vya kigaidi vinatokomezwa katika ukanda wetu wa SADC," Amesema Dkt. Masisi.

"Ni jukumu letu sote kuipa ushirikiano Jamhuri ya Kidemocrasia ya Congo hasa upande wa Mashariki mwa DRC na kuhakikisha kuwa amani ya nchi hiyo inalindwa kwa kutokomezwa kwa vikundi vya kigaidi vinavyochangia kutoweka kwa amani nchini humo, na ndiyo maana leo tumekutana hapa ili tuweze kuona na jinsi gani ya kumsaidia mwenzetu DRC," Ameongeza Dkt. Masisi

Pamoja na mambo mengine, Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama  inawajibika kukuza amani na usalama katika eneo la SADC na pia ina wajibu wa kuongoza na kuzipatia nchi Wanachama mwongozo kuhusu mambo ambayo yanatishia amani, ulinzi na usalama.

Ni mara ya kwanza kwa Wakuu wan chi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC - TROIKA) kukutana ana kwa ana tangu ulipotokea ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (Covid-19).

Mkutano huo ulihudhuriwa na, Rais wa Botswana Mhe. Dkt. Mokgweetsi Masisi, Rais wa Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa, Rais wa Malawi Mhe. Lazarus Chikwera, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Felix Tshisekedi, Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Msumbiji Bw. Jaime Neto aliyemuwakilisha Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati wa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi wa Utatu wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, nchi zinazochangia Vikosi vya ulinzi na amani vya Umoja wa Mataifa kwenye Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Msumbiji  uliofanyika leo Tarehe 27, Novemba 2020, mjini Gaborone Botswana

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati wa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi wa Utatu wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, nchi zinazochangia Vikosi vya ulinzi na amani vya Umoja wa Mataifa kwenye Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Msumbiji  uliofanyika leo Tarehe 27, Novemba 2020, mjini Gaborone Botswana

Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi wa Utatu wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, nchi zinazochangia Vikosi vya ulinzi na amani vya Umoja wa Mataifa kwenye Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Msumbiji  uliofanyika leo Tarehe 27, Novemba 2020, mjini Gaborone Botswana





Thursday, November 26, 2020

MAWAZIRI SADC - TROIKA WAKUTANA KWA DHARURA BOTSWANA

 Baraza la Mawaziri wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama wakutana katika mkutano wa dharura na kujadili masuala ya siasa, ulinzi na usalama.

Mkutano huo umefanyika leo mjini Gaborone, Botswana ambapo ulitanguliwa na mkutano wa Makatibu Wakuu wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ulioanza asubuhi na kumalizika mchana.

Kupitia mkutano huo, mawaziri wameweza kujadili masuala ya hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda ya SADC na kupendekeza njia mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwenye siasa, ulinzi na usalama ndani ya ukanda wa SADC.

Pamoja na mambo mengine, Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama  inawajibika kukuza amani na usalama katika eneo la SADC na pia ina wajibu wa kuongoza na kuzipatia nchi Wanachama mwongozo kuhusu mambo ambayo yanatishia amani, ulinzi na usalama.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) (mwenye tai nyekundu) akifuatilia mkutano wa dharura wa baraza la Mawaziri wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama uliofanyika Mjini Gaborone. Kulia mwa Waziri ni Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Mnyepe akifuatiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge

Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ukiwa ukiimba wimbo wa SADC kabla ya kuanza kwa mkutano wa dharura wa baraza la Mawaziri


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana Dkt. Lemogang Kwape akifungua mkutano wa Dharura wa baraza la mawaziri, kushoto kwake ni Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stegomena Taxi

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stegomena Taxi mara baada ya kumaliza mkutano wao     


MAKATIBU WAKUU SADC - TROIKA WAKUTANA KUJADILI SIASA NA USALAMA

Makatibu Wakuu wa SADC -TROIKA wamekutana na kujadiliana Mambo mbalimbali yakiwemo masuala ya hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ndani ya SADC mjini Gaborone, Botswana.

Awali, Mkutano wa Makatibu Wakuu ulifunguliwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana, Bw. Gaeimelwe Goitsemang ambae pia alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo.

Ni mara ya kwanza kwa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ( SADC) kukutana ana kwa ana tangu ulipotokea ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (Covid-19).

Kwa upande wa Makatibu wakuu waliohudhuria katika Mkutano huo kutoka Tanzania ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe.

Mkutano wa Makatibu Wakuu utafuatiwa na Mkutano wa Dharua wa Baraza la Mawaziri wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano katika Siasa, Ulinzi na Usalama baadae mjini Gaborone.


Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ukifuatilia Mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC -TROIKA uliofanyika mjini Gaborone, Botswana


Mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC -TROIKA ukiendelea

Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ngazi ya Makatibu Wakuu ukifuatilia mkutano  

Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, akiwasilisha mada katika Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Asasi ya SADC ya ushirikiano katika siasa, ulinzi na Usalama unaondelea Mjini Gaborone, Botswana