Tanzania imeendelea
kuhimiza umuhimu wa mataifa makubwa kuzifutia madeni nchi za Jumuiya ya nchi za
Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS) zilizoathiri na janga la COVID-19 pamoja
na kuyataka mataifa hayo kuhakikisha kwamba chanjo ya COVID-19 itakayopatikana
inazifikia nchi zote za Jumuiya hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba
John Kabudi (Mb) ambaye pia ni Rais wa Baraza la Mawaziri la OACPS wakati
alipokuwa anawasilisha hotuba yake katika Mkutano wa 39 wa Bunge la pamoja
baina ya nchi za ACP na EU na Mkutano wa 111 wa Baraza la Mawaziri kutoka nchi
za Jumuiya ya OACPS uliofanyika jana kwa njia ya Mtandao (Video Conference) jijini
Dar es Salaam.
"Kutokana na jukumu
langu kama Rais wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS nimehutubia kwa njia
ya video Bunge la pamoja la Ulaya na ACP (ACP-EU Joint Parliamentary Assembly).
Katika hotuba yangu nimehimiza umuhimu wa mataifa makubwa kuendelea kuzifutia
madeni nchi za OACPS zilizoathiri na janga la COVID-19, pamoja na kuyataka
mataifa hayo kuhakikisha kwamba chanjo ya COVID-19 itakayopatikana inazifikia
nchi zote za Jumuiya yetu ya OACPS," Amesema Prof. Kabudi
Halikadhalika, Prof. Kabudi
ameelezea hatua iliyofikiwa na nchi za OACPS ikiwemo Tanzania katika kujenga
democrasia, uchumi, biashara na maendeleo ya watu ikiwemo suala la kulinda na
kuheshimu haki za binadamu. Aidha, aliwajulisha juu ya changamoto zinazozikabili nchi za OACPS katika
kutimiza adhma yao ya maendeleo, ikiwemo janga la ugonjwa wa COVID -19,
mabadiliko ya tabia nchi, ugumu wa kuyafikia masoko ya ulaya, masuala ya amani
na usalama ikiwemo suala la wakimbizi.
Kwa upande wake Waziri wa
Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani, Dkt. Gerd Muller, ambaye pia ni Raisi wa
Baraza la Mawaziri la Umoja wa Ulaya alimhakikishia
Prof. Kabudi kuwa Umoja wa Ulaya (EU) utaendeleza ushirikiano wake na nchi za
OACPS katika kuhakikisha kuwa uchumi wa Jumuiya hiyo unazidi kuimarika.
"Naomba kutumia fursa
hii kukuhakikishia kuwa sisi ka EU tupo tayari kushikamana na Jumuiya ya OACPS
kuimarisha uhusiano wetu kiuchumi, kisiasa, kidiplomasia lakini pia kulinda na
kuapa kipaumbele masuala yote yanayohusu haki za binadamu," Amesema Dkt.
Muller.
Mbali na Dkt. Muller
wengine waliohutubia katika mkutano huo ni pamoja na Jutta Urpilanen, Kamishna
wa Ubia wa Kimataifa kutoka EU ambaye nae pia alisisitiza kuendeleza mshikamano
baina ya nchi za EU na OACPS.
Katika hatua nyigine, Prof.
Kabudi ameeleza kuwa kumalizika kwa mkutano wa 39 wa Bunge la pamoja baina ya
nchi za ACP na EU kumetoa fursa ya kufanyika kwa mkutano wa wa Baraza la
Mawaziri wa nchi za OACPS unaotegemewa kuanza kufanyika kwa njia ya mtandao
(Video Conference) kuanzia tarehe 13 hadi 17.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa
katika mkutano huo, masuala muhimu yatakayo jadiliwa ni pamoja na Mapambano
dhidi ya ugonjwa Corona, majadiliano ya mkataba mpya wa ubia mpya baina ya nchi
za OACPS na Umoja wa Ulaya, Mageuzi (reforms) ndani ya Sekretariati ya OACPS, kusimamia
kusainiwa kwa Mkataba ulioboreshwa wa Georgetown (the Revised Georgetown
Agreement) na nchi za OACPS pamoja na Mikakati ya kufanya shughuli za Jumuiya
ziguse zaidi Maisha ya wananchi.
Itakumbukwa kuwa Agosti 1,
2020 Tanzania ilikabidhiwa jukumu la kuongoza Jumuiya ya nchi za Afrika,
Caribbean na Pasifiki (OACPS) kwa ngazi ya Mawaziri na kwa ngazi ya balozi
Brussels.
Jukumu hilo ni heshima
kubwa kwa Tanzania na ni ishara ya wazi ya jumuiya ya kimataifa kutambua kazi
kubwa anayofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli ndani ya nchi na hivyo kutamani pia ushawishi wake huo uwe katika
ngazi ya kimataifa hususan katika jumuiyan hii ya OACPS.
Hii ni mara ya tatu
Tanzania kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
Jumuiya hii tangu ilipoanzishwa mwaka 1975. Tanzania ilikuwa Mwenyekiti mwaka
1992 na mwaka 2014. Chini ya Uongozi wa Tanzania vipaumbele vikuu ni pamoja na
kupambana na ugonjwa wa corona na athari zake, kusimamia kukamilishaji wa
majadiliano ya mkataba mpya wa ubia kati yan chi za OACPS na Umoja wa
Ulaya, kusimamia mageuzi makubwa ndani
ya Jumuiya ya OACPS ili iendane na wakati na kuelekeza rasilimali zake kwenye
maeneo muhimu yenye tija kwa wanachama.
Aidha, Tanzania pia imelenga kuimarishaji
ushiriano miaongoni mwa nchi za OACPS (Connectivity) na kufanya mashauriano na
wabia wetu wengine wa maendeleo ukiwemo Umoja wa Ulaya katika kuweka mifumo
mizuri zaidi ya kuimarisha biashara, ongezeko la thamani ya mazao ya kilimo,
matumizi ya digitali na fursa zaidi za masoko.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) na Rais wa Baraza la Mawaziri la OACPS akisisitiza jambo wakati alipokuwa anawasilisha hotuba yake katika Mkutano wa 39 wa Bunge la pamoja baina ya nchi za ACP na EU jana jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya Mtandao (Video Conference). Picha na Nelson Kessy
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) na Rais wa Baraza la Mawaziri la OACPS akichangia mada katika Mkutano wa 39 wa Bunge la pamoja baina ya nchi za ACP na EU jana jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya Mtandao (Video Conference). Picha na Nelson Kessy |