Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula
(Mb) amekutana kwa mazungumzo na mabalozi watatu wanaowakilisha nchi zao hapa
nchini pamoja na kupokea nakala ya hati za utambulisho za balozi mteule wa
Italia hapa nchini.
Mabalozi
hao wamekutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini
Dar es Salaam ni Balozi wa Burundi Mhe. Gervais Abayeho, Balozi wa Uingereza
Mhe. David Concar pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Manfredo Fanti.
Pamoja
na mambo mengine, Viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano
katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu Biashara na Uwekezaji na Utamaduni.
“Leo
nimekutana na mabalozi watatu kutoka Burundi, Uingereza na Umoja wa Ulaya na
nimejadiliana nao masuala mbalimbali ya ushirikiano katika masuala ya uchumi,
biashara na uwekezaji na mahusiano baina yetu na nchi zao,” amesema Balozi
Mulamula
Balozi
Mulamula ameongeza kuwa “mabalozi wote watatu wameahidi kuendeleza ushirikiano
wa kidiplomasia kwa manufaa ya nchi zetu………lakini pia tumejadili mipango ya
kimkakati kutoka kwa Umoja wa Ulaya na Uingereza ambapo wangependa kuona
inaendelezwa katika awamu hii,” amesema Balozi Mulamula.
Nae
Balozi wa Burundi nchini Tanzania Mhe. Abayeho amesema uhusiano wa Burundi na
Tanzania ni wa miaka mingi na wamefurahia kuuona uhusiano huo ukiendelea
kuboreka zaidi na tunaamini uhusiano huo utaendelea kudumu kwa miaka mingi.
“Uhusiano
wa Burundi na Tanzania ni uhusiano wa muda mrefu na tunafurahia kuona unazidi
kuimarika. Mbali na masuala ya uhusiano umependekeza utekelezwaji wa miradi mikubwa
kama vile ujenzi wa bandari, barabara na reli uharakishwe kwa manufaa ya nchi
zote mbili,” Amesema Balozi Abayeho
Kwa upande
wake Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar amesema katika kikao
chake na Mhe. Waziri wamejadili namna ya kuboresha uhusiano baina ya Uingereza
na Tanzania na jinsi ya kufanya kazi kwa pamoja katika kudumisha na kuendeleza
uhusiano huo.
Balozi
wa Umoja wa Ulaya, Mhe. Manfredo Fanti amesema kuwa uhusiano wa kidiplomasia
uliopo baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ni wa zaidi ya miaka 46 na
umekuwa ukinufaisha pande zote mbili hivyo Umoja wa Ulaya utaendelea
kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kuwa inapata manendeleo kijamii na
kiuchumi.
Katika
tukio jingine, Mhe. Waziri Mulamula amepokea nakala ya hati za utambulisho
kutoka kwa Balozi Mteule wa Italia hapa nchini Mhe. Marco Lombardi.
“Tanzania
na Italia tuna uhusiano mzuri katika maeneo mbalimbali ikiwemo utalii,
uwekezaji na elimu na tumejadiliana mambo aliyoagizwa na serikali yake katika
kudumisha uhusiano wa Italia na Tanzania.
Kwa
Upande wake Balozi Mteule, Mhe. Lombardi amesema Italia na Tanzania zina
masuala mengi ya kushirikiana katika sekta mbalimbali za kiuchumi,kijamii na
utamaduni na kwamba yuko nchini kuhakikisha
hayo yote yanatekelezeka kwa maslahi ya nchi zote mbili.
“Tunaamini
kupitia maongezi yetu ya leo tutaendelea kuimarisha uhusiano wetu wa kiuchumi
na kisiasa kwa maslahi ya Italia na Tanzania, lakini pia nimemhakikishia Mhe.
Waziri kuwa Italia itaendelea kuwa bega kwa bega na Tanzania katika kuhakikisha
mahusiano yake ya kidiplomasia yanakua na kuimarika,” amesema Mhe.
Lombardi
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula
(Mb) akiongea na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Mhe. Manfredo Fanti wakati
wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula
(Mb) akimsikiliza Balozi wa Burundi hapa nchini Mhe. Gervais Abayeho wakati wa
mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Balozi
wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati wa
mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula
(Mb) akimsikiliza Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar wakati wa
mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula
(Mb) akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule wa Italia
hapa nchini Mhe. Marco Lombardi jijini Dar es Salaam