Na Mwandishi wetu, Dar
Tanzania
imezindua rasmi maadhimisho ya kitaifa ya Kumbukumbu ya Maadhimisho ya Miaka 40
tangu
kuanzishwa kwa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) tarehe 1 Aprili 1980.
Akiongelea uzinduzi wa
maadhimisho hayo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema Tanzania
ikiwa ni miongoni mwa nchi 16 wanachama wa SADC
inajivunia mafanikio
yaliyopatikana ambayo yanaenzi mchango mkubwa wa Viongozi Wakuu waanzilishi
wa SADC ambao maono yao yaliweka msingi wa ukombozi wa kisiasa na kiuchumi kwa nchi za Kanda ya Kusini mwa Afrika.
Balozi Mulamula amesema
wakati SADC ikiadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, Tanzania imejipanga
kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu SADC
na fursa zake kiuchumi, kijamii na kisiasa na itaongeza hamasa kwa raia
wake ili wachangamkie fursa zinazopatikana ndani ya jumuiya hiyo.
“Pamoja na mambo mengine,
tumejipanga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mtangamano wa
SADC na faida za uanachama kwenye Jumuiya hii ikiwa ni pamoja na fursa zilizopo
za kiuchumi, kijamii na kisiasa, kuangazia
mafanikio yaliyofikiwa katika masuala ya amani na usalama na pia maendeleo ya
kiuchumi kwa watu wote katika Kanda ya Kusini mwa Afrika; na kuongeza hamasa kwa makundi mbalimbali kama
wafanyabiashara, vijana, wanawake, makundi maalum na wananchi kwa ujumla
kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zinazopatikana kupitia uanachama wa
SADC,” amesema Balozi Mulamula.
Waziri Mulamula amesema katika
kuadhimisha miaka 40 ya
SADC, Tanzania imeandaa
mihadhara kuhusu umuhimu wa SADC kwa Tanzania na Kanda ya Kusini mwa Afrika ambapo mihadhara hiyo itafanyika katika baadhi ya vyuo
vikuu vya hapa
nchini. Amesema mhadhara wa
kwanza utafanyika tarehe 19
Mei, 2021 katika Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM) mhadhara
wa pili utafanyika katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) tarehe 21 Mei, 2021 mhadhara
wa tatu utafanyika katika
Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) tarehe 26
Mei 2021 na mhadhara
wa hitimisho utafanyika katika Chuo cha Diplomasia (CFR) tarehe 27
Mei, 2021
Balozi Mulamula ameyataja
mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka hiyo 40 ya SADC kuwa ni pamoja na harakati
za ukombozi hususan kwa nchi za Kusini mwa Afrika na kuimarika
kwa hali ya Ulinzi na Usalama na masuala ya demokrasia na utawala bora katika
nchi za SADC
“Itakumbukukwa kuwa,
Tanzania wakati wa uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ilifanya kazi kubwa
ya kusaidia harakati za ukombozi hususan kwa nchi za Kusini mwa Afrika. Kadhalika,. Kadhalika,
Tanzania chini ya Uongozi
wa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilikuwa
Mwenyekiti wa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kwa kipindi
cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti 2018 hadi Agosti 2019 ambapo katika kipindi hicho cha uenyekiti mchango wa Tanzania ulifanikisha masuala mbalimbali ndani ya SADC kukamilika ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa hali ya Ulinzi na Usalama na masuala
ya demokrasia na utawala bora katika nchi za SADC,” amesema Waziri Mulamula
Ameyataja mafanikio
mengine kuwa ni pamoja na kuzinduliwa kwa mfumo wa uombaji na utoaji vyeti
vya utambuzi wa Uasili wa Bidhaa kwa njia ya mtandao, kuzinduliwa kwa Baraza la Biashara la SADC, kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme wa SADC wa
megawati 3,595 sawa na asilimia 90 ya lengo la kuzalisha megawati 4000, kuandaliwa kwa Dira ya maendeleo ya SADC ya mwaka
2050 pamoja na Mpango Elekezi wa Maendeleo ya Kikanda (RISDP) wa Mwaka
2020-2030.
“Mafanikio mengine ni kuridhiwa
kwa lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha nne za SADC, kupitishwa kwa Azimio la Kuondolewa Vikwazo vya
iuchumi vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe tangu mwaka 2000. Azimio hilo
liliridhia tarehe 25 Oktoba ya kila
mwaka kuwa siku maalum ya kupinga vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Zimbabwe,” amesema Balozi Mulamula.
Aidha, kumbukumbu
ya maadhimisho hayo kwa ngazi ya kikanda itahitimishwa tarehe 5 Juni, 2021 kwa
mhadhara wa umma utakaofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na
Serikali wa SADC utakaofanyika kuanzia tarehe 30 Mei hadi 8 Juni 2021 jijini Maputo,
Msumbiji.
Kaulimbiu ya maadhimisho
haya ni: “Miaka 40 ya SADC ya Kuimarisha
Amani na Usalama, Kuhamasisha Maendeleo na Ustahimilivu wa Changamoto Zinazoikabili Dunia” .
SADC
ilianzishwa kutoka kwa uliokuwa Mkutano wa Uratibu wa Maendeleo Kusini mwa Afrika
(Southern African Development Coordination Conference-SADCC) (SADCC) ambao ilianzishwa rasmi Lusaka,
Zambia mwezi Aprili 1980 baada
ya Nchi za Mstari wa Mbele kuridhia Azimio la Lusaka lililojulikana kama “Kusini
mwa Afrika: Kuelekea Ukombozi wa Kiuchumi ambao pamoja na mambo mengine, ulilenga kuimarisha sekta muhimu za kuchochea maendeleo ya kanda kama vile Uchukuzi na
Mawasiliano, Kilimo na Chakula, Viwanda, Maendeleo ya Rasilimali Watu na Nishati.
Nchi Wanachama waanzilishi wa SADCC ni Angola, Botswana, Lesotho, Malawi,
Msumbiji, Swaziland, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
Mwezi
Agosti 1992, Wakuu wa Nchi na Serikali waliokutana jijini Windhoek, Namibia walisaini
Mkataba wa kuibadilisha SADCC kuwa SADC na
kutoa fursa ya kutafsiri upya misingi ya ushirikiano
miongoni mwa Nchi Wanachama kutoka kwenye muungano usio rasmi na kuwa muungano
wa kisheria. SADC ina wanachama 16 ambao ni Angola, Botswana, Comoros, Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi,
Mauritius, Msumbiji, Namibia, Ushelisheli, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na
Zimbabwe.
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula |