Sunday, November 28, 2021

TANZANIA KUSHIRIKI MKUTANO JUKWAA LA USHIRIKIANO KATI YA CHINA NA AFRIKA

 


Na mwandishi wetu, Dakar

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaoanza leo tarehe 28 hadi 30 Novemba 2021 jijini Dakar nchini Senegal.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ataongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo.

 

Katika Ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, Marais wa Nchi Wenyeviti Wenza wa Mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Senegal Mhe. Macky Sall na Rais  wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping watahutubia Mkutano huo.

 

Mkutano huo wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika unatanguliwa na Mkutano wa Maafisa Waandamizi unaoanza leo tarehe 28 Novemba 2021 hapa Jijini Dakar, Senegal ambapo  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mpango Zanzibar Dkt. Juma Akil na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bibi Amina Shaaban watashiriki.

 

Mkutano huo utakaowashirikisha viongozi na wawakilishi kutoka nchi za Bara la Afrika na Jamhuri ya Watu wa China pamoja na mambo mengine utajikita katika majadiliano ya maeneo yafuatayo:- Ushirikiano wa Kisiasa, Ushirikiano wa Kiuchumi, Ushirikiano wa Maendeleo ya Kijamii, Utamaduni na Ushirikiano kati ya Watu na Watu, Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama, Mapinduzi ya Kijani, Ubadilishanaji Uzoefu katika masuala ya Uongozi Bora pamoja na Maendeleo ya Kitaasisi ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika.

RAIS SAMIA NA RAIS MUSEVENI WAFUNGA KONGAMANO LA WAFANYABIASHARA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museven wameshiriki katika kufunga Kongamano la Wafanyabiashara kati ya Tanzania na Uganda lililofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam

Pamoja na mambo mengine, Viongozi hao wameahidi kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta ya nishati na gesi ili kufungua fursa kwa wananchi wa pande zote mbili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufungaji wa Kongamano la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda lililohudhuriwa na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufungaji wa Kongamano la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda lililohudhuriwa na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni mara baada ya kufunga Kongamano la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda lililofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam  


Baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali wakifuatilia ufungaji wa Kongamano la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda lililofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam  


Sehemu ya Mawaziri na Wafanyabiashara wakifuatilia ufungaji wa Kongamano la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda lililofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam  




 

Saturday, November 27, 2021

TANZANIA NA UGANDA ZAKUBALINA KUIMARISHA USHIRIKIANO

 Na Waandishi wetu, Dar

Tanzania na Uganda zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati zikiwemo nishati, utalii, usafirishaji, viwanda, kilimo na uvuvi kwa maslahi ya wananchi wa pande zote mbili.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni yaliyofanyika leo tarehe 27 Novemba 2021, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Akitoa taarifa ya mazungumzo baina yao kwa  waandishi wa habari, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania na Uganda zimeendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ya uwekezaji na biashara kwa miaka mingi ambapo hadi sasa Uganda ni nchi ya pili kwa uwekezaji nchini Tanzania kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

“Tumezungumza masuala mengi na Mhe. Rais Museveni na tumekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kindugu uliopo kati yetu hususan kwenye sekta za manufaa kwetu sote. Pia tumekubaliana kuimarisha biashara na uwekezaji baina yetu na ninafurahi kuwajulisha kuwa hadi sasa Uganda  ni nchi ya pili kwa uwekezaji nchini Tanzania kwa ukanda wa Afrika Mashariki ambapo ipo miradi 45 yenye thamani ya Dola milioni 114 na imewezesha kutoa ajira kwa watanzania 2150”, amesema Mhe. Samia.

Kuhusu masuala ya biashara, Mhe. Rais Samia amesema mwenendo wa biashara kati ya Tanzania na Uganda ni mzuri ambapo hadi kufikia mwaka 2020 ujazo wa baishara kati ya nchi hizo umeongezeka hadi kufikia Shilingi bilioni 607 kutoka shilingi bilioni 200 mwaka 20214.

Kadhalika, viongozii hao wamewaagiza Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya biashara wa Tanzania na Uganda kukutana mara kwa mara ili kutatua changamoto mbalimbali za ufanyaji biashara na kuwataka kukutana katika kipindi cha miezi miwili ijayo kujadili namna ya kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha vilivyopo baina ya nchi hizo kwa lengo la kurahisisha ufanyaji biashara.

Rais Samia ameongeza kuwa pia wamekubaliana kufungua Ofisi ya Bandari nchini Uganda ili kurahisisha na kukuza biashara kati ya Tanzania na Uganda.

Akizungumzia kuhusu Ugonjwa wa UVIKO 19, Mhe. Rais Samia amesema wamekubaliana kuanzisha kiwanda cha pamoja cha kuzalisha dawa na chanjo kwa ajili ya binadamu na wanyama kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo UVIKO 19.

Aidha, Rais Samia ametumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Rais Museveni kwa kufadhili ujenzi wa Shule ya Msingi huko Wilayani Chato, Mkoani Geita na kusema kitendo hicho ni cha kuigwa kwani Mhe. Rais Museveni anatambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa Tanzania.

Rais Samia amesema pia katika mazungumzo yao wamewaagiza Mawaziri wa Mambo ya Nje kufanya mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda mwezi Disemba ili kuweka mikakati ya kutekeleza makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa kwa nyakati tofauti na nchini hizi mbili.

Kwa upande wake, Rais Museveni amemshukuru mwenyeji wake kwa mwaliko na kusisitiza kwamba  ushirikiano huo wa kindugu  kati ya Tanzania na Uganda utaimarishwa  na kuenziwa kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Akizungumzia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki, Rais Museveni amesema kuwa matayarisho ya msingi kuhusu kuanza kwa ujenzi wa mradi wa bomba hilo yamekamilika.

Mhe. Rais Museveni yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine, atashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda, atatembelea Bandari ya Dar es Salaam na mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na kukabidhi shule ya msingi iliyojengwa Wilayani Chato kwa ufadhili wake.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimtambulisha mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni kwa wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akisalimiana na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala. Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb), Balozi wa Tanzania Nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima pamoja na Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Naimi Aziz


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni Ikulu Jijini Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akiteta jambo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam 


Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam


Baadhi ya Mawaziri, Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi waandamizi serikalini wakifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Ikulu Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akisoma tamko la pamoja kati ya Tanzania na Uganda, Ikulu Jijini Dar es Salaam

Friday, November 26, 2021

Maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa EAC yakamilika


Na Mwandishi Maalum, Arusha

Mawaziri wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) watakutana jijini Arusha katika Mkutano wao wa 41 wa Baraza la Mawairi uliopangwa kufanyika tarehe 29 Novemba 2021.

Makatibu Wakuu wamekamilisha maandalizi yote yanayohitajika ya mkutano huo, zikiwemo nyaraka za taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Jumuiya, vyombo na Taasisi zake katika kikao kilichofayika tarehe 25 na 26 Novemba 2021.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine ameongoza Makatibu Wakuu wenzake katika kikao hicho, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome; Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro; Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Ikulu, Zanzibar, Bw Mussa Haji Ali na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah.

Mkutano wa Mawaziri ambao utakuwa chini ya uenyekiti wa Kenya unatarajiwa kufanya maamuzi na kutoa maelekezo kuhusu utekeleaji wa masuala ya mtangamano katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya biashara, miundombinu, afya, ajira, fedha na uanzishwaji wa taasisi mpya hususan taasisi za fedha zitakazosimamia Umoja wa Fedha.

Waheshimiwa Mawaziri pia watapitia na kupitisha ratiba ya shughuli za EAC kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2022. Shughuli hizo zinajumuisha mikutano ambapo kwa kanuni za EAC asilimia 50 ya mikutano inafanyika katika nchi wanachama na asilimia 50 iliyosalia inafanyika makao makuu ya Jumuiya. Licha ya makao makuu ya EAC kuwa Tanzania, bado nchi hiyo inapewa mgawo wa mikutano ya asilimia 50 inayofanyika katika nchi wanachama.

Mkutano wa Mawaziri unatarajiwa kuhitimishwa kwa Mawaziri kushuhudia uwekaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa majukumu (performance contracts) kati ya Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Katibu Mkuu wa EAC na baina ya Katibu Mkuu wa EAC na Naibu Makatibu Wakuu na Wakurugenzi wa Idara mbalimbali za EAC.

Meza Kuu wakati wa Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu Wakuu ikiendesha kikao jijini Arusha.

Ujumbe wa Makatibu Wakuu wa Tanzania ukiwa katika Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu Wakuu. Kutoka kushoto ni  Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Ikulu, Zanzibar, Bw Mussa Haji Ali na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah.

Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kenya ukifuatilia kikao 

Ujumbe wa Tanzania kutoka Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali unaoshiriki mkutano huo.

Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mjadala wa mkutano wa Makatibu Wakuu.


Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Ellen Maduhu akifuatilia kwa makini mjadala wa mkutano.

TANZANIA, USWISI KUIMARISHA USHIRIKIANO ZAIDI

 Na Mwandishi Wetu, Dar

Tanzania na Uswisi zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za afya, elimu na uchumi kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa pande zote mbili.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokuwa katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi jana jioni jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula amesema kuwa katika miaka 40 ya Ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi, ushirikiano umeimarika na nchi hizi zimekuwa zikiufurahia kwa kipindi chote, na kuongeza kuwa “Uhusiano kati ya Tanzania na Uswisi ni mzuri na imara na umekuwa na manufaa kwa pande zote mbili,” amesema Balozi Mulamula

“Tunapozindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Uswisi na Tanzania 2021-2024, ambao pamoja na mambo mengine, umejikita katika kuimarisha taasisi za serikali, kulinda na kuboresha afya na maisha ya vijana. Napongeza juhudi zinazofanywa na Uswisi katika maandalizi na ukamilishaji wa mpango wa maendeleo ambao sasa unatupeleka katika hatua nyingine ya utekelezaji,” ameongeza Balozi Mulamula.

Waziri Mulamula ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikichukua hatua madhubuti katika kupitia na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini ambapo Serikali na sekta binafsi wanafanya kazi kwa kutunga na kuboresha sera zitakazolinda na kuwezesha sekta binafsi kukua. 

Pia Balozi Mulamula amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kurekebisha Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996. Utaratibu huu unafanywa kwa njia shirikishi ambayo inahusisha sekta ya umma na binafsi. Mipango hii itachangia katika kuweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji na biashara kwa wawekezaji na biashara kutoka mataifa makubwa duniani na washirika wengine wa kibiashara.

Kwa upande wake, Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot amesema kuwa ushirikiano wa Uswisi na Tanzania umelenga zaidi uboreshaji wa barabara za vijijini, maendeleo ya kilimo, sekta ya afya na uwezeshaji wa asasi za kiraia. Aliongeza kusema kuwa, miradi ya maendeleo ya Uswisi nchini Tanzania imepanuka na kujumuisha shughuli mbalimbali katika nyanja za utawala, uvumbuzi, kuongeza ujuzi, mafunzo ya ufundi stadi na utamaduni.

“Ushirikiano wetu umekuwa na mafanikio mengi na katika kipindi cha miaka 40 iliyopita ambapo Uswisi imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa katika sekta za afya, ujenzi wa taasisi na mafunzo ya wafanyakazi wa afya,” amesema Balozi Chassot

Balozi Chassot ameongeza kuwa, Uswisi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kutoa msaada wa kuimarisha taasisi za serikali ili kuongeza mapato ya umma na kutoa huduma bora za umma, zenye usawa na zinazofaa zaidi kwa wananchi wote, kupunguza vikwazo vya kijamii na kiuchumi pamoja na kuimarisha matarajio ya kiuchumi kwa vijana. 

Tunatazamia kuimarisha zaidi ushirikiano wetu na washirika wetu serikalini na mashirika ya kiraia katika kutekeleza agenda ya kimataifa ya kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Dazi amesema kuwa wameridhishwa na hatua za maendeleo ambazo Tanzania imepiga na kuahidi kuendelea kushirikiana zaidi katika kuwainua wananchi kiuchumi.

“Uswisi imekuwa ikishirikiana na Tanzania kwa zaidi ya miaka 40 na tutaendelea kuudumisha ushirikiano huu kuwainua vijana kiuchumi ili kuwawezesha kufikia malengo yao kijamii na kisiasa,” amesema Bi. Dazi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akihutubia katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi jana jioni jijini Dar es Salaam


Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot akihutubia katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi jana jioni jijini Dar es Salaam 


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Dazi akihutubia katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Dazi  


Sehemu ya wageni waalikwa walioshiriki katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi jana jioni jijini Dar es Salaam

  


 

Thursday, November 25, 2021

SERIKALI YAZIHAKIKISHIA KAMPUNI ZA USWISI MAZINGIRA SALAMA YA BIASHARA, UWEKEZAJI

 Na Waandishi wetu, Dar

Serikali ya Tanzania imezihakikishia kampuni za Uswisi mazingira salama ya biashara na uwekezaji nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi Mulamula amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita imetilia mkazo katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kupitia sheria na kuondoa baadhi ya kodi zilizokuwa ni kikwazo kwa wawekezaji.

“Serikali imepitia sheria zetu na kuweza kuondoa kodi zilizokuwa kero............na kupitia pia sheria ya uwekezaji kwa lengo la kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi pamoja na ujumbe wake wameoneshwa kuridhishwa na juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na kuahidi kuendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uswisi kuja kuwekeza Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi amesema pamoja na mambo mengine, wamejadiliana mazingira ya biashara na uwekezaji na vitu ambavyo kampuni za Uswisi zinahitaji ili kuwekeza zaidi Tanzania.

“Tumeridhishwa na juhudi za Serikali ya Tanzania za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na tumemhakikishia Waziri Mulamula kuwa tutaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara kutoka Uswisi kuja kuwekeza Tanzania,” amesema Bi. Daanzi

Bi. Daanzi ameongeza kuwa mbali na kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji pia kuna maeneo ya ushirikiano ambayo Serikali ya Uswisi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha maisha ya watanzania.

Katika tukio jingine, Balozi Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China Nchini Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao pamoja na mambo mengine, wamejadili kuhusu Mkutano wa nane (8) wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 - 30 Jijini Dakar nchini Senegal.

Katika Mkutano huo Rais wa China Mhe.  Xi Jinpign anatarajiwa kuhutubia kwa njia ya Mtandao ambapo Tanzania itawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.

Mkutano huo utawajumuisha viongozi na wawakilishi kutoka Bara la Afrika na China ambapo utatoa fursa ya viongozi hao kujadili na kuangalia jinsi ambavyo China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitatu 2018 - 2021 kwenye  maeneo ya ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda barani Afrika, ujenzi wa miundombinu ya nishati, usafirishaji, habari na mawasiliano, kukuza wigo wa biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.

Maeneo mengine ni kampeni ya mapinduzi ya kijani, mpango maalum wa mafunzo ya ufundi, kuboresha sekta ya Afya, ulinzi na usalama na ushirikiano katika masuala ya habari, utamaduni sanaa na michezo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zaadi ya picha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Daanzi, Balozi wa Uswisi Nchini Mhe. Didier Chassot, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swahiba Mndeme. Wengine ni ujumbe ulioambatana na Bi. Daanzi. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akimkaribisha Balozi wa China Nchini Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi wa China Nchini Mhe. Chen Mingjian akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Wednesday, November 24, 2021

MAWIZIRI WA EAC KUKUTANA ARUSHA

Na. Mwandishi Maalum, Arusha

Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaendelea jijini Arusha katika ngazi ya maafisa waandamizi. Mkutano huo ulioanza  tarehe 22 Novemba 2021 utahitimishwa na Kikao cha Mawaziri wa Nchi za Jumuiya kitakachofanyika tarehe 29 Novemba 2021.

Tanzania ambayo ni mwanachama muasisi wa Jumuiya hiyo inashiriki kikamilifu katika mkutano huo ambapo Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen P. Mbundi anaongoza ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya maafisa waandamizi.

Maafisa waandamizi wanaandaa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa shughuli za Mtangamano wa Afrika Mashariki ambazo zitawasilishwa kwenye ngazi ya Makatibu Wakuu na hatimaye ngazi ya Mawaziri kwa ajili ya kutolea maamuzi na maelekezo.

Waheshimiwa Mawaziri pia watapokea na kupitia taarifa za utekelezaji wa vyombo na Taasisi za EAC, zikiwemo Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kamisheni ya Kiswahili ambayo Makao Makuu yake yapo Zanzibar na Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika jitihada za Tanzania za kukuza lugha ya Kiswahili duniani, Waheshimiwa Mawaziri watapokea taarifa ya maendeleo ya mchakato wa kubadilisha sheria na taratibu za EAC ili kuwezesha kuanza rasmi matumizi ya  lugha ya Kiswahili pamoja na Kifaransa kama ilivyoelekezwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Februari 2021. Aidha, Waheshimiwa Mawaziri watapokea taarifa kuhusu mchakato wa uhakiki wa maombi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa mwanachama mpya wa EAC.

Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika kikao cha ngazi ya maafisa waandamizi, Balozi Stephen P. Mbundi akifuatilia kwa makini majadiliano ya mkutano wa EAC.  
Mwenyekiti wa kikao kutoka Kenya akiendesha kikao cha maafisa waandamizi.

Baadhi ya ujumbe wa Tanzania ambao ni Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika kikao cha ngazi ya maafisa waandamizi, Balozi Stephen P. Mbundi,  Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombimu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota (mwenye peni) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Bw. Benjamini Mwesiga (aliyesimama) wakijadili jambo wakati wa kikao cha maafisa waandamizi cha EAC.  

Ujumbe a Tanzania ukifuatilia majadiliano kuhusu agenda mbalimbali za kikao cha maafisa waandamizi wa EAC.

Wajumbe mbalimbali wakifuatilia majadiliano ya kikao cha EAC

Ujumbe kutoka Uganda ukifuatilia kikao cha EAC