Tuesday, January 18, 2022

WAZIRI MULAMULA ASISITIZA UTEKELEZAJI DIPLOMASIA YA UCHUMI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Mauritius Balozi Prof. Emmanuel Mbennah na kusisitiza juu ya utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kwa maslahi ya Taifa

Mazungumzo ya viongozi hao yamelenga kusisitiza utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi baina ya Wizara na Balozi za Tanzania ili kuweza kutumia fursa zilipo katika mataifa mbalimbali kunufaisha Taifa.

Vilevile, Waziri Mulamula amesisitiza uwajibikaji kwa balozi zote za Tanzania ili kuweza kufikia malengo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukuzaji na utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Mauritius Balozi Prof. Emmanuel Mbennah katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Mauritius Balozi Prof. Emmanuel Mbennah yakiendelea 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Mauritius Balozi Prof. Emmanuel Mbennah



Monday, January 17, 2022

MKUTANO WA NNE WA TUME YA KUDUMU YA PAMOJA KATI YA TANZANIA NA UGANDA WAFUNGULIWA JIJINI KAMPALA, UGANDA

Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Uganda umeanza leo tarehe 17 Januari 2022 katika ngazi ya Wataalamu Jijini Kampala, Uganda. 

Mkutano huu wa awali pamoja na mambo mengine utajadili masuala ya ushirikiano yaliyokubaliwa baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda. Mkutano huu utafuatiwa na mkutano katika ngazi ya Makatibu Wakuu utaofanyika tarehe 18 Januari 2022 na utamalizika kwa Mkutano ngazi ya Mawaziri utaofanyika tarehe 19 Januari 2022.

Lengo la Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ni kujadili na kutathmini hatua za utekelezaji zilizofikiwa katika masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye mkutano wa tatu uliofanyika mwezi Septemba 2019 jijini Dar es salaam, Tanzania.

Pia, kutathmini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika ziara zilizofanywa na Marais wa pande zote mbili katika nyakati tofauti, tangu kumalizika kwa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na Uganda. 

Vilevile, mkutano huu utashuhudia utiwaji saini wa mikataba takribani sita itakayohusisha sekta mbalimbali za ushirikiano pamoja na kuruhusu maeneo mapya ya ushirikiano. Kadhalika utajadili ushirikiano katika ujenzi wa miradi ya kimkakati unaofanywa na mataifa hayo hususan ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) unaofanywa na Serikali ya Tanzania ambao unatarajiwa kunufaisha nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tanzania na Uganda zinashirikiana katika sekta za Siasa na Diplomasia, Mawasiliano, Fedha na Uchumi, Nishati, Maendeleo na ujenzi wa Miundombinu, Elimu na Mafunzo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo na Uvuvi, Maji na Mazingira, Afya na Elimu. 

=====================================================

Waziri wa Nchi, Mambo ya Nje (uhusiano wa Kikanda) wa Uganda akifungua Mkutano wa Nne wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika leo tarehe 17 Januari 2022 katika ngazi ya Wataalamu jijini Kampala, Uganda. Katika Ufunguzi huo Mhe. Mulimba amewahimiza Wataalamu kuwa na namna bora ya kuratibu ufutiliaji wa masuala ya ushirikiano yanayohitaji utekelezaji au utatuzi wa haraka badala ya kusubiri vikao vya waheshimiwa Maraisi.

Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo ambapo pamoja na mambo mengine Balozi Naimi alieleza kuwa mkutano utajadili na kutathimini utekelezaji katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano, utekelezaji wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaofanywa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na kushuhudia utiwaji saini wa mikataba takribani sita ya ushirikiano baina ya mataifa hayo.


Picha ya pamoja Waziri wa Nchi, Mambo ya Nje (uhusiano wa Kikanda) Mhe. John Mulimba pamoja na viongozi katika ngazi ya Wataalamu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na Uganda unaofanyika leo tarehe 17 Januari 2022 jijini Kampala , Uganda.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Aziz Mlima akifafanua utaratibu wa majadiliano ndani ya mkutano huo.


Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania wakifuatilia mkutano.

Ujumbe kutoka Tanzania.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania

Ujumbe kutoka Uganda ukifuatilia mkutano.

Viongozi wakitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kumalizika kwa zoezi la ufunguzi wa Mkutano huo.


BALOZI WA TANZANIA NCHINI OMAN AKUTANA NA WAWAKILISHI WA TAASISI ZINAZOTOA MISAADA NCHINI ZILIZOPO OMAN

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Abasi Kilima akikabidhi tuzo maalum kwa Mwakilishi wa Taasisi za Misaada ya Kijamii zenye makao yake nchini Oman ambazo hutoa huduma za kijamii hapa nchini. Tuzo hizo  zilitolewa kwa Taasisi mbili  zilizofanya vizuri nchini ambazo ni Tuelekezane Peponi na Attaqwa. Hafla hiyo fupi ilifanyika hivi karibuni wakati wa mkutano wa kwanza kati ya Mhe. Balozi Kilima na Wawakilishi wa Taasisi hizo.

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Balozi Kilima akikabidhi tuzo nyingine kwa Mwakilishi wa Taasisi za Misaada ya Kijamii zenye makao yake nchini Oman ambazo hutoa huduma za kijamii hapa nchini. Hafla hiyo ya utoaji tuzo ilifanyika hivi karibuni wakati wa mkutano wa kwanza kati ya Mhe. Balozi Kilima na Wawakilishi wa Taasisi hizo.

Mmoja wa Wawakilishi wa  Taasisi za Misaada ya Kijamii zenye makao yake nchini Oman ambazo hutoa huduma za kijamii hapa nchini akizungumza wakati wa wakati wa mkutano wa kwanza kati ya Mhe. Balozi Kilima na Wawakilishi hao.

Mhe. Balozi Kilma (katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Taasisi za Misaada ya Kijamii zenye makao yake nchini Oman ambazo hutoa huduma za kijamii hapa nchini. 
===========================================

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Abasi Kilima, hivi karibuni amekutana kwa mara ya kwanza na Wawakilishi wa Taasisi za Misaada ya Kijamii zenye makao yake nchini Oman ambazo zinatoa huduma za kijamii nchini Tanzania.

Katika hotuba ya kuwakaribisha Wawakilishi hao, Mhe. Balozi alisema Taasisi hizo zina mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii ya Watanzania na kuwataka waendelee na huduma zao hizo. Vilevile, alizitaka Taasisi hizo kutoa taarifa za miradi ya kijamii wanayoitekeleza nchini Tanzania ili mchango wao uweze kutambulika rasmi Serikalini kwani alisema ingawa mchango wao ni mkubwa kwa taifa lakini Taasisi hizo haziwasilishi rasmi taarifa zao.


Akitaja baadhi ya huduma zinazotolewa na Taasisi hizo alisema zipo Taasisi zinazochimba visima na hivyo zimekuwa zikisaidia kampeni ya Serikali ya "Kumtua ndoo mama". Vilevile, zipo Taasisi zinazotoa huduma za elimu, kusaidia yatima, kujenga nyumba za makazi na nyumba za ibada. Aliendelea kusema kuwa, kwa kuwa viongozi wa Taasisi hizo wana asili ya Tanzania na bado wana mafungamano makubwa na nchi yao ya asili, Serikali inawatambua kama Diaspora na hivyo uwasilishaji wa taarifa za huduma wanazozitoa utasaidia lengo la Serikali la kuwapa hadhi maalum.


Mhe. Balozi Kilima alizitaka Jumuiya hizo kuwa kitu kimoja na kukutana mara moja au mbili kila mwaka kujadili masuala yao. Miongoni mwa Taasisi alizokutana nazo ni pamoja na Alwadood International
, Istiqama International, Attaqwa, Tuelekezane Peponi, Sundus, Coco Charity na Alfirdaus. Pia alitumia fursa hiyo kuzipa tuzo maalum Taasisi mbili zilizofanya vizuri nchini Tanzania. Taasisi hizo ni Tuelekezane Peponi na Attaqwa. Taasisi nyengine zilizofanya vizuri zilipewa Tuzo wakati wa Sherehe za Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.


Katika mkutano huo, Wawakilishi wa Taasisi hizo walipata fursa ya kuelezea changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo ushuru kwa bidhaa na vifaa wanavyoleta nchini kwa ajili ya Misaada na kuiomba Serikali iwaondolee ushuru kwa bidhaa hizo. Kadhalika, walieleza changamoto nyengine ya kuchelewa kupata usajili kwa baadhi ya Taasisi, upatikanaji wa vibali na tozo za viza. Pia, wameomba Serikali iwapatie utambulisho maalum ili waweze kuingia nchini mara kwa mara kutekeleza miradi ya Kijamii.


Akitoa ufafanuzi wa changamoto hizo, Mhe. Balozi Kilima alisema ni vyema Taasisi hizo ziwasiliane na Ubalozini pale zinapohitaji kupeleka misaada ya kijamii ili Ubalozi uweze kuwatambulisha rasmi katika Mamlaka za Serikalini. Aidha, kuhusu viza aliwashauri kuomba   viza ya kuingia mara kwa mara (Multiple entry visa) au viza ya kutembelea jamaa (family visit visa).

Pamoja na majibu hayo, alisema Serikali inaendelea na mchakato wa kuandaa mpango maalum wa kuwatambua Diaspora na kuwapatia hadhi maalum itakayowarahisishia utekelezaji wa shughuli zao za kijamii nchini.

Taasisi hizo kwa pamoja zimechimba visima virefu 200, visima vifupi 5000, zimejenga nyumba za yatima 17, Madrasa 62, na Misikiti 47. Aidha, Taasisi ya Alwadood inakusudia kuleta nchini mtambo wa kuchimbia visima virefu wenye thamani ya USD 170,000.


 




 


 

Saturday, January 15, 2022

BALOZI HEMEDI MGAZA AKUTANA NA BALOZI WA TANZANIA NCHINI KUWAIT

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemedi Mgaza (kulia)amefanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhe. Said Shaibu Mussa alipokuja kuaga uongozi wa Wizara tarehe 14 Januari 2022 jijini Dodoma.

Viongozi hao walijadili hali halisi ya utekelezaji wa majukumu ndani ya Idara ya Mashariki ya Kati na kuweka mikakati madhubuti ya usimamizi wa majukumu katika dawati la Kuwait linaloratibiwa na idara hiyo.
Kwa pamoja wameazimia kufanya kazi kwa ushirikiano, kusimamia miradi ya ushirikiano inayoendela katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu inayofadhiliwa na Mfumo wa Kuwait hususani miradi ya kilimo, maji, ujenzi wa miundombinu, afya, elimu na ajira za kitaalamu.

Balozi Mgaza akimkaribisha Mhe. Said Shaibu Mussa katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Friday, January 14, 2022

WAZIRI MULAMULA AWAHIMIZA MABALOZI KUTEKELEZA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) amewasisitiza mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nje ya nchi kuweka mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu ya kidiplomasia wenye maslahi mapana kwa uchumi wa Taifa.

Mhe. Mulamula ameyasema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhe. Said Shaibu Mussa aliyekuja kumuaga ofisisni kwake leo tarehe 14 Januari 2022 katika ofisi za Wizara, jijini Dodoma.

Mazungumzo baina ya wawili hao yalijikita katika kuangalia namna bora ya kuboresha utendaji wa ofisi za balozi za Tanzania sambamba na Wizara ili kuweza kutumia fursa zilipo kunufaisha Taifa.

“Nasisistiza balozi zetu kutekeleza majukumu kwa kuhakikisha fursa za kiuchumi zinawekewa msisistizo sambamba na mafanikio yanayopatikana yanatangazwa kikamilifu ili kuweza kuuhabarisha uuma namna ya kuzitumia fursa zinazopatikana”. Alisema Mhe. Waziri

Pia ameeleza umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kufikia malengo tarajiwa katika sekta ambazo serikali ya Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na mataifa wanayowakilisha.

Naye Balozi Said Shaibu Mussa amemshukuru Mhe. Waziri kwa maelekezo ya kiteundaji aliyoyapata sambamba na kuahidi kufanya kazi kwa ubunifu katika majukumu hayo mapya ili kuongeza maeneo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Kutwait.

Tanzania na Kuwaita zimekuwa zikishirikiana katika sekta za kilimo, afya, ujenzi wa miundombinu ya barabara na maji.

====================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhe. Said Shaibu Mussa alipokuja kumuaga ofisini kwake leo tarehe 14 Januari 2022 jijini Dodoma.

Mazungumzo yakiendelea. Kulia ni Msaidizi wa Waziri, Bw. Seif Kamtunda akifatilia mazungumzo.

Mhe. Waziri Mulamula akimkabidhi vitendea kazi Mhe. Said Mussa.



WAZIRI MULAMULA AMUAGA BALOZI WA MALAWI NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana na Balozi wa Malawi nchini Mhe. Glad Chembe Munthali leo tarehe 14 Januari 2022 katika ofisi za Wizara jijini Dodoma .

Katika mazungumzo yao Mhe. Waziri Mulamula amempongeza Mhe. Munthali kwa kumaliza salama muda wake wa utumishi katika nafasi ya Balozi hapa nchini na amemtakia utumishi mwema katika majukumu mengine mapya atakayopangiwa.

"Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Malawi kwakuwa ushirikiano wetu umejikita katika kuhakikisha maendeleo ya watu na Taifa yanapatikana katika pande zote mbili za ushirikiano'', alisema Waziri Mulamula.

Pia akaeleza miradi ya ushirikiano inayofanywa baina ya Tanzania na Malawi itaendelea kusimamiwa kwa karibu mpaka pale atakapoteuliwa mwakilishi mwingine kushika nafasi hiyo.

Naye Balozi Munthali alitumia nafasi hiyo kutoa shukurani zake pamoja na za Serikali ya Malawi akieleza kuwa miaka mitatu ya utumishi wake hapa nchini imekuwa ya mafanikio kufuatia ushirikiano uliotolewa na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza majukumu yake.

"Tanzania kwangu ni nyumbani, sisi ni majirani na siku zote watu wetu wamekuwa na muingiliano kupitia shughuli za kiuchumi na kijamii", alisema Balozi Munthali

Pia, Mhe. Munthali alimpongeza Mhe. Waziri Mulamula kwa utaratibu mzuri uliowekwa na Wizara katika kuhakikisha taratibu zote za Mabalozi na Wawakilishi wa Kimataifa zinasimamiwa na kuruhusu utekelezaji wa majukumu yao.

Tanzania na Malawi zimekuwa zikishirikiana katika sekta ya ujenzi wa miundombinu, huduma za jamii, biashara na masoko. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Malawi aliyemaliza muda wake hapa nchini Mhe.Glad Chembe Munthali. Viongozi hao wamekutana leo tarehe 14 Januari 2022 katika katika ofisi za Wizara jijini Dodoma .

Waziri Mulamula akimkabidhi zawadi ya picha Mhe. Munthali.
Picha ya Pamoja. Kulia ni Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Azizi na kulia ni Afisa Mambo ya Nje, Bw. Ali Ubwa.

 

TANZANIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA MISRI KATIKA KUBORESHA SEKTA YA AFYA

Serikali ya Tanzania imepokea tani 16 za Dawa, Vifaa Tiba na Vifaa Kinga ikiwa ni msaada wenye thamani ya shillingi milioni 864 kutoka Serikali ya Misri.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali wakati wa hafla fupi ya kupokea shehena ya dawa hizo iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof.  Abel Makubi amesema Tanzania inaishukuru Serikali ya Misri kwa msaada huo muhimu kwa wananchi wa Tanzania na kwamba itandelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Misri hususan katika kuboresha sekta ya afya na kuahidi kuusimamia kikamilifu msaada huo ili uwafikie walengwa kwa wakati.

Pia aliongeza kusema kuwa,  msaada huo umewasili wakati mwafaka ambao Tanzania inaendelea kuboresha sekta ya afya kwa kusogeza huduma za afya kwa wananchi pamoja na kuongeza upatikanaji wa Dawa na Vifaa Tiba katika maeneo ya mijini na vijijini.


Aidha, alipongeza ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Misri ambao umekuwa wa manufaa makubwa tangu kuanzishwa kwake na kupongeza jitihada zinazofanywa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha Sekta ya Afya nchini ambapo alisema msaada huo ni miongoni mwa matokeo ya ziara ya Mhe. Rais aliyoifanya nchini Misri mwezi Novemba, 2021.


"Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na pia kwa niaba ya Waziri wa Afya. Mhe. Ummy Mwalimu napokea msaada huu wa Dawa na Vifaa Tiba wenye thamani zaidi ya shilingi milioni 800 kutoka Serikali ya Misri. Kama Serikali, tunaendelea kuboresha na kusogeza huduma za afya kwa wananchi hivyo msaada huu utachangia jitihada hizo. Ninakuomba Mhe. Balozi ufikishe salamu zetu za shukrani kwa Mhe. Abdel Fattah Al-Sisi, Rais wa Misri kwa msaada huu ambao tumeupokea kwa dhati na utatimiza lengo lilokusudiwa la kuwasaidia wananchi wa Tanzania" alisema Dkt. Makubi.


Kwa upande wake, Balozi wa Misri hapa nchini. Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania na inaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi makini wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuwaletea watanzania maendeleo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.


Kadhalika, Mhe. Balozi Abulwafa alieleza kuwa, mbali na ushirikiano wa Tanzania na Misri kwenye sekta ya afya, Nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutoa fursa za mafunzo ya kuwajengea uwezo watu wa sekta ya afya na fani mbalimbali kwa watanzania.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifelo Sichwale, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Bw. Daudi Msasi, Kaimu Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Celestine Kakele na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.

 Balozi wa Misri hapa nchini, Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa (katikati) akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi (wa pili kulia) msaada wa Dawa na Vifaa Tiba kutoka Serikali ya Misri. Wengine katika picha ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe ( wa pili kushoto), Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifelo Sichalwe (wa kwanza kushoto) na Mwambata Jeshi wa Ubalozi wa Misri, Brigedia Sherif Farag Mohamed (wa kwanza kulia). Hafla ya makabidhiano ya msaada huo imefanyika jijini dar es Salaam hivi karibuni.
Mhe. Balozi Abulwafa akimkabidhi Prof. Makubi huku viongozi wengine wakishuhudia. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Itifaki na Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Celestine Kakele.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi kwa pamoja na Balozi wa Misri nchini, Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa wakisaini Hati ya Makabidhiano ya Dawa na Vifaa Tiba vilivyopokelewa nchini kutoka Misri
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi kwa pamoja na Balozi wa Misri nchini, Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa wakibadilishana Hati ya Makabidhiano waliyosaini wakati wa mapokezi ya Dawa na Vifaa Tiba  kutoka Misri
Balozi wa Misri nchini, Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada wa Dawa na Vifaa Tiba  kkwa Serikali ya Tanzania
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi akizungumza  kwa niaba ya Serikali mara baada ya kupokea msaada wa  Dawa na Vifaa Tiba  kutoka Misri
Viongozi wakiwa katika picha ya pamoja
Picha ya pamoja ya viongozi na wadau mbalimbali

Afisa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi Faith Masaka akibadilishana mawazo na Afisa kutoka Ubalozi wa Misri hapa nchini, Bw. Mahmoud Hamdy Khalifa wakati wa hafla ya makabidhiano ya Dawa na Vifaa Tiba kutoka Misri


























 

Thursday, January 13, 2022

WAZIRI MULAMULA APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA KWA MABALOZI WATEULE WA SAUDI ARABIA, KOREA, INDONESIA NA MOROCCO NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mhe. Abdullah bin  Ali Alsheryan. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma. 
Mara baada ya makabidhiano viongozi hao walipata fursa ya kuzungumza juu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia uliopo baina ya mataifa hayo pamoja na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano. 
Balozi Mulamula akimkaribisha Mhe.Abdullah bin  Ali Alsheryan katika ofisi za Wizara zilizopo mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Kim Sun Pyo. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma. 
Mara baada ya makabidhiano hayo Waziri Mulamula alimhakikishia Mhe.Kim Sun Pyo kuwa serikali ya Tanzania itampa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake mapya katika kipindi chake atakachohudumu nchini. Jamhuri ya Korea imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta za teknolojia ya mawasiliano, elimu, afya, utalii na ujenzi wa miundobinu.
Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ceasar Waitara na Afisa Mambo ya Nje, Bw. Halmeinsh Lunyumbu wakifuatilia mazungumzo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Indonesia, Mhe. Triyogo Jatmiko. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma. 

Mhe. Balozi Mulamula na Mhe. Triyogo Jatmiko walijadili juu ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara na masoko, viwanda, elimu, utalii na kufungua fursa nyingine za kiuchumi kupitia ushirikiano imara wa kidiplomasia uliopo baina ya mataifa hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Ufalme wa Morocco, Mhe.Zacharia El Guoumiri. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma. 

Mazungumzo baina ya Mhe.Balozi Mulamula na Mhe. Balozi Zacharia El Guoumiri yalijikita katika kuimarisha ushirikiano baiba ya Tanzania na Morocco hususani katika sekta za michezo, elimu, maendeleo ya jamii na kuinua ujasiliamali kwa lengo la kukuza viwanda ili kuweza kuwanufaisha wananchi mataifa yao. 

Mazungumzo yakiendelea, kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Azizi akifatilia mazungumzo hayo.

SADC YAKUBALIANA KUENDELEA KUISADIA MSUMBIJI KULINDA AMANI

Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyoko nchini Msumbiji ulioanza jana tarehe 11 Januari 2022 nchini Malawi umemalizika leo tarehe 12 Januari 2022 ambapo Nchi wanachama wa SADC wamekubaliana kuendelea kuisaidia Jamhuri ya Msumbiji katika kuhakikisha Amani na usalama vinapatikana.  

Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali, wamekubaliana  kuendelea kujitolea kulinda amani na usalama nchini Msumbiji hasa katika Jimbo la Cabo Delgado licha ya nchi nyingi kuendelea kukabiliana na changamoto ya ugonjwa wa uviko 19.

Akifunga Mkutano huo leo, Rais wa Jamhuri ya Malawi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Lazarus Chakwera amewashukuru wakuuu wa Nchi na Serikali kwa Ushirikiano na umoja ambao nchi wanachama wa SADC wamekuwa wakionesha katika kuisaidia Jamhuri ya Msumbiji kupambana na ugaidi.

“Lazima tuungane kwa pamoja na kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Msumbiji inakuwa na Amani na Usalama……hivyo basi ni jukumu letu sisi sote katika kuhakikisha wananchi wa Msumbiji wanakuwa na amani kwani bila amani hakuna maendeleo,” amesema Rais Chakwera.

Awali akisoma tamko la pamoja, Katibu Mendaji wa SADC Bw. Elias Magosi amesema Wakuu wa Nchi na Serikali wameipongeza SADC kwa dhamira yake isiyoyumba ya kusimamia na kutetea amani na usalama, na kwa kutumia rasilimali zake katika kushughulikia na kupambana na ugaidi katika jimbo la Cabo Delgado.

Mkutano huo pia umepongeza hatua ya mshikamano iliyooneshwa kwa ahadi za chakula zilizotolewa na Jamhuri ya Malawi, Afrika Kusini na Zimbabwe ili kupunguza matatizo yanayowakabili wakimbizi  katika Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.

Rais wa Jamhuri ya Malawi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Lazarus Chakwera akifunga Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC Msumbiji 



Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC Msumbiji 




Mkutano ukiendelea


Wakuu wa Nchi na Wawakilishi wa Wakuu wa nchi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC Msumbiji