Thursday, January 13, 2022

SADC YAKUBALIANA KUENDELEA KUISADIA MSUMBIJI KULINDA AMANI

Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyoko nchini Msumbiji ulioanza jana tarehe 11 Januari 2022 nchini Malawi umemalizika leo tarehe 12 Januari 2022 ambapo Nchi wanachama wa SADC wamekubaliana kuendelea kuisaidia Jamhuri ya Msumbiji katika kuhakikisha Amani na usalama vinapatikana.  

Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali, wamekubaliana  kuendelea kujitolea kulinda amani na usalama nchini Msumbiji hasa katika Jimbo la Cabo Delgado licha ya nchi nyingi kuendelea kukabiliana na changamoto ya ugonjwa wa uviko 19.

Akifunga Mkutano huo leo, Rais wa Jamhuri ya Malawi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Lazarus Chakwera amewashukuru wakuuu wa Nchi na Serikali kwa Ushirikiano na umoja ambao nchi wanachama wa SADC wamekuwa wakionesha katika kuisaidia Jamhuri ya Msumbiji kupambana na ugaidi.

“Lazima tuungane kwa pamoja na kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Msumbiji inakuwa na Amani na Usalama……hivyo basi ni jukumu letu sisi sote katika kuhakikisha wananchi wa Msumbiji wanakuwa na amani kwani bila amani hakuna maendeleo,” amesema Rais Chakwera.

Awali akisoma tamko la pamoja, Katibu Mendaji wa SADC Bw. Elias Magosi amesema Wakuu wa Nchi na Serikali wameipongeza SADC kwa dhamira yake isiyoyumba ya kusimamia na kutetea amani na usalama, na kwa kutumia rasilimali zake katika kushughulikia na kupambana na ugaidi katika jimbo la Cabo Delgado.

Mkutano huo pia umepongeza hatua ya mshikamano iliyooneshwa kwa ahadi za chakula zilizotolewa na Jamhuri ya Malawi, Afrika Kusini na Zimbabwe ili kupunguza matatizo yanayowakabili wakimbizi  katika Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.

Rais wa Jamhuri ya Malawi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Lazarus Chakwera akifunga Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC Msumbiji 



Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC Msumbiji 




Mkutano ukiendelea


Wakuu wa Nchi na Wawakilishi wa Wakuu wa nchi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Jamhuri ya Msumbiji na Nchi zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC Msumbiji 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.