Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amesaini Kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha Rais wa UAE, Sheikh Khalifa bin Zayed bin Sultan Al Nahyan katika Ubalozi wa nchi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Friday, May 20, 2022
Thursday, May 19, 2022
Balozi wa Tanzania, Kuwait Awasilisha Hati za Utambulisho
Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhe. Said Mussa akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Naibu Amiri na Mwanamfalme wa Kuwait, Sheikh Mishal Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah jijini Kuwait. |
Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Mhe. Said Mussa akiwa katika mazungumzo na Naibu Amiri na Mwanamfalme wa Kuwait, Sheikh Mishal Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah jijini Kuwait baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho. |
Tuesday, May 17, 2022
BALOZI MULAMULA ATETA NA UJUMBE WA WAFANYABIASHARA SWITZERLAND
Na Mwandishi Wetu, Dar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Nchini Switzerland katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Balozi Mulamula ameuhakikisha ujumbe wa wafayabiashara hao kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ni salama na hivyo wasisite kuwekeza.
“Serikali imejitahidi sana kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hivyo nawasihi kutumia fursa hiyo kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo, kilimo, nishati, madini na nyinginezo," alisema Balozi Mulamula
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya 'Global Network', Bw. Stefan Barny emeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa maboresho makubwa katika sekta ya biashara na uwekezaji.
“Mazingira ya biashara hapa Tanzania nilikuwa nayasikia tu, ila baada ya kuja na kuonana pamoja na kujadiliana na wadau wa sekta za biashara na uwekezaji tumeridhishwa na mazingira ya biashara hapa Tanzania,” alisema Bw. Barny.
Bw. Barny ameongeza kuwa atawashawishi wafanyabiashara wenzake kutoka Uswisi kuja kuwekeza Tanzania kwan fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana Tanzania ni nyingi.
“Tumepanga kuwekeza katika sekta ya kilimo hasa katika sekta za kilimo hasa katika usindikaji wa mazao ya chakula, biashara na uwekezaji, madini na nishati....tumepanga kufungua kiwanda rasmi hapa Tanzania mwakani,” aliongeza Bw. Barny
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Balozi wa Switzerland hapa Nchini, Mhe. Didier Chassot, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga
Monday, May 16, 2022
WAZIRI MULAMULA ASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO U.A.E
Na Mwandishi wetu, Dar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), nchini kufuatia kifo cha Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Sheikh Khalifa bin Zayed Al-Nahyan kilichotokea tarehe 13 Mei 2022.
Baada ya kusaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa UAE nchini, Jijini Dar es Salaam Balozi Mulamula ametoa salamu za pole kwa Serikali ya UAE na kuwasihi wananchi wake kuendelea kuwa watulivu wakati huu wa msiba wa kuondokewa na kiongozi wao.
“Kusaini kitabu cha maombolezo ni ishara ya ushirikiano, umoja na undugu wetu na ndugu zetu wa UAE. Kifo cha Rais wa UAE, Sheikh Khalifa bin Zayed Al-Nahyan kimewagusa pia Watanzania kwa kuwa Tanzania na UAE zina uhusiano mzuri,” alisema Balozi Mulamula.
Aliyekuwa Rais wa UAE, Sheikh Khalifa bin Zayed Al-Nahyan alifariki dunia tarehe 13 Mei, 2022 akiwa na umri wa miaka 73 baada ya kuugua kwa muda.
Friday, May 13, 2022
UNAIDS YAPONGEZA JITIHADA ZA SERIKALI KUKABILIANA NA UKIMWI
Na Mwandishi wetu, Dar
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ukimwi (UNAIDS) limepongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mkazi wa UNAIDS nchini, Dkt. Leo Zekeng alipoagana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini.
Dkt. Zekeng amepongeza jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi hasa katika eneo la utoaji wa elimu kwa jamiii, kuanzishwa kwa Sera ya kudhibiti Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI pamoja na mikakati mbalimbali ya kupambana na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
“Nilipowasili Tanzania miaka mitano iliyopita takriban asilimia 62 ya Watanzania walikuwa wanafahamu hali ya afya zao hasa kwa ugonjwa wa UKIMWI, ila sasa nafurahi kuwa takribani asilimia 90 ya Watanzania wanafahamu hali ya afya zao, hili ni jambo kubwa sana katika jamii,” alisema Dkt. Zekeng.
Dkt. Zekeng amesema malengo ya UNAIDS ni kuhakikisha kuwa kufikia mwaka 2025 hakutakuwa na mtoto atakayezaliwa na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Akizungumza katika tukio hilo, Balozi Mulamula amempongeza Dkt. Zekeng kwa kazi nzuri ya kutoa elimu na kampeni dhidi ya Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ambapo kupitia kampeni hizo maambukizi ya ugonjwa huo nchini yamepungua kwa kiasi kikubwa.
“Elimu kuhusu maambukizi ya Virusi vya UKIMWI imekuwa msaada mkubwa katika jamii yetu, tunawashukuru UNAIDS kwa misaada ya dawa hasa ARVs pamoja na kampeni mbalimbali za kuelimisha jamiii juu ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI ambapo hadi sasa jamii imepata uelewa wa kujikinga na ugonjwa huo na maambukizi yamepungua kwa kiasi kikubwa,” alisema Balozi Mulamula.
Balozi Mulamula ameongeza kuwa miaka ya nyuma kulikuwa na unyanyapaa mkubwa katika jamii zetu lakini kutokana na elimu kuhusu maambukizi ya virusi vya UKIMWI pamoja na kampeni mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na UNAIDS kwa umma zimesaidia kupunguza unyanyapaa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi nchini.
Aidha, Waziri Mulamula amemsihi Dkt. Zekeng kuwa balozi mzuri wa Tanzania kokote aendako Duniani ambapo Dkt. Zekeng ameahidi kuwa balozi mzuri wa Tanzania na kusisitiza kuwa Tanzania ni nyumbani kwake hivyo wakati wote atakuwa balozi mzuri.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiagana na Mkurugenzi Mkazi wa UNAIDS nchini, Dkt. Leo Zekeng katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Thursday, May 12, 2022
SERIKALI YAELEZEA MAFANIKIO ZIARA ZA RAIS MAREKANI, UGANDA NA ROYAL TOUR
Na Mwandishi Wetu, Dar
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, amefafanua mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, nchini Marekani iliyojumuisha uzinduzi wa Filamu ya “Tanzania; The Royal Tour." Pamoja na ziara ya Rais nchini Uganda.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Bi. Yunus amesema ziara ya Rais nchini Marekani imekuwa na faida ya kusainiwa kwa mikataba saba kati ya kampuni za Marekani na Tanzania zenye lengo la kufanya biashara na uwekezaji nchini yenye gharama za zaidi ya shilingi Trilioni 11.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameelezea ziara ya Rais nchini Uganda ambayo iliwezesha kufanyika kwa mkutano maalum na wadau wa sekta za mafuta na gesi kuhusiana na ujenzi wa bomba la mafuta.
"Tulikuwa na mkutano maalum juu ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania, tayari hatua ya ulipaji fidia kwa wananchi imekamilika na ujenzi wa bomba hilo utaanza hivi karibuni", alisema Balozi Mulamula.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Rais ya kuitangaza Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi, amesema Filamu ya Royal Tour imeonesha mafanikio makubwa sana na kwa sasa filamu hiyo imeendelea kusambazwa katika vituo vya televisheni karibu 300 kati ya 350 nchini Marekani na kwa hapa nchini tayari filamu hiyo imesambazwa katika vituo vyote vya televisheni.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema filamu ya Royal Tour ina manufaa ya moja kwa moja kwa Taifana inatarajiwa kuleta wawekezaji, watalii na wafanyabiashara na kuongeza kuwa wao kama Wizara wameandaa mkutano na wadau ili kupanga mikakati ya kuwekeza katika sekta ya utalii.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB), Bw. Amos Nko amesema TTB inatangaza kwa kasi vivutio vya utalii ili kuvutia watalii wengi kuja nchini.
MWAKILISHI MKAZI WA AfDB AWASILISHA BARUA ZA UTAMBULISHO
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Bibi. Patricia Laverley amewasilisha Barua za Utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Libarata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Baada ya kupokea barua za utambulisho, viongozi hao pamoja na mambo mengine, walijadiliana masuala ya miundombinu endelevu pamoja na uboreshaji wa mazingira katika sekta binafsi.
Bibi. Laverley amemhakikishia Balozi Mulamula ushirikiano wa kutosha kutoka AfDB katika kuchochea utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na bank hiyo hapa nchini.
Nae Balozi Mulamula amemhakikishia ushirikiano wa kutosha kutoka Serikalini wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini na kuonmgeza kuwa AfDB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya Tanzania jambo ambalo ni ishara ya uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na bank hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Libarata Mulamula akipokea barua za utambulisho kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Bibi. Patricia Laverley katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Libarata Mulamula akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa AfDB nchini Tanzania, Bibi. Patricia Laverley katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Libarata Mulamula na Mwakilishi Mkazi wa AfDB nchini Tanzania, Bibi. Patricia Laverley yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Libarata Mulamula akiagana na Mwakilishi Mkazi wa AfDB nchini Tanzania, Bibi. Patricia Laverley yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
TANZANIA, JAMAICA KUONGEZA MAENEO MAPYA YA USHIRIKIANO
Na Mwandishi Wetu, Dar
Serikali ya Tanzania na Jamaica zimeahidi kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za utalii, biashara na uwekezaji pamoja na elimu kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Jamaica Mhe. Kamina Smith katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
“Leo nimekutana na Mhe. Smith na tumejadili na kudhamiria kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za utalii, biashara na uwekezaji, elimu, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi pamoja na vijana
Tanzania na Jamaica tumedhamiria kufanya kazi kwa karibu katika kutafuta njia bora ya kufungua fursa mpya kwa maslahi ya mataifa yote mawili,” alisema Balozi Mulamula
Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Jamaica Mhe. Kamina Smith amesema kuwa Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na Jamaica ambapo uhusiano huo umekuwa ni chachu ya maendeleo inayopelekea kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za utalii, biashara na uwekezaji na elimu.
“Ushirikiano uliopo baina ya mataifa yetu mawili umekuwa chachu ya maendeleo na lengo la ushirikiano huu ni kukuza, kuendeleza na kuimarisha uchumi wetu,” alisema Mhe. Smith
Katika tukio jingine, Waziri Mulamula amekutana na Kufanya Mazungumzo na Balozi wa Misri nchini, Mhe. Mohamed Gaber Abouelwafa.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala ya kuendeleza na kuimarisha uhusiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, elimu, pamoja na afya.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Jamaica, Mhe. Kamina Smith katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Jamaica, Mhe. Kamina Smith akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Jamaica, Mhe. Kamina Smith yakiendelea katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza Balozi wa Misri nchini, Mhe. Mohamed Gaber Abouelwafa walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza Balozi wa Misri nchini, Mhe. Mohamed Gaber Abouelwafa walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Misri nchini, Mhe. Mohamed Gaber Abouelwafa yakiendelea katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
WAZIRI WA ULINZI AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA AU KUHUSU MASUALA YA ULINZI NA USALAMA
Mhe. Dkt. Stergomena Tax
(Mb), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kisekta wa Mawaziri wenye dhamana ya
kusimamia Ulinzi, Amani na Usalama kutoka Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika
uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 12 Mei, 2022.
Mkutano huu ambao ni wa
kwanza kufanyika ana kwa ana tangu mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19 mwaka 2020, ulitanguliwa
na Mkutano wa Wataalam ambao ulifanyika tarehe 09 na 10 Mei, 2022 na kufuatiwa
na Mkutano wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi, Amani na Usalama ambacho uliofanyika tarehe
11 Mei, 2022.
Pamoja na mambo mengine,
mkutano huo unafanyika kwa lengo la kujadili ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika,
Mashirika ya Kikanda na Nchi Wanachama kuhusu Majeshi ya Akiba ya Afrika. Pia,
mkutano utapitia na kupitisha Sera mbili kuhusu umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa
ulinzi wa watoto na haki zao wakati wa Operesheni za Kulinda Amani barani
Afrika (Child Protection in African Union Peace Support Operations (2021) and
Mainstreaming Child Protection in the African Peace and Security Architecture).
Kadhalika, mkutano huo ni
sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Umoja wa Afrika kuhusu Ugaidi na Mabadiliko ya Serikali kinyume cha Katiba
ambao umepangwa kufanyika Malabo, Guinea ya Ikweta tarehe 28 Mei, 2022.
Ujumbe wa Mhe. Waziri Tax unamjumuisha pia Mhe. Hamad Masauni (Mb), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Nyakoro Sirro na Maafisa wengine Waandamizi wa Serikali.
Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kisekta wa Mawaziri wenye dhamana ya kusimamia Ulinzi, Amani na Usalama kutoka Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 12 Mei, 2022. Pichani ni Wajumbe walioshiriki Mkutano huo akiwemo Dkt.Tax |
Wednesday, May 11, 2022
WADAU WA UTALII WATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUTANGAZA UTALII
Na Mwandishi wetu, Dar
Wadau wa Utalii watakiwa kutumia ubunifu zaidi katika kutangaza vivutio vya utalii wa ndani ili kukuza sekta ya utalii na kuongezea pato la taifa.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga alipotoa salamu za Wizara katika Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022 lililofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
“Kuna mambo yanayojitokeza katika mazingira ya sasa kwenye sekta ya utalii ambayo ni muhimu sana kuhusisha ubunifu wa teknolojia katika kutangaza vivutio vya utalii,” alisema Balozi Kasiga .
Balozi Kasiga ameeleza kuwa haiwezekani kuendelea kutangaza utalii kwa njia tulizokuwa tunatumia zamani, ndiyo maana wabunifu wa teknolojia wametuonesha mchango wa teknolojia katika kutangaza vivutio vya utalii na sasa tunaona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amejadiliwa sana kutokana na kutangaza uzinduzi wa filamu ya ‘Royal Tour’ ambayo imeelezea kwa undani vivutio vya utalii nchini kwa teknolojia ya juu zaidi.
Pamoja na mambo mengine, Balozi Mindi amewasihi wabunifu kuendelea kutumia teknolojia kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.
Kupitia kongamano hilo washiriki wamejadili namna ubunifu na teknolojia vinaweza kutumika kama njia mbadala ya kutangaza vivutio vya utalii na kuwavutia watanzania waweze kutembelea vivutio hivyo.
Aidha, kupitia Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022, teknolojia ya ‘Safari Wallet’ imezinduliwa na kijana wa Kitanzania ambapo inapatikana katika tovuti ya ‘Safari Wallet’ na inatumika kuwasaidia wadau wa utalii kuchagua sehemu za kutembelea kwa urahisi na haraka zaidi vivutio vya utalii nchini
Balozi Kasiga ameeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itajitahidi kuiwasilisha teknolojia ya ‘safari wallet’ katika nyanja za kimataifa ikiwemo ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Ukanda wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na mataifa mengine ili kuweza kutangaza zaidi vivutio vya utalii nchini.
Naye Naibu Balozi wa Uholanzi nchini, Mhe. Job Runhaar amesema teknolojia ni nyenzo muhimu katika kutangaza sekta ya utalii nchini.
Sisi kama wadau wa teknolojia tumefurahishwa sana na uzinduzi wa teknolojia ya Safari Wallet. Teknolojia hii ikitumika vizuri kutangaza vivutio vya utalii itasaidia kuchangia ongezeko la mapato ya serikali na maendeleo ya wabunifu kwa ujumla,” amesema Mhe. Runhaar
Kongamano la ubunifu limeandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) linaloendelea katika wiki ya Ubunifu lililozinduliwa Mei 10, 2022 Jijini Dar es Salaam ambapo wadau wa ubunifu walipata nafasi ya kujadili masuala yanayohusu ubunifu na hatua wanazochukua kuendeleza sekta ya ubunifu ili kuwa na tija kwa Watanzania.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akisalimiana na Naibu Balozi wa Uholanzi nchini, Mhe. Job Runhaar katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Naibu Balozi wa Uholanzi nchini, Mhe. Job Runhaar akiongea na washiriki wa Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022 (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam
|
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akiongea na waandishi wa Habari katika Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022 |
Baadhi ya wanajopo walioshiriki Kongamano la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022 |
BALOZI ADELARDUS KILANGI AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA RAIS WA BRAZIL
Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Mhe. Prof. Adelardus Kilangi akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Brazil, Mhe. Jair Bolsonaro wakati wa hafla iliyofanyika hivi karibuni katika Ofisi za Rais za Palacio Do Planalto zilizopo Brasilia, Brazil |
Mhe. Rais Bolsonaro akionesha Hati za Utambulisho za Mhe. Balozi Kilangi mara baada ya kuzipokea wakati wa hafla iliyofanyika hivi karibuni katika Ofisi za Rais za Palacio Do Planalto zilizopo Brasilia, Brazil |
Mhe. Balozi Kilangi akiwa katika mazungumzo na Mhe. Rais Bolsonaro mara baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho |
Mhe. Balozi Kilangi akiwa na Mhe. Rais Bolsonaro |
Tuesday, May 10, 2022
BALOZI SOKOINE ATETA NA BALOZI MALAWI, COMORO
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amekutana kwa mazungumzo Balozi wa Malawi nchini, Mhe. Andrew Kumwenda pamoja na Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Dkt. Ahamada El Badaoui leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Awali akizungumza na Balozi wa Malawi nchini, Balozi Sokoine amemhakikishia ushirikiano wa Wizara na Serikali kwa ujumla wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.
Kwa Upande wake Balozi wa Malawi nchini, Mhe. Kumwenda ameishukuru Serikali kwa ushirikano inaompatia tangu alipowasili nchini na ameahidi kuendeleza uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Malawi kwa maslahi ya pande zote mbili.
Katika tukio jingine, Balozi Sokoine amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini, Dkt. Ahamada El Badaoui ambapo pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Comoro.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akizungumza na Balozi wa Malawi nchini, Mhe. Andrew Kumwenda katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Mazungumzo ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Balozi wa Malawi nchini, Mhe. Andrew Kumwenda yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akizungumza na Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Dkt. Ahamada El Badaoui leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam |
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiagana na Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Dkt. Ahamada El Badaoui baada ya kumaliza mazungumzo yao |