Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) utafanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini kuanzia tarehe 16 hadi 19 Julai, 2022.
Mkutano huo umetanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu unaofanyika tarehe 16 na 17 Julai 2022 ambapo ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kamati hii unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma M. Rajab ambaye anamwakilisha Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine.
Mkutano wa 24 unalenga pamoja na mambo mengine kupokea na kujadili agenda mbalimbali zikiwemo mapitio ya utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 23 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya kanda; na tathmini ya hali ya Ulinzi na Usalama katika Kanda pamoja na Tathmini ya athari zitokanazo na mgogoro unaoendelea katika bara la Ulaya.
Viongozi wengine kutoka Tanzania wanaoshiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu ni pamoja na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Lt. Jenerali Salum Othman, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.
Ujumbe wa Tanzania kwa ngazi ya Mawaziri unatarajiwa kuongozwa na Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye ataambatana na Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Sehemu ya Ujumbe wa Serikali ya Angola ukishiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu |
Sehemu ya Ujumbe wa Serikali ya Botswana ukishiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu |
Viongozi wengine akiwemo Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala (kushoto) wakati wa kikao cha maandalizi |
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Bw. Shija akifuatilia kikao cha maandalizi cha ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu |
Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akishiriki kikao cha maandalizi kilichohusisha ujumbe wa Tanzania. |