Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewasisitiza Diaspora wote Duniani kutumia huduma za kifedha kupitia kwa watoa huduma waliosajiliwa ili kuendelea kuchangia uchumi wa Tanzania.
Dkt. Tax ametoa wito huo jijini Dar es Salaam aliposhiriki uzinduzi wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliyoanzishwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kupitia huduma ya kutuma fedha ya M-Pesa.
Amesema, upo umuhimu mkubwa kwa Diaspora kutumia huduma za kifedha zilizosajiliwa ili kuhakikisha usalama wa fedha zao na kuweka kumbukumbu sawa. Amesema kwa mujubu wa Takwimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania Diaspora walichangia uchumi wa Taifa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 30 mwaka 2019 na mwaka 2021 Diaspora walichangia uchumi wa Taifa kwa Dola za Kimarekani milioni 569 sawa na kuchangia asilimia 0.8 ya pato la Taifa.
Mhe. Dkt. Tax ameipongeza Kampuni ya Vodacom kwa kuwekeza katika ubunifu na kuboresha huduma zao wakati wote ili kuendana na mahitaji ya wananchi kulingana na mabadiliko ya Teknolojia.
Amesema anaipongeza Kampuni hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiunganisha Afrika kupitia huduma zao ambapo kwa sasa wamepanua wigo kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kuongeza ukanda wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) jambo ambalo litawawezesha Diaspora kwenye maeneo hayo kutuma na kupokea fedha pasipo kikwazo chochote.
“Sekta ya fedha ni sekta muhimu katika nchi yoyote, Serikali inaona jambo hili ni kubwa kwa sababu ya umuhimu wa sekta ya fedha lakini kwa kutambua kwa sasa dunia ipo katika uchumi wa kidigitali. Uchumi wa kidigitali unafanya kazi kidigitali hivyo nawasihi Diaspora kutumia huduma hii ili kuweza kuchangia maendeleo ya taifa kwa kuwa benki na taasisi nyingine zinazotoa huduma za kifedha zimerahisisha biashara na uwekezaji na shughuli za kiuchumi kwa ujumla,” alisema Dkt. Tax.
Kadhalika Mhe. Dkt. Tax ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kutoa miongozo mbalimbali inayowawezesha watoa huduma za fedha nchini kuandaa huduma zenye manufaa kwa wanannchi na kuahidi Serikali kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi ili kutimiza lengo la kuwainua wananchi kiuchumi kupitia huduma mbalimbali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Vodacom M-pesa, Bw. Epimack Mbeteni amesema kuzinduliwa kwa huduma ya M-Pesa katika ukanda wa SADC kumetoa fursa ya kuongeza wigo wa kutuma na kupokea pesa katika nchi nyingi zaidi barani Afrika hususan nchi za SADC.
“Wateja wetu wanaweza kupokea na kutuma fedha katika ukanda wa Sadc, sasa tumeiunganisha Afrika na M-Pesa, jambo hili litachangia ukuaji wa uchumi wa taifa letu,” amesema Bw. Mbeteni
Bw. Mbeteni ameongeza kuwa uzinduzi wa huduma hiyo utarahisisha ufanyaji wa biashara na huduma nyingine za kijamii. Uzinduzi wa huduma hiyo uliongozwa na kauli mbiu ya “Dunia Kijiji, Afrika ni M-Pesa”. Katika uzinduzi huo, Dkt. Tax aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Godwin Gondwe.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwasilisha hotuba ya ufunguzi aliposhiriki uzinduzi wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliyoanzishwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kupitia huduma ya kutuma fedha ya M-Pesa
Mkurugenzi wa Vodacom M-pesa, Bw. Epimack Mbeteni akiongea na washiriki wakati wa uzinduzi wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) |
Washiriki wakifuatilia mkutano wa uzinduzi wa wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za SADC |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za SADC |
Washiriki wakifuatilia mkutano wa uzinduzi wa wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za SADC |