Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) amekitaka Chuo cha Diplomasia (CFR) kuongeza wigo wa program zake ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadae.
Dkt. Tax ametaka ongezeko hilo la wigo lifanyike kwa kuwatumia wataalamu wa ndani na nje ya chuo ambao wana uwezo na maono mapana.
Waziri Dkt. Tax ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya 25 ya Chuo hicho ambapo aliwatunuku vyeti wahitimu 990 katika ngazi ya Astashahada ya Juu, Shahada ya kwanza, Stashahada na Astashahada katika fani ya diplomasia.
“Mahitaji ya utaalamu katika Diplomasia yanaendelea kupanuka, kulingana na mahitaji yanayoendelea kujitokeza Kitaifa na Kimataifa,hususan katika Diplomasi ya Uchumi. Hivyo ni muhimu kwa Chuo kupanua progamu zake ili kukidhi mahitaji ya sasa, na siku za usoni. Hatua hii iende sanjari na kuwatumia wataalamu ndani ya Chuo, na nje ya Chuo, wenye uwezo na maono mapana,” alisema Dkt. Tax.
Dkt. Tax amekipongeza Chuo cha CFR kwa kazi nzuri wanayoifanya na kutoa wahitimu wenye ueledi na mahiri wanaotambulika kitaifa na kimataifa na kuwataka wahakikishe wanatekeleza mikakati yao kikamilifu na hivyo kukamilisha lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho
Amewataka kuhakikisha wanashirikiana na taasisi nyingine ili kuongeza elimu na ujuzi na hivyo kunufaisha wanafunzi wao hasa ikizingatiwa kuwa dunia ya sasa inahitaji ushirikiano na taasisi nyingine.
Amesema CFR kimetoa wahitimu mahiri na ni matarajio ya Serikali kuwa kila mtumishi atatimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuzingatia maadili ya kiutumishi ili kuendelea kutoa wahitimu wenye ubora wa kitaaluma wenye maadili mema na mwenendo mwema.
Amewataka wanachuo wanaobaki kuendelea kujifunza kwa bidii na kuiga mfano wa wanaohitimu wa tabia njema na mwenendo mwema na kujituma katika masomo yao ili kuendelea kuilinda sifa nzuri ya chuo tangu kuanzishwa kwake.
Amekitaka chuo kuongeza mafunzo ya strategia, kufanya tafiti mahsusi na kutoa ushauri kwa serikali na wadau wengine katika sehemu ya strategia na diplomasia na kuweka mikakati ya pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali na wadau wake jinsi ya kuwa na mwelekeo sahihi wa kukabiliana na changamoto zinazoikabili Tanzania na dunia kwa ujumla.
“Chuo lazima kiongeze mafunzo ya strategia, kifanye tafiti mahsusi na kutoa ushauri kwa serikali na wadau wengine katika sehemu ya strategia na diplomasia. Tafiti kama hizo zitachangia kuimarisha diplomasia na kuweka mikakati ya pamoja ya jinsi ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili Tanzania na dunia kwa ujumla,’ alisema Dkt. Tax
Amekitaka chuo cha CFR kuhakikisha kinaelimisha taifa kupitia mijadala na makongamano ili kupanua uelewa na kujenga uzalendo kwa kujumuisha jamii katika masuala ya strategia na diplomasia na kuongeza kuwa diplomasia na strategia ni vitu vipana, na vyote vinagusa kila eneo na kwamba ni vizuri Chuo kikajipanga kwendana na dunia inavyokwenda.
“Chuo hiki hakina budi kuendelea kuelimisha taifa kwa mijadala na makongamano kwa lengo la kupanua uelewa kujenga uzalendo na kujumuisha jamii katika masuala ya strategia na diplomasia, haya hayako nje ya wigo wa shughuli zenu, diplomasia ni kitu kipana na strategia ni kitu kipana pia na vyote vinahusu karibu kila eneo, kwa hiyo ni vizuri tukaenda na dunia inavyokwenda, sasa tunaongelea diplomasia ya uchumi lakini pia ipo diplomasia ya ulinzi na katika maeneo mbalimbali, tujipange vyema kwa kujua dunia inaenda namna gani na mafunzo tunayotoa yanaendaje katika kukabiliana na changamoto tulizonazo katika eneo hili,” alisisitiza Dkt. Tax