Tuesday, November 29, 2022

SERIKALI, UNAIDS WAZINDUA RIPOTI YA HALI YA UKIMWI DUNIANI 2022

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Ukimwi (UNAIDS) wamezindua Ripoti ya Ukimwi Duniani kwa Mwaka 2022 leo Jijini Dar es Salaam.

Hafla ya Uzinduzi wa ripoti hiyo imeongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Mhe. George Simbachawene kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa 

Wakati wa uzinduzi huo Mhe. Simbachawene amesema idadi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini yamepungua kwa asilimia 50 kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi 54,000 mwaka 2021. 

Waziri Simbachawene amesema pia idadi ya vifo vinavyotokana na Virusi vya Ukimwi kupungua kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka 64,000 mwaka 2010 hadi 29,000 mwaka 2021.

“Tanzania imeongeza juhudi za kuzuia maambukizi ya VVU ambapo maambukizi mapya katika miaka minne (2017-2021) iliyopita yalipungua kwa asilimia 38,” alisema Simbachawene. 

“Kama nchi tunaungana na kukubaliana na kaulimbiu ya Siku ya UKIMWI Duniani ya mwaka 2022 ya ‘kukusekana kwa usawa ni hatari’ ili kuhakikisha kuwa kila mtu nchini Tanzania anapata huduma bora za afya na VVU. Ili kukabiliana na tofauti katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za afya, Tanzania imeandaa muswada wa bima ya Afya kwa Wote kwa lengo la kuhakikisha Huduma ya Afya kwa Wote. Dhamira ya Mkakati wa Kitaifa wa Afya wa 2021 - 2026 ni kutoa huduma za afya endelevu zenye viwango vinavyokubalika kwa wananchi wote bila vikwazo vya kifedha, kwa kuzingatia usawa wa kijiografia na kijinsia, aliongeza Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la UKIMWI (UNAIDS), Bi. Winnie Byanyima amesema kwa mujibu wa ripoti mpya ya UNAIDS iliyozinduliwa inabainisha kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kukabiliana na kukosekana kwa usawa katika mapambano dhidi ya UKIMWI duniani. 

“Tunahitaji kushughulikia changamoto ya kukosekana kwa usawa kwa wanawake hasa wenye VVU. Asilimia 50 ya wanawake wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia wanauwezekano wa kupata VVU. Katika nchi 33 duniani tangu mwaka 2015 - 2021 sawa na asilimia 41 ya wanawake walioolewa wenye umri wa miaka 15 - 24 wanaweza kufanya maamuzi yao wenyewe juu ya afya ya ngono. Njia pekee yenye ufanisi wa kukomesha unyanyasaji kwa waathirika wa UKIMWI na kufikia malengo ya maendeleo endelevu ni kuhakikisha afya, haki na ustawi wa pamoja vinapatikana kwa wakati,” alisema Bi. Byanyima

Tanzania imekuwa imefanikiwa kupunguza maambukizi na vifo vitokanavyo na ukimwi kwa asilimia 50, jitihada hizo zimeifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano duniania katika udhibiti wa ugonjwa huu, ameongeza Bi. Byanyima 

Bi. Byanyima ameongeza viongozi wa mataifa mbalimbali dunia wanapaswa kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa haki, huduma, sayansi bora na dawa, kwani kwa kufanya hivyo hakutasaidia tu waliotengwa bali pia kusaidia kila mmoja.

Nae mwakilishi wa Baraza la watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi Tanzania (Nacopha), Bi. Bahati Haule amesema kuna umuhimu wa jamii kupewa elimu dhidi ya masuala ya usawa na unyanyapaa kwa waathirika wa VVU kwa kuwa wengi wa walioathirika wamekuwa wakitengwa na kunyanyapaliwa katika jamii zinazowazunguka.

“Ni wakati muafaka kwa dunia na jamii zetu zinazotuzunguka kuungana pamoja katika kupinga unyanyasji dhidi ya waathirika wa VVU pamoja na kuhakikisha usawa katika haki na huduma vinapatikana, alisema Bi. Bahati 

Ripoti ya Siku ya Ukimwi Duniani 2022 inaongozwa na kauli mbiu ambayo ni kukusekana kwa usawa ni hatari.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Mhe. George Simbachawene akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Ukimwi Duniani kwa Mwaka 2022 leo Jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel (kulia) na Mkurugenzi Mkaazi wa UNAIDS nchini Tanzania Bw. Martin Odiit 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la UKIMWI (UNAIDS), Bi. Winnie Byanyima, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya Ukimwi Duniani kwa Mwaka 2022. Kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel na kushoto ni mwakilishi wa Baraza la watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi Tanzania (Nacopha), Bi. Bahati Haule.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Mhe. George Simbachawene akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya Ukimwi Duniani kwa Mwaka 2022 Jijini Dar es Salaam

Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Mhe. George Simbachawene pamoja naMkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la UKIMWI (UNAIDS), Bi. Winnie Byanyima katika  uzinduzi wa Ripoti ya Ukimwi Duniani kwa Mwaka 2022 Jijini Dar es Salaam









No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.