Thursday, November 10, 2022

MABALOZI WAFANYA ZIARA HOSPITALI YA CCBRT

Mabalozi wanaoziwakilisha nchi za Palestina, Indonesia na Vietnam hapa nchini wamefanya ziara katika Hospitali ya CCBRT na kujionea utoaji wa huduma za afya na kazi mbalimbali zinazofanywa na Hospitali hiyo pamoja na kuangalia maeneo ya ushirikiano.

Ziara ya mabalozi hao imefanyika leo Jijini Dar es Salaam ambapo mabalozi waliofanya ziara katika hospitaali hiyo ni Balozi wa Palestina nchini, Mhe. Hamdi Mansour AbuAli, Balozi wa Indonesia nchini, Mhe. Triyogo Jatmiko na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien.

Akiongea wakati wa ziara hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Bi. Brenda Msangi amesema kuwa ziara ya mabalozi hao imelenga kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazotolewa na hospitali hiyo na kwamba CCBRT inaamini kuwa baada ya ziara hiyo mabalozi watapata fursa ya kujionea maeneo ya ushirikiano baina ya nchi zao hospitali hiyo.

“Tunategemea baada ya ziara hii mabalozi wataona maeneo ya ushirikiano, sisi kama CCBRT tuna maeneo matatu ambayo tunapenda kushirikiana nao, eneo la kwanza ni utoaji wa huduma, vifaa na vifaa tiba, na mwisho ni kuwajengea uwezo wataalamu wetu. Maeneo yote haya ni muhimu hasa ukizingatia CCBRT inatoa huduma bobezi na za kibingwa,” amesema Bi. Msangi

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza amesema kuwa mabalozi wamefanya ziara katika hospitali hiyo kwa lengo la kujionea utoaji wa huduma mbalimbali zinazotolewa na CCBRT na kupata fursa kuona maeneo ya ushirikiano baina ya nchi zao na CCBRT.

“Katika ziara ya mabalozi hapa CCBRT, mabalozi wameonesha kuridhishwa na shughuli zinazofanywa na hospitali hii, na baada ya ziara hii watawasiliana na nchi zao na kuona maeneo ya ushirikiano katika kuboresha zaidi sekta ya afya,” amesema Balozi Mgaza.  

Naye Balozi wa Palestina nchini, Mhe. Hamdi Mansour AbuAli amesema ameridhishwa na huduma zinazotolewa na CCBRT katika kuboresha afya za watanzania nchini na kuahidi kuwasiliana na serikali ya Palestina kuona ni jinsi gani serikali yake inaweza kushirikiana na hospitali hiyo katika kuboresha sekta ya afya nchini Tanzania. 

“Nimekuwa nikipita maeneo haya mara kwa mara lakini sikujua kuwa huduma nzuri zinatolewa hapa CCBRT, nawapongeza kwa jitihada hizi za kuuelimisha umma kuhusu magonjwa mbalimbali na njia za kuyakabili. Naahidi baada ya ziara hii nitawasiliana na Serikali yangu na kuona ni maeneo gani tunaweza kushirikiana katika kuboresha sekta ya afya,” amesema Balozi AbuAli

Kadhalika, Balozi wa Indonesia nchini, Mhe. Triyogo Jatmiko amesema kazi inayofanywa na hospitali ya CCBRT katika kuwahudumia watanzania hususan akina mama wenye changamoto ya fistula na watu wenye ulemavu wa viungo ni kazi kubwa na inayoigusa jamii.

“Jitihada zinazofanywa na serikali ya Tanzania katika kuboresha vituo vya afya ni nzuri……nimeguswa na jinsi hospitali hii inavyowahudumia wananchi, baada ya ziara hii tutakaa na kuangalia maeneo ya ushirikiano,” amesema Balozi Jatmiko.

Ziara hiyo iliratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Hemed Mgaza pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Ceaser Waitara.

Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Bi. Brenda Msangi akizungumza na Balozi wa Palestina nchini, Mhe. Hamdi Mansour AbuAli, Balozi wa Indonesia nchini, Mhe. Triyogo Jatmiko na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Hemed Mgaza pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Ceaser Waitara pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa CCBRT. 

Mabalozi wakiwa katika kituo cha mabinti cha CCBRT wakati walipofanya zaira hospitalini hapo 

Mabalozi wakiwajulia hali akina mama wanaokabiliwa na changamoto ya Fistula katika hospitali ya CCBRT

Balozi wa Indonesia nchini, Mhe. Triyogo Jatmiko akisalimiana na mtoto anayetumia mguu wa bandia katika karakana ya viungo tiba saidizi na viungo bandia katika hospitali ya CCBRT wakati mabalozi walipofanya ziara hospitalini hapo. Wengine pichani ni Balozi wa Palestina nchini, Mhe. Hamdi Mansour AbuAli, Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien, Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Bi. Brenda Msangi, (Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Hemed Mgaza pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Ceaser Waitara) kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Balozi wa Palestina nchini, Mhe. Hamdi Mansour AbuAli akionesha mabalozi wenzake kitu wakati wa ziara ya mabalozi hao katika hospitali ya CCBRT 

Mabalozi wakiwa katika picha ya pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT Bi. Brenda Msangi pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Hospitali hiyo 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.