Friday, December 2, 2022

DKT. TAX AWATUNUKU SHAHADA MBALIMBALI WAHITIMU 7,777 WA CHUO KIKUU CHA DODOMA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma leo tarehe 02 Desemba 2022 ametunuku Shahada mbalimbali Wahitimu wa fani mbalimbali katika Mahafali ya 13 yaliyofayika katika Ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.

Dkt. Tax amewapongeza wahitimu wote kwa kuhitimu masomo yao kwa mafanikio na kuwataka kusherehekea ushindi wa kumaliza chuo kwa kiasi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mahafali hayo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Lugano Kusiluka amesema anapongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha elimu nchini na kuwataka watanzania kuendelea kumuunga mkono na kumuombea ili aendelee kuwa na maono makubwa ya kuliinua Taifa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu.

“Kwa niaba ya Menejimenti, Watumishi na Wanafunzi wote wa Chuo Kikuu cha Dodoma natoa pongezi kwa Mhe. Rais Samia kwa mageuzi makubwa ya kijamii na kiuchumi hapa Tanzania. Wajibu wetu ni kuendelea kumuunga mkono na kumuombea ili Mungu amlinde na kumpa maono makubwa zaidi kwa ajili ya Taifa hili” alisema Prof. Kusiluka.

Pia amesema anampongeza Mhe. Rais Samia kwa kumteua Dkt. Tax kuwa Mkuu wa Chuo hicho kwani tangu kuteuliwa kwake Chuo hicho kinakwenda mbele katika masuala mbalimbali ikiwemo uboreshaji elimu.

Amesema Chuo hicho kinaendelea kujiimarisha ili kutimiza lengo la kutoa elimu bora kwa Watanzania ambapo hivi sasa chuo kinaendelea kutekeleza maboresho mbalimbali kupitia mpango unaoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ambao pamoja na mambo mengine umejikita katika kuboresha mitaala, teknolojia na kujenga madarasa ya kutosha.

Ameongeza kusema kuwa, Chuo hicho kinaendelea kutoa wahitimu bora ambapo hivi karibuni Chuo hicho kimeshika nafasi ya kwanza kwa wanafunzi wa sheria kushinda kwenye mashindano ya Kimataifa ya Sheria katika masuala ya Kibinadamu kwa Kanda ya Afrika.

Aidha, amesema Chuo hicho kinaendelea kukamilisha usajili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo wa 2023/2024 na kwamba usajili huo ukikamilika Chuo kitakuwa na jumla ya wanafunzi 34,574 wa fani mbalimbali sawa na asilimia 94 ya lengo la Chuo hicho la kudahili wanafunzi 40,000.

Kadhalika aliwapongeza wahitimu wote na kuwaasa kuwa makini na kutumia taaluma waliyoipata kujiendeleza na kuliendeleza Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Prof. Rwekaza Mukandala amesema Baraza hilo ambalo ni chombo muhimu cha kusimamia utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali ya maendeleo ya Chuo, linayo nia thabiti ya kutekeleza Mpango Mkakati wa Chuo hicho wa Mwaka 2021/2025 pamoja na kukamilisha miradi yote ya maendeleo ya Chuo hicho.

Pia amewaasa wahitimu kuwa mabalozi na taswira ya Chuo hicho popote wanapokwenda kwa kuzingatia yale yote waliyojifunza na kuwapongeza kwa elimu waliyoipata ambayo alisema ni rasilimali yao ya kudumu ambayo hakuna wa kuwapokonya.

Mhe. Dkt. Tax ametunuku Shahada za Awali, Uzamili, Uzamivu, Stashahada na Astashahada kwa wahitimu takribani 7,777 wa fani mbalimbali wa Chuo hicho katika mahafali ya 13 yaliyofanyika kwa siku mbili Chuoni hapo kuanzia tarehe 01 hadi 02 Desemba 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma akitangaza kuwatunuku Shahada mbalimbali wahitimu wa Chuo hicho wakati wa sherehe ya Mahafali ya 13 yaliyofanyika chuoni hapo tarehe 1 na 2 Disemba 2022
Meza Kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Taifa ukiibwa kwenye sherehe ya mahafali ya 13 ya Chuo Kikuu cha Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (katikati), Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Lugano Kusiluka (kushoto) na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Prof. Rwekaza Mukandala (kulia) wakiwa katika maandamano ya Kitaaluma kwenye Mahafali ya 13 ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
Sherehe za Mahafali ya 13 ya Chuo Kikuu cha Dodoma yakiwa yanaendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma akiingia katika ukumbi wa Chimwaga wa Chuo Kikuu cha Dodoma kushiriki Mahafali ya 13 ya Chuo hicho
Sherehe za Mahafali ya 13 ya Chuo Kikuu cha Dodoma yakiwa yanaendelea

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.