Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewakaribisha wawekezaji kutoka Vietnam kuja nchini kuwekeza katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na Kilimo.
Mhe. Waziri Tax ameyasema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Vietnam na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo Mhe. Nguyen Manh Hung alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma hivi karibuni.
Mhe. Dkt Tax amesema Tanzania inathamini ushirikiano kati yake na Vietnam ambayo imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano na kwamba kupitia ushirikiano huo Tanzania imejipanga kunufaka katika sekta hiyo na nyingine zenye manufaa kati ya nchi hizi mbili.
Ameongeza kusema nchi hiyo ambayo tayari imewekeza kwenye sekta ya Mawasiliano hapa nchini kupitia Kampuni ya Simu ya Halotel, bado inakaribishwa kuwekeza zaidi katika sekta hiyo hususan kwenye miundombinu ya kidijiti na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuhakikisha wawekezaji wanafanikisha malengo yao lakini pia Taifa linanufaika kupitia uwekezaji.
“Tanzania inaendelea kujiimarisha katika Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi. Kama ulivyosema Mhe. Waziri, Vietnam ni miongoni mwa nchi 10 duniani zilizopiga hatua kubwa katika sekta hiyo, naendelea kuhimiza wawekezaji zaidi kutoka nchini kwako kuja kuwekeza kwenye sekta hiyo lakini pia na sekta nyingine kama Kilimo hususan kile cha biashara na usindikaji wa mazao ya kilimo” alisema Dkt. Tax.
Kwa upande wake, Mhe. Nguyen Manh Hung amepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali yanachangia maendeleo ya wananchi.
Akizungumzia uwekezaji kupitia kampuni ya Viettel ambayo ni kampuni mama ya mtandao wa simu wa Halotel hapa nchini, amesema nchi yake imewekeza mtaji wa takribani Dola bilioni moja katika miundombinu ya mtandao huo ambao umejikita kuwahudumia zaidi wananchi wa vijijini na kwamba hadi sasa Mtandao huo umeajiri watanzania 1,000.
Sehemu ya ujumbe ulioambatana na Mhe. Mahn Hung akiwemo Balozi wa Vietnam nchini Mhe. Nguyen Nam Tien (kulia) wakifuatilia mazungumzo |
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mazungumzo. Kushoto ni Bw. John Kambona, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.