Saturday, December 3, 2022

RAIS DKT. SAMIA AWATAKA WANAWAKE KUFANYA KAZI KWA BIDII

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasihi viongozi wanawake vijana kufanya kazi kwa bidii ili kufikia utekelezaji wa Ajenda 2030 ya Maendeleo Endelevu na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063. 

Mhe. Dkt. Samia ametoa wasaa huo wakati akifungua Kongamano la nne la Wanawake Vijana wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (AWLN) lililofanyika visiwani Zanzibar na kuwataka wanawake kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kuchangia maendeleo katika sekta mbalimbali kwenye jamii zao.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Samia amebainisha kuwa Tanzania inatambua na kuzingatia uwezo wa kitaaluma wa wanawake katika kufanya kazi na hivyo kupelekea idadi ya viongozi wanawake kuongezeka katika vyombo vya maamuzi (Bunge) kutoka asilimia 21.5 kwa mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 37 mwaka 2020. 

“Idadi ya Majaji wanawake imeongezeka kutoka aslimia 34 mwaka 2005 hadi aslimia 39 mwaka 2022, Mabalozi wanawake na Makamishna Wakuu kutoka asilimia 3 mwaka 2005 hadi asilimia 21 mwaka 2022, Wakuu wa Mikoa Wanawake wamepanda kutoka aslimia 10 mwaka 2005 hadi asilimia 23 mwaka 2022, pamoja na Wakuu wa Wilaya Wanawake wameongezeka kutoka asilimia 19 mwaka 2005 hadi 29 mwaka 2022,” alisema Dkt. Samia

“Tunataka kuhakikisha kwamba wanawake wanaingia kwenye masoko ya kikanda na kuyatumia masoko hayo kama hatua ya kwenda mbali zaidi hadi kwenye masoko ya nje,” aliongeza Rais Dkt. Samia

Kwa Upande wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la watu wa Ethiopia, Mhe. Sahle-Work Zewde amesema kuwa ni wakati muafaka kwa Bara la Afrika kufanya mabadiliko ya uongozi kwa kuwapa nafasi za uongozi wanawake vijana ili waweze kuchangia maendeleo katika katika jamii zao pamoja na kuwahamasisha wengine kuwa wanawake wanaweza.

“Tunaamini kuwa wanawake vijana wakiendelezwa na kupatiwa mafunzo na ujuzi wa taaluma mbalimbali wataongoza vyema zaidi kuliko ilivyo kwa sasa, mfano wakipatiwa mafunzo ya usuluhishi wa migogoro watakuwa na msaada mkubwa wa kuchagiza amani katika jamii zetu,” alisema Mhe. Zewde

Awali akiongea katika kongamano hilo, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Zlatan Milisic, amesema ni muhimu katika jamii wanawake kujumuishwa katika nafasi za maamuzi ili kupunguza migogoro katika jamii.

“Endapo wanawake vijana watashirikishwa katika hatua rasmi na zisizo rasmi za kufanya maamuzi ili kushughulikia changamoto mbalimbali katika jamii zetu itasaidia kuwajengea uwezo na kuwapatia maendeleo yao wenyewe,” alisema Bw. Millisci.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba ya ufunguzi wakati wa  Kongamano la nne la Wanawake Vijana wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (AWLN) lililofanyika visiwani Zanzibar 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la watu wa Ethiopia, Mhe. Sahle-Work Zewde akizungumza na washiriki wa Kongamano la nne la Wanawake Vijana wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (AWLN) lililofanyika visiwani Zanzibar  

Viongozi waandamizi wa Serikali wakifuatilia Kongamano

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini (UN), Bw. Zlatan Milisic akiwasilisha salamu za UN kwa washiriki wa Kongamano la AWLN 





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.