Monday, December 5, 2022

WAZIRI AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA MABALOZI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa Umoja wa Ulaya, Italia na Marekani na Uingereza katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Tax amekutana kwa nyakati tofauti na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfredo Fanti, Balozi wa Italia nchini Mhe. Marco Lombardi, Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Donald Wright pamoja na Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar. 

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Tax amejadili na mabalozi hao masuala ya kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zao hususan katika kutekeleza diplomasia ya uchumi, sekta ya kilimo, elimu, miundombinu, nishati, utalii, ulinzi na takwimu.

Waziri Tax amewahakikishia mabalozi hao utayari wa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuendelea kushirikiana na nchi zao kutukeleza diplomasia ya uchumi kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Serikali ya awamu ya sita imetoa kipaumbele katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi pamoja na kuendeleza ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta za kilimo, elimu, miundombinu, nishati, utalii, ulinzi,” alisema Dkt. Tax.

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Manfredo Fanti amesema Umoja wa Ulaya unaridhishwa na mazingira ya biashara nchini ambayo ni ishara kuwa wafanyabiashara kutoka nchi za umoja huo wataendelea kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali kwa maslahi ya pande zote mbili. 

Kadhalika Balozi wa Italia nchini Mhe. Marco Lombardi amesema Tanzania ni nchi yenye utulivu na uchumi wake umeendelea kuimarika jambo ambalo linawafanya waitaliano kuendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali. 

Balozi Lombardi ameongeza kuwa wawekezaji wengi wa Italia wako tayari kuwekeza katika sekta za kilimo, miundombinu, elimu, takwimu, uchumi wa bluu pamoja na kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Naye Balozi wa Marekani nchni, Mhe. Donald Wright amesema serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na kuhakikisha Tanzania inatekeleza na kufanikisha vipaumbele vyake ilivyojiwekea kijamii na kichumi hususan biashara na uwekezaji, nishati na utalii.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar, pamoja na mambo mengine, amesema serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza na kuimarisha uhusiano wake na Tanzania na kutoa uzito kwa mambo ya kimkakati yanayotekelezwa na serikali hususan biashara na uwekezaji, utalii, kilimo na miundombinu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Manfredo Fantiwalipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimsikiliza Balozi wa Italia nchini Mhe. Marco Lombardi walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Donald Wright akifafanua jambo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.