Tanzania
na Oman zimedhamiria kuchukua jitihada za makusudi kuimarisha ushikiano wa
kiuchumi baina ya nchi hizo zenye uhusiano madhubuti wa kihistoria.
Hayo
yamebainishwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo, Mhe. Dkt. Stergomena L.
Tax (Mb) na mwenyeji wake, Mhe. Sayyid Badr Al Busaidi
walipokutana pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya
Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe
11 Desemba 2022.
Katika
hotuba zao za kufunga Mkutano wa Pili wa JPC, Viongozi hao walieleza kuwa nchi
zao zimekubaliana kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Kufuatilia Utekelezaji wa
Maazimio ya Mkutano huo ili kuwa na tija kwa pande zote mbili.
Kamati
hiyo pamoja na mambo mengine, itahakikisha kuwa rasimu zote za mikataba na makubaliano zinakamilika na kutiwa saini ili
kujenga mazingira ya kisheria ya kuimarisha uhusiano wa kindugu uliopo baina ya
Tanzania na Oman.
Maeneo
yaliyojadiliwa na ujumbe wa nchi hizo na kuwekewa mikakati ya utekelezaji ni
pamoja na kilimo, elimu, nishati, biashara, uwekezaji, mawasiliano, mifugo na
usafirishaji. Maeneo mengine ni uvuvi, utalii, michezo, utamaduni, madini,
uhamiaji, fedha na udhibiti wa majanga ya moto.
Mkutano wa JPC kati ya Tanzania na Oman ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax; Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato; Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu; Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab; Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Ndugu Kheri Mahimbali; na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Ndugu Mwanahamisi Adam.
Meza Kuu wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe 11 Desemba 2022. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.