Sunday, December 18, 2022

WAJASIRIAMALI WAASWA KUONGEZA UBUNIFU, UBORA WA BIDHAA

Wajasiriamali Wadogo na wa kati wamehimizwa kuendelea kuongeza ubunifu na ubora wa huduma na bidhaa wanazozalisha ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya ushindani katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (African Continental Free Trade Area - AfCFTA). 

Rai hiyo imetolewa na Waziri anayesimamia Masuala ya Afrika Mashariki Mhe. James Magode wa Uganda kwenye hafla ya kufunga Maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati, maarufu Juakali yaliyofanyika katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda. 

Amesema pamoja na kazi nzuri inayoendelea kufanywa na wajasiriamali, wasiridhike na hatua ya mafanikio waliyoifikia bali waendelee kuongeza ubunifu na ubora zaidi wa huduma na bidhaa wanazozalisha ili kujiweka katika nafasi nzuri ya ushindani hasa katika nyakati hizi za soko huria. 

Waziri Magode amesema Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya hiyo wanaendelea kutengeneza mazingira wezeshi zaidi kwa wafanyabiashara ili waweze kuendesha shughuli zao kwa uhuru na kwa faida zaidi. 

“Katika ngazi ya Jumuiya Nchi Wanachama kwa kushirikiana na Sekretarieti na wadau wengine sote tumekubaliana na tunaahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uendeshaji ya biashara yatakayowezesha Wafanyabishara wadogo, kati, wa kubwa sio tu kunufaika na soko la Afrika Mashariki bali soko kubwa la Afrika katika mpango wa AfCFTA”.  Mhe. Waziri Magode

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia musuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote ametoa rai kwa Jumuiya kuendelea kuenzi na kutumia lugha ya Kiswahili katika kuendesha biashara kwa kuwa ndiyo lugha pekee itayako wezesha kuunganisha wafanyabiasha wengi zaidi katika jumuiya na kurahisisha ufanyaji wa biashara. 

Amesema Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki imepokea mapendekezo ya wajasiriamali ya kuomba maonesho hayo yafanyike walau mara mbili kwa mwaka kutokana na umuhimu wake na kwamba mapendekezo hayo yataafikishwa katika ngazi husika kwa mashauriano na maamuzi zaidi.

Sherehe za kufunga maonesho hayo ziliambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo ugawaji wa zawadi kwa washiriki, vyeti vya ushiriki na burudani mbalimbali. 

Aidha, Jamhuri ya Burundi imepewa dhamana ya kuandaa maonesho yajayo ya 23 ya Afrika Mshariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati yanayotarajiwa kufanyika mwakani 2023.
Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia musuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote akikabidhi cheti kwa mshiriki wa maonesho kutoka Jamhuri ya Congo kwa kufanya vizuri katika ngazi ya kitaifa.
Waziri anayesimamia Masuala ya Afrika Mashariki Mhe. James Magode wa Uganda akihutubia kwenye sherehe za kufunga Maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati, maarufu Juakali yaliyofanyika katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
Picha ya pamoja na Meza Kuu na Wajasiriamali waliopata vyeti na tuzo za kufanya vizuri zaidi kwenye Maonesho ya 22 ya Juakali yaliyofanyika katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
Waziri anayesimamia Masuala ya Afrika Mashariki Mhe. James Magode wa Uganda na Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia musuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote wakikabidhi tuzo kwa mshiriki mdogo zaidi wa manoesho kutoka nchini Burundi.
Kikundi cha ngoma kutoka nchini Burundi kikisherehesha kwenye sherehe ya kufunga Maonesho ya 22 ya Juakali iliyofanyika katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.