Friday, March 10, 2023

TANZANIA NA LATVIA ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amewakaribisha wawekezaji kutoka Jamhuri ya Latvia kuja nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Kilimo na TEHAMA.


Balozi Dkt. Shelukindo ametoa wito huo leo tarehe 10 Machi, 2023 alipozungumza na Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Latvia, Bw. Nils Jansons aliyemtembelea ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kumsalimia na kumpongeza kwa kuteuliwa hivi karibuni  kwenye wadhifa huo.


Amesema Tanzania inayo ardhi ya kutosha kwa uwekezaji wa kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara hivyo wawekezaji kutoka Latvia ambayo ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri kwenye sekta ya kilimo duniani wanakaribishwa.


“Nimefurahishwa na  ziara yako hapa Tanzania. Latvia ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika sekta ya kilimo duniani. Tunaunga mkono ushirikiano na Tanzania kwenye sekta hiyo na tunawakaribisha wawekezaji wenye tija kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali hususan kilimo na TEHAMA ” alisema Balozi Dkt. Shelukindo.


Awali akizungumza kwenye Majadiliano ya Kwanza ya Kisiasa baina ya Tanzania na Latvia, Balozi Swahiba Mndeme, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amesema Tanzania inathamini ushirikiano uliopo baina yake na Latvia na kwamba majadiliano hayo ambayo  yanalenga kuimarisha ushirikiano baina ya pande mbili, yamekuja wakati muafaka kwa nchi hizi mbili ili kuziwezesha kujiwekea malengo na mikakati mipya ya kuuimarisha  ushirikiano ambao ulikuwa hafifu miaka ya nyuma.


“Tanzania inathamini ushirikiano uliopo baina yake na Latvia na tunapongeza uamuzi wenu wa kuja ili kama nchi mbili rafiki tuzungumze na kukubaliana namna ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wetu”, alisema Balozi Mndeme.


Aidha, amesema Tanzania kupitia ushirikiano na nchi za Umoja wa Ulaya ikiwemo Latvia imeendelea kunufaika kupitia sekta za biashara, utalii na uwekezaji huku akitoa mfano wa sekta ya utalii ambayo kwa kiasi kikubwa imewavutia watalii wengi kutoka nchi za Ulaya kwa takribani asilimia 80 ya watalii wote wanaoingia Tanzania.


Amesema katika medani za kimataifa hususan agenda ya Mabadiliko ya Tabianchi, Tanzania inazisisitiza nchi zilizoendelea ikiwemo Latvia kutimiza ahadi yao ya kuchangia kiasi cha Dola za Marekani Bilioni Moja kila mwaka ili kuziwezesha nchi zinazoendelea ikwemo Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ongezeko la joto na ukame.


Naye, Bw. Jansons ameeleza utayari wa Serikali ya Latvia wa kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali za manufaa kwa pande mbili na kusisitiza kuwa nchi hiyo ina mpango wa kuteua Mwakilishi wa Heshima wa nchi hiyo hapa nchini ili kushughulikia masuala yote ya ushirikiano.

“Naunga mkono hoja zote tulizojadiliana ikiwemo ya kuzikumbusha nchi zilizoendelea kutimiza ahadi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Latvia inayo nia ya dhati ya kuimarisha ushirikiano na Tanzania kwa manufaa ya pande hizi mbili,” alisema Bw. Jansons.


Kupitia majadiliano hayo, Tanzania na Latvia zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za Kilimo, Tehama, Utalii, Biashara na Uwekezaji, Mazingira na Uchukuzi hususan kwa kuimarisha matumizi bora ya Bandari.


Pia nchi hizi mbili zimedhamiria kusaini Mkataba wa Ushirikiano katika sekta ya Anga (BASA) baada ya majadiliano ya awali kukamilika kwa ajili ya kukuza Utalii na Biashara baina ya pande mbili; Kuunganisha Vyuo Vikuu vya Kilimo vya pande mbili kwa ajili ya kukuza matumizi ya teknolojia katika sekta ya Kilimo; na Kuunganisha Taasisi Kuu za Biashara na Uwekezaji za pande mbili kwa lengo la kukuza Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Latvia ambapo hivi karibuni ujumbe wa Wawekezaji kutoka Latvia watafanya ziara ya kikazi nchini kwa ajili ya kufahamu na `kutumia fursa za Biashara zilizopo nchini. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo akizungumza na Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Latvia, Bw. Nils Jansons alipomtembelea ofisi kwake jijini Dodoma tarehe 10 Machi 2023. Pamoja na mambo mengine Viongozi hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Latvia
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akifuatilia mazungumzo kati ya Balozi Dkt. Shelukindo na Bw. Jansons hawapo pichani
Mazungumzo yakiendelea
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo akimpatia Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Latvia, Bw. Nils Jansons zawadi ya mchoro wa  picha ya wanyama watano mashuhuri "Big Five" inayotangaza utalii wa Tanzania.
Balozi Dkt. Shelukindo akiagana na Bw. Jansons mara baada ya kukamilisha mazungumzo yao
Picha ya pamoja


.........Majadiliano ya Kwanza ya Kisiasa kati ya Tanzania na Latvia

Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (wa kwanza kulia) akiongoza Majadiliano ya Kwanza ya Kisisasa kati ya Tanzania na Latvia yaliyofanyika jijini Dodoma tarehe 10 Machi 2023 kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Latvia, Bw. Nils Jansons (wa kwanza kushoto)
Balozi Mndeme (kulia) akizungumza wakati wa Majadiliano ya Kwanza ya Kisiasa kati ya Tanzania na Latvia yaliyofanyika jijini Dodoma tarehe 10 Machi 2023. Wengine katika picha ni Bibi. Agnes Kiama (kushoto) na Bi. Kisa Mwaseba, Maafisa Mambo ya Nje
Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Latvia, Bw. Nils Jansons (kushoto) akiwa na Mjumbe aliyefuatana naye, Bw. Tils Indans.








 

TANZANIA YAFUNGUA RASMI OFISI ZA UBALOZI NCHINI NAMIBIA

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imefungua rasmi Ofisi za Ubalozi jijini Windhoek, Namibia.

Hafla ya ufunguzi wa ofisi hizo za ubalozi ulihudhuriwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, Mabalozi wa nchi za Afrika, viongozi wa Serikali ya Tanzania na viongozi wa jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini humo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Dkt. Tax ameishukuru Jamhuri ya Namibia hususan Wizara ya Mambo ya Nje kwa ushirikiano ilioutoa katika hatua zote za kuanzisha ofisi hiyo na kuelezea kuwa kushiriki kwao katika tukio hilo la kihistoria la ufunguzi ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo.

Amesema  Tanzania kama mama wa lugha ya Kiswahili inaendelea na jitihada  za kuhakikisha lugha hiyo inatangazwa na kuenea kwa kasi kupitia Balozi zake, vyuo vya kimataifa na majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

“Wakati huu ambapo Serikali za Tanzania na Namibia zipo kwenye mazungumzo ya lugha ya Kiswahili kuwa sehemu ya lugha ya chaguo katika shule za Namibia, Ubalozi umefungua maktaba ndogo yenye vitabu na majarida ya Kiswahili kwa ajili ya watu wenye nia ya kujifunza kiswahili kuja kujisomea” alisema Dkt. Tax

Naye Mhe. Dkt. Ndaitwah akizungumza katika hafla hiyo alieleza kuwa kwasasa nchi hizo mbili zina makazi ya ubalozi katika miji mikuu ambapo ni hatua muhimu katika kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo na watu wake.

Kadhalika, amempomgeza Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba kwa kuchagua jengo lenye ubora na la kisasa kwa ajili ya ofisi za ubalozi huo ambalo ni rafiki kwa mazingira.

‘’ Tanzania ikiwa mpambanaji wa bara la Afrika na Kusini mwa Afrika siku zote imekuwa pamoja nasi na hivyo sisi wanamibia tutakapokuja kujisomea na kufanya tafiti katika maktaba hii ya Kiswahili inayofunguliwa leo tutakuwa katika mazingira salama” alisema Mhe. Ndaitwah.

Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia ulianza utekelezaji wa majukumu yake ya kidiplomasia tarehe 20 Februari 2020 na kufanya Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba kuwa Balozi wa kwanza kuwaiwakilisha Tanzania katika nchi hiyo.

Hafla ya ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia imefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia unaofanyika jijini Windhoek Namibia kuanzia tarehe 8 hadi 10 Machi 2023 ambapo Mhe. Dkt. Tax anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo.

Wakati huo huo, Waziri Dkt. Tax alifanya mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Namibia ambao walijitambulisha kitaaluma ni Madaktari wa Binadamu.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Waziri aliwasihi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania wanapokuwa nje ya nchi na kuendelea na zoezi la kujiandikisha linalofanyika kwa watanzania wenye taaluma mbalimbali waliopo nje ya nchi ili waweze kutambulika na kuisaidia nchi yao katika taaluma hizo pale wanapohitajika.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kushoto) pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah wakikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia.
   

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia. Mhe. Dkt. Tax ameishukuru Jamhuri ya Namibia kwa ushirikiano ilioutoa katika hatua za kuanzisha ubalozi huo  na uwepo wao katika tukio hilo muhimu na la kihistoria kwa nchi hizo mbili.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia. Mhe. Dkt. Ndaitwah ameeleza kuwa uwepo wa ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia ni ishara kubwa na muhimu katika kuendeleza na kuimarisha uhusiano uliopo kwa maslahi ya nchi hizo na watu wake.


     Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kushoto) na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah wakisoma kitabu cha Kiswahili katika makataba ya kiswahili iliyopo katika ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Namibia mara baada ya kukata utepe kuashiria ufunguzi wa ofisi hiyo.


 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah katika picha ya pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba (kushoto) wakati wa hafla ya ufunguzi wa ofisi za Ubalozi jijini Windhoek, Namibia.


     Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah katika picha ya pamoja na Mabalozi wa nchi za Afrika wanaowakilisha nchini Namibia wakati wa hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi za Ubalozi jijini Windhoek, Namibia.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah katika picha ya pamoja na Watumishi wa ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia wakati wa hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi za Ubalozi jijini Windhoek, Namibia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah katika picha ya pamoja na Watanzania wanaoishi nchini Namibia wakati wa hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi za Ubalozi jijini Windhoek, Namibia.


 


Wednesday, March 8, 2023

TANZANIA, NAMIBIA KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI




Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia, ngazi ya Maafisa Waandamizi, Balozi Fatma Rajab (kushoto) akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 8 hadi 10 Machi 2023.  Kulia, ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Namibia, Balozi Penda Naanda.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab (wa pili kutoka kushoto walioketi), Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Namibia, Balozi Penda Naanda (watatu kutoka kushoto walioketi), Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba (wa kwanza koshoto walioketi), Balozi wa Jamhuri ya Namibia nchini Tanzania, Mhe. Lebius Tobius katika picha ya pamoja na Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi wa Serikali ya Tanzania na Namibia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia ngazi ya Maafisa Waandamizi unaofanyika jijini Windhoek, Namibia. 

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba akifatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia, ngazi ya Maafisa Waandamizi unaofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 8 hadi 10 Machi 2023

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab (kulia) akihutubua wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia, ngazi ya Maafisa Waandamizi unaofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 8 hadi 10 Machi 2023, kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz.

Ujumbe Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia ngazi ya Maafisa Waandamizi ukifuatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 8 hadi 10 Machi 2023

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ikifuatilia mkutano huo

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ikifuatilia mkutano huo

Ujumbe wa Jamhuri ya Namibia katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia ngazi ya Maafisa Waandamizi wakifatilia hafla ya ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 8 hadi 10 Machi 2023

 

BALOZI MBAROUK AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI MBALIMBALI DOHA QATAR

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) kwa nyakati tofauti amekutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Vallamvelly Muraleedharan pamoja na Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Uhusiano wa Jumuiya za Kimataifa Mhe. Michelle Sison, Doha nchini Qatar.   

Mazungumzo hayo yamefanyika kando ya Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi zinazoendelea (LDCs) unaendelea Doha nchini Qatar.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.  Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Vallamvelly Muraleedharan. Mazungumzo hayo yamefanyika kando ya Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi zinazoendelea (LDCs) unaendelea Doha nchini Qatar.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.  Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akiagana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Vallamvelly Muraleedharan, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea (LDCs) unaendelea Doha nchini Qatar.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Uhusiano wa Jumuiya za Kimataifa Mhe. Michelle Sison. Mazungumzo hayo yamefanyika kando ya Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi zinazoendelea (LDCs) unaendelea Doha nchini Qatar.

Mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Uhusiano wa Jumuiya za Kimataifa Mhe. Michelle Sison yakiendelea Doha nchini Qatar. Mazungumzo hayo yamefanyika kando ya Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi zinazoendelea (LDCs) unaendelea Doha nchini Qatar.





Tuesday, March 7, 2023

DKT. TAX AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA UINGEREZA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili namna ya kuboresha uhusiano baina ya  Tanzania na Uingereza na jinsi ya kufanya kazi kwa pamoja katika kudumisha na kuendeleza uhusiano huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar akifafanua jambo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax) walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam