Shirika la Ndege la Saudi Arabia limeanza rasmi safari za ndege za moja kwa moja kutoka Saudia Arabia hadi Tanzania.
Akiongea katika hafla ya mapokezi ya Ndege ya Shirika la Ndege la Saudia Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (Mb) amesema kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja kutoka Saudia hadi Tanzania ni moja ya matunda ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliyofanya nchini Saudi Arabia Mwezi, Juni 2022.
“Kuanzishwa kwa safari hizi, kutachangia kuimarisha mazingira ya kibiashara na uwekezaji yatakayopelekea uhitaji wa usafiri wa anga wa moja kwa moja kutoka Tanzania kwenda Saudi Arabia,” Alisema Prof. Mbarawa
Prof. Mbarawa aliongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) za mwaka 2022, idadi ya abiria wa kimataifa nchini imeongezeka kwa asilimia 55 kutoka abiria 1,694,085 katika mwaka 2021 hadi kufikia abiria 2,618,119 mwaka 2022.
“Awali abiria walilazimika kupitia mataifa mengine ili kufika Saudi Arabia, uzoefu unaonyesha kuwa walitumia takribani saa kumi ili kukamilisha safari zao. Hivyo, kwa kutumia Shirika hili, abiria wataweza kusafiri kwenda Jeddah moja kwa moja na watatumia saa Nne na dakika arobaini,” aliongeza Prof. Mbarawa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) alisema kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja kutoka Saudia Arabia hadi Tanzania ni matokea ya uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya mataaifa hayo.
“Tunategemea kupitia safari hizi tutakuza na kuimarisha biashara, uwekezaji, viwanda na utalii nchini……..kwa sasa Urari wa biashara kati ya Tanzania na Saudia Arabia umefikia Dola za Kimarekani 18,000,0000,” alisema Balozi Mbarouk. Tanzania imekuwa ikiuza bidhaa mbalimbali nchini Saudi Arabia hususan nyama, matunda na maua.
Naye Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Bw. Fahad Alharbi alisema Saudi Arabia imefurahi kuanzishwa kwa safari hiyo ya kihistoria na yote hiyo imewezekana kutokana na uhusiano mzuri ilionao na Serikali ya Tanzania.
“leo tumeshuhudia uzinduzi rasmi wa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi Tanzania. Ni Imani yangu kuwa safari hizi zitachangia kuimarisha biashara na uwekezaji, utalii pamoja na usafirishaji kwa kiasi kikubwa," alisema Bw. Alharbi. Shirika la Ndege la Saudi Arabia litafanya safari zake kuja nchini mara nne kwa wiki.
Februari, 2023 Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Mwadini na Meneja Mkuu wa Masoko, Kanda ya Kati wa Shirika la Ndege la Saudi Arabia Bw. Abdulrahman Alabdulwahab walikutana na kujadili maandalizi ya uzinduzi wa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Saudi Arabia.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao pia walijadili mikakati ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania ili kuongeza idadi ya watalii na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa za Tanzania hususan nyama na matunda.
Hafla ya uzinduzi wa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi Tanzania zilihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Mwadini, Balozi wa Comoro Nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed pamoja na viongozi wengine wa Serikali.
Ndege ya Shirika la Ndege la Saudi Arabia ikiwasili rasmi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam
|
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi Tanzania |
|
Wageni wakipokelewa baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam |
|
Picha ya pamoja |
|
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,akiwasilisha salamu za Wizara katika hafla ya mapokezi ya Ndege ya Shirika la Ndege la Saudia Jijini Dar es Salaam |
|
Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Bw. Fahad Alharbi akitoa salamu za Saudi Arabia katika hafla ya mapokezi ya Ndege ya Shirika la Ndege la Saudia Jijini Dar es Salaam |