Friday, April 14, 2023

NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JAMHURI YA SLOVENIA AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA SIKU TATU


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Slovenia Mhe. Tanja Fajon na ujumbe wake amewasili nchini tarehe 13 Aprili 2023 kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Ziara hiyo inalenga kuimarisha na kukuza uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na Slovenia sambamba na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Waziri Fajon katika siku yake ya kwanza nchini amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax jijini Dodoma, ambapo mazunguzo yao yalijikita kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kuanisha maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Slovenia. 

Mazungumzo hayo pia yalihusisha uandaaji wa mazingira na utaratibu wa kusainiwa kwa Hati za Makubaliano katika maeno mapya ya ushirikiano yaliyoainishwa. 

Maeneo mapya ya ushirikiano yaliyoibuliwa wakati wa mazungumzo hayo ni uzalishaji dawa (pharmaceuticals), usimamizi wa rasilimali maji, utunzaji wa mazingira, ulinzi na usalama, uchumi wa buluu, sayansi na teknolojia, kilimo, Elimu,biashara na uwekezaji. 

Mbali na hayo Waziri Dkt. Tax alitumia fursa hiyo kumweleza Waziri Fajon kuhusu juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mafanikio yaliyopatikana nchini kutokana na juhudi hizo ikiwemo kupatikana kwa maridhiano ya kisiasa, kuimarika kwa Demokrasia, Haki za Banadamu, uhuru wa vyombo vya habari na uzingatiwaji wa usawa wa jinsia katika maendeleo.

Waziri Fajon kwa upande wake ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika kuboresha mazingira ya Demokrasia na Utawala Bora nchini sambamba na kuendelea kusimamia vyema maendeleo ya uchumi licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali duniani zinazo dhoofisha ustawi wa uchumi. 

Ziara hii ni muendelezo wa matokeo ya juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Mataifa mengine duniani. 

Waziri Fajon akiwa nchini anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Viongozi mbalimbali Serikalini.
Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimpokea Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Slovenia Mhe.Tanja Fajon alipowasili katika Ofisi ya Wizara Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Slovenia Mhe. Tanja Fajon wakiwa katika picha ya pamoja punde baada kuwasili Wizarani Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Slovenia Mhe.Tanja Fajon walipokuna kwa mazungumzo katika jijini Dodoma
Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Slovenia Mhe. Tanja Fajon wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe walioambatana nao. 
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Balozi Swahiba Mndeme akifuatilia mazungumzo yaloyokuwa yakiendelea baina ya Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Slovenia Mhe. Tanja Fajon yaliyofanyika jijini Dodoma
Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Slovenia Mhe. Tanja Fajon yakiendelea.
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina ya Waziri Dkt. Tax na Waziri Fajon (hayupo pichani)
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Slovenia Mhe. Tanja Fajon akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (hayupo pichani). 
Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akifafanua jambo alipokuwa katika mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Slovenia Mhe. Tanja Fajon (hayupo pichani)

Thursday, April 6, 2023

SERIKALI YAAINISHA MAFANIKIO ZAIRA YA MAKAMU WA RAIS WA MAREKANI NCHINI

Serikali imewasihi watanzania kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali ikiwemo Marekani na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuliletea maendeleo taifa. 

Wito huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) alipozungumza na waandishi wa Habari kuelezea mafanikio ya ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris aliyoifanya nchini tarehe 29 – 31 Machi, 2023.

Dkt. Tax amesema ziara ya Mhe.Kamala Harris, nchini imekuwa na mafanikio makubwa katika kuimarisha na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kuitangaza Tanzania duniani.  

Amesema kupitia ziara hiyo, Serikali ya Marekani ilitoa ahadi mbalimbali kwa Serikali ya Tanzania na Mikataba na Hati za Makubaliano kusainiwa ambapo Serikali ya Marekani itajenga kiwanda kikubwa nchini kitakachokuwa cha pekee barani Afrika.  Kiwanda hicho cha kuchakata madini ya Nikel yanayotumika kutengenezea betri za gari za umeme kwa ajili ya soko la Marekani na duniani ifikapo mwaka 2026. 

Amesema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na Kampuni ya Life Zone Metals na kampuni ya TechMet zinazomilikiwa kwa ubia na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Fedha la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (DFC).  Ameongeza kuwa kiwanda hicho kitatoa ajira kwa watanzania na kuchangia katika pato la Taifa.

Dkt. Tax alisema Amesema Mkataba wa Msaada wa Maendeleo kati ya Tanzania na Serikali ya Marekani kupitia USAID wa Dola za Marekani bilioni 1.1 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ulisainiwa.

“Mkataba wa Msaada wa Maendeleo kati ya Tanzania na Serikali ya Marekani kupitia USAID wa kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.1 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ulisainiwa; na Hati ya Makubaliano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marekani ilisainiwa pia. Kupitia Makubaliano hayo Serikali ya Marekani itatoa ushauri wa kitaalam na kujenga uwezo kwa wataalam kuhusu usimamizi wa bandari za Tanzania, hususan katika upanuzi wa bandari, vifaa vya kisasa na uendelezaji wa Bandari,” alisema Dkt. Tax.

Dkt. Tax aliongeza kuwa pamoja na Mkataba huo na Hati za Makubaliano hizo zilizosainiwa, Tanzania itanufaika kupitia ahadi mbalimbali ikiwemo Serikali ya Marekani kuahidi kutoa nyongeza ya Dola za Marekani milioni 1.3 kupitia Shirika la Misaada la Marekani USAID kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya kuendelea kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Serikali ya Marekani itatoa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.0 kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wa Afrika walio katika sekta ya Umma, na sekta binafsi kushiriki shughuli za kiuchumi na kijamii; Serikali ya Marekani kuingia Makubaliano na Tanzania yatakayowezesha Marekani kuuza bidhaa za usafirishaji, uchukuzi, teknolojia ya digitali na nishati safi zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500.

Serikali ya Marekani kupitia USAID itatoa Dola za Marekani 600,000 kwa ajili ya kushirikiana na kampuni za mawasiliano na teknolojia ya sekta binafsi na Serikali ili kupanua huduma za nishati safi na kutoa umeme kwa takriban vituo 100 vya afya katika maeneo ya magharibi, kati, na kusini mwa Tanzania. Mradi huo utawezesha kampuni za mawasiliano ya simu kuimarisha huduma za takwimu na kuwezesha vituo vya afya kutumia mifumo ya kidijitali kutoa huduma.

Serikali ya Marekani kuendelea kuwekeza katika Mpango wa Dharura wa Rais wa Kusaidia UKIMWI (PEPFAR) na Tanzania kuendelea kunufaika ambapo Marekani inapanga kuwekeza Dola za Marekani milioni 433 katika kipindi cha miaka miwili ijayo. 

Serikali ya Marekani kupitia Mpango wa Rais wa kupambana na Malaria kutenga kiasi cha Dola za Marekani milioni 39 kwa mwaka 2024. Mradi huo unalenga kupambana na malaria ikiwa ni pamoja na kusambaza vyandarua, dawa za malaria, vifaa vya uchunguzi wa haraka wa malaria na dawa za kuzuia malaria kwa wajawazito ambapo Tanzania itaendelea kunufaika.

Serikali ya Marekani itatenga Dola za Marekani milioni 16.4 katika Bajeti ya Marekani ya Mwaka 2024 kwa ajili ya kuendeleza demokrasia, haki, na programu za utawala nchini. 

Vilevile Serikali ya Marekani kupitia USAID inatarajia kutoa Dola za Marekani milioni 1 za ziada kwa ajili ya programu ambazo utekelezaji wake utaanza mwaka huu.

Serikali ya Marekani kuipatia Tanzania kiasi cha Dola za Marekani milioni 1 kwa ajili ya miradi inayolenga kuondoa vikwazo vya uhuru wa kujieleza kwa umma na vyombo vya habari vya Tanzania na Serikali ya Marekani itatoa Dola za Marekani 400,000 kusaidia kazi ya Kituo cha Demokrasia kuleta pamoja wadau kujadili mageuzi zaidi ya kidemokrasia na sheria na kuwajengea uwezo vijana kushiriki kwenye shughuli za kisiasa.

Mafanikio mengine ni Serikali ya Marekani kutoa Dola za Marekani milioni 16 kwa ajili ya mpango wa Kilimo Tija unaolenga kusaidia wakulima nchini, hususan wanawake na vijana katika kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula; na Tanzania na Marekani kuanzisha majadiliano ya kuongeza muda wa ukomo wa visa (Visa ya miaka mitano).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akiwaeleza waandishi wa Habari (hawapo pichani) mafanikio ya ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris aliyoifanya nchini tarehe 29 – 31 Machi, 2023
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akiwaeleza waandishi wa Habari (hawapo pichani) mafanikio ya ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris aliyoifanya nchini tarehe 29 – 31 Machi, 2023



SERIKALI YAIHAKIKISHIA JUMUIYA YA KIMATAIFA IMEDHIBITI UGONJWA WA MARBURG

Serikali kupitia Wizara za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Afya imekutana na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi na taasisi zao hapa nchini  na kuwatoa hofu juu ya ugonjwa wa Mabarg ambao tayari umedhibitiwa.

Akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua za kukabiliana na kudhibiti ugonjwa wa marbug tangu ulipoanza na hadi sasa hakuna maambukizi mapya.

“Napenda kuwatoa hofu Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kuwa Tanzania ni salama na hivyo tuendelee kufanya kazi zetu kama kawaida kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya,” alisema Dkt. Tax 

Akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Afya, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu amesema tangu ugonjwa huo ulipoibuka Serikali imechukua hatua za haraka za kudhibiti ugonjwa huo na hadi sasa hakuna maambukizi tena.

“Jumla ya visa vya ugonjwa huo vimebaki 8 na kati yao watu 5 wamefariki ,watatu wanaendelea na matibabu na mgonjwa mmoja ameruhusiwa na wagonjwa waliolazwa wanaendelea vizuri,” alisema Prof. Nagu

Kwa Upande wake Kiongozi wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comorro nchini, Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed ameipongeza Serikali kwa hatua ilizochukua za kutoa taarifa za ugonjwa wa Maburg kwa wakati.

“Tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua ilizochukua kuukabili ugonjwa wa Maburg ikiwemo utoaji sahihi wa taarifa, elimu kwa umma kuhusu ugonjwa huo,” alisema Dkt. El Badaoui Mohamed.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni Kiongozi wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comorro nchini, Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed (kushoto) na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu (kulia)

Balozi wa Marekani Nchini, Mhe. Michael Battle akichangia jambo wakati wa mkutano wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Rwanda Nchini, Mhe. Maj. Gen. Charles Karamba akichangia jambo wakati wa mkutano 

Balozi wa Rwanda Nchini, Mhe. Regina Hess akichangia jambo wakati wa mkutano 

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akieleza jambo kwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wakati wa mkutano















VACANCY ANNOUNCEMENT






 

Friday, March 31, 2023

MAKAMU WA RAIS WA MAREKANI AMALIZA ZIARA YA KIHISTORIA NCHINI


Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris ameondoka nchini baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya siku tatu iliyofanyika kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Akiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Mhe. Kamala ameagwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango ambaye aliongozana na Mhe. Mama Mbonimpa Mpango na Viongozi wengine wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax.

Mhe. Kamala ambaye kwenye ziara hii alifuatana na mwenza wake, Mhe. Douglas Emhoff pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Marekani, pamoja na mambo mengine alikutana na mwenyeji wake Mhe. Rais Dkt Samia tarehe 30 Machi 2023 kwa mazungumzo rasmi ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kwa pamoja walizungumza na waandishi wa habari kuhusu makubaliano waliyofikia kwenye mazungumzo yao.

Kupitia ziara hii, Serikali ya Marekani na Tanzania zimeahidi kuimarisha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, usalama wa mitandao, TEHAMA, Afya, usalama wa chakula, usafirishaji huku pia Marekani ikitangaza kutoa Dola za Marekani milioni 500 kupitia Benki ya Exim ili kuwezesha upatikanaji wa kugharamia upelekeaji wa huduma na bidhaa katika sekta za miundombinu, usalama wa mitandao, usafirishaji, teknolojia ya kidigiti, nishati na miradi ya nishati jadidifu.

Kadhalika Serikali ya Marekani ina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata madini ya nikeli yanayotumika kutengeneza betri za umeme wa magari ifikapo mwaka 2026.

Ziara ya Mhe. Kamala nchini ni matokeo ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani, ililenga pamoja na mambo mengine, kuimarisha ushirikiano hususan kwenye maeneo ya kimkakati ya ushirikiano kama vile biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na utunzaji wa mazingira, TEHAMA, usafirishaji, bandari na masuala ya utawala bora na demorasia.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akisalimiana na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kondoka nchini baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya siku tatu iliyofanyika kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akiwa na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakati akimuaga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya siku tatu nchini
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax kwenye hafla ya kumuaga Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokuwa akiondoka nchini baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku tatu nchini. 
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Elsie Kanza kwenye hafla ya kumuaga Makamu huyo iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Serikali wakimuaga Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris alipokuwa akiondoka nchini baada ya kuhitimisha ziara yake
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akiwa ameongozana na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam  muda mfupi kabla ya kuondoka nchini baada ya kuhitimisha ziara yake ya kihistoria ya siku tatu
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris  akisalimiana na Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocol - CP) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Yusuph Mndolwa kwenye hafla ya kumuaga Makamu huyo iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga kwenye hafla ya kumuaga Makamu huyo iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris na mwenza wake Mhe. Doug Emhoff  wakiwapungia Watanzania walijiotekeza kumuaga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

Thursday, March 30, 2023

TANZANIA NA MAREKANI ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongeza kuimarika kwa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani hususan kwenye sekta zinazochangia kuboresha maisha ya watanzania kama afya, elimu, kilimo, miundombinu, usalama wa chakula, demokrasia na utawala bora.

Mhe. Dkt. Rais Samia ameyasema hayo wakati wa mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kumalizika kwa mazunguzo rasmi kati yake na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Amesema kupitia ushirikiano na Marekani, magonjwa kama Kifua Kikuu na UKIMWI sio tishio tena hapa nchini kwani kupitia program mbalimbali zinazotekelezwa kwa ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, kama Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) maambukizi ya magonjwa haya kwa wananchi yamepungua kutoka asilimia 7.2 mwaka 2012 hadi asilimia 4.7 mwaka 2017.

Kuhusu vifo vitokanavyo na Malaria, Mhe. Dkt. Rais Samia amesema vimepungua kutoka milioni 7.7 mwaka 2015 hadi kufikia vifo milioni 3.5 mwaka 2021.

“Lengo letu ni kutokomeza malaria kabisa katika jamii yetu ya Tanzania. Pia tunakaribisha wawekezaji wenye tija kutoka Marekani kuwekeza kwenye viwanda vya utengenezaji wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI ili zitengenezwe hapa nchini kwetu", amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.

Mhe. Rais Dkt. Samia pia amesema anaikaribisha Marekani katika maeneo mapya ya ushirikiano hususan kwenye uvuvi katika bahari kuu, utafiti wa gesi na uchumi wa buluu.

Pia Mhe. Rais Samia ameiomba Marekani kupitia upya suala la utoaji visa ili kuwawezesha watanzania kupata visa za muda mrefu kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma.

Kwa upande wake, Mhe. Kamala amesema Serikali ya Marekani inao Mpango mpya wa kushirikiana na Tanzania katika kusaidia miradi ya Teknolojia ya kidijiti, Usafirishaji na Nishati.

Amesema Serikali hiyo kupitia Benki ya Exim watasaini Hati ya Makubaliano na Tanzania ambayo itawezesha upatikanaji wa Dola za Marekani milioni 500 kugharamia upelekeaji wa huduma na bidhaa katika sekta za miundombinu, usalama wa mitandao, usafirishaji, teknolojia ya kidigiti, nishati na miradi ya nishati jadidifu.

Vilevile amempongeza Rais Samia kwa kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha demokrasia nchini hususan kwenye masuala ya maridhiano na vyama vya siasa pamoja na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.

Amesema Marekani chini ya uongozi wa Mhe. Rais Joe Biden inaunga mkono agenda za kuimarisha Demokrasi anchini na itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ya ushirikiano kama vile usalama wa chakula, afya, kuwasaidia wanawake na vijana Demokrasia na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Vilevile amesema katika kuimarisha ushirikiano na Tanzania, Marekani ina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata madini ya nikeli yanayotumika kutengeneza betri za umeme wa magari ifikapo mwaka 2026.

Mhe. Kamala ameishukuru na kuipongeza Tanzania kwa kuchangia ulinzi wa amani duniani na kwamba nchi hiyo inaunga mkono jitihada zote zinazofanywa na Tanzania katika kuhakikisha Kanda ya Maziwa Makuu inakuwa na amani na utulivu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakifurahia jambo alipowasili Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris alipowasili Ikulu ya Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris akisaini kitabu cha wageni alipowasili Ikulu ya Dar es Salaam.
Mhe.Rais Dkt. Samia (kulia) akiongoza kikao kati yake na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris (kushoto) 


Wednesday, March 29, 2023

KAMALA AWASILI NCHINI

Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris amewasili nchini tarehe 29 Machi, 2023 kuanza ziara yake ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi, 2023.

Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijiji Dar es Salaam Mhe. Kamala amepokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.

Mhe. Kamala atapokelewa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atampokea Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 30 Machi 2023 ambapo mapokezi hayo yatafuatiwa na mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili baina ya viongozi hao.

Vilevile, akiwa nchini, Mhe. Kamala ataweka shada la maua katika Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam kama ishara ya kuwakumbuka wahanga wa mabamu yaliyolipuliwa kwenye Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam mwaka 1998. 

Pia atatembelea Taasisi ya Tanzania Startup Association ya Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukutana na Wajasiriamali Vijana pamoja nakushiriki Futari iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake Mhe. Dkt. Rais Samia.

Katika ziara hii Mhe. Kamala amefuatana na mwenza wake Mhe. Doug Emhoff pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Marekani.

Mapokezi ya Mhe. Kamala yameongozwa na Mhe. Dkt. Mpango na kumshirikisha Mama Mbonipa Mpango pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Waziri wan chi, Ofisi ya Rais-Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dkt. Saada Mkuya na Mkoa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla.
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akifurahia jambo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alipokuwa akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris na mwenza wake Mhe. Doug Emhoff wakiwasalimia Watanzania waliojitokeza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuwalaki walipowasili nchini usiku wa tarehe 30 Machi, 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris alipowasili nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakifurahia shamrashamra za mapokezi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere 
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akiwasalimia washereheshaji waliojitokeza kumpokea wakati akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakibadilishana mawazo alipowasili  katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Balozi wa Marekani nchini Mhe. Michael Battle
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Elsie Sia Kanza 
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam