Thursday, April 6, 2023

SERIKALI YAAINISHA MAFANIKIO ZAIRA YA MAKAMU WA RAIS WA MAREKANI NCHINI

Serikali imewasihi watanzania kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali ikiwemo Marekani na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuliletea maendeleo taifa. 

Wito huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) alipozungumza na waandishi wa Habari kuelezea mafanikio ya ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris aliyoifanya nchini tarehe 29 – 31 Machi, 2023.

Dkt. Tax amesema ziara ya Mhe.Kamala Harris, nchini imekuwa na mafanikio makubwa katika kuimarisha na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kuitangaza Tanzania duniani.  

Amesema kupitia ziara hiyo, Serikali ya Marekani ilitoa ahadi mbalimbali kwa Serikali ya Tanzania na Mikataba na Hati za Makubaliano kusainiwa ambapo Serikali ya Marekani itajenga kiwanda kikubwa nchini kitakachokuwa cha pekee barani Afrika.  Kiwanda hicho cha kuchakata madini ya Nikel yanayotumika kutengenezea betri za gari za umeme kwa ajili ya soko la Marekani na duniani ifikapo mwaka 2026. 

Amesema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na Kampuni ya Life Zone Metals na kampuni ya TechMet zinazomilikiwa kwa ubia na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Fedha la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (DFC).  Ameongeza kuwa kiwanda hicho kitatoa ajira kwa watanzania na kuchangia katika pato la Taifa.

Dkt. Tax alisema Amesema Mkataba wa Msaada wa Maendeleo kati ya Tanzania na Serikali ya Marekani kupitia USAID wa Dola za Marekani bilioni 1.1 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ulisainiwa.

“Mkataba wa Msaada wa Maendeleo kati ya Tanzania na Serikali ya Marekani kupitia USAID wa kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.1 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ulisainiwa; na Hati ya Makubaliano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marekani ilisainiwa pia. Kupitia Makubaliano hayo Serikali ya Marekani itatoa ushauri wa kitaalam na kujenga uwezo kwa wataalam kuhusu usimamizi wa bandari za Tanzania, hususan katika upanuzi wa bandari, vifaa vya kisasa na uendelezaji wa Bandari,” alisema Dkt. Tax.

Dkt. Tax aliongeza kuwa pamoja na Mkataba huo na Hati za Makubaliano hizo zilizosainiwa, Tanzania itanufaika kupitia ahadi mbalimbali ikiwemo Serikali ya Marekani kuahidi kutoa nyongeza ya Dola za Marekani milioni 1.3 kupitia Shirika la Misaada la Marekani USAID kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya kuendelea kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Serikali ya Marekani itatoa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.0 kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wa Afrika walio katika sekta ya Umma, na sekta binafsi kushiriki shughuli za kiuchumi na kijamii; Serikali ya Marekani kuingia Makubaliano na Tanzania yatakayowezesha Marekani kuuza bidhaa za usafirishaji, uchukuzi, teknolojia ya digitali na nishati safi zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500.

Serikali ya Marekani kupitia USAID itatoa Dola za Marekani 600,000 kwa ajili ya kushirikiana na kampuni za mawasiliano na teknolojia ya sekta binafsi na Serikali ili kupanua huduma za nishati safi na kutoa umeme kwa takriban vituo 100 vya afya katika maeneo ya magharibi, kati, na kusini mwa Tanzania. Mradi huo utawezesha kampuni za mawasiliano ya simu kuimarisha huduma za takwimu na kuwezesha vituo vya afya kutumia mifumo ya kidijitali kutoa huduma.

Serikali ya Marekani kuendelea kuwekeza katika Mpango wa Dharura wa Rais wa Kusaidia UKIMWI (PEPFAR) na Tanzania kuendelea kunufaika ambapo Marekani inapanga kuwekeza Dola za Marekani milioni 433 katika kipindi cha miaka miwili ijayo. 

Serikali ya Marekani kupitia Mpango wa Rais wa kupambana na Malaria kutenga kiasi cha Dola za Marekani milioni 39 kwa mwaka 2024. Mradi huo unalenga kupambana na malaria ikiwa ni pamoja na kusambaza vyandarua, dawa za malaria, vifaa vya uchunguzi wa haraka wa malaria na dawa za kuzuia malaria kwa wajawazito ambapo Tanzania itaendelea kunufaika.

Serikali ya Marekani itatenga Dola za Marekani milioni 16.4 katika Bajeti ya Marekani ya Mwaka 2024 kwa ajili ya kuendeleza demokrasia, haki, na programu za utawala nchini. 

Vilevile Serikali ya Marekani kupitia USAID inatarajia kutoa Dola za Marekani milioni 1 za ziada kwa ajili ya programu ambazo utekelezaji wake utaanza mwaka huu.

Serikali ya Marekani kuipatia Tanzania kiasi cha Dola za Marekani milioni 1 kwa ajili ya miradi inayolenga kuondoa vikwazo vya uhuru wa kujieleza kwa umma na vyombo vya habari vya Tanzania na Serikali ya Marekani itatoa Dola za Marekani 400,000 kusaidia kazi ya Kituo cha Demokrasia kuleta pamoja wadau kujadili mageuzi zaidi ya kidemokrasia na sheria na kuwajengea uwezo vijana kushiriki kwenye shughuli za kisiasa.

Mafanikio mengine ni Serikali ya Marekani kutoa Dola za Marekani milioni 16 kwa ajili ya mpango wa Kilimo Tija unaolenga kusaidia wakulima nchini, hususan wanawake na vijana katika kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula; na Tanzania na Marekani kuanzisha majadiliano ya kuongeza muda wa ukomo wa visa (Visa ya miaka mitano).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akiwaeleza waandishi wa Habari (hawapo pichani) mafanikio ya ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris aliyoifanya nchini tarehe 29 – 31 Machi, 2023
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akiwaeleza waandishi wa Habari (hawapo pichani) mafanikio ya ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris aliyoifanya nchini tarehe 29 – 31 Machi, 2023



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.