Baadhi ya wageni waliohudhuria hafla ya maadhimisho
ya miaka 29 ya Uhuru wa Jamhuri ya
Afrika Kusini iliyofanyika jijini Dar es Salaam wakifuatilia hafla hiyo |
Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) ameshiriki hafla ya maadhimisho ya miaka 29 ya Uhuru wa Jamhuri ya Afrika Kusini iliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuwaita wawekezaji wengi zaidi waje kuwekeza nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Balozi Mbarouk amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Afrika Kusini kuendelea kuuenzi uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo ambao uliasisiwa na viongozi waasisi wa mataifa hayo.
“Tanzania itaendelea kutumia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Afrika Kusini na nitoe wito kwa wawekezaji wengi zaidi wa Afrika Kusini waje Tanzabia kuwekeza hasa ikizingatia kuna fursa katika maeneo ya kilimo, uzalishaji, mifugo, viwanda vya dawa, usafiri, utalii, madini na viwanda vya kusindika mazao ya chakula,”alisema.
Amesema wakati Taifa la Afrika Kusini likiadhimisha siku ya uhuru wake Tanzania itaendelea kushirikiana na Afrika Kusini ili kuhakikisha nchi zote zinanufaika na uwepo wa uhusiano huo.
Amesema ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Afrika Kusini umeoneshwa zaidi na ziara ya kitaifa aliyoifanya nchini Afrika Kusini Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kufanyika kwa mikutano ya pamoja kati ya nchi hizi.
Akizungumza katika hafla hiyo Balozi wa Afrika Kusini nchini Mhe. Noluthando Mayende- Malepe amesema Afrika Kusini inajali na kuthamini mchango mkubwa ambao Tanzania imetoa katika harakati za ukombozi wa nchi hiyo na kuifanya Tanzania kuwa nyumbani kwa wapigania uhuru wa Afrika Kusini.
“Tunaishukuru sana serikali na wananchi wa Tanzania kwa mambo yote ambayo Tanzania imeifanyia Afrika Kusini wakati wote hadi kufikia kupata uhuru wetu, kwakweli sisi tunawashukuru sana, niwahakikishie kuwa Afrika Kusini itaendelea kuuthamini mchango wenu katika uhuru wetu na tutaendelea kuuenz uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliopo kati ya nchi zetu mbili hizi, alisema.
Ameahidi kuwa Tanzania na Afrika Kusini zitaendelea kushirikiana katika mambo mengi ambayo nchi mbili hizi zimekuwa zikiyafanya.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na waheshimiwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.