Timu ya wanawake ya kuvuta kamba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jana tarehe 25 Aprili 2023, imemenyana vikali na timu ya Wizara ya Uchukuzi kwenye mchezo wa kuvuta kamba katika hatua ya robo fainali uliofanyika mjini Morogoro, katika mashindano ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Mei Mosi yanayoendelea mjini humo.
Katika mtanange huo wa vuta nikuvute uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri, timu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilipoteza mchezo huo dhidi ya Wizara ya Uchukuzi ambayo ilijinyakulia ushindi wa alama 2. Timu ya Wizara ya Uchukuzi ndiye bingwa mtetezi wa mchezo huo, ikishikilia rekodi ya kushinda kwa miaka 6 mfululizo.
Timu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imefanikiwa kufika katika hatua hiyo ya robo fainali baada ya kushinda michezo miwili katika ngazi ya makundi na 16 bora dhidi ya TAMISEMI na RAS Ruvuma.
Akizungumzia mchezo huo mwalimu anayekinoa kikosi cha kuvuta kamba cha Wananawake cha Wizara ya Mambo ya Nje Bw. Andrew Salia ameeleza kuwa licha ya kupungukiwa wachezaji wawili kwenye kikosi chake kwa sababu ya majeraha, bado kilikuwa imara kiasi cha kutoa upinzani mkali kwa bingwa huyo wa mara sita mfululizo.
Aidha Bw. Salia ametoa pongezi kwa kikosi chake kwa kufanikiwa kufuzu na kushiriki hatua ya robo fainali ya mashindano hayo yenye hamasa na ushindani mkubwa. Vilevile amehahidi kuwa ataendelea kukinoa kikosi chake ili kiweze kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.
Timu ya wanawake ya kuvuta kamba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikijitahidi kumshinda mpinzani wake Wizara ya Uchukuzi |
Timu ya wanawake ya kuvuta kamba ya Wizara ya Uchukuzi ikionesha umahiri wake katika mchezo huo dhidi ya mpinzani wake Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.