Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inakamilisha mfumo wa Kidigitali wa uandikishaji wa Diaspora unaotarajiwa kukamilika mwezi June 2023 ili kuwezesha ukusanyaji endelevu wa takwimu za Diaspora.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma tarehe 14 Aprili 2023 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alipojibu swali la Mhe. Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi aliyetaka kujua idadi ya Diaspora wa Tanzania na mchango wao katika uchumi wa nchi.
Mhe. Balozi Mbarouk amesema Diaspora kama walivyo raia wengine wa Tanzania wana mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi na maendeleo kwa ujumla kupitia shughuli mbalimbali wanazozifanya ikiwemo utumaji wa fedha za kigeni nchini (remittances), uwekezaji, kuleta mitaji, utaalam na teknolojia ambayo huchangia katika kukuza uzalishaji wa mazao, bidhaa na huduma mbalimbali zenye tija kiuchumi.
Ameongeza kuwa, Diaspora pia wanachangia uchumi wa nchi kwa kutangaza fursa za kiuchumi, biashara, utalii na uwekezaji zinazopatikana nchini na kwamba kwa mujibu wa taarifa kutoka Balozi za Tanzania na maeneo yake ya Uwakilishi, hadi sasa idadi ya Diaspora wa Tanzania ni Milioni 1.5.
Amesema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la utumaji wa fedha za kigeni nchini kutoka kwa Diaspora hadi kufikia Shilingi Trilioni 2.6 mwezi Desemba 2022.
“Diaspora huchangia katika maendeleo ya nchi kwa kutuma fedha za kigeni nchini (Remittances); kuwekeza, kuleta mitaji, utaalamu na Teknolojia inayoweza kuchangia kukuza uzalishaji wa mazao, bidhaa na huduma mbalimbali zenye tija kiuchumi. Mathalan katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Desemba 2022, Diaspora walituma nchini kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 1.1 sawa na Shilingi Trilioni 2.6. Vilevile, katika kipindi hicho Diaspora wamewekeza kupitia ununuzi wa nyumba na viwanja wenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.4 na ununuzi wa Hisa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.5” amesema Balozi Mbarouk.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.