Friday, April 28, 2023

NJE SPORTS CHUPUCHUPU KUTWAA UBINGWA WA KARATA

Timu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje Sports) iliyopo jijini Morogoro kushiriki katika michezo mbalimbali inayoendelea mjini hapo kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Mei Mosi imejitosa kuwania ushindi katika mchezo wa karata na drafti. 

Katika michezo hiyo iliyochezwa kwa nyakati tofauti ilianza na hatua ya makudi na kufuatiwa na robo fainali, nusu fainali, na fainali. 

Kwa upande wa mchezo wa karata Nje Sports iliwakilishwa na Bw. Peter Ndatila na Bi. Nyanzala Lupeja. Bi. Lupeja ambaye aliwakilisha upande wa Wanawake - Nje Sports alifanikiwa kufika hatua fainali na kuibuka mshindi wa 4 baada ya kuonesha umahiri wa hali ya juu uliomfanya kuvuka hatua ya makundi, robo na nusu fainali. Bi. Lupenja kupitia kundi B2 alifanikiwa kufuzu baada kujikusanyia alama 6 katika michezo 6 aliyocheza. 

Wakati huo huo ushindani mkali hulioshuhudiwa kwa upande wa Wanaume katika mchezo huo, ulitosha kufifisha juhudi na makali ya Bw. Ndatila na kumfanya ashindwe kufuzu katika hatua ya makundi. Bw. Ndatila alifanikiwa kujikusanyia alama 5 katika kundi D baada ya kusuluhu katika michezo yote 5 aliyocheza. Wachezaji wawili waliofanikiwa kufuzu kwenda robo fainali katika kundi hilo walijikusanyia alama 8 na 7 katika michezo 5 iliyochezwa.

Kwa upande wa mchezo wa drafti Nje Sports iliwakilishwa na Bw. Shaban Maganga ambaye licha ya kuonesha makali yake na kutoa upinzani mkali katika mchezo huo hakufanikiwa kuvuka kwenda hatua ya makundi. Bw. Maganga alijikusanyia alama 6 katika kundi E na kushika nafasi ya 4 kati ya washiriki 7 wa kundi hilo. Wachezaji wawili waliofanikiwa kupita kwenda robo fainali katika kundi hilo walijikusanyia alama 11 na 10 katika michezo 6 iliyochezwa.

Mashindano hayo ya michezo kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Mei Mosi yanatarajiwa kuhitimishwa katika siku hizi mbili za mwishoni mwa Juma (Ijumaa na Jumamosi) mjini Morogoro, ambapo watumishi, wakazi wa Morogoro na maeneo jirani watapata fursa ya kutazama fainali katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha na kuvuta kamba. 
Usajili wa washiriki wa mchezo wa drafti ukiendelea kwenye mashindano ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanya wa Jamhuri mjini Morogoro
Mchezaji wa drafti wa Nje Sports Bw. Shaaban Maganga akijisajili kushiriki mchezo uliofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro
Mchezaji wa karata wa Nje Sports Bw. Shaaban Maganga (kushoto) akimkabili mpinzani wake katika mchezo wa karata uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro
Mchezo ukiendelea
Mchezaji wa karata wa Nje Sports Bi. Nyanzala Lupeja (kulia) akimkabili mpinzani wake katika mchezo wa karata uliofanyika Jamhuri mjini Morogoro
Mchezaji wa karata wa Nje Sports Bi. Nyanzala Lupeja (kushoto) akimkabili mpinzani wake katika mchezo wa karata uliofanyika Jamhuri mjini Morogoro
Mchezaji wa karata wa Nje Sports Bw. Peter Ndatila akimkabili mpinzani wake katika mchezo wa karata uliofanyika Jamhuri mjini Morogoro
Mchezo ukiendelea
Mchezo ukiendelea

RAIS KAGAME AHITIMISHA ZIARA YA KIKAZI NCHINI

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam wakati akiondoka kurejea nchini Rwanda


Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame akiagana na viongozi mbalimbali katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kabla ya kurejea nchini Rwanda

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax wakimuaga Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Ndege ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame na ujumbe wake ikiwa tayari kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kurejea nchini Rwanda

Ndege ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame na ujumbe wake ikiondoka katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kurejea nchini Rwanda



 

Thursday, April 27, 2023

RAIS SAMIA NA RAIS KAGAME WAKUBALIANA KUIMARISHA BIASHARA

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam 

Rais wa Jamhuri ya Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam 

WATANZANIA WALIOKWAMA SUDAN WAWASILI NCHINI SALAMA






Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akisalimiana na mmoja wa Watanzania waliorejeshwa na Serikali kutoka Sudan ambako kuna mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati ya Jeshi la Sudan na Jeshi la Msaada wa Haraka (RSF). Mtanzania huyo amepata changamoto za kiafya kwa kupata mshituko kufuatia matukio ya mapigano hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akiongea na Balozi wa Tanzania nchini Sudan, Mhe. Silima Kombo Haji baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kutoka Sudan ambako kuna mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati ya Jeshi la Sudan na Jeshi la Msaada wa Haraka (RSF)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) wa pili kulia; Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kulia); Balozi wa Tanzania nchini Sudan, Mhe. Silima Kombo Haji na Mkurugenzi wa Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz wakiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kuwapokea Watanzania waliorejeshwa na Serikali kutoka Sudan ambako kuna mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati ya Jeshi la Sudan na Jeshi la Msaada wa Haraka (RSF).

Watanzania waliorejeshwa na Serikali kutoka Sudan ambako kuna mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati ya Jeshi la Sudan na Jeshi la Msaada wa Haraka (RSF) wakiwa wanakamilisha taratibu za uhamiaji ili waweze kukutana na familia zao zilizokuwa zinawasubiri uwanjani hapo

Watanzania waliorejeshwa na Serikali kutoka Sudan ambako kuna mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati ya Jeshi la Sudan na Jeshi la Msaada wa Haraka (RSF) wakiwa wanakamilisha taratibu za uhamiaji ili waweze kukutana na familia zao zilizokuwa zinawasubiri uwanjani hapo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akiongea na baadhi ya wazazi waliofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuwapokea vijana wao waliorejeshwa na Serikali kutoka Sudan.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akiongea na vyombo vya habari vilivyofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kushuhudia tukio la kuwapokea Watanzania waliorejeshwa na Serikali kutoka Sudan.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akiongea na familia zilizofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuwapokea wapendwa wao walirejeshwa na Serikali kutoka Sudan. 







 

RAIS KAGAME AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA KIKAZI

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame,  awasili nchini kwa Ziara ya Kikazi ya siku mbili tarehe 27 - 28 April, 2023. Mheshimiwa Rais Paul Kagame na Ujumbe wake  amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax (Mb.)

Katika mapokezi hayo Dkt. Tax aliambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu – Zanzibar Mhe. Jamal Kassim Ali, Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makala, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Balozi wa Rwanda Nchini, Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali.

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame akipokea zawadi ya maua baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ziara ya kikazi ya siku mbili

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame akisalimiana na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ziara ya kikazi ya siku mbili

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame akisalimiana na Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ziara ya kikazi ya siku mbili



Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax




Wednesday, April 26, 2023

RAIS WA JAMHURI YA RWANDA MHESHIMIWA PAUL KAGAME KUFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI KUANZIA TAREHE 27 - 28 APRIL, 2023

 


UHOLANZI YARIDHISHWA NA MAZINGIRA YA BIASHARA, DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA

Uholanzi imeoneshwa kuridhishwa na mazingira ya biashara na uwekezaji, demokrasia, haki za binadamu na utawala bora nchini.

Hayo yamebainishwa na Balozi wa Uholanzi nchini, Mhe. Wiebe de Boer wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku maalum ya Mfalme wa Uholanzi iliyofanyika tarehe 25 Aprili 2023 Jijini Dar es Salaam.

Balozi Boer alisema mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji nchini wafanyabiashara wengi kutoka Uholanzi wamewekeza Tanzania. “Kadhalika tumefurahishwa na kuridhishwa na demokrasia nchini, haki za binadamu na utawala bora pamoja na kufunguliwa kwa majukwaa na mikutano ya kisiasa nchini,” Alisema Balozi Boer.

Mbali na kuwekeza katika biashara na uwekezaji pia wafanyabiashara wa Uholanzi wamewekeza pia katika sekta za utalii pamoja na kilimo.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) alieleza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendeleza uhusiano wa karibu na ushirikiano uliopo kati ya pande zote mbili.

Dkt. Tax alisema kuwa Uholanzi imeendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwamo kilimo, mifugo, uvuvi, elimu, nishati, afya, miundombinu, mawasiliano, utalii, usafiri pamoja na mafuta na gesi.

“Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji nchini, (TIC) hadi kufikia mwezi Machi, 2023 Kampuni kadhaa za Uholanzi zimewekeza Tanzania kwa kiasi cha (USD milioni 1,079.78), na kutengeneza ajira zaidi ya 15,607 katika sekta za kilimo, ujenzi, nishati, maendeleo ya rasilimali watu, mafuta na gesi, mawasiliano, utalii na usafiri,” alisema Dkt. Tax

“Naomba kutumia fursa hii kuzialika Kampuni na wawekezaji kutoka Uholanzi kuwekeza katika fursa zilizopo na kuwekeza nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika miradi ya kimkakati na yenye maslahi mapana ya pande zote mbili,” alisema Dkt. Tax

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepata mafanikio makubwa katika kuweka mazingira rafiki na mazuri ya biashara kupitia mageuzi ya kiutawala na kisheria na uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya miundombinu,” alisema Dkt. Tax 

Pamoja na mambo mengine Dkt. Tax aliongeza kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Sita zimewezesha kupungua kwa gharama za kufanya biashara nchini Tanzania na kuwezesha ufanisi na uundaji wa huduma rahisi, msingi wa kuchochea shughuli za kiuchumi, na hivyo kuongeza uwekezaji, na kuimarishwa kwa biashara nchini.

Baadhi ya washiriki walioshiriki katika hafla ya maadhimisho ya Siku maalum ya Mfalme wa Uholanzi iliyofanyika tarehe 25 Aprili 2023 Jijini Dar es Salaam

Baadhi ya washiriki walioshiriki katika hafla ya maadhimisho ya Siku maalum ya Mfalme wa Uholanzi iliyofanyika tarehe 25 Aprili 2023 Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Uholanzi nchini, Mhe. Wiebe de Boer akizungumza na washiriki walioshiriki katika hafla ya kuadhimisha Siku maalum ya Mfalme wa Uholanzi iliyofanyika tarehe 25 Aprili 2023 Jijini Dar es Salaam

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia katika hafla ya kuadhimisha Siku maalum ya Mfalme wa Uholanzi iliyofanyika tarehe 25 Aprili 2023 Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia katika hafla ya kuadhimisha Siku maalum ya Mfalme wa Uholanzi iliyofanyika tarehe 25 Aprili 2023 Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Manfredo Fanti katika hafla ya maadhimisho Siku maalum ya Mfalme wa Uholanzi iliyofanyika tarehe 25 Aprili 2023 Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar katika hafla ya maadhimisho ya Siku maalum ya Mfalme wa Uholanzi iliyofanyika tarehe 25 Aprili 2023 Jijini Dar es Salaam


TIMU YA KUVUTA KAMBA KWA UPANDE WA WANAWAKE YA NJE SPORTS YAKWAMA KUVUKA ROBO FAINALI

Timu ya wanawake ya kuvuta kamba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jana tarehe 25 Aprili 2023, imemenyana vikali na timu ya Wizara ya Uchukuzi kwenye mchezo wa kuvuta kamba katika hatua ya robo fainali uliofanyika mjini Morogoro, katika mashindano ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Mei Mosi yanayoendelea mjini humo.

Katika mtanange huo wa vuta nikuvute uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri, timu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilipoteza mchezo huo dhidi ya Wizara ya Uchukuzi ambayo ilijinyakulia ushindi wa alama 2. Timu ya Wizara ya Uchukuzi ndiye bingwa mtetezi wa mchezo huo, ikishikilia rekodi ya kushinda kwa miaka 6 mfululizo.

Timu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imefanikiwa kufika katika hatua hiyo ya robo fainali baada ya kushinda michezo miwili katika ngazi ya makundi na 16 bora dhidi ya TAMISEMI na RAS Ruvuma. 

Akizungumzia mchezo huo mwalimu anayekinoa kikosi cha kuvuta kamba cha Wananawake cha Wizara ya Mambo ya Nje Bw. Andrew Salia ameeleza kuwa licha ya kupungukiwa wachezaji wawili kwenye kikosi chake kwa sababu ya majeraha, bado kilikuwa imara kiasi cha kutoa upinzani mkali kwa bingwa huyo wa mara sita mfululizo.

Aidha Bw. Salia ametoa pongezi kwa kikosi chake kwa kufanikiwa kufuzu na kushiriki hatua ya robo fainali ya mashindano hayo yenye hamasa na ushindani mkubwa. Vilevile amehahidi kuwa ataendelea kukinoa kikosi chake ili kiweze kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.
Timu ya wanawake ya kuvuta kamba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikijipanga kamkabili mpinzani wake timu ya Wizara ya Uchukuzi kwenye mchezo uliofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro

Timu ya wanawake ya kuvuta kamba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikijitahidi kumshinda mpinzani wake Wizara ya Uchukuzi





Timu ya wanawake ya kuvuta kamba ya Wizara ya Uchukuzi ikiwa tayari kumkabili mpinzani wake Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye mchezo uliofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro

Timu ya wanawake ya kuvuta kamba ya Wizara ya Uchukuzi ikionesha umahiri wake  katika mchezo huo dhidi ya mpinzani wake Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki