Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana na Watetezi wa Haki za Binadamu na kutambua mchango wao kwenye maendeleo ya nchi.
Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 27 Oktoba 2023 na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Prof. Remy Ngoy Lumbu mara baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Tanzania kuhusu Hali ya Watetezi wa Haki za Binadamu kwenye kikao cha 77 cha Tume hiyo kinachoendelea jijini Arusha.
Prof. Lumbu amesema kuwa amefurahishwa na taarifa ya Tanzania iliyowasilishwa kwenye kikao hicho kuhusu ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Watetezi wa Haki za Binadamu na kuishukuru nchi hiyo kwa kutambua na kuthamini mchango wa Watetezi wa Haki za Binadamu kama washirika muhimu katika maendeleo ya nchi.
Pia ameeleza kuwa, kauli ya Serikali hiyo ya kufungua milango yake kwa ajili ya kushirikiana na watetezi wa haki za binadamu ni ya kupigiwa mfano na nchi nyingine na kuuunga mkono wito wa Serikali ya Tanzania wa kuwataka watetezi wa haki za binadamu kuendelea kuheshimu katiba ya nchi na miongozo yote inayosimamia haki za binadamu na watu nchini humo.
“Naomba ujumbe wa Tanzania mfikishe salamu zangu za pongezi kwa Mhe. Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana na kuwalinda watetezi wa haki za binadamu nchini kwake. Nimefurahishwa pia na kauli ya Serikai ya Tanzania kwamba milango yake ipo wazi wakati wote kwa ajili ya kuwapokea na kushirikiana na watetezi hao wa haki za binadamu,” alisema Mhe. Prof. Lumbu.
Awali akiwasilisha Taarifa ya Tanzania kuhusu Hali ya Watetezi wa Haki za Binadamu, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Richard Kilanga amesema kuwa Serikali za Tanzania Bara na Zanzibar zimeendelea kushirikiana na watetezi wa haki za binadamu nchini katika kuboresha masuala yote yanayohusu usimamizi, uimarishaji, na ulinzi wa haki za binadamu nchini.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuyawezesha mashirika hayo na watetezi wa haki za binadamu kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ambapo amesema hadi sasa Tanzania inayo mashirika yasiyo ya kiserikali 9,900.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafahamu umuhimu wa watetezi wa haki za binadamu ndiyo sababu zipo sheria mbili zinazosimamia. Ipo Sheria ya Mashirika yasiyo ya kiserikali na Sheria ya Jumuiya za Kiraia kwa pande zote mbili Bara na Visiwani” alisema Bw. Kilanga.
Ameongeza kusema Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na mashirika hayo katika kukuza na kulinda haki za binadamu na watu nchini pamoja na kujenga uchumi wa nchi ambapo ameeleza kuwa kwa mwaka 2022 mashirika hayo yamechangia kiasi cha Shilingi Trilioni 2.24 sawa na Dola za Marekani milioni 800 kwenye uchumi wa nchi.
“Hakuna shaka kwamba Serikali inatambua mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali, mkiwemo watetezi wa haki za binadamu katika kukuza na kulinda haki za binadamu na watu pamoja na kuleta maendeleo nchini, hususan kwa kuzingatia Mpango Kazi wa Tatu wa Nchi wa Mwaka 2021/22-2025/26 inayotekeleza agenda ya nchi ya Maendeleo ya 2025. Mpango Kazi huu uliandaliwa kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya Kiserikali na kwamba Mashirika hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Kazi huo” alisema Bw. Kilanga.
Kadhalika, Bw. Kilanga amesema kutokana na jitihada za kuimarisha na kusimamia utekelezaji wa haki za binadamu nchini zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini, mwezi Mei 2022 ulimtunukia zawadi kwa kutambua mchango wake katika kulinda na kutetea haki za binadamu na utawala wa sheria nchini.
Vilevile ameongeza kusema milango ya Serikali ipo wazi kwa watetezi wa haki za binadamu katika kuendelea kushirikiana na Serikali ili kutimiza lengo la pamoja la kila mwananchi kunufaika na haki za binadamu na watu huku akisisitiza wajibu wa taasisi za watetezi wa watu wa kuendelea kutii sheria za nchi na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 26 (1).
Kikao cha Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kilifunguliwa rasmi jijini Arusha tarehe 20 Oktoba 2023 na kinatarajiwa kumalizika tarehe 09 Novemba, 2023. Pamoja na mambo mengine kikao kinapokea na kujadili agenda mbalimbali zinazohusu haki za binadamu katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.