Tuesday, October 24, 2023

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI YA KUINUA VIJANA KIUCHUMI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inainua ustawi wa vijana kiuchumi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Angellah Kairuki (Mb.) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) katika Maadhimisho ya miaka 78 ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam. 

Waziri Kairuki amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikutumia njia mbalimbali kuhakikisha vijana wanapiga hatua kiuchumi.

"Kwa upande wa Tanzania Bara, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 inafanyiwa mapitio ili kuakisi hali ya sasa ya maendeleo ya vijana, vipaumbele na changamoto," Mhe. Kairuki alisema. 

Waziri Kairuki ametaja moja ya mkakati ni kuwezesha vijana kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ambalo hutoa mikopo kwa vijana wajasiriamali na uanzishwaji wa zaidi ya mifuko 45 maalum katika wizara na idara mbalimbali ili kuhakikisha kuwa vijana wanawezeshwa kiuchumi. 

Waziri Kairuki ameongeza kuwa Tanzania imehakikisha kuna ongezeko la upatikanaji wa huduma za ushauri nasaha rafiki kwa vijana kupitia programu ya Afya ya Ujinsia na Haki za Uzazi na kuongeza upatikanaji wa huduma za matunzo na matibabu ya VVU. 

Amesema kupitia Mpango wa Kujenga Kesho Bora – YOUTH INITIATIVE FOR AGRIBUSINESS, Serikali inatarajia kuongeza ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo na kuharakisha kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kwa ajili ya maisha endelevu na bora. 

Waziri Kairuki  amewaasa vijana kuwa wabunifu na kutumia teknolojia ambayo ni nguzo muhimu za kukuza uwezeshaji wa vijana.

"Ni muhimu kusaidia wajasiriamali wachanga katika kubadilisha mawazo yao kuwa biashara zinazofaa, endelevu kupitia kujenga uwezo na upatikanaji wa masoko na matumizi ya teknolojia na uvumbuzi." amesema.

Naye Mratibu Mkazi wa UN Tanzania, Bw. Zlatan Milišić alisema Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi zake utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuandaa na kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) pamoja na kuwawezesha vijana kutimiza malengo yao.

Bw. Milisic amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuwawezesha vijana kutimiza malengo yao na ya Serikali kwa ujumla.

Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuwekeza leo kwa ajili ya kesho kwa kuinua vijana wa Kitanzania”.

Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Angellah Kairuki akihutubia katika Maadhimisho ya miaka 78 ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Angellah Kairuki akikagua gwaride katika Maadhimisho ya miaka 78 ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Angellah Kairuki katika picha ya pamoja wanafunzi na Viongozi mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya miaka 78 ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.