Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imemtunukia Tuzo ya Heshima Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake katika kutetea, kulinda na kuimarisha haki za binadamu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana kwa niaba ya Mhe. Rais Samia wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu Afrika na maadhimisho ya miaka 20 ya Itifaki ya Maputo kuhusu Haki za Wanawake yaliyofanyika jijini ARusha tarehe 21 Oktoba 2023.
Akieleza sababu za kumtunuku Mhe. Rais Dkt Samia tuzo hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Janet Ratatouille Sallah-Njie amesema Mhe. Rais Dkt. Samia amekuwa kiongozi wa mfano barani Afrika katika kusimamia na kuimarisha haki za binadamu kuanzia ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Amesema Mhe. Rais Samia amefanikiwa kusimamia haki za binadamu kwa kuimarisha usawa wa kijinsia nchini, kuimarishaupatikanaji wa huduma za afya na elimu kwa wasichana, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kupambana na ukatili wa kijinsia, kuimarisha demokrasia na maridhiano, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa vyombo vya habari.
Ameongeza kusema ni bahati ya pekee kwa Afrika kuadhimisha miaka 20 ya Itifaki ya Maputo ya Haki za Wanawake kwenye ardhi ambayo Rais wake ndiye mwanamke pekee mwenye wadhifa huo wa juu barani humo.
“Hakuna namna bora ya kusherehekea miaka 20 ya Itifaki ya Maputo ya Haki za Wanawake zaidi ya kusherehekea hapa Tanzania ambapo Kiongozi wa nchi ndiye Rais pekee mwanamke barani Afrika. Tuna kila sababu ya kumtunuku tuzo hii siyo tu kwa sababu ni mwanamke bali pia ni kutokana na hatua kubwa za maendeleo alizopiga na mchango wake kwenye masuala ya haki za binadamu nchini kwake na kwenye medani za kimataifa,” amesisitiza Mhe. Sallah-Njie
Amesema nafasi ya Rais Samia ambaye anasismama kama balozi wa usawa wa kijinsia duniani ni chachu na mfano wa kuigwa kwa wanawake na wasichana wa Afrika katika kuwahamasisha na kuwatia moyo katika kufanyia kazi ndoto zao kwa kushinda vikwazo mbalimbali na kwamba wana uwezo wa kushika nafasi kubwa na za juu za uongozi.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mhe. Balozi Dkt. Chana ameishukuru Tume hiyo kwa kumtunuku tuzo Mhe. Rais Dkt. Samia na kumuelezea Mhe. Rais kama mwanamke kiongozi shujaa, mtetezi wa haki za binadamu na watu, mchapakazi na mtoto wa Afrika ambaye ni mwelewa na ameleta maendeleo nchini.
Amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia kumekuwa na kasi kubwa katika kuleta maendeleo na kuwezesha mifumo ya upatikanaji haki kwenye Nyanja mbalimbali ikiwemo utoaji wa haki huru, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kuabudu, uhakika wa chakula, kuwawezesha vijana kujiajiri, uwezeshaji wanawake na kuanzishwa kwa mpango wa msaada wa kisheria wa Dkt. Samia.
Pia amesema katika kipindi hiki cha awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia idadi ya wanawake katika vyombo vya utoaji maamuzi ikiwemo Mahakama, Bunge na Serikalini kwa ujumla imeongezeka.
“Mhe. Dkt. Samia mara baada ya kuingia madarakani alianzisha falsafa ya R4 kwa maana ya maridhiano na upatanishi, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi mpya. Huu ni utaratibu wenye lengo la kustawisha na kudumisha amani, umoja, undugu na maridhiano kwa wananchi ili kuchocea maendeleo,” amesema Mhe. Balozi Chana.
Mhe. Balozi Chana akizungumza mara baada ya kupokea Tuzo kwa niaba ya Mhe. Rais Dkt. Samia |
Mhe. Dkt Chana akizungumza |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.