Tuesday, October 31, 2023

UHUSIANO KATI YA MISRI NA ZANZIBAR NI MZURI LICHA YA MISRI KUFUNGA UBALOZI MDOGO ZANZIBAR

Serikali imeeleza leo kwamba, Uhusiano kati ya Misri na Zanzibar umeendelea kukua na kuimarika licha ya Serikali ya Misri kufunga Ubalozi wake mdogo Zanzibar kwenye miaka ya 1990.

Hayo yalielezwa Bungeni leo na Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipokuwa akijibu Swali la nyongeza la Mhe. Ali Juma Mohamed, Mbunge wa Shaurimoyo, aliyetaka kujua sababu za nchi ya Misri kufunga Ubalozi wake Mdogo Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Waziri alifahamisha kwamba Misri haikutoa sababu za kufunga Ubalozi wake mdogo Zanzibar. Hata hivyo, alieleza zaidi kuwa pamoja na kufungwa kwa ofisi hizo, mahusiano na ushirikiano kati ya Misri na Zanzibar yameendelea kukua na kuimarika siku hadi siku kupitia Ubalozi wake uliopo Dar es Salaam.

Awali, katika suala lake la msingi, Mhe. Mohamed alitaka kujua idadi ya Balozi ndogo zilizopo Zanzibar, ambapo alijibiwa kuwa hadi kufikia Agosti, 2023, nchi zilizofungua Ofisi ndogo za Ubalozi Zanzibar ni China; India; Msumbiji; Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Aidha, Mheshimiwa Naibu Waziri alieleza kuwa suala la kufungua na kufunga Ubalozi ni suala la kawaida katika ulimwengu wa Kidiplomasia. Alitaja sababu za nchi kufunga Ubalozi kuwa ni pamoja na; Kutetereka au kuharibika kwa mahusiano ya nchi husika; nchi kubadili mwelekeo wa kimaslahi na kistrategia; kukosekana kwa usalama katika nchi husika; na mwisho ni hali ya kiuchumi ambapo nchi hufunga Ubalozi au Konseli Kuu kwa ajili ya kubana matumizi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akijibu swali Bungeni jijini Dodoma 

Waheshimiwa Wabunge wakisikiliza majibu ya swali kutoka kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk 


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.