Tuesday, October 31, 2023

TANZANIA YASHIRIKI MAONESHO YA KIMATAIFA YA UTALII YA JAPAN (JAPAN TOURISM EXPO 2023) KWA MAFANIKIO

Tanzania imeshiriki kwa mafanikio makubwa katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism EXPO 2023), yaliyofanyika kuanzia tarehe 26 - 29 Oktoba 2023 Jijini Osaka, Japan.  

Maonesho hayo, yamekuwa ya kwanza kufanyika katika jiji hilo baada ya janga la UVIKO – 19 na yameshirikisha takriban makampuni ya watalii 1,275 kutoka nchi zipatazo 70 duniani.

Katika ufunguzi wa Maonesho hayo, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda aliinadi Tanzania kuwa ni nchi yenye vivutio mbalimbali vya utalii hususan, Ngorongoro, Serengeti, Kilimanjaro na Zanzibar.  

Kadhalika, Balozi Luvanda aliwataka mawakala wa utalii wa Japan waliojumuika na mawakala wa Tanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za utalii. Aidha, alifanya mazungumzo na Kamishna wa Taasisi ya Utalii ya Japan kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye sekta ya utalii, kwenye mikutano ya pembezoni mwa Maonesho hayo. 

Balozi Luvanda alitumia fursa hiyo kuelezea Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Swahili (Swahili Internation Tourism Expo – S!TE) ya mwaka 2024 yatakayofanyika nchini mwezi Oktoba 2024 ambapo wadau mbalimbali wa utalii wa Japan wamehamasika kujiandikisha ili waweze kushiriki kwa lengo la kujiunganisha kibiashara na mawakala wa utalii wa Tanzania. 

Pamoja na mambo mengine, Tanzania imepata fursa ya kuzindua rasmi filamu ya The Tanzania Royal Tour Jijini Osaka, iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kijapani, tukio ambalo limepata muitikio mkubwa na hamasa kubwa miongoni mwa wajapani wanaoishi katika jiji hilo na majiji jirani. Tukio kama hilo lilifanyika mwaka jana Jijini Tokyo, wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Utalii nchini Japan ya mwaka 2022.

Taasisi za utalii za Tanzania zilizoshiriki katika maonesho hayo ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na makampuni binafsi ya utalii ya Tanzania yakiwemo, GOSHEN Afrika Safari na MAULY Tours. 

Jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinalenga kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya utalii ili hatimaye kufikia watalii milioni tano na mapato bilioni sita kwa mwaka 2025. 

Katika Maonesho hayo, mawakala wa utalii Japan wamevutiwa na vivutio vya utalii vya Tanzania pamoja na uwekezaji katika sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kuingia ubia na makampuni ya utalii ya ndani. Aidha, wajapani wengi wamevutiwa kuitembelea Tanzania hususan, baada ya Serikali ya Japan kufungua mipaka yake hivi karibuni kufuatia kupungua kwa janga la UVIKO-19.

Japan ni soko linalochipukia (emerging market) baada ya janga la UVIKO – 19 na ni nchi yenye watu takriban milioni 123 ambapo, inaelezwa kuwa watu takriban milioni 23 sawa na asilimia 45 wana tabia ya kutoka kwenda kutalii nje ya nchi. 

Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda akielezea jambo kwa wawakilishi wa Taasisi ya Utalii ya Japan katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism EXPO 2023), yaliyofanyika tarehe 26 - 29 Oktoba 2023 Jijini Osaka, Japan

Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda akielezea jambo kwa wawakilishi wa Taasisi ya Utalii ya Japan katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism EXPO 2023), yaliyofanyika tarehe 26 - 29 Oktoba 2023 Jijini Osaka, Japan

Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Japan, Dkt. Kazusue Konoike akielezea bidhaa za Tanzania kwa washiriki wa Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism EXPO 2023), yaliyofanyika tarehe 26 - 29 Oktoba 2023 Jijini Osaka, Japan

Baadhi ya wahudhuriaji kwenye Banda la Tanzania wakipokea maelezo ya bidhaa za Tanzania wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism EXPO 2023), yaliyofanyika tarehe 26 - 29 Oktoba 2023 Jijini Osaka, Japan

Balozi Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda kwenye picha ya pamoja na washiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism EXPO 2023), yaliyofanyika tarehe 26 - 29 Oktoba 2023 Jijini Osaka, Japan



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.