Tanzania na India zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye maeneo ya kimkakati ambayo yana manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili ikiwemo maji, kilimo, nishati, teknolojia, afya, ulinzi na usalama, utamaduni na michezo, uchukuzi na biashara na uwekezaji.
Hayo yamebainishwa wakati wa mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari mara baada ya mazungumzo ya faragha kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi yaliyofanyika katika jengo la kupokelea wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi tarehe 09 Oktoba 2023.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mhe. Rais Dkt. Samia ameipongeza Serikali ya India kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Tanzania hususan kwenye maeneo ya kimkakati kama maji, afya, kilimo, teknolojia, ulinzi na usalama, na baiashara na uwekezaji.
Pia amesema Tanzania inapongeza uamuzi wa Serikali ya India wa kuanziasha kampasi ya kwanza la Taasisi ya Teknolojia ya India nje ya nchi hiyo ambayo itaanzishwa hivi karibuni Zanzibar na kuutaja uamuzi huo kama heshima na upendeleo kwa Tanzania kwani utawanufaisha watanzania, Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumzia biashara baina ya nchini hizi, Mhe. Rais Samia amesema, thamani ya ufanyaji biashara kati ya Tanzania na India imeendelea kuongezeka ambapo kwa takwimu zilizopo nchini biashara kati ya nchi hizi mbili imeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 3.1 mwaka 2022 kutoka Dola za Marekani Bilioni 2.6 mwaka 2017.
Kwenye medani za ushirikiano wa kimataifa, Mhe. Rais Samia amempongeza Waziri Mkuu Modi kwa kuandaa kwa mafanikio Mkutano wa Wakuu wa Nchi za G20 uliofanyika nchini hapa mwezi Septemba 2023 ambapo Afrika kupitia Umoja wa Afrika imefanikiwa kuwa mwanachama wa kudumu wa Umoja huo.
“Siwezi kusita kuipongeza India kwa kufanikiwa kuandaa Mkutano wa G20 ambao ulishuhudia Afrika inakuwa mwanachama kamili wa G20, nampongeza Waziri Modi kwa kutetea mpango wa kupunguza madeni kwa mataifa madogo na kutangaza mpango wa dharura wa kuhamasisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya nchi zinazoendelea ili kuwezesha upatikanaji wa teknolojia ya nishati safi ifikapo mwaka 2050” amesema Mhe. Rais Samia.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Modi ameitaja Tanzania kama mshirika wake wa karibu na mkubwa katika maendeleo barani Afrika na kwamba nchi hizo zimekubaliana kuupeleka ushirikiano uliopo katika viwango vya juu kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na India.
Amesema India itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ya kukuza ujuzi, usambazaji maji, teknolojia ya habari na mawasiliano na uhusiano wa watu wa India na Tanzania, nishati safi na ulinzi na usalama.
Pia ameongeza kusema nchi hizo zimekubaliana kuwa na mpango wa miaka mitano wa ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama hususan katika maeneo ya kujenga uwezo, mafunzo na ulinzi baharini.
Akizungumzia ushirikiano katika biashara, Mhe. Modi amesema nchi hizo zimekubaliana kuangalia uwezekano wa kuongeza biashara kwa kutumia sarafu za nchi zao kwa lengo la kupunguza gharama na matumizi ya Dola za Marekani.
Wakati wa Mkutano huo, Mhe. Rais Samia na Mhe. Modi walishuhudia ubadilishanaji wa Hati Sita za Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Hati 14 na Mkataba mmoja zilizosainiwa kati ya Tanzania na India wakati wa ziara hii. Hati hizo zinagusa sekta za Uchukuzi, Utamaduni, Michezo, Uwekezaji, TEHAMA na Elimu.
Mhe. Dkt. Rais Samia yupo nchini India kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 8 hadi 11 Oktoba, 2023.
Uadilishanaji wa Hati za Makubaliano ukiendelea |
Mhe. Rais Samia akiwa na Mhe. Modi mara baada ya kuwasili katika jengo la kupokelea wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09 Oktoba 2023 |
Mhe. Rais Samia akiwa na Mhe. Modi mara baada ya kuwasili katika jengo la kupokelea
wageni wa kitaifa la Hyderabad House jijini New Delhi, India tarehe 09
Oktoba 2023 |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.