Saturday, October 7, 2023

WAZIRI MAKAMBA ATUA INDIA KUELEKEA ZIARA YA KIHISTORIA YA MHE. RAIS DKT. SAMIA NCHINI HUMO










 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki   Mhe. January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt.Subrahmanyam Jaishankar ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atakayoifanya nchini humo kuanzia  tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2023.



Katika mazungumzo yao yaliyofanyika hivi karibuni jijini New Delhi, viongozi hao pamoja na mambo mengine wamelezea matarajio yao ya kuimarika zaidi kwa ushirikiano kati ya Tanzania na India kupitia ziara hiyo ya kihistoria.



Kwa upande wake , Mhe. Makamba amemshukuru mwenyeji wake kwa kumkaribisha nchini humo lakini pia kwa maandalizi mazuri ya ziara ya Mhe.  Rais Dkt. Samia nchini humo.



Kadhalika, Mawaziri hao walibadilishana taarifa kuhusu ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili na kukubaliana kuongeza jitihada ili kufikia malengo ya pamoja ya kuinua kuwango cha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili na kuhakikisha ushirikiano uliopo unazaa matokeo tarajiwa.



Mhe. Rais Dkt. Samia anatarajiwa kuwasili India tarehe 8 Oktoba 2023 kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu.



Wakati  wa ziara hiyo kutashuhudiwa ubadilishanaji wa mikataba  mbalimbali ya ushirikiano katika sekta za uwekezaji, uchukuzi,  afya, maji na nyingine nyingi.



Ziara hiyo pamoja  na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India hususan  kwenye maeneo ya kimkakati  na manufaa kwa Tanzania ikiwemo afya, maji, elimu uchumi wa buluu,  teknolojia, kilimo, na biashara na uwekezaji. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki   Mhe. January Makamba akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt.Subrahmanyam Jaishankar ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atakayoifanya nchini humo kuanzia  tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2023. Mazungumzo yao yalifanyika katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje ya India jijini New Delhi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizunguza na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe.Binaya Srikanta Pradhan jijini New Delhi kabla ya Mhe. Makamba kukutana na Waziri wa mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. Jaishankar
Mhe. Waziri Makamba akimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega wakati wa kikao cha kupokea taarifa kuhusu ushirikiano wa Tanzania na India mara baada ya Mhe. Makamba kuwasili nchini India tarehe 6 Oktoba 2023 kwa ajili ya kutathmini na kukamilisha maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo kuanzia tarehe 8 hadi 1 Oktoba 2023
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega (kulia) akiwa na Mkrugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga (kushoto) wakati wa kikao na Mhe. Waziri Makamba (hayupo pichani) baada ya kuwasili nchini India. Wengine katika picha ni Mkuu wa utawala Ubalozini, Bw. Deogratius Dotto na Afisa Mwandamizi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Bi. Latifah

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. John Kambona (kulia) akiwa na Afisa Mwandamizi wa Idara hiyo Bi. Eliet Magogo na Katibu wa Mhe. Waziri Makamba, Bw. Seif Kamtunda wakati wa kikao cha ujumbe wa Tanzania na Mhe. Waziir Makamba (hayupo pichani) jijini New Delhi kuelekea ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini India tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2023
Mhe. Makamba akizungumza na Mkurugenzi wa masuala ya ushirikiano wa India na Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya India mara baada ya kuwasili nchini humo kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega

Picha ya pamoja













 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.