Tuesday, October 10, 2023

RAIS DKT. SAMIA ATUNIKIWA SHAHADA YA HESHIMA YA UDAKTARI INDIA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mwanamke wa kwanza kutunikiwa  Shahada ya  Heshima ya Udaktari wa Falsafa na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India na kuitoa shahada hiyo kwa Watoto  wa  kike wanaoishi  katika  mazingira magumu nchini.


Akiipokea Shahada hiyo, ambayo ni ya kwanza kwake kutoka ugenini,  Rais  Samia amesema anakishukuru Chuo  hicho kwa heshima hiyo ambayo ni kubwa na kwamba anaitoa kwa watoto wa kike wa Tanzania  wanaoishi katika mazingira magumu na pembezoni  mwa nchi ambapo amewaka  kutokukata tamaa kutokana na mazingira waliyopo na kuitaka jamii kushirikiana kuwawezesha watoto hao kufikia ndoto zao.



"Mimi ni matokeo ya jozi nyingi za macho na mikono ya watu walioona uwezo ndani yangu wakanilea na kunishika mkono," amesisitiza Rais  Dkt. Samia.



Ameeleza kuwa ameitoa tuzo hiyo kwa watoto hao kutokana na mazingira halisi aliyopitia tangu akiwa shule ya msingi hadi kufikia nafasi aliyonayo nayo sasa.

 

Pia amesema anawashukuru watu mbalimbali wakiwemo wazazi wake, familia, Chama cha Mapinduzi na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwa mchango wao uliomwezesha kufikia hatua hiyo muhimu katika maisha.

 

“Shahada hii inanikumbusha mbali nikiwa mtoto mdogo nikienda shule katika kijiji nilichozaliwa cha Kizimkazi huko Unguja, Zanzibar, huku mama yangu akiwa ni mama wa nyumbani  na baba mwalimu. Nawashukuru kwa kunipatia muda ulioniwezesha kufikia ndoto zangu za elimu, siasa na hatimaye kufikia nafasi niliyo nayo sasa" amesema Rais Dkt. Samia.



Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Santishree Dhulipudi Pandit amesema Chuo hicho kimetunuku Mhe. Rais Samia  Shahada hiyo kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India, Diplomasia ya Uchumi, mchango wake katika maisha ya kila siku ya wananchi wa Tanzania na mafanikio yake kikanda na kimataifa.

 

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa India Mhe.  Dkt. Subrahmanyam Jaishankar ameielezea Shahada hiyo kama alama ya kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na India.

 

Taarifa kutoka chuoni hapo zinasema kuwa, Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969, ni viongozi wawili tu ambao wamewahi kutunukiwa shahada hiyo, Rais wa Russia Vladmir Putin pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Hayati Shinzo Abe. 


 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan akitunikiwa Shahada ya  Heshima ya Udaktari wa Falsafa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India, Prof. Santishree Dhulipudi Pandit. Mhe. Rais Dkt. Samia ameitoa Shahada hiyo kwa watoto wa kike nchini ili kuwapa moyo wa kuendelea na jitihada mbalimbali kwa ajili ya mafanikio yao ya baadaye. Mhe. Rais Dkt. Samia anakuwa  mwanamke wa kwanza kupata shahada hiyo kutoka Chuo hicho.

Mhe. Rais Dkt. Samia akizungumza mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari
Viongozi mbalimbali walioshiriki hafla ya Mhe. Rais Dkt. Samia ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari
Sehemu nyingine ya viongozi
Sehemu ya ujumbe wa India


Sehemu nyingine ya ujumbe wa India




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.