Monday, October 23, 2023

UN KUADHIMISHA MIAKA 78 YA KUANZISHWA KWAKE

Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania unatarajia kuadhimisha miaka 78 tangu ilipoanzishwa mwaka 1945.

Akizungumza na waandishi wa Habari kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda amesema maadhimisho ya miaka 78 ya Umoja wa Mataifa yatafanyika tarehe 24 Oktoba 2023 katika viwanja vya Karemjee Jijini Dar es Salaam.

Balozi Kaganda amesema wakati UN ukiadhimisha miaka 78 tangu kuanziswa kwake, Tanzania inajivunia kuwa mwanachama wa Umoja huo na imekuwa ikifanya vizuri katika baadhi ya maeneno ya malengo ya maendeleo endelevu hususan katika masuala ya chakula, elimu, jinsia, nishati, maji, amani na usalama.

“Tanzania tunajivunia kufanya vizuri katika masuala ya chakula, elimu, jinsia, nishati, maji pamoja na amani na usalama. Lakini kuna changamoto ya umasikini ambayo imekuwa ikikabili ulimwengu na nchi zinazoendelea ambapo tunahitaji kuongeza nguvu ya kukabiliana nayo,” alisema Balozi Kaganda.

Balozi kaganda aliongeza kuwa Tanzania inajisikia fahari kama mwanachama wa UN kwa kusimamia kikamilifu misingi ya Umoja huo na kuendelea kutoa mchango wake katika kutekeleza malengo adhimu.

“Tanzania imekuwa ikishiriki kikamilifu katika operesheni za ulinzi wa amani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa, utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo, kulinda na kuchochea haki za binadamu na utawala wa sheria na kushiriki katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa, yakiwemo maendeleo endelevu yanayotekelezwa wakati huu,” alisema Balozi Kaganda.

Kwa Upande wake Mratibu Mkazi wa UN Tanzania, Bw. Zlatan Milišić alisema Umoja wa Mataifa unafurahia kuadhimisha miaka 78 tangu kuanzishwa kwake na miaka 62 ya ushirikiano kati yake na Tanzania ambapo wakati wote zimekuwa na uhusiano mzuri na imara na Tanzania imekuwa ikichangia kikamilifu katika kuchagiza ajenda ya maendeleo ya kimataifa, katika kuandaa na kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

"Tunapoadhimisha miaka 78 ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, tunatambua ushirikiano mzuri na imara kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Mataifa ambapo umekuwa ukichagiza Malengo ya Maendeleo Endelevu katika jamii," alisema Bw. Milišić.

Maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuwekeza leo kwa ajili ya kesho kwa kuinua vijana wa Kitanzania”. Maadhimisho hayo yataongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki, (Mb.).

Mratibu Mkazi wa UN Tanzania, Bw. Zlatan Milišić akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianmo wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam

Mratibu Mkazi wa UN Tanzania, Bw. Zlatan Milišić akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianmo wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda. 

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianmo wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.