Friday, October 20, 2023

RAIS DKT. MWINYI AFUNGUA KIKAO CHA 77 CHA TUME YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea na jitihada mbalimbali katika kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kutekelezwa kwa mujibu wa mikataba ambayo Tanzania ni mwanachama.

 

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati akifungua Kikao cha 77 cha Kawaida cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kilichofanyika jijini Arusha tarehe 20 Oktoba 2023.

 

Mhe. Dkt. Mwinyi ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi  wa kikao hicho amesema kuwa jitihada za Serikali za kulinda na kuimarisha haki za binadamu zimewezesha kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya upatikanaji wa haki mbalimbali zikiwemo haki ya usawa mbele ya sheria, uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kuabudu, haki ya kumiliki mali, na uhuru wa vyombo vya habari.

 

“Kwa taarifa ni kwamba kutokana na uhuru huo wa vyombo vya habari, hivi sasa Tanzania ina vyombo vya habari vingi ikiwemo Radio 210,Televisheni 56, Magazeti 288 pamoja na mitandao mbalimbali ya kijamii. Pia tumefikia hatua kubwa ya kuimarika kwa uhuru wa kidemokrasia, haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia,” amesema Mhe. Rais Dkt. Mwinyi.

 

Kadhalika ameongeza kusema,  Tanzania na Afrika kwa ujumla  inaheshimu haki za binadamu na watu kwa kuzingatia utamaduni, maadili na tunu kama waafrika ambapo katika kutekeleza jukumu hili Serikali ya Tanzania inasimamia haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kanuni na taratibu zilizopo.

 

“Katika Katiba yetu, haki za binadamu zimeainishwa kuanzia Ibara ya 12 hadi 24 lakini pia Katiba yetu kuanzia Ibara ya 25 hadi 30 imeanisha wajibu wa kila raia” amesisitiza Mhe. Rais Dkt. Mwinyi.

 

Pia ameeleza kuwa katika kuhakikisha haki za binadamu na watu zinalindwa na kutetewa kikamilifu hapa nchini, Serikali ilianzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo ni Taasisi ya Kitaifa yenye jukumu la kulinda, kutetea na kuhifadhi haki hizo.

 

Akizungumzia hali ya ulinzi wa haki za binadamu barani Afrika amesema bado jitihada za pamoja zinahitajika ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazorejesha nyuma jitihada hizo ikiwemo mapinduzi ya Serikali zilizo madarakani, vita vya wenyewe kwa wenyewe, mila na desturi zisizofaa, ukatili wa kijinsia, athari hasi za utandawazi na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu haki zao.

 

Mhe. Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo pia kuwahamasisha washiriki kutenga muda wao na kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana kote nchini pamoja na Zanzibar.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Prof. Remy Ngoy Lumbu ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuheshimu haki za binadamu na kuitaja  amani iliyopo kama alama na kielelezo cha ulinzi wa haki  hizo za binadamu.

“Nchi hii inaheshimu haki za binadamu na amani inatawala. Tanzania ina utamaduni wa kutatua changamoto zao kwa njia ya amani na katika hili tunapaswa kujifunza” alisisitiza Mhe. Lumbu.

 

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Mwinyi imeendelea kulinda na kuheshimu haki za binadamu kwa kuboresha mazingira na huduma za kijamii ikiwemo afya, maji, miundombinu na elimu.

 

Awali akimkaribisha Mhe. Dkt. Mwinyi kuzungumza, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kikao hicho muhimu kufanyika nchini na kwamba kikao hicho pamoja na mambo mengine kitajadili namna bora ya kuendelea kusimamia masuala ya haki za binadamu na watu barani Afrika.

 

Pia Mhe. Dkt. Chana amesema kikao hicho ambacho kilitanguliwa na vikao viwili vya Asasi za kiraia na Taasisi za Haki za Bianadamu, kimehudhuriwa na takribani wadau 1,000 kutoka Serikalini, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Asasi za Kiraia, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akifungua rasmi Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha tarehe 20 Oktoba 2023. Mhe. ais Dkt. Mwinyi alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi huo. Kikao hicho kitafanyika kuanzia tarehe 20 Oktoba 2023 hadi 09 Novemba 2023
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 20 Oktoba 2023 hadi 09 Novemba 2023.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu

Mwenyekiti wa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Mhe. Prof. Remy Ngoy Lumbu naye akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu
Sehemu ya Viongozi na wageni waalikwa wakishiriki Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu
Sehemu nyingine ya washiriki

Picha ya pamoja




 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.