Serikali ya Tanzania
itaendelea kukuza na kuhamasisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili ili kuimarisha
biashara inayovuka mipaka hususan katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) ikiwemo Malawi.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe.
Agnes Kayola alipokitembelea Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha nchini humo
kwa lengo la kujadiliana na Uongozi wa Chuo hicho kuhusu namna bora ya
kuanzisha ushirikiano baina na taasisi za elimu za Tanzania hususani katika
kufundisha Lugha ya Kiswahili.
Katika mazungumzo yake na Mkuu wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya
Habari wa Chuo hicho, Dkt. Kizito Elijah, Mhe. Balozi Kayola alisema kuwa, upo
mwingiliano mkubwa wa kibiashara baina ya Tanzania na Malawi unaosababisha
mahitaji makubwa ya kujifunza lugha ya Kiswahili ili kurahisisha mawasiliano
katika biashara.
Aliongeza kusema Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia na kutekeleza makubaliano
yote yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini humo mwezi Julai 2023 ikiwemo
masuala ya ufundishaji wa Kiswahili nchini Malawi.
Kwa upande wake, Dkt. Elijah alisema kuwa, Chuo hicho kimepanga kuanzisha Kituo
cha Lugha na kuonesha nia ya kushirikiana na Tanzania hususan Taasisi za Elimu
na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ili kutekeleza azma ya kufundisha
Lugha ya Kiswahili chuoni hapo na kwamba chuo hicho kipo tayari kuanzisha
ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Tanzania ikiwa ni pamoja na kubadilishana
wakufunzi na wanafunzi.
Wakati huohuo, Mhe. Balozi Kayola ameitembelea Kampuni ya Kitanzania ya
Bakhresa ambayo imewekeza nchini Malawi tangu mwaka 2003 katika viwanda vya
uzalishaji Unga wa ngano, sabuni za kufulia na inatarajia kukamilisha kiwanda
cha kutengeneza mafuta ya kupikia mwezi Mei 2024.
Akiwa katika Kampuni hiyo Mhe. Balozi Kayola amepongeza uwekezaji mkubwa
uliofanyika na kuwahamasisha kuendelea kukuza wigo wa uwekezaji wa bidhaa
mbalimbali nchini humo kwani mahitaji bado ni makubwa.
Kadhalika, Mhe. Balozi Kayola alipata fursa ya kukutana na Jumuiya ya
Watanzania waishio katika Mkoa Kusini, Malawi ikiwa ni mara yake ya kwanza
tangu ateuliwe kuiwakilisha Tanzania nchini humo.
Katika mazungumzo yake na Jumuiya hiyo aliwaasa kuendelea kuwa wawakilishi
wazuri wa nchi yao kwa kufuata sheria za nchi waliyopo ili kulinda
taswira nzuri ya Tanzania.
Pia alisisitiza umuhimu wa wao kuendelea kujiandikisha kwenye Mfumo wa
Kidigitali wa kuwatambua Diaspora (Diapora Digital Hub) ili iwe rahisi
kuwaunganisha na fursa mbalimbali za biashara, masoko, na uwekezaji zilizopo
nchini pamoja na kurahisisha utoaji wa msaada wakati wa dharura zinazoweza
kuwapata katika nchi wanazoishi.
Mhe. Balozi Kayola alitumia fursa hiyo pia kuwajulisha kuhusu hatua kubwa ya
maendeleo iliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.
Rais Dkt. Samia huku akitaja Miradi mikubwa inayokamilishwa ikiwemo Mradi wa
Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere, Mradi wa Reli ya Kisasa ya SGR na miradi
mingine kwenye sekta ya Kilimo, Biashara na Uwekezaji.
Vilevile, Mhe. Balozi Kayola aliwaeleza Diapora hao kuwa, Ubalozi upo tayari
kushirikiana nao na kuwasisitiza kuwa huru katika kuwasilisha maoni,
mapendekezo na ushauri kwa manufaa mapana ya Tanzania.
|
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola akizungumza na Mkuu
wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya Habari wa Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha Malawi, Dkt.
Kizito Elijah alipokitembelea Chuo hicho kwa lengo la kujadiliana na
Uongozi wa Chuo hicho kuhusu namna bora ya kuanzisha ushirikiano baina na
taasisi za elimu za Tanzania hususani katika kufundisha Lugha ya Kiswahili. |
|
Mkuu
wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya Habari wa Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha Malawi, Dkt.
Kizito Elijah wakati wa mkutano kati yake na Balozi Kayola (hayupo pichani)
|
|
Mhe. Balozi Kayola akiagana na Dkt. Elijah mara baada ya kukamilisha mazungumzo baina yao | |
|
|
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola akipata maelezo alipotembelea Kampuni ya Kitanzania ya Bakhresa iliyowekeza nchini Malawi tangu mwaka 2003 kwenye viwanda vya kutengeneza unga wa ngano na sabuni za kufulia.
|
|
Mhe. Balozi Kayola akiendelea kupata maelezo wakati wa ziara yake kwenye moja ya kiwanda cha Kamapuni ya Kitanzania ya Bakhresa ambayo imewekeza nchini Malawi
|
|
Mhe. Balozi Kayola akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Kampuni ya Bakhresa Malawi Limited akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw. Mahesh Josyabhatla (wa pili kulia)
|
|
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola akizungumza na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Mkoa wa Kusini mwa Malawi alipowatembelea kwa ajili ya kujitambulisha ikiwa ni mara ya kwanza tangu ateuliwe kuiwakilisha Tanzania nchini humo
|
|
Sehemu ya Watanzania wanaoishi Mkoa wa Kusini, Malawi wakifuatilia mkutano kati yao na Mhe. Balozi Kayola (hayupo pichani)
|
|
Mwenyekiti wa Watanzania wanaoishi Mkoa wa Kusini Malawi, Bw. Suleiman Marijani akizungumza wakati wa Mkutanoo kati ya Jumuiya hiyo na Balozi Kayola
|