Friday, February 9, 2024

DKT. SHELUKINDO AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KUSHIRIKI MKUTANO WA KAMATI YA SIASA NA DIPLOMASIA YA SADC

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa Kamati ya Siasa na Diplomasia (Inter-State Politics and Diplomacy Committee — ISPDC) ya SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 09 Februari, 2024.

Mkutano huo umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Bi. Etambuyu Gundersen ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Makatibu Wakuu ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.

Mkutano huo uliitishwa kujadili masuala ya kisiasa na diplomasia katika kanda. Aidha, Mkutano umetoa salamu za pole kwa Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Namibia kufuatia kifo cha Hayati Dkt. Hage Geingob, Rais wa Jamhuri ya Namibia na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama kilichotokea hivi karibuni.






RAIS WA POLAND AWASILI TANZANIA KWA ZIARA YA KITAIFA

 











Rais wa Jamhuri ya Poland, Mheshimiwa Andrzej Duda amewasili nchini kwa Ziara ya Kitaifa ya siku mbili.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais Duda na mkewe Agata Kornhauser-Duda wamepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba, Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Mudrick Soraga na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.

Ziara hii ni ya kwanza kwa Rais kutoka Poland kutembelea Tanzania tangu kuanza kwa ushirikiano wa uwili kati ya nchi hizi ikilenga kuimarisha ushirikiano katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta za kilimo, kodi, viwanda na biashara, utalii, elimu, usafiri, afya, tiba za mifugo, na maji.

Kwa kupitia ziara hii maeneo mapya ya ushirikiano yataibuliwa kati ya Tanzania na Poland kupitia sekta za ulinzi na usalama, nishati, madini, ulinzi wa mitandao, utamaduni na uchumi wa buluu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan atampokea rasmi Rais Duda Ikulu, Dar es salaam Februari 9, 2024 kwa mazungumzo na baadaye watazungumza na waandishi wa habari.

Akiwa nchini, Rais Duda anatarajiwa kutembelea mradi wa matibabu ya dharura katika Hospitali ya Aghakhan, Dar es Salaam kujionea utekelezaji wa mradi huo ambao Serikali ya Poland imetoa msaada wa Dola za Kimarekani milioni 1.136  kufadhili mradi huo wenye lengo la kutoa msaada kwa sekta ya matibabu na kusaidia elimu ya wahudumu wa afya katika mkoa wa Dar es Salaam.




Thursday, February 8, 2024

DKT. KIBESSE ATETA NA GAVANA WA KAUNTI YA KISUMU

Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse amefanya ziara katika Kaunti ya Kisumu ambapo pamoja na mambo mengine, amekutana kwa mazungumzo na Gavana wa Kaunti ya Kisumu – Kenya, Mhe. Prof. Peter Nyon’go, tarehe 8 Februari 2024. 

 Balozi Kibese na Gavana Nyong’o wamekubaliana kuandaa mkutano wa ujirani mwema kati ya mikoa ya Tanzania na Kenya inayopakana kwenye eneo la Ziwa Victoria ili kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano wa kijamii, kibishara na kiusalama katika maeneo hayo ikiwemo mikoa ya Mwanza na Mara kwa upande wa Tanzania na Kisumu na Migori kwa upande wa Kenya

Vilevile wamekubaliana kufuatilia mpango wa kuwa na miundombinu ya barabara inayopita kwenye mwambao wa Ziwa Victoria upande wa Tanzania na Kenya.

Gavana wa Kaunti ya Kisumu – Kenya, Mhe. Prof. Peter Nyon’go akizungumza na  Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Bernard Kibesse (kushoto) alipomtembelea Ofisini kwake katika Kaunti ya Kisumu




WAZIRI MAKAMBA AKUTANA NA KATIBU WA NEC SIASA NA UHUSIANO WA KIMATAIFA WA CCM

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amekutana kwa mazungumzo na Katibu wa NEC Siasa na uhusiano wa kimataifa (SUKI), Ndugu Rabia Abdallah Hamid katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Lengo la kikao cha viongozi hao ni kuangalia jinsi ambavyo Wizara inavyotekeleza Diplomasia ya Uchumi na uhusiano wa Kimataifa kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). 






Tuesday, February 6, 2024

WAZIRI MAKAMBA AKUTANA NA VIONGOZI WA TAASISI YA AMANI YA MARTI AHTISAARI.

 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akizungumza na Balozi wa Finland nchini Mhe. Thereza Zitting walipokutana  katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam na kuzungumza na wawakilishi wa taasisi ya Amani ya Martti Ahtisaari.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akizungumza alipokutana na Balozi wa Finland nchini Mhe. Thereza Zitting na wawakilishi wa taasisi ya Amani ya Martti Ahtisaari (hawapo katika picha) walipokutana  katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam.


 Balozi wa Finland nchini Mhe. Thereza Zitting akizungumza katika kikao na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba walipokutana  katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam na kuzungumza na wawakilishi wa taasisi ya Amani ya Martti Ahtisaari.

Mkuu wa Taasisi ya Marrti Ahtisaari Kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara Bi. Tiina Kukkamaa-Bah akizungumza katika kilichofanyika katika Ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam kati ya taasisi hiyo na Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akizungumza katika na Balozi wa Finland nchini Mhe. Thereza Zitting  na wawakilishi wa taasisi ya Amani ya Martti Ahtisaari walipokutana  katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akizungumza katika picha ya pamoja na Balozi wa Finland nchini Mhe. Thereza Zitting  na wawakilishi wa taasisi ya Amani ya Martti Ahtisaari walipokutana  katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


 


                
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba amekutana na kuzungumza na viongozi wa taasisi ya Amani ya Martti Ahtisaari katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana na kufanya kazi pamoja ili kumuenzi na kuendeleza falsafa ya Mwanzilishi wa Taasisi hiyo na  Rais wa zamani wa Finland Haya Martti Ahtisaari katika kutafuta amani na kutatua migogoro duniani.

Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Waziri Makamba amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na taasisi hiyo ili kuendelea kuenzi azma ya hayati Martti Ahtasaari ya kutafuta amani na kutatua migogoro duniani.

“Tupo tayari kufanya kazi na taasisi yenu, tuko tayari kuandaa makubaliano rasmi kupitia Kituo cha Uhusiano cha Kimataifa. Pia, tuko tayari kuendelea kuwa marafiki wakubwa na kushiriki katika mashauriano kuhusu jinsi taasisi yenu itakavyoona inafaa, tunaweza kufuatilia jitihada za kutafuta amani katika eneo la ukanda wetu,” alisema Mhe. Waziri Makamba.

Balozi wa Finland nchini Mhe. Theresa Zitting  alisema Finland iko tayari kushirikiana na kufanya kazi na Tanzania kwa kuwa wanaona kuna nafasi Tanzania inaweza kushiriki katika kutafuta amani na usalama.

Naye Mkuu wa Taasisi ya Marrti Ahtisaari Kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara Bi. Tiina Kukkamaa-Bah amesema Tanzania na viongozi wake walikuwa marafiki wazuri wa muasisi wa taasisi yao na kwa hali hiyo ndio maana wanapanga kushirikiana na Tanzania ili kuunga mkono jitihada za muanzilishi wao kutafuta amani na usalama katika eneo  la Kusini mwa jangwa la Sahara kupitia Ukanda wa Maziwa Makuu, SADC, Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Taasisi ya Martti Ahtisaari ni shirika lisilo la kiserikali la nchini Finland linalofanya kazi ya kuzuia na kutatua migogoro kupitia mazungumzo  na upatanishi, ilianzishwa mwaka 2000 na Rais wa zamani wa Finland na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Hayati Martti Ahtisaari.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


 

Monday, February 5, 2024

USHAWISHI WA TANZANIA DUNIANI UTATEGEMEA NA UBORA WA SERA YA MAMBO YA NJE INAYOREKEBISHWA

    Imeelezwa kuwa ili Tanzania iweze kufikia malengo ya Maendeleo iliyojiwekea, lazima iwe na Sera Bora ya Mambo ya Nje inayozingatia maoni na matakwa ya makundi yote ya wadau nchini. 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Ikulu Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Kongamano la wadau la kukusanya maoni kuhusu marekebisho ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 lililofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar tarehe 05 Februari 2024. 

Kongamano hilo ambalo ni la tatu kufanyika ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kushirikisha wananchi kutoa maoni yatakayozingatiwa katika zoezi la kurekebisha Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001. 

Mwenye dhamana ya kusimamia Sera hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) ametaja sababu za Wizara yake kuratibu makongamano hayo ambapo alisema linalofuata litafanyika Pemba tarehe 10 Februari 2024.

Alieleza kufanyika kwa makongamano hayo ni utekelezaji wa misingi ya utawala bora ambayo inasisitiza umuhimu wa kushirikisha wadau katika utungaji wa Sera za nchi, ikiwemo Sera ya Mambo ya Nje. 

Alieleza pia kuwa Sera ni Tamko linalotoa mwongozo namna nchi itakavyoshughulikia ushirikiano na uhusiano wake na dunia. Hivyo, utungaji wa Tamko muhimu kama hilo lazima lishirikishe wadau wote. 

Mhe. Makamba aliwambia washiriki wa Kongamano hilo kuwa Tanzania ina ushawishi mkubwa duniani tofauti na nguvu zake za kiuchumi na kijeshi kutokana na kuwa na Sera bora ya Mambo ya Nje. Hivyo, ili iendelee kuwa na ushawishi huo duniani lazima itungwe Sera imara itakayozingatia maoni ya wadau wote.

Aliendelea kueleza kuwa Sera ya Mambo ya Nje ina uhusiano wa moja kwa moja na malengo ya Maendeleo ya nchi. Hivyo, mchakato wa utungaji wa Sera ya Mambo ya Nje lazima ushirikishe wadau kwa kuwa maendeleo ni jambo linalomgusa kila mmoja. 

Alihitimisha hotuba yake kwa kutaja baadhi ya mambo yaliyosababisha Serikali kufanya marekebisho ya Sera hiyo. Mambo hayo ni pamoja na mabadiliko yanayotokea duniani kama mabadiliko ya tabianchi, uvumbuzi wa teknolojia mpya, kuibuka kwa wadau wapya wa maendeleo wenye nguvu na ushawishi na Watanzania wengi hawakuwepo wakati wa utungaji wa Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001. 

Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe. Idrisa Mustafa Kitwana: Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Ikulu Zanzibar, Bw. Salehe Juma Mussa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Balozi Stephen Mbundi, Naibu Katiibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa, Mabalozi wa Tanzania Nje ya Nchi, Mabolozi Wastaafu akiwemo Balozi Amina Salum Ali, viongozi wa Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia, Wakuu wa taasisi za Serikali na Sekta Binafsi, Wakuu wa Vyombo vya habari, wanazuoni na wananchi kwa ujumla. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu-Zanzibar, Mhe.  Ali Suleiman Ameir akitoa hotuba ya ufunguzi ya Kongamano la Wadau kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 lililofanyika Hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar tarehe 05 Februari 2024
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akitoa neno wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wadau kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 lililofanyika Hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar tarehe 05 Februari 2024

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Ikulu Zanzibar, Bw. Salehe Juma Mussa akitoa neno wakati wa 
Kongamano la Wadau kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 lililofanyika Hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar tarehe 05 Februari 2024

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa akimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba kuhutubia Kongamano la Wadau kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 lililofanyika Hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar tarehe 05 Februari 2024

Watu mbalimbali walioshiriki Kongamano la Wadau kuhusu kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 lililofanyika Hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar tarehe 05 Februari 2024
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Justin Kisoka akiwasilisha mada kuhusu maeneo muhimu yanayopendekezwa katika marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje

Wadau mbalimbali wakifuatilia Kongamano la kukusanya maoni ya marekebisho ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 lililofanyika Hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar tarehe 05 Februari 2024





Wednesday, January 31, 2024

BALOZI MBAROUK APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA KWA BALOZI MTEULE WA BURUNDI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Leontine Nzeyimana.

Akipokea Nakala hizo Mhe. Mabarouk amemuhakikishia Mhe. Nzeyimana ushirikiano wa dhati utakaomwezesha kuitumikia Burundi kwa tija katika muda wake wa uwakilishi hapa nchini.

Vilevile, alieleza kuwa Tanzania na Burundi licha ya kuwa na ushirikiano wa ujirani pia ni ndugu kufuatia mwingiliano wa wananchi wa Nchi hizi mbili hususan kwenye masuala ya biashara.

“Tanzania itaendelea kuweka mikakati imara ya kukuza ushirikiano wa kibiashara sambamba na kusimamia ujenzi wa miundombinu inayounganisha nchi hizo ili kurahisisha shughuli za usafirishaji”. Mhe. Balozi Mbarouk

Naye Balozi Mteule, Mhe. Leontine Nzeyimana alishukuru kwa mapokezi mazuri aliyopata tangu alipowasili nchini na kwamba ana matumaini makubwa ya kupata ushirikiano utakaomwezesha kutekeleza majukumu yake ya uwakilishi kikamilifu.

Viongozi hao pia wamekubaliana kuendelea kuratibu utekelezaji wa makubaliano yaliyoafikiwa na Nchi zao kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ili kuleta tija kwa pande zote.

Pamoja na mambo mengine, kupitia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Burundi nchini, Mhe. Evaristi Ndayishimye Tanzania ilikabidhi eneo la bandari kavu katika eneo la Kwala mkoani Pwani ili kukuza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo.

Asilimia 95 ya mizigo ya Burundi husafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam hivyo, bandari kavu ni chachu kubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akisalimiana na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana katika Ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana katika Ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma
Picha ya pamoja

WAZIRI MAKAMBA ANADI FURSA ZA BIASHARA, UWEKEZAJI ITALIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amenadi fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana nchini katika mkutano wa wafanyabiashara, viongozi wa siasa na wa kijamii nchini Italia.

Katika mkutano huo, Waziri Makamba amewaeleza wafanyabiashara na wawekezaji wa Italia fursa mbalimbali za biashara zinazopatikana nchini  pamoja na mageuzi makubwa ya kuboresha mazingira ya uwekezaji yanayofanyika chini ya Uongozi imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Makamba amesema mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ni salama na rafiki kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ili kuhakikisha wafanyabiashara wanatekeleza majukumu yao katika mazingira rafiki na salama. 

Kadhalika Waziri Makamba amesema kuwa Tanzania inazingatia misingi ya utawala bora pamoja na kuzungukwa na nchi saba ambazo hazina bandari na hivyo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma kwenda katika nchi hizo.

Waziri Makamba ameongeza kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ya Tanzania ni salama kwa sababu Tanzania imeridhia sheria na mikataba ya kimataifa inayolinda mitaji na uwekezaji wa kigeni pamoja na Serikali kutambua sekta binafsi kama injini ya maendeleo ya kiuchumi.

“Napenda kuwasihi wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Italia kuja kuwekeza Tanzania kwani licha ya kuwa na mzingira salama, pia kuna fursa za kuwekeza katika sekta mbalimbali kama nishati, utalii, kilimo, afya na elimu,” alisema Waziri Makamba.

Kadhalika, Waziri Makamba ameongeza kuwa kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa Soko Huru la pamoja la Afrika (AfCFTA) ambalo linahusisha watu zaidi ya bilioni 1.5 hali ambayo itawezesha wafanyabiashara wa Italia kuwafikia watu hao kupitia soko hilo.

Waziri Makamba amesema kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Italia katika kutekeleza Mpango wa Mattei kwa maslahi ya pande zote mbili, na kuwasisitiza kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji nchini Tanzania na visiwani Zanzibar. 

Akiongea awali katika mkutano huo, Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari amesema kuwa utekelezaji wa mpango wa Mattei utakapoanza utazingatia maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na wadau ambapo miradi ya kipaumbele kwa nchi nane za awali za Afrika ikiwemo Tanzania. 

Tanzania ni moja kati ya nchi nane za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha  Euro bilioni 5 za awali kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiteta jambo na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari katika ofisi za chama hicho, Jijini Roma Italia



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na  wafanyabiashara, viongozi wa siasa na wa kijamii nchini Italia



Tuesday, January 30, 2024

TANZANIA YASISITIZA MPANGO WA MATTEI UZINGATIE MAHITAJI STAHIKI YA AFRIKA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mhe. January Makamba (Mb.) ambaye anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia amesisitiza umuhimu wa mpango wa Mattei kuzingatia mahitaji sahihi ya Afrika ili uweze kuleta matokeo stahiki barani Afrika.

Mheshimiwa Makamba alieleza kuwa mpango huo ukizingatia mahitaji stahiki ya Afrika changamoto nyingi zinazokabili nchi zilizoendelea zinazosababishwa na ukosefu wa maendeleo barani Afrika zitaondoka.

Awali akihutubia katika mkutano wa Nne wa Italia-Afrika, Waziri Mkuu wa Italia, Mhe. Giorgia Meloni amesema mpango wa Mattei utagusa masuala ya usalama wa nishati na matumizi ya nishati mbadala, maendeleo ya miundombinu, usalama wa chakula, elimu na mafunzo ya ufundi pamoja na kupambana na wahamiaji haramu, ameeleza 

Serikali ya Italia inatarajia kushiriki kwa kiasi kikubwa kukuza maendeleo barani Afrika kwa kupitia Mpango wake Mpya wa Mattei.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat ameomba Afrika ipewe muda wa kuchanganua Mpango wa Mattei kwanza kabla ya kuanza utekelezaji wa mpango huo.

"Tunahitaji kubadilisha maneno kuwa vitendo kwa sababu ni vyema tukajadiliana na kuona ni njia gani zinatumika kutekeleza miradi inayopendekezwa katika Mpango wa Mattei ili kuepuka kuwa na furaha na ahadi ambazo hazitekelezwi,” amesema Mahamat.

Viongozi wakuu wa baadhi ya nchi za Afrika; mawaziri, maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa, wawakilishi kutoka taasisi na mashirika ya kimataifa wafanyabiashara pamoja na mashirika ya kifedha wameshiriki mkutano huo unaoendelea Roma, Italia.

Waziri Mkuu wa Italia, Mhe. Giorgia Meloni akihutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akishiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia. Katika Mkutano huo, Mhe. Makamba anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Viongozi mbalimbali walioshriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia wakiwa katika picha ya pamoja







Monday, January 29, 2024

TANZANIA KUNUFAIKA NA MIRADI YA MPANGO WA MATTEI

Tanzania imechaguliwa kuwa moja ya nchi nane za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha  Euro bilioni 5 za awali kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Miradi hiyo ya kipaumbele kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ipo katika sekta ya nishati, elimu na kilimo.

Taarifa hiyo imetolewa na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) pembezoni mwa Mkutano wa Nne wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia unaendelea Roma, Italia.  

Mhandisi Cestari alieleza kuwa utekelezaji wa mpango huo utaanza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika na Italia, ambapo Serikali ya nchi hiyo itafadhili miradi ya kipaumbele kwa nchi nane za awali za Afrika. Hatua hiyo itahusisha pia kugharamia gharama za upembuzi yakinifu ya miradi itakayopendekezwa. 

Kama hatua ya utekelezaji ya mpango huo, ujumbe wa wataalam kutoka Chemba ya Biashara ya Italia ikiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Mhe. Dkt. Edmondo Cirielli unatarajiwa kuwasili nchini Tanzania ndani ya mwezi mmoja kwa ajili ya kukutana na timu ya wataalam ya upande wa Tanzania kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali za utiaji saini wa ushirikiano huo wa pande mbili utakaohusisha utekelezaji wa miradi itakayopitishwa na pande mbili. 

“Serikali ya Italia imetenga kiasi cha Euro bilioni 5 za awali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo katika nchi nane za kipaumbele za Afrika ikiwemo Tanzania,” alisema Mhandisi Cestari. 

Kwa Upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ameipongeza Serikali ya Italia kwa kuonesha nia ya kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ambapo sekta ya nishati, elimu na kilimo zimepewa kipaumbele. 

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo umelenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili kupitia mpango mpya wa Mattei, (Mattei Plan).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Ujumbe wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italian ukiongozwa na Rais wa Chama hicho, Mhandisi Alfredo Cestari pamoja na  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Mhe. Dkt. Edmondo Cirielli




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari 































Sunday, January 28, 2024

WAZIRI MAKAMBA ATETA NA MKURUGENZI MKUU IOM

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amekutana  kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope jijini Roma, Italia.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Makamba ameipongeza IOM kwa kazi inazofanya nchini katika masuala ya Uhamiaji na amemuhakikishia Bi. Pope kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kufanya kazi na Shirika hilo kwa ukaribu zaidi.

Mhe. Waziri Makamba amesema Shirika hilo limekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala ya wakimbizi, majanga ya asili na kwamba ni matumaini yake kuwa Tanzania na IOM zitaendelea kushirikiana kwa manufaa ya pande zote mbili.

Waziri Makamba ameipongeza IOM kwa kuendelea na zoezi la kuwarejesha nyumbani raia wa Ethiopia waliokuwa katika magereza mbalimbali nchini na kuongeza kuwa kitendo hicho kimesaidia Tanzania kukabiliana na changamoto ya msongamano wa watu katika magereza yake.

Kwa upande wake, Bi. Pope ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa jinsi inavyoshirikiana na Shirika la IOM katika kutekeleza majukumu yake na kuahidi kuwa na mpango maalum wa kuendeleza ushirikiano  na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha majukumu yake. Aliongeza kuwa Shirika hilo litahakikisha kuwa wahamiaji wanapata haki zao za msingi na kuwa katika mazingira salama nchini.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope jijini Roma, Italia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akimfafanulia jambo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope Jijini Roma, Italia

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba walipokutana kwa mazungumzo Jijini Roma, Italia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope Jijini Roma, Italia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (IOM) Bi. Amy Pope baada ya kumaliza kikao chao Jijini Roma, Italia