Monday, April 22, 2024

RAIS SAMIA ARIDHISHWA NA KAZI YA MABALOZI NA KUWATAKA KUONGEZA JUHUDI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwahutubia Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania sehemu mbalimbali duniani waliokusanyika mjini Kibaha kwa warsha ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje

Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapongeza Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani kwa kazi nzuri ya uwakilishi ambayo inaonekana kwa kuongezeka kwa masoko ya bidhaa za Tanzania, biashara, uwekezaji, utalii na teknolojia nchini.

Mhe. Rais Samia ametoa pongezi hizo leo Aprili 22, 2024 alipokuwa anawahutubia Mabalozi hao kwa njia ya mtandao ambao wamekusanyika mjini Kibaha kwa warsha ya siku 4 ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje iliyoanza Aprili 21 na itakamilika Aprili 24, 2024.

Mhe. Rais Samia amesema kuwa nchi inawategemea sana Mabalozi katika utekelezaji wa majukumu yao Ili iweze kusonga mbele kiuchumi na kwa kuliona hilo, Rais Samia amesema amechukua hatua mbalimbali ili kuibadilisha Wizara ya Mambo ya Nje iwe ya kisasa zaidi na kuwa na uwezo wa kuitangaza nchi.

Lengo la Mabadiliko hayo ni kuifanya nchi iendelee kuheshimika na kuwa na ushawishi zaidi duniani kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma wakati wa harakati za ukombozi na baada ya ukombozi.

Hatua ambazo Mhe. Rais Samia alizitaja kuwa ni pamoja na kuteua Naibu Waziri na Katibu Mkuu wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, kuanzisha Idara ya Diplomasia ya Uchumi, kusaini mikataba ya Kuzuia Utozaji wa Kodi mara Mbili na Kulinda Vitega Uchumi na nchi mbalimbali duniani, kuridhia mkakati wa uendelezaji wa majengo ya ofisi za Mabalozi na makazi na mchakato wa uboreshaji wa Sera ya Mambo ya Nje na Hadhi Maalum kwa raia wenye asili ya Tanzania wanaoishi Nje ya nchi ambao umefikia hatua nzuri.

Mhe. Rais aliwasihi Mabalozi kuwa jicho la Tanzania kwenye maeneo yao ya uwakilishi ili nchi isipitwe na mabadiliko makubwa yanayotokea duniani. 

Mhe. Rais pia alizungumzia misingi sita ya Sera ya Mambo ya Nje ambayo Nchi yetu inaisimamia tangu ilipopata uhuru na kutufikisha hapa tulipo. Aliitaja misingi hiyo kuwa ni pamoja na kulinda uhuru wa kujiamulia, kuheshimu mipaka ya nchi; kulinda uhuru, haki za binadamu na usawa wa kidemokrasia; kudumisha ujirani mwema; kuunga mkono Umoja wa Mataifa, kuendeleza mshikamano wa Umoja wa Afrika na kuunga mkono Sera ya kutofungana na Upande Wowote.

Rais Samia aliwambia mabalozi katika maboresho ya Sera ya Mambo ya Nje yanayoendelea, amependekeza kuongeza msingi wa saba ambao ni kulinda maslahi ya kiuchumi na maadili ya watu. Katika msingi huu, Mhe. Rais alisisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali za nchi yetu na utamaduni wake. Alisema nchi yetu imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwemo madini hadimu. Alisema endapo nchi haitakuwa na mpango madhubuti wa kulinda rasilimali hizo na kunufaifika nazo, basi badala ya kuwa fursa kwa Taifa zinaweza kugeuka kuwa janga.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kulinda Utamaduni wetu kwani kuna juhudi za makusudi zinazoendelea duniani za kulazimishwa tamaduni zilizo kinyume na maadili yetu.

Mhe. Rais Samia alihitimisha hotuba yake kwa kuwakumbusha Mabalozi kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pande mbili, Tanzania Bara na Zanzibar, hivyo katika majukumu yao ya uwakilishi, wakumbuke vipaumbele vya Zanzibar, hususan kukuza utalii na uchumi wa buluu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwahutubia Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania sehemu mbalimbali duniani waliokusanyika mjini Kibaha kwa warsha ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje
Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania sehemu mbalimbali duniani waliokusanyika mjini Kibaha kwa warsha ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje wakifurahia jambo wakati Rais wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwahutubia kwa njia ya mtandao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwahutubia Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania sehemu mbalimbali duniani waliokusanyika mjini Kibaha kwa warsha ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje
Mabalozi wakifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan
Sehemu ya Mabalozi na Viongozi wa Wizara wakifurahia jambo wakati Rais wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwahutubia kwa njia ya mtandao.

Sehemu ya mabalozi wa wakifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kwa njia ya mtandao.
Sehemu ya mabalozi wa wakifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kwa njia ya mtandao.
Sehemu ya mabalozi wa wakifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kwa njia ya mtandao.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwasilisha mada kwenye warsha ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje
Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwasilisha mada kwenye warsha ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania sehemu mbalimbali duniani kwanjia ya mtandao waliokusanyika mjini Kibaha kwa warsha ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje
Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwasilisha mada kwenye warsha ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje
Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwasilisha mada kwenye warsha ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje







Saturday, April 20, 2024

MABALOZI WA TANZANIA WAJIFUNGIA KIBAHA KUTAFAKARI NA KUJIPANGA UPYA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na Mabalozi kuelekea warsha inayotarajiwa kuanza tarehe 21 Aprili 2024 mjini Kibaha, Pwani

Mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani na Wakuu wao wa utawala wamejifungia katika Chuo cha Uongozi Cha Mwalimu Julius Nyerere mjini Kibaha kwa siku 4 kuanzia tarehe 20 hadi 24 Aprili 2024. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) ametaja sababu za kujifungia huko kuwa ni pamoja na kukutana kama familia ya wanadiplomasia wa zamani na wa sasa ili kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ambayo imejikita katika diplomasia ya uchumi.

Mhe. Makamba alisema kazi ya diplomasia ni moja ya kazi muhimu duniani na kupitia kazi hiyo Tanzania imejitangaza na kusikika, hasa kupitia misimamo yake na umahiri wa wanadiplomasia iliyokuwa nao.

Hivyo, vikao hivyo ni muhimu kwa ajili ya kupata mwendelezo huo, kwani vinatoa fursa ya kutafakari upya na kupanga mikakati ya namna bora zaidi ya kutekeleza majukumu ya Wizara hiyo ambayo ni moja ya nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi nchini.

Alisema mfumo wa kikao hicho ambao ni tofauti kabisa na mifumo ya vikao vilivyofanyika miaka ya nyuma ni kwamba wanadiplomasia watapewa fursa ya kubadilishana kinaga ubaga changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao, kutafakari kwa pamoja namna bora ya kuzitafutia ufumbuzi na baadaye kuweka mpango kazi wa utekelezaji. 

Aliwahakikishia kuwa Serikali itajitahidi kutoa nyenzo ilizo nazo ili kazi hiyo muhimu iweze kutekelezwa na kuleta matokeo chanya yanayotarajiwa.

"Tutafakari majukumu yetu, masuala mahususi ya kuzingatia pamoja na kutathimini nyenzo zetu za utekelezaji ili wote tuwe katika uelewa na mwelekeo mmoja wa kufanikisha malengo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mama yetu, Mwana diplomasia namba moja, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan". Mhe. Makamba alisema.

Warsha hiyo ya Mabalozi inajumuisha pia Makatibu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara wakiongozwa na Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Wakurugenzi, Wakurugenzi Wasaidizi, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na baadhi ya wadau wanaoshirikiana kwa karibu na Wizara katika utekelezaji wa majukumu ya Diplomasia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza kwenye kikao kazi kuelekea warsha ya Mabalozi inayotarajiwa kuanza tarehe 21 Aprili 2024 mjini Kibaha, Pwani
Sehemu ya Mabalozi wakifurahia jambo wakati Waziri Makamba akizungumza kwenye kikao cha maandalizi kuelekea warsha ya Mabalozi inayotarajiwa kuanza tarehe 21 Aprili 2024 mjini Kibaha, Pwani
Mwenyekiti wa Umoja wa Mabalozi Wastaafu Mhe. Balozi Aziz Ponary Mlima akizungumza kwenye kikao cha maandalizi kuelekea warsha ya Mabalozi inayotarajiwa kuanza tarehe 21 Aprili 2024 mjini Kibaha, Pwani

Friday, April 19, 2024

MHE. RAIS SAMIA AWAKARIBISHA WAFANYABIASHARA WA UTURUKI KUSHIRIKI MAONESHO YA SABASABA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa mwaliko rasmi kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Uturuki kushiriki Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba yanayotarajiwa kufanyika nchini mwishoni mwa mwezi Juni 2024.

 

Mhe. Rais Dkt. Samia ametoa mwaliko huo wakati akifungua rasmi Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki lililofanyika leo tarehe 19 Aprili 2024 jijini Istanbul na kuhudhuriwa na zaidi ya wafanyabiashara  na wakezaji 150 kutoka nchi hizi mbili.

 

Amesema maonesho hayo ya biashara ambayo ni makubwa Afrika Mashariki hutoa fursa ya kuwakutanisha wafanyabiashara na kuwawezesha kubadilishana taarifa na uzoefu, kujua taarifa mpya za masoko na bidhaa pamoja na  kuuza bidhaa zao.

 

Kadhalika Mhe. Rais Samia ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uturuki kuja kuwekeza nchini na kuitaja Tanzania kama nchi yenye fursa lukuki kama vile ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, Hifadhi za wanyama kwa ajili ya utalii, nishati, madini ikiwemo Tanzanite ambayo hupatikana nchini Tanzania pekee na fursa za biashara na uwekezaji.

 

 Amesema Serikali yake imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji  ambapo pamoja na mambo mengine imewekeza katika kujenga miundombinu inayoiunganisha Tanzania na nchi nyingine jirani ikiwemo Reli ya Kisasa ya SGR.

 

Vilevile, Mhe. Rais Samia alitumia fursa hiyo kuzipongeza Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizi mbili kwa kuandaa kwa mafanikio Kongamano hilo ambalo ni jukwaa muhimu katika kukuza ushirikiano kwenye sekta ya biashara na uwekezaji.

 

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yilmaz ambaye alishiriki Kongamano hilo, amesema nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta ambazo nchi hiyo imepiga hatua ikiwemo Utalii, Usafirishaji, Biashara na Uwekezaji.

 

Awali akizungumza kwenye Kongamano hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesisitiza umuhimu wa nchi hizi mbili kushirikiana na Sekta Binafsi katika kufikia malengo ya kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi wa mataifa haya.

 

Kadhalika ametoa rai kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Tanzania kuunga mkono juhudu nyingi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na mataifa mbalimbali ikiwemo Uturuki ili kutengeneza mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara za kuvuka mipaka kwa Watanzania.

 

Mhe. Rais Samia yupo nchini Uturuki kwa ziara ya kitaifa kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Mhe. Recep Tayyip Erdogan.

Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akifungua rasmi Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki lililofanyika jijini Istanbul, Uturuki tarehe 19 Aprili 2024. Pamoja na mambo mengine Mhe. rais Samia alitumia nafasi hiyo kuwaalika wafanyabiashara kutoka Uturuki kushiriki Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Juni 2024

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji akizunumza wakati wa Kongamano la Baishara kati ya Tanzania na Uturuki

Mhe. Rais Dkt. Samia akiwa na Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yilmaz pamoja na viongozi wengine akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki
Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yilmaz akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki

Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki likiendelea
Mhe. Rais Samia na Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Yilmaz na viongozi wengine wakiwa wamesimama kwa ajili ya heshima ya nyimbo za mataifa haya mawili zikipigwa wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki lililofanyika Jijini Istanbul tarehe 19 Aprili 2024


Mkurugenzi wa Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga (mwenye tai y abuluu) akiwa na wageni waalikwa na wafanyabiashara kutoka Tanzania kwenye Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki.

Mkurugenzi wa Sheria atika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Dkt. Gift Kweka akiwa na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Mariam Killo wakishiriki Kongamano la Baiashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki

Kongamano likiendelea

Sehemu ya Wafanyabiasha na wawekezaji wa Uturuki wakishiriki Kongamano

Mhe. Waziri Makamba akibadilishana mawazo na mmoja wa wageni waalikwa walioshiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki

Kongamano likiendelea

Sehemu ya washiriki wa Kongamano

Mhe. Rais Samia na Viongozi wengine wakishiriki sehemu ya utaratibu wa ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki



 

Thursday, April 18, 2024

WIZARA YA MAMBO YA NJE YAJIVUNIA KUIMARIKA KWA DIPLOMASIA, MIAKA 60 YA MUUNGANO


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) ametaja mafanikio ya Wizara katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Balozi Mbarouk ametaja mafanikio hayo jijini Dodoma Aprili 18, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya Wizara katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania. 

Balozi Mbarouk amesema Wizara inajivunia kuendelea kuimarika kwa ushirikiano na uhusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali duniani na hivyo kupata mafanikio katika sekta mbalimbali kupitia ushirikiano wa uwili na ujirani mwema baina yake na mataifa mengine, 

“Mafanikio haya yamepatikana kupitia ushirikiano uliopo ambao unatekelezwa kupitia taratibu maalum ikiwemo mikutano ya Tume za Ushirikiano wa Pamoja. Ushirikiano huu umeleta mafanikio kupitia kusainiwa Mikataba na Hati za Makubaliano (MoUs) ili kutekeleza maeneo mahsusi katika sekta mbalimbali za siasa, kiuchumi na kijamii,” alisema. 

Amesema kupitia mikutano hiyo Tanzania imenufaika na kuongezeka kwa biashara na uwekezaji ambapo bidhaa za kilimo, mifugo, matunda na mbogamboga zimepata masoko katika nchi mbalimbali. 

Amesema Tanzania imenufaika na fursa za mafunzo ya muda mrefu na mfupi yanayofadhiliwa na nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza, Uturuki, Marekani, Misri, India, Indonesia, China, Hungary, Japan, New Zealand, Australia, Urusi, Ujerumani, Cuba, Korea, Yugoslavia, Uholanzi, Ubelgiji, Algeria, Sudan, Saudi Arabia, Thailand na Pakistan. 

Amesema Tanzania imefanikiwa kuwa sehemu ya kuanzishwa kwa jumuiya za kikanda kama Umoja wa Afrika; Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Nchi zilizo katika Maziwa Makuu (ICGLR) na kupitia uanachama katika jumuiya hizo Tanzania imetekeleza programu katika sekta mtangamano za siasa, ulinzi na Usalama; Miundombinu; Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji. 

“Tanzania imekuwa sehemu ya utekelezaji wa dhana ya kutatua changamoto za kidunia kwa pamoja yaani Multilateralism, kuwa mbia anayeaminika na kukubalika katika maamuzi mbalimbali duniani hasa katika mashirika ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa na kuwa mbia kwenye vyombo mbalimbali ikiwemo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa; Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; Benki ya Dunia na Shirika la Biashara Duniani (WTO),” alisema. 

Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa sehemu ya maamuzi katika maeneo ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi; ulinzi na usalama; utatuzi wa migogoro; maendeleo endelevu na utafutaji rasilimali kwa ajili ya maendeleo ambapo kupitia jukwaa hilo imepata fursa ya kutoa misimamo yake kwa masuala muhimu ikiwemo mgogoro wa Isarel na Palestina na suala la Sahara Magharibi na kuwa sehemu ya kuunga mkono Sera ya Kutofungamana na Upande wowote (NAM) na kuunga mkono ajenda ya msimamo wa Kundi la 77 na China katika majukwaa ya Kimataifa kwa maslahi mapana ya Taifa. 

Amesema Tanzania inajivunia mchango wake katika juhudi za kulinda Amani Duniani na hivyo kutekeleza malengo ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje na moja ya malengo mahsusi ya Umoja wa mataifa. 

Amesema pia Tanzania imekuwa ikishiriki kulinda Amani kupitia Misheni za Kikanda ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa na baadhi ya maeneo ambayo Tanzania imechangia walinda amani ni pamoja na Lebanon; Darfur; Abyei; Liberia; Sudan Kusini; Sudan; DRC; Msumbiji na Afrika ya Kati na kuongeza kuwa Tanzania imeshiriki kikamilifu katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo na diplomasia kwenye nchi na maeneo mbalimbali ikiwemo, Darfur; Cambodia; Sudan Kusini; Burundi na Kenya. 

Amesema Tanzania kuwa mwenyeji wa Taasisi za Kimataifa kama ishara ya kuaminika na kukubalika na nchi nyingine. Tanzania imeendelea kufungua Balozi na Ofisi za Uwakilishi katika nchi mbalimbali za kimkakati ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hususan Diplomasia ya Uchumi. 

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefungua Balozi mpya mbili za Vienna, Austria na Jakata, Indonesia na Konseli Kuu mbili za Lugumbashi na Guangzhou, China ambapo ufunguzi wa Balozi hizo unaifanya Tanzania kuwa na Balozi na Ofisi za Uwakilishi 45 na Konseli Kuu TANO huku ikiwa ni mwenyeji wa nchi na mashirika ya kimataifa zaidi ya 90 zikiwemo Konseli Kuu ambazo baadhi yake zipo Zanzibar kama vile China, Oman, India na Umoja wa Falme za Kiarabu. 

Amesema Tanzania imefanikiwa kutoa viongozi mahiri kuongoza taasisi za kikanda na kimataifa ikiwa ni ishara ya kuaminiwa na mataifa mengine na kutaja baadhi ya nafasi hizo kuwa ni uteuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Kilele wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika utakaofanyika Paris, Ufaransa mwezi Mei 2024. 

Amesema Tanzania pia ilitoa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo Dkt. Salim Ahmed Salim aliongoza Vikao Vinne vya Baraza hilo mwaka 1979 na 1980 na Dkt. Salim Ahmed Salim alihudumu kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika (OAU). Watanzania wengine ni Dkt. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa kwanza kutoka Afrika; Balozi Getrude Mongela kuwa Rais wa Bunge la Afrika; Dkt. Stergomena Tax kuwa katibu Mtendaji wa SADC; Balozi Juma Mwapachu katibu Mkuu wa EAC; Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.), Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR); Profesa Anna Tibaijuka kuwa Naibu Katibu Mkuu na Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT) na Mkuu wa Ofisi za Umoja wa Mataifa Nairobi (UNON), Bi. Joyce Msuya, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb.) kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Dkt. Tulia ni mwanamke wa kwanza kutoka barani Afrika kushika wadhifa huo. 

Amesema Tanzania imechangia katika juhudi za kubidhaisha Kiswahili ndani na nje ya nchi na kutoa ushawishi wa matumizi yake kama nyenzo ya diplomasia, usuluhishi wa migogoro; ukombozi na uhuru katika nchi za bara la Afrika. 

Amesema Viongozi wa Tanzania katika awamu zote na sasa wakiongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi; Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) wamekuwa wakifanya ziara za kimkakati katika nchi mbalimbali kwa lengo la kukuza na kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na nchi hizo. 

Amesema Wakuu wa Nchi waliotembelea Tanzania katika miaka ya hivi karibun ni pamoja na: Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni; Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame; Rais wa Burundi, Mhe. Everiste Ndayishimiye; Rais wa DRC, Mhe. Felix Tshisekedi; Rais wa Msumbiji, Mhe. Fillipe Nyusi; Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema; Rais wa Malawi, Mhe. Lazarous Chakwera; Rais wa Poland, Mhe. Andrzej Duda; Rais wa Ujerumani, Mhe. Frank-Walter Steinmeier; Rais wa Romania, Mhe. Klaus Werner Iohannis; Rais wa Hungary, Mhe. Katalin Novak; Rais wa Indonesia, Mhe. Joko Widodo; Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris; Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Valdes Mesa; Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Abiy Ahmed na Naibu Waziri Mkuu wa China Mhe. Liu Guozhong na Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto. 

Amesena Serikali imeimarisha ushiriki wa Watanzania waishio Nje ya Nchi na Raia wa Nchi nyingine Wenye Asili ya Tanzania katika maendeleo ya Taifa na kuchukua hatua za Kisera kwa kujumuisha masuala ya Diaspora katika mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 na imekamilisha mfumo wa kiditali wa kukusanya na kutunza taarifa za Diaspora ambapo mpaka sasa Diaspora wa Tanzania wapatao 1403 wamejiandikisha katika mfumo huo na hivyo kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi za idadi ya Diaspora, mahali walipo, ujuzi na uzoefu walionao huku mfumo pia ukiwawezesha Diaspora kupata taarifa kuhusu fursa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali na sekta binafsi nchini. 

Amesema Serikali iko katika hatua za kukamilisha kutoa Hadhi Maalum (Special Status) kwa Raia wa Nchi Nyingine Wenye Asili ya Tanzania ili kuwezesha kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya Taifa.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akiongea na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Miaka 60 Muungano wa Tanzania katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) alipokuwa akiongea nao kuhusu mafanikio ya Miaka 60 Muungano wa Tanzania katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akisisitiza jambo wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Miaka 60 Muungano wa Tanzania katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) hayupo pichani alipokuwa akiongea nao kuhusu mafanikio ya Miaka 60 Muungano wa Tanzania katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.