Friday, April 19, 2024

MHE. RAIS SAMIA AWAKARIBISHA WAFANYABIASHARA WA UTURUKI KUSHIRIKI MAONESHO YA SABASABA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa mwaliko rasmi kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Uturuki kushiriki Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba yanayotarajiwa kufanyika nchini mwishoni mwa mwezi Juni 2024.

 

Mhe. Rais Dkt. Samia ametoa mwaliko huo wakati akifungua rasmi Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki lililofanyika leo tarehe 19 Aprili 2024 jijini Istanbul na kuhudhuriwa na zaidi ya wafanyabiashara  na wakezaji 150 kutoka nchi hizi mbili.

 

Amesema maonesho hayo ya biashara ambayo ni makubwa Afrika Mashariki hutoa fursa ya kuwakutanisha wafanyabiashara na kuwawezesha kubadilishana taarifa na uzoefu, kujua taarifa mpya za masoko na bidhaa pamoja na  kuuza bidhaa zao.

 

Kadhalika Mhe. Rais Samia ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uturuki kuja kuwekeza nchini na kuitaja Tanzania kama nchi yenye fursa lukuki kama vile ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, Hifadhi za wanyama kwa ajili ya utalii, nishati, madini ikiwemo Tanzanite ambayo hupatikana nchini Tanzania pekee na fursa za biashara na uwekezaji.

 

 Amesema Serikali yake imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji  ambapo pamoja na mambo mengine imewekeza katika kujenga miundombinu inayoiunganisha Tanzania na nchi nyingine jirani ikiwemo Reli ya Kisasa ya SGR.

 

Vilevile, Mhe. Rais Samia alitumia fursa hiyo kuzipongeza Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizi mbili kwa kuandaa kwa mafanikio Kongamano hilo ambalo ni jukwaa muhimu katika kukuza ushirikiano kwenye sekta ya biashara na uwekezaji.

 

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yilmaz ambaye alishiriki Kongamano hilo, amesema nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta ambazo nchi hiyo imepiga hatua ikiwemo Utalii, Usafirishaji, Biashara na Uwekezaji.

 

Awali akizungumza kwenye Kongamano hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesisitiza umuhimu wa nchi hizi mbili kushirikiana na Sekta Binafsi katika kufikia malengo ya kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi wa mataifa haya.

 

Kadhalika ametoa rai kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Tanzania kuunga mkono juhudu nyingi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na mataifa mbalimbali ikiwemo Uturuki ili kutengeneza mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara za kuvuka mipaka kwa Watanzania.

 

Mhe. Rais Samia yupo nchini Uturuki kwa ziara ya kitaifa kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Mhe. Recep Tayyip Erdogan.

Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akifungua rasmi Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki lililofanyika jijini Istanbul, Uturuki tarehe 19 Aprili 2024. Pamoja na mambo mengine Mhe. rais Samia alitumia nafasi hiyo kuwaalika wafanyabiashara kutoka Uturuki kushiriki Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Juni 2024

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji akizunumza wakati wa Kongamano la Baishara kati ya Tanzania na Uturuki

Mhe. Rais Dkt. Samia akiwa na Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yilmaz pamoja na viongozi wengine akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki
Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yilmaz akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki

Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki likiendelea
Mhe. Rais Samia na Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Yilmaz na viongozi wengine wakiwa wamesimama kwa ajili ya heshima ya nyimbo za mataifa haya mawili zikipigwa wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki lililofanyika Jijini Istanbul tarehe 19 Aprili 2024


Mkurugenzi wa Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga (mwenye tai y abuluu) akiwa na wageni waalikwa na wafanyabiashara kutoka Tanzania kwenye Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki.

Mkurugenzi wa Sheria atika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Dkt. Gift Kweka akiwa na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Mariam Killo wakishiriki Kongamano la Baiashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki

Kongamano likiendelea

Sehemu ya Wafanyabiasha na wawekezaji wa Uturuki wakishiriki Kongamano

Mhe. Waziri Makamba akibadilishana mawazo na mmoja wa wageni waalikwa walioshiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki

Kongamano likiendelea

Sehemu ya washiriki wa Kongamano

Mhe. Rais Samia na Viongozi wengine wakishiriki sehemu ya utaratibu wa ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki



 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.