Thursday, April 18, 2024

MHE. RAIS SAMIA ATUNUKIWA SHAHADA YA HESHIMA YA UDAKTARI NCHINI UTURUKI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) katika Uchumi na Chuo Kikuu cha Ankara cha nchini Uturuki ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kuboresha maisha ya watanzania kupitia mageuzi mbalimbali pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi mbaimbali duniani ikiwemo Uturuki.


Akizungumza kupokea tuzo hiyo kwenye hafla iliyofanyika katika Chuo hicho jijini Ankara leo tarehe 18 Aprili 2024, Mhe. Rais Samia amelishukuru Baraza la Chuo kwa kumpatia heshima hiyo kubwa kwake na kwa Watanzania wake kwa waume na  kukipongeza Chuo hicho kwa kuendelea kutoa elimu yenye ubora na kuiweka Uturuki kuwa miongoni mwa nchi zinazotoa elimu ya juu bora duniani.

 

“Nilipopokea taarifa kuhusu kutunukiwa shahada hii nilijiuliza, wametumia vigezo gani hadi kufikia uamuzi huu, Waziri wangu wa Mambo ya Nje alinipatia orodha yenye vigezo hivyo nikakubali, nawashukuru sana” alisema Rais Dkt. Samia

 

Mhe. Rais Samia amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Uturuki katika kufikia malengo yake ya kukuza  uchumi kupitia ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, kilimo, uwekezaji na ushirikiano baina ya watu wa nchi hizi mbili.

 

Baraza la Chuo Kikuu cha Ankara kwa kauli moja liliamua kumtunukia Mhe. Rais Dkt. Samia Shahada hiyo ya heshima, kwa kutambua Uongozi wake wa kipekee ambao umeleta mageuzi makubwa ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi nchini Tanzania. Mageuzi  hayo yameboresha ustawi wa Watanzania; na kuimarisha sifa ya Tanzania ulimwenguni; na yamekuza mahusiano ya kibiashara, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine, ikiwemo Uturuki.


Hafla ya kukabidhiwa tuzo hiyo imeongozwa na Prof. Necdet Ünüvar, Mkuu wa Chuo, na kushuhudiwa na Wahadhiri  na wanafunzi wa Chuo hicho pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Tanzania na Uturuki akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa.

Shahada hii ni ya pili kwa Mhe. Rais Samia kutunukiwa kutoka ugenini ambapo Shahada ya kwanza ya aina hiyo alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India mwezi Oktoba 2023.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ankara cha nchini Uturuki,  Prof. Necdet Ünüvar, akimtunuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) katika Uchumi katika hafla iliyofanyika Chuoni hapo tarehe 18 Aprili 2024 wakati wa ziara ya kitaifa ya Mhe. Rais Samia nchini humo.
Mhe. Rais Dkt. Samia akiwa katika picha ya pamoja na Prof. Ünüvar pamoja na Waziri anayeshughulikia masuala ya Familia na Huduma za Jamii wa Uturuki, Mhe.Mahinur Ozdemir Goktas mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi na Chuo Kikuu cha Ankara

Mhe. Rais Dkt. Samia akifuwa ukumbini kabla ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi na Chuo Kikuu cha Ankara. Kutoka kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akifuatiwa na Prof.Ünüvar pamoja na Mhe. Waziri Mahinur



Taratibu mbalimbali zikiendelea kabla ya Mhe. Rais Samia kutunukiwa Shahada yake ya Udaktari. Pichani ni viongozi wakiwa wamesimama kwa heshima ya nyimbo za mataifa yao

Mhe. Rais Dkt. Samia akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Chuo cha Ankara, Wakufunzi na Viongozi mbalimbali

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.