Kampuni
za Denmark zimealikwa kuja kuwekeza nchini katika sekta za uchukuzi, nishati,
madini, mazingira na uchumi wa buluu ambazo ni moja ya sekta za kipaumbele za
Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mwaliko
huo umetolewa wakati wa mikutano baina ya Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na
Masuala ya Hali ya Hewa wa Denmark, Mhe. Dan Jorgensen na Waziri wa Fedha, Mhe.
Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na
Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na
Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo iliyofanyika jijini Dodoma leo Aprili 5,
2024.
Waziri
Nchemba alisema Serikali inajenga miundombinu ya reli ya kiwango cha kimataifa
(SGR) ambapo Serikali ya Denmark imesaidia kipande cha kutoka Morogoro hadi
Makutupora ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 90. Alisema Serikali
inakaribisha wawekezaji kuendesha reli hiyo ambapo itakapokamilika itaunganisha
Tanzania na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Rwanda.
Dkt.
Nchemba pia alizitaka kampuni za Denmark kuchangamkia fursa za ujenzi wa
barabara ya mwendo kasi (express way) ya kutoka Dar Es Salaam hadi Dodoma
ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kupunguza msongamano wa magari katika
barabara hiyo kuu nchini.
Kwa
upande wake, Dkt. Jafo alisisitiza umuhimu wa Denmark kushirikiana na Tanzania
katika programu za utunzaji wa mazingira ikiwemo uwekezaji katika sekta ya
nishati jadidifu. Aliiomba Denmark kuunga mkono jitihada zinazofanywa na
Serikali katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Misaada
inayohitajika, alisema kuwa ni pamoja na kujenga uwezo wa watumishi, misaada ya
kiufundi na rasilimali mbalimbali zikiwemo fedha.
Prof.
Mkumbo, kwa upande wake alisisitiza umuhimu wa kampuni za Denmark kuja kuwekeza
katika viwanda vya kuongeza thamani (processing industries) hususan katika
madini hadimu nchini. Alisema fursa katika sekta hiyo ni kubwa kwa kuwa Tanzania
ina takribani aina 10 za madini hayo.
Aliiomba
Denmark kuunga mkono jitihada za Serikali za kuchochea sekta binafsi nchini
ambayo mchango wake bado uko chini, licha ya umuhimu wake katika kuongeza ajira
na kuondoa umasikini nchini. “Tunaomba kuungwa mkono katika misaada ya
kiufundi, elimu ya ufundi, urasimishaji wa sekta binafsi, kuchochea uhai wa
sekta binafsi ili tuweze kujenga uwezo wa watu wetu hasa vijana kuwa na mbinu
za kujiajiri wenyewe”, Prof. Mkumbo alisema.
Waheshimiwa
Mawaziri walihitimisha mazungumzo yao kwa kuishukuru Denmark kwa misaada
inayoipatia Tanzania katika sekta mbalimbali. Ulitolewa mfano wa msaada wa
Krone bilioni 1.95 uliotolewa na Denmark kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa
kipindi cha mwaka 2014 hadi 2021.
Kwa
upande wake, Mhe. Jorgensen alieleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi za mwanzo
kabisa barani Afrika kuanza ushirikiano wa kidiplomasia na Denmark katika miaka
ya 1960. Hivyo, ameahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa kuzingatia vipaumbele
vitakavyobainishwa na pande zote mbili.
Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mazungumzo. |
Mazungumzo yakiendelea. |
Dkt. Mwigulu akimuaga Mhe. Dan Jørgensen. |
Picha ya pamoja |
Waziri wa Maendeleo na Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jørgensen akizungumza na Mhe. Prof. Mkumbo jijini Dodoma tarehe 5 Aprili, 2024. |
Picha ya pamoja. |
Picha ya pamoja. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.